Siku ya Kimataifa ya Michezo kwa Ajili ya Maendeleo na Amani: “International Day of Sport for Development and Peace; IDSDP” inaadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Aprili. Siku ya Kimataifa ya Michezo kwa Ajili ya Maendeleo na Amani: “International Day of Sport for Development and Peace; IDSDP” inaadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Aprili.  (ANSA)

Papa Leo XIV: Siku ya Kimataifa ya Michezo Kwa Ajili ya Maendeleo Na Amani 2026

Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumatatu ya Oktava ya Pasaka amekumbushia kwamba, tarehe 6 Aprili Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Michezo Kwa Ajili ya Maendeleo na Amani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, lugha ya michezo katika ujumla wake ni kukuza na kudumisha: Udugu wa kibinadamu; ni mahali panapowajumuisha watu na ni mahali pa ujenzi wa amani; mahali pa watu kukutana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Kimataifa ya Michezo kwa Ajili ya Maendeleo na Amani: “International Day of Sport for Development and Peace; IDSDP” inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Aprili. Itakumbukwa kwamba, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 23 Agosti 2013 lilipitisha Azimio la Siku ya Kimataifa ya Michezo kwa ajili ya Maendeleo na Amani. Tarehe 6 Aprili ilichaguliwa na Jumuiya ya Kimataifa ili kuenzi ufunguzi wa Michezo ya Olympiki iliyofanyika kunako tarehe 6 Aprili 1896 huko Athens nchini Ugiriki. Lengo la maadhimisho ya michezo Kimataifa ni kutambua na kuthamini majukumu ya michezo katika maisha ya watu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV anawahimiza wanamichezo duniani kote, kupitia shughuli zao za michezo wawe kweli ni mashuhuda wa udugu wa kibinadamu na wajenzi wa amani. Wawe ni mfano bora wa maadili na utu wema. Kwa hakika michezo inaweza kutekeleza dhamana na majukumu yake ulimwenguni kwa kukuza na kudumisha: maridhiano na maelewano kati ya watu wa Mataifa. Michezo iwe ni kwa ajili ya michezo na kamwe isigeuzwe kuwa ni biashara. Michezo ibaki katika maana yake halisi. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Michezo kwa Ajili ya Maendeleo na Amani: “International Day of Sport for Development and Peace; IDSDP” kwa Mwaka 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alikumbushia kwamba, tarehe 6 Aprili Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Michezo Kwa Ajili ya Maendeleo na Amani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, lugha ya michezo katika ujumla wake ni kukuza na kudumisha: Udugu wa kibinadamu; ni mahali panapowajumuisha watu na ni mahali pa ujenzi wa amani.

Michezo ni shule ya utu wema,  haki na amani
Michezo ni shule ya utu wema, haki na amani   (AFP or licensors)

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Michezo ya Olympiki kuanzia tarehe 6 Februari hadi tarehe 22 Februari 2026 na kuanzia tarehe 6 Hadi tarehe 15 Machi 2026 imefanyika Michezo ya Olimpiki, huko Milano na Cortina, Kaskazini mwa Italia, Baba Mtakatifu Leo wa XIV amewatumia barua washiriki wa michezo hii huku akionesha: Thamani ya michezo: Michezo na ujenzi wa amani; tunu msingi za michezo katika majiundo; Mchezo, shule ya maisha na ya kisasa; Michezo na maendeleo binafsi; Mambo yanayohatarisha tunu msingi za michezo; Mashindano na utamaduni wa watu kukutana; Michezo, Mahusiano na mang’amuzi; sanjari na Mpango mkakati wa michezo kwa ajili ya kuwa na maisha tele! Kipindi chote cha mashindano ya Olimpiki, vita na misigano yote ya kisiasa na kijamii ilisitishwa ili kutoa fursa kwa wananchi kufurahia michezo na hivyo michezo ikawa ni fursa ya kujenga na kudumisha amani; ukuaji wa udugu wa kibinadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, vita, kinzani na mipasuko ni dalili za kushindwa kwa ubinadamu. Dunia ina kiu ya amani kumbe, kuna haja ya kutumia nyenzo zitakazo saidia kusitisha matumizi mabaya ya madaraka na hivyo kujikita katika utawala wa haki na sheria. Tunu msingi za michezo katika majiundo ili kuweza kuwa na maisha tele pamoja na utimilifu wake. Rej. Yn 10:10. Mama Kanisa hana budi kutekeleza dhamana na utume wake hapa ulimwenguni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu katika michezo kama anavyosema Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa kuhusu utaratibu kwa wanariadha: “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate. Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika.” 1Kor 9:24-25. Hiki ni kielelezo cha mashindano ya kiroho; na kwamba Binadamu ni umoja wa mwili, roho na nafsi na hivyo Mama Kanisa anakazia umuhimu wa michezo katika maisha ya mwanadamu kama mambo muhimu sana katika kuhubiri na kufundisha.

Michezo ni fursa ya kujenga na kudumisha amani
Michezo ni fursa ya kujenga na kudumisha amani   (This asset - including all text, audio and imagery - is provided by Imagn Images. Reuters Connect has not verified or endorsed t)

Mchezo, shule ya maisha na ya kisasa mambo ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee na walezi katika maisha na kazi; Ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, Mama Kanisa anaona michezo kama fursa ya kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha kama vile: Udugu wa kibinadamu, mshikamano na amani. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema mapumziko yatumike kuimarisha afya ya kiroho na kimwili na kwamba, michezo pia inaweza kuimarisha, kustawisha na kukuza mahusiano ya kidugu kati ya wanadamu wa hali zote, mataifa na makabila mbalimbali. Kumbe, wakristo wanahimizwa kushiriki katika michezo, huku ikikolezwa na roho ya kiutu na ya kikristo. Rej. Gaudium et spes, n.61. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Mama Kanisa amekazia pia umuhimu wa michezo, utamaduni na elimu na kwamba, michezo ni lugha inayofahamika na wengi na kikolezo cha watu kukutana; kujadiliana na kwamba, bado kuna mengi ya kujifunza kutoka katika tamaduni za watu mbalimbali, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni. Michezo na maendeleo binafsi: Michezo ni chanzo cha furaha, mahali mtu anapoweza kujieleza kutoka katika undani wake; ni mahali pa kuonesha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali uchoyo na ubinafsi, unajielekeza katika mafao ya wengi; michezo inatoa fursa ya watu kukutana na hivyo kukuza na kudumisha udugu; ni mahali pa kuratibu kinzani na migogoro, kwa kusameheana na kusahau. Makocha wanayo kazi na dhamana nyeti katika kujenga umoja kama timu, kati ya wachezaji. Michezo inamwendeleza mtu mmoja mmoja sanjari na kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii; kumbe michezo lazima ijitahidi kuwalenga watu wote ndani ya jamii, kwani ni sehemu muhimu sana ya maendeleo ya binadamu.

Siku ya Kimataifa ya Michezo Kwa ajili ya Maendeleo na Amani 2026
Siku ya Kimataifa ya Michezo Kwa ajili ya Maendeleo na Amani 2026

Mambo yanayohatarisha tunu msingi za michezo ni pamoja na: Rushwa, michezo kufungamanishwa sana na masilahi ya kiuchumi na kifedha; kwa kujikita zaidi katika kutafuta na kupata ushindi kwa njia zozote zile, ambazo nyingine zinakwenda kinyume kabisa cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Masilahi ya kibiashara yanaonekana kufifisha tunu msingi za michezo zinazopaswa kulindwa na kudumishwa. Michezo kwa sasa inaonekana kuzima kiu ya uchu wa mali na fedha katika hili Mwinjili Mathayo anasema: “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.” Mt 6:24-26. Uchu wa mali na fedha unadhalilisha tasnia ya michezo na kuitumbukiza katika rushwa, kama ilivyo pia kwa jamii nzima. Mashindano na utamaduni wa watu kukutana na kukua kwa pamoja; kujenga na kudumisha mahusiano ya amani; kwa kutambua mapungufu ya kila mmoja; kwa kuheshimiana na kwamba, ushindi ni matokeo ya nidhamu, udumifu na uaminifu. Mashindano ni mchakato wa kusafiri kwa pamoja katika furaha, mafanikio na hata kushindwa kwao; tayari kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kumbe, michezo inapaswa kuwa ni chemchemi ya umoja katika tofauti zake msingi; zinazopania pamoja na mambo mengine kujenga familia ya binadamu inayosimikwa katika ukarimu, majadiliano na hali ya kuaminiana. Michezo, Mahusiano na mang’amuzi mintarafu ushindi na kushindwa, mambo yanayopaswa kusimikwa katika ukweli na unyenyekevu. Wanamichezo wajifunze kukubali matokeo, bila kukata wala kukatishwa tamaa; Kukubali ushindi, bila majivuno wala kejeli, bali wapokee ukweli katika hali ya ukomavu, kwa kutambua udhaifu wao na fursa ambazo ziko mbele yao daima. Kamwe michezo isichukue nafasi ya dini katika maisha ya mwanadamu, kwani itapoteza utambulisho wake na kwamba, wanamichezo watambulike kuwa ni watu wenye: mwili, roho na nafsi.

Michezo: Umoja, Upendo na Mshikamano
Michezo: Umoja, Upendo na Mshikamano   (Henning Bagger)

Baba Mtakatifu Francisko anatambua dhamana na jukumu la michezo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Michezo kwa asili inaweza kujenga jamii iliyo wazi, inayosimikwa katika mshikamano pasi na maamuzi mbele. Ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na wadau wa michezo, ambao hawaangalii tu ushindi na faida, bali wadau watakaojielekeza katika michezo ili kukoleza urafiki wa kijamii na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu tarehe 19 Machi 2022, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, aliridhia kuchapwa kwa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Katiba ilianza kutumika rasmi tarehe 5 Juni 2022, Sherehe ya Pentekoste na hivyo kuchukua nafasi ya Katiba ya Kitume “Pastor bonus” ya tarehe 28 Juni 1988 iliyoanza kutumika rasmi 1 Machi 1989. Kardinali José Tolentino Calaça de Mendonça T.O.S.D., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika Katiba hii ya Kitume, Ibara ya 154 anaonesha umuhimu wa utamaduni na michezo katika maisha na utume wa Kanisa kwa kukabidhi dhamana hii kwa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu. Michezo ni fursa muhimu sana inayoweza kuwaunganisha watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Ni mahali muhimu sana pa mazoezi yanayoweza kupyaisha na kuboresha maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Michezo ni shule muhimu sana ya maisha ya kiroho na kimwili na ndiyo maana Mji wa Vatican hata katika udogo wake duniani, bado una kikosi kazi katika michezo ya aina mbalimbali duniani. Michezo inasaidia kujenga utamaduni na madaraja ya watu wa Mungu kukutana hata katika tofauti zao msingi, ili kukamilishana.

Papa Leo XIV anathamini sana michezo
Papa Leo XIV anathamini sana michezo

Baba Mtakatifu Francisko, katika uzinduzi wa Waraka wa “Dare il meglio di sè”, yaani “Kujitoa Kikamilifu”:Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu” uliochapishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema kwamba, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika ngazi mbalimbali, ili kufikia lengo maalum. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu na furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbali mbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika.

Siku ya Michezo Kimataifa 2026
06 Aprili 2026, 16:24