Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 23 Mei 2026 anafanya hija ya kichungaji eneo la Acerra, maarufu kama "Terra dei Fuochi" yaani “Ardhi ya moto” Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 23 Mei 2026 anafanya hija ya kichungaji eneo la Acerra, maarufu kama "Terra dei Fuochi" yaani “Ardhi ya moto”  

Hija ya Kichungaji ya Papa Leo XIV Acerra: Utunzaji Bora wa Mazingira

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Juma la “Laudato si”, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 23 Mei 2026 anafanya hija ya kichungaji eneo la Acerra, maarufu kama "Terra dei Fuochi" yaani “Ardhi ya moto” eneo ambalo limeathiriwa sana na taka maalum na hatari zilizotupwa eneo hili kinyume cha sheria, taratibu na kanuni za nchi na mashirika pamoja na makampuni ya uhalifu. Sumu zitokanazo na taka ni tishio kwa usalama, ustawi na mendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sumu zitokanazo na taka ni tishio kubwa kwa usalama, ustawi, maendeleo na afya ya binadamu. Zinasambaa kupitia hewa chafu, maji yasiyo safi na salama sanjari na udongo ulioharibika. Kemikali hizi husababisha magonjwa sugu ya mfumo wa kupumua, saratani, na kuharibu viumbe hai. Mbinu kuu zinazofanya sumu za taka ziwe hatari kwa maisha ni pamoja na: Uchafuzi wa hali ya hewa: Utupaji mbaya na uchomaji wa taka zinazotoa gesi na chemikali hatari angani. Kuvuta hewa hii huathiri mapafu na mfumo wa fahamu. Uchafuzi wa maji: Taka zinazooza na kemikali huingia kwenye vyanzo vya maji, na kusababisha magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu au kuhara. Sumu kwenye Udongo: Kilimo katika udongo wenye taka zenye sumu husababisha mazao yaliyochafuliwa ambayo ni hatari sana kwa usalama na maisha ya binadamu. Kujikinga na athari hizi kunahitaji usimamizi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, Dominika tarehe 17 Mei 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amewaambia waamini na mahujaji kwamba, Mama Kanisa anaadhimisha Juma la “Laudato si” litakalofikia kilele chake Dominika tarehe 24 Mei 2026, Sherehe ya Pentekoste. Maadhimisho haya yanayofanyika sehemu mbalimbali za dunia, yakilenga kukuza na kudumisha utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, yanaragibishwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Juma la “Laudato si”, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 23 Mei 2026 anafanya hija ya kichungaji eneo la Acerra, maarufu kama "Terra dei Fuochi" yaani “Ardhi ya moto” eneo ambalo limeathiriwa sana na taka maalum na hatari zilizotupwa eneo hili kinyume cha sheria, taratibu na kanuni za nchi na mashirika pamoja na makampuni ya uhalifu.

Sumu zitokanazo na taka ni tishio kwa usalama na maisha ya binadamu
Sumu zitokanazo na taka ni tishio kwa usalama na maisha ya binadamu

Hili ni eneo linalopatikana katika Majimbo ya Napoli na Caserta. Uchafuzi huu wa mazingira nyumba ya wote, kimekuwa ni chanzo kikuu cha kusambaa kwa magonjwa ya Saratani sanjari na uchafuzi mkubwa wa mazingira. Askofu Antonio Di Donna wa Jimbo la Acerra, Kusini mwa Italia anasema, hili ni eneo ambalo limekumbwa na magonjwa ya kudumu, ukosefu wa haki na hasa haki ya mazingira salama, lakini Kanisa limekuwa mstari wa mbele kukemea uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, kwa kujikita katika kutafuta na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, kama Kristo Yesu alivyofanya kwa kuwaganga watu waliokuwa wameelemewa na magonjwa, akawalisha wenye njaa na kuwasamehe wale waliokuwa wanaogolea katika dimbwi la dhambi pamoja na kuwatangazia watu wa Mungu Habari Njema ya Wokovu. Mama Kanisa amekuwa mstari wa mbele kupambana na umaskini wa hali, kipato, kimaadili na utu wema, mambo yanayopelekea uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Hii ni changamoto kubwa tena ni ya kitaifa kwani si tu kwa eneo la Acerra peke yake. Eneo hili lina changamoto kubwa za maisha ya kijamii, ukosefu wa fursa za ajira; uwepo wa uhalifu wa makundi pamoja na uchumi dhaifu na kwamba, uchafuzi wa mazingira umesababisha magonjwa na vifo vingi. Kanisa limekuwa daima mstari wa mbele kuwahudumia waathirika wa uchafuzi huu wa mazingira nyumba ya wote. Kanisa limesikiliza na kujibu kilio cha maskini na dunia Mama Mama; Kanisa limejitosa kuelimisha vijana wa kizazi kipya kutambua umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira; Limeendelea kuwa ni sauti ya watu wasiokuwa na mazingira bora ya kuishi pamoja na kuragibisha majadiliano katika ukweli na uwazi. Jambo la msingi ni kwa familia zenyewe kuwajibika katika ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Uchafuzi wa mazingira ni hatari kwa maisha na maendeleo
Uchafuzi wa mazingira ni hatari kwa maisha na maendeleo   (AFP or licensors)

Itakumbukwa kwamba, Hayati Baba Mtakatifu Francisko alikuwa ametia nia ya kwenda kutembelea Casserta kunako mwaka 2020, lakini ikashindikana. Papa Leo X1V alipojulishwa kuhusu eneo hili mara moja alikubali kwani ni kiongozi anayependa kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji.Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; “Rerum Novarum.” Kilele cha hija hii ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Leo XIV ni pale atakapokutana na familia ambazo zimeathirika kwa kiwango kikubwa kutoka na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote; atakuwa ni shuhuda wa Injili ya faragha pamoja na sala kwa ajili ya ulinzi na tunza viumbe hai. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mwamko wa ukuaji wa ufahamu kuhusu umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira; kwa kujikita katika usafi; ushirikiano kati ya Taasisi zinazosimamia ulinzi na utunzaji wa mazingira; afya na maisha.

Hija ya Kichungaji

 

 

21 Mei 2026, 17:32