Papa Leo XIV: Urbi et Orbi: Tarehe 11 Aprili 2026: Kesha La Kuombea Amani Duniani

Papa Leo XIV: “Urbi et Orbi” Sherehe ya Pasaka, megusia kuhusu: Nguvu ya upendo wa Mungu ambao ni Mungu mwenyewe, anayeumba, mwaminifu milele yote, Mungu anayesamehe na kukomboa; hii ni nguvu inayowakirimia walimwengu amani. Papa anawaalika waamini kuungana pamoja naye katika mkesha wa kuombea amani duniani utakaofanyika tarehe 11 Aprili 2026, Mkesha wa Dominika ya Huruma ya Mungu, Kanisa kuu la Mt. Petro, Mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Salam, Baraka na Ujumbe wa Kitume kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” ulianza kutolewa kwa mara ya kwanza katika historia na maisha ya Kanisa na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1974. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, ujumbe huu unawafikia watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mfumo wa matangazo yanayorushwa kwa njia ya satellite saba. Baba Mtakatifu Leo XIV katika maadhimisho ya Sherehe za Pasaka ya Bwana Dominika tarehe 5 Aprili 2026 ameongoza kwanza: Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Leo XIV katika Salam, Baraka na Ujumbe wake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” Sherehe ya Pasaka, amegusia kuhusu: Nguvu ya upendo wa Mungu ambao ni Mungu mwenyewe, anayeumba, mwaminifu milele yote, Mungu anayesamehe na kukomboa; hii ni nguvu inayowakirimia walimwengu amani; Ufufuko wa Kristo ni chemchemi ya matumaini; Msalaba wa Kristo ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya binadamu, chemchemi ya maisha mapya na amani, mwaliko wa kuongokea katika Injili ya amani ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka kwa wafu, ni Mfalme Mshindi. Pasaka ya Bwana ni ushindi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; mwanga dhidi ya giza la dhambi na mauti na kwamba, huu ni ushindi wa Mwana mpendwa wa Mungu ambao umemgharimu Kristo Yesu mateso makali kama Mwanakondoo na kifo cha Msalaba na hivyo kuwa ni mwanzo wa ukombozi wa binadamu wote sanjari na kazi ya uumbaji iliyokuwa chini ya uzito wa dhambi na utawala wa adui wa kale, yaani Shetani, Ibilisi.

Papa Leo XIV: Ujumbe wa Kitume: Urbi et Orbi 2026
Papa Leo XIV: Ujumbe wa Kitume: Urbi et Orbi 2026

Hii ni nguvu ya Mungu ambayo ni upendo wa Mungu ambao kimsingi ni Mungu mwenyewe anayeumba, mwaminifu milele yote; Mungu anayesamehe na kukomboa. Kristo, Mfalme Mshindi alijiachilia mikononi mwa Mungu Baba Mwenyezi, akatekeleza mapenzi ya Baba yake wa Mbinguni katika majadiliano kwa vitendo, akafanyika Neno, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, na hivyo kuwakirimia wanadamu maisha; akateswa na hatimaye akafa Msalabani. Nguvu ya Kristo Mfufuka ni sawa na mbegu ya ngano iliyozikwa ardhini, ikamea na kukua hadi kuwa mti mkubwa na tena ni sawa na mtu aliyejeruhiwa vibaya, akashinda hisia zake na hatimaye, akamwombea yule mtesi wake. Hii ndiyo nguvu, inayowaletea walimwengu amani kwa sababu ni chanzo cha uhusiano unaoheshimu watu wote katika ngazi mbalimbali na wala haujikiti katika kutafuta faida binafsi wala kuutekeleza katika hali ya upweke, bali unachangia katika kudumisha mchakato unaowahusisha wengine. Kristo Yesu kwa kufufuka kwake anawaimarisha waja wake mintarafu uhuru wao; mbele ya Kaburi tupu, anawajaza matumaini na mshangao kama ilivyokuwa kwa wafuasi wake; hofu na mashaka kama ilivyokuwa kwa wale walinzi wa Kaburi na Mafarisayo walioshindwa kumtambua yule aliyehukumiwa kufa ambaye sasa amefufuka kweli kweli! Waamini wamwachie fursa Kristo Mfufuka ili aweze kuwashangaza, kwa wongofu wa nyoyo zao katika upendo mkuu alio nao juu yao, ili mwenye silaha mkononi aweze kuziweka chini.

Kristo Yesu ni chimbuko la amani ya kweli duniani
Kristo Yesu ni chimbuko la amani ya kweli duniani   (AFP or licensors)

Hii ni amani inayosimikwa katika majadiliano; katika ukweli na uwazi, kama njia ya kuweza kukutana na wengine badala ya kuwatala. Huu ni mwaliko wa kuondokana na mazoea ya vita na hivyo kugeuka kuwa ni watu wasiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine na vifo vya maelfu ya watu, chuki na uhasama na matokeo yake yanaendelea kushuhudiwa katika masuala ya kiuchumi na kijamii na kwamba, huu ndio utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani.Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, Msalaba ni kielelezo cha mateso, mahangaiko na kifo, changamoto kwa walimwengu ni kutofanya mazoea na utamaduni wa dhambi na kifo na kwamba, watu wanaoogopa kifo, wapende Ufufuko kama anavyosema Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Waamini wapende Ufufuko kwani unawakumbusha kwamba, ubaya na dhambi hauna neno la mwisho kwani umeshindwa na Ufufuko. Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amewakirimia walimwengu maisha na uzima wa milele. Yn 14:27. Amani ya Kristo Mfufuka ni ile inayosimikwa katika toba na wongofu wa ndani kwa ajili ya amani ya Kristo Yesu, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kupaaza sauti zao ili kuwafanya watu wasikie kilio cha sauti ya nyoyo zao. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja naye katika mkesha wa kuombea amani duniani utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumamosi, tarehe 11 Aprili 2026, Mkesha wa Dominika ya Huruma ya Mungu.

Mwaliko wa kuungana na Papa Leo XIV Kusali kwa ajili ya amani duniani
Mwaliko wa kuungana na Papa Leo XIV Kusali kwa ajili ya amani duniani

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana, anasema Baba Mtakatifu Leo XIV iwe ni fursa ya kuonesha utashi wa kutotaka kutawala, nguvu na mabavu na matokeo yake, wamwombe Kristo Mfufuka aweze kuwakirimia walimwengu amani inayoendelea kusiginwa sehemu mbalimbali za dunia kutokana na vita, chuki na tabia ya kutojali, hali inayowafanya walimwengu kuwa wanyonge mbele ya ubaya na dhambi. Huu ni mwaliko kwa waamini kuweka mbele ya Kristo Mfufuka mateso na mahangaiko ya watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia; watu wenye kiu na amani ya kweli, inayoweza kutolewa na Kristo Yesu Mfufuka peke yake. Huu ni mwaliko kwa waamini kujiaminisha mbele ya Kristo Mfufuka kwa kumfungulia nyoyo zao, kwani ni Kristo peke yake anayeweza kufanya yote kuwa ni mapya. Rej Ufu21:5. Hatimaye, Baba Mtakatifu amewasalimi waamini kutoka katika sehemu mbalimbali za dunia kwa lugha kumi, ikiwemo lugha ya Kilatini: “Felix sit vobis Domini resurrectionis festivitas! Iesu resuscitati, inter nos adstantis, laetitiam cum omnibus communicate.”

Urbi et Orbi 2026
05 Aprili 2026, 16:05

Sala ya Malkia wa Mbingu ni nini?
 

Utenzi wa Malkia wa Mbingu ni kati ya tenzi nne za Bikira Maria (nyingine ni:Tunakimbilia Ulinzi wako,  Salam Malkia wa Mbingu, Salam Malkia). Kunako mwaka 1742, Papa Benedikto XIV alipoandika kwamba, waamini wasali Sala ya Malkia wa Mbingu wakiwa wamesimama, kama alama ya ushindi dhidi ya kifo, wakati wa Kipindi cha Pasaka, yaani kuanzia Domenika ya Ufufuko wa Bwana hadi Sherehe ya Pentekoste. Hii ni Sala ambayo husaliwa mara tatu kwa siku kama ilivyo pia Sala ya Malaika wa Bwana: Asubuhi, Mchana na Jioni ili kuweka wakfu Siku kwa Mwenyezi Mungu na Bikira Maria.

Utenzi huu kadiri ya Mapokeo ulianza kutumika kunako karne ya VI au Karne X, lakini kuenea kwake kunaanza kujitokeza katika nyaraka mbali mbali kati kati ya Karne ya XIII, ilipoingizwa kwenye Kitabu cha Sala za Kanisa cha Wafranciskani. Hii ni Sala inayoundwa na maneno mafupi manne yanayohitimishwa na Alleluiya na sala ya waamini wanaomwelekea Bikira Maria, Malkia wa mbingu, ili kufurahia pamoja naye kuhusu Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Francisko tarehe 6 Aprili 2015 wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, siku moja baada ya Sherehe ya Pasaka, aliwashauri waamini kuwa na moyo wa furaha wanaposali sala hii. “Tunamwendea Bikira Maria, tukimwomba afurahi, kwa sababu yule Mwanaye mpendwa aliyekuwa amemchukua mimba amefufuka kweli kweli kama alivyosema; tunajiaminisha kwa sala na maombezi ya Bikira Maria. Kimsingi furaha yetu ni mwangi wa furaha ya Bikira Maria kwani ndiye aliyetunza na anaendelea kutunza matukio mbali mbali ya maisha ya Yesu. “Tusali sala hii kwa furaha ya kuwa waana wa Mungu ambao wanafurahi kwa sababu Mama yao anafurahi”

 

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >