Askofu mkuu Amel Shimon Nona amechaguliwa kuwa ni Patriaki mpya wa Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo na kuamua kuchukua Jina la Paulos III. Askofu mkuu Amel Shimon Nona amechaguliwa kuwa ni Patriaki mpya wa Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo na kuamua kuchukua Jina la Paulos III.  

Patriaki Paulus III wa Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo

Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo imemchagua Askofu mkuu Amel Shimon Nona kuwa ni Patriaki mpya na kuamua kuchukua Jina la Paulos III. Hadi kuchaguliwa kwake, Patriaki Paulos III alikuwa ni Mkuu wa Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo huko Sydney, Australia na New Zealand. Patriaki Paulos III alizaliwa tarehe Mosi, Novemba 1967, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 11 Januari 1991 na Tarehe 13 Novemba, 2009 akateuliwa kuwa Askofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV Ijumaa tarehe 10 Aprili 2026 alikutana na kuzungumza na Wajumbe Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo (Chaldean Catholic Church) wanaohudhuria mkutano mkuu wa uchaguzi ambao umewakutanisha mjini Roma kuanzia tarehe 9 Aprili hadi Jumatano tarehe 15 Aprili 2026, ili kufanya uchaguzi wa Patriaki mpya wa Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo. Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo linapata chimbuko lake katika Mapokeo ya zamani ya Kanisa, mahali ambapo panafumbata historia ya wokovu; ni mahali penye amana na utajiri wa imani, tamaduni, ari na moyo wa kimisionari, kumbe wanaalikwa kutunza amana na utajiri huu kwa ujasiri na uaminifu. Ni Kanisa ambalo limepitia changamoto kubwa na limebaki na makovu ya vita, alama zinazogeuka kuwa ni kielelezo cha matumaini, ufufuko na maisha mapya.

Wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo
Wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo   (patriarcato caldeo)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema katika mwanga wa Kristo Mfufuka, maadhimisho ya Sinodi hii ni mwaliko wa kuondokana na hofu pamoja na woga, kwa kujikita kikamilifu katika uchaguzi wa Patriaki mpya atakayeliongoza Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo, kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu awe ni chemchemi ya maelewano yanayobubujika kutoka katika sakafu ya Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu. Patriaki mpya atakayechaguliwa awe kweli ni Baba katika imani, kielelezo cha umoja na ushirika, mnyenyekevu na awe ni mtu anayejielekeza katika ujenzi wa ushirika wa Kanisa katika upendo, huku akionesha heshima kwa kila mwamini. Rej 1Kor 13: 4-8. Patriaki mpya awe ni mtu wa heri, mtakatifu katika maisha ya kila siku, mchungaji mwenye kipaji na utamaduni wa kusikiliza kwa makini na anayetambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma na kwamba, awe ni mtu anayejitahidi kuwa ni sauti ya kinabii katika maisha na utume wa Kanisa.

Papa Leo XIV akiwa na wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad
Papa Leo XIV akiwa na wajumbe wa Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad   (@Vatican Media)

Patriaki mpya awe ni mtu wa sala, shuhuda, mjenzi na mragibishaji wa umoja katika upendo, kwa kushirikiana na kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro sanjari na kukuza majadiliano ya kiekumene na waamini wa Makanisa mengine. Ni katika muktadha huu, wajumbe Sinodi ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo Dominika tarehe 13 Aprili 2026 imemchagua Askofu mkuu Amel Shimon Nona kuwa ni Patriaki mpya wa Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo na kuamua kuchukua Jina la Paulos III. Hadi kuchaguliwa kwake, Patriaki Paulos III alikuwa ni Mkuu wa Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo huko Sydney, Australia na New Zealand. Patriaki Paulos III alizaliwa tarehe Mosi, Novemba 1967, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 11 Januari 1991, huko Baghdad. Tarehe 13 Novemba, 2009 Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu wa Mosul na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 8 Januari 2010. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 15 Januari 2015 akamteuwa kuwa Askofu mkuu “Ad Personam” wa Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo huko Sydney na hatimaye kusimikwa rasmi tarehe 7 Machi 2015. Tangu wakati huo, Patriaki Paulos III amejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya shughuli za kichungaji, akajikita katika machapisho mbalimbali yenye amana na utajiri mkubwa wa kitaalimungu, ukaribu wake kwa watu wa Mungu na ushuhuda wa imani yake kwa Kristo Yesu na Kanisa lake katika nyakati za mateso, nyanyaso na madhulumu dhidi ya Kanisa Katoliki la Baghdad ya Wakaldayo (Chaldean Catholic Church.)

Patriaki Paulos III
13 Aprili 2026, 16:35