2026.05.12 Ilikuwa tarehe 13 Mei 1981,Papa Yohane Paulo II alipigwa risasi katika Uwanja wa Mtakatifu Petro. 2026.05.12 Ilikuwa tarehe 13 Mei 1981,Papa Yohane Paulo II alipigwa risasi katika Uwanja wa Mtakatifu Petro. 

13 Mei 1981:Siku ya shambulio dhidi ya Papa Yohane Paulo II lilishtua ulimwengu

Miaka 45 tangu shambulio dhidi ya Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa Katekesi katika Uwanja wa Mtakatifu Petro,kumbukumbu ya tukio hilo inaendelea kuhusishwa na mada za maombi,msamaha na imani kwa Mungu zinazoakisiwa katika maneno ya Papa na warithi wake.

Vatican News

Miaka arobaini na tano imepita tangu shambulio dhidi ya Papa Yohane Paulo  II katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mnamo tarehe 13 Mei 1981, tukio lililoashiria historia ya Kanisa na kuvutia umakini wa jamii ya kimataifa. Kumbukumbu ya siku hiyo bado inahusishwa sio tu na picha kutoka Uwanja wa Mtakatifu Petro, bali pia na maneno ya maombi, msamaha, na imani kwa Mungu yaliyotamkwa katika miaka iliyofuata na Papa na warithi wake. Mnamo Mei 1981, muktadha wa kijamii na kisiasa wa kimataifa ulioneshwa na mvutano mpya kati ya Mashariki na Magharibi. Uvamizi wa Kisovieti wa Afghanistan ulikuwa umezidisha hali ya Vita Baridi, huku wasiwasi ukiongezeka Ulaya Mashariki kuhusu kuibuka kwa chama huru cha wafanyakazi Solidarność huko Poland. Nchini Italia, miaka ya ugaidi na vurugu za kisiasa zenye msimamo mkali zinazojulikana kama Anni di Piombo - Miaka ya Uongozi  mgumu- zilitikisa jamii hadi kiini.

Tarehe 13 Mei 1981

Kwa hiyo siku ya Jumatano, tarehe 13 Mei 1981, Uwanja wa Mtakatifu Petro ulijaa mahujaji waliokusanyika kwa ajili ya Katekesi ya kila juma. Papa Yohane Paulo II alikuwa akiwasalimia waamini kutoka kwenye gari jeupe aina ya jeep ambalo kwa kawaida hutumika kuzunguka uwanja wakati risasi zilipofyatuliwa karibu naye. Papa alijeruhiwa vibaya na mara moja akasafirishwa hadi Hospitali ya Gemelli ya Roma. Miongoni mwa walioripoti tukio hilo moja kwa moja alikuwa mwandishi wa habari wa Radio ya Vatican,  Benedetto Nardacci, ambaye sauti yake ilielezea mkanganyiko na ukimya uliofuata shambulio hilo. Akitazama umati katika uwanja huo, alielezea watu wakiwa wamesimama kimya na wakisubiri habari, huku Maaskofu na Mapadre  wakiwaalika waamini kumwombea Papa apate nafuu.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Habari ya Kiti Kitakatifu baadaye ilithibitisha kwamba Papa alikuwa amepigwa risasi tumboni na alikuwa akifanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Gemelli. Taarifa hiyo iliongeza kuwa, ingawa hali yake ilikuwa mbaya, kulikuwa na "matumaini ya kupona." Siku nne baadaye, wakati wa ujumbe wa Sala ya Malkia wa Mbingu kutokea  hospitalini, Papa Yohane Paulo II aliwahutubia waamini na kuzungumzia hadharani msamaha kwa Mehmet Ali Ağca, mtu aliyehusika na shambulio hilo. Alihakikisha sala zake kwa ajili ya mshambuliaji huyo na kujikabidhi tena kwa Bikira Maria kwa maneno haya: "Totus tuus ego sum" kwa kilatini ikiwa na maana  "Mimi ni wako kabisa."

Mateso yalibadilishwa kupitia upendo

Katika miaka iliyofuata, matukio ya tarehe 13 Mei 1981 yalihusishwa kwa karibu na ibada ya Papa kwa Mama Yetu wa Fatima. Papa Yohane Paulo II alielezea mara kwa mara imani yake kwamba maisha yake yalihifadhiwa kupitia maombezi yake. Wakati wa Misa ya mazishi ya Papa Yohane Paulo II  mnamo tarehe 8 Aprili 2005, Kardinali Joseph Ratzinger (Mrithi wake) alitafakari ushuhuda wa marehemu Papa wa mateso na imani. Akirejea vifungu kutoka kwa kitabu cha mwisho cha Yohane Paulo II, "Kumbukumbu na Utambulisho," alizungumzia mateso yaliyobadilishwa kupitia upendo na kuunganishwa na fumbo la Kristo.

"Papa Francisko:Maisha yetu na ulimwengu viko mikononi mwa Mungu"

Papa Francisko pia alikumbuka shambulio hilo wakati wa Katekesi yake  tarehe 12 Mei 2021, usiku wa kuamkia siku hiyo. Akirejea uhusiano kati ya tarehe ya shambulio hilo na ukumbusho wa kiliturujia wa Mama Yetu wa Fatima, alisema tukio hilo linawakumbusha wanadamu kwamba "maisha yetu na historia ya ulimwengu iko mikononi mwa Mungu." Kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane Paulo II inaendelea kusikika katika maisha ya Kanisa.

"Msiogope. Kubali mwaliko wa Kanisa na wa Kristo Bwana"

Mnamo tarehe 11 Mei 2025, muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwake kuwa  katika Kiti cha Petro, Papa Leo XIV aliwahutubia vijana wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu akirudia maneno yanayohusiana kwa karibu na Upapa wa Papa Wojtyła kwamba: “Msiogope! Kubali mwaliko wa Kanisa na wa Kristo Bwana.” Juma moja  moja baadaye, tarehe 18 Mei 2025, kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Karol Wojtyła, Papa Leo XIV aliongoza Misa iliyoashiria mwanzo wa huduma yake ya  kuwa katika kiti cha Kharifa wa Mtume Petro.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

12 Mei 2026, 16:54