Kauli mbiu ya Mkutano huu ni "Kuhudumia, Kuandamana, Kuongoza. Misingi na Mienendo ya Uongozi katika Mashirika.” Kauli mbiu ya Mkutano huu ni "Kuhudumia, Kuandamana, Kuongoza. Misingi na Mienendo ya Uongozi katika Mashirika.”   (@Vatican Media)

Hotuba ya Papa Leo XIV Kwa Waratibu wa Vyama, Mashirika na Jumuiya mpya 2026

Waratibu wa vyama vya kitume, mashirika ya kikanisa na jumuiya mpya, kuanzia tarehe 21-22 Mei 2026 wamekuwa na mkutano wao wa mwaka, ili kujadili pamoja na mambo mengine: "Kuhudumia, Kuandamana, Kuongoza. Misingi na Mienendo ya Uongozi katika Mashirika.” Haya ni mambo makuu yanayopaswa kumwilishwa mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Ikumbukwe kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma inayopaswa kusimikwa katika ujenzi wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Ili kuweza kukabiliana na changamoto zote hizi, Baba Mtakatifu Francisko kunako 15 Agosti 2016 katika barua yake binafsi, “Motu Proprio” “Sedula mater” alianzisha Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kama sehemu ya mchakato wa Sekretarieti kuu ya Vatican kusoma alama za nyakati na kujibu kwa ufasaha na weledi mkubwa changamoto mamboleo katika maisha na utume wa Kanisa hususan katika maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu Francisko katika barua hii anasema, Mama Kanisa, mwingi wa huruma na mapendo, katika historia ya maisha na utume wake, amekuwa karibu sana kwa waamini walei, familia pamoja na kuhimiza Injili ya uhai, kama kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa walimwengu. Kanisa linatambua na kuthamini mchango wa waamini walei katika maisha na utume wake, kwani hawa wamepewa changamoto ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao Baraza linawahamasisha waamini walei kuhakikisha kwamba, wanalitegemeza Kanisa kwa karama na mapaji yao sanjari na kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini walei watambue: dhamana, wajibu na haki zao msingi ndani ya Kanisa. Vyama na mashirika ya kitume ni muhimu sana katika kufunda, kulea, kukuza na kudumisha imani inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawahamasisha waamini walei kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baraza liko mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha utume wa vijana wa kizazi kipya, kwa kutambua kwamba, vijana ni jeuri na matumaini ya Kanisa kwa leo na kwa siku za usoni.

Papa Leo XIV: Uongozi ni kuonesha njia, ni huduma
Papa Leo XIV: Uongozi ni kuonesha njia, ni huduma   (@Vatican Media)

Ni katika mkutadha huu, waratibu wa vyama vya kitume, mashirika ya kikanisa na jumuiya mpya, kuanzia tarehe 21 Mei hadi 22 Mei 2026 wamekuwa na mkutano wao wa mwaka, ili kujadili pamoja na mambo mengine: "Kuhudumia, Kuandamana, Kuongoza. Misingi na Mienendo ya Uongozi katika Mashirika.” Haya ni mambo makuu yanayopaswa kumwilishwa mintarafu mwanga na tunu msingi za Kiinjili. Ikumbukwe kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma inayopaswa kusimikwa katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari; kwa kulinda na kudumisha karama na malengo makuu ya vyama na mashirika ya Kikanisa, sanjari na kujikita katika mchakato wa malezi na makuzi wa wanachama wao. Wajumbe hawa kwa muda wa siku mbili wamechambua pamoja na mambo mengine kuhusu: Taalimungu ya uongozi ndani ya Kanisa; Changamoto na uwajibikaji katika uongozi ili kutafuta nyenzo msingi zinazoweza kusaidia kukabiliana na changamoto hizi: Uongozi kwa mtindo wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, Shuhuda katika uongozi; Upatanisho kama kielelezo cha uongozi. Wajumbe hawa, Alhamisi tarehe 21 Mei 2026 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye katika hotuba yake amegusia kuhusu: Uongozi katika Jumuiya ya Kikanisa. Kanisa lilianzishwa na Kristo Yesu kama ishara ya daima ya mapenzi yake ya wokovu kwa ulimwengu wote na ni mahali palipopendelewa na Mwenyezi Mungu, ambapo watu wote, katika kila zama, wanaweza kupokea matunda ya ukombozi na kupata maisha mapya ambayo Kristo Yesu anawakirimia waja wake. Kwa maana hii, asili ya Kanisa ni kisakramenti: hakika ina mwelekeo wa nje na wa kitaasisi pamoja na miundo yake, na wakati huo huo, ni ishara ya ufanisi ya ushirika ambayo kwayo waamini wanashiriki katika maisha yenyewe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Uongozi katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Uongozi katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, sifa hizi maalum hazina budi kuwepo katika utawala wake, kwa ajili ya kuelekeza mafao ya kiroho kwa ajili ya waamini. Hakika, Mtakatifu Paulo anaorodhesha kati ya karama: “Kuna miujiza,” anaandika, “na karama za kuponya, na kusaidia, na kutawala, na kunena kwa lugha mbalimbali” (1Kor 12:28). Kwa vyama vya kitume, mashirika ya kikanisa na jumuiya mpya, uongozi katika mifumo hii umekabidhiwa kwa waamini walei na unaonesha ushiriki wao katika ofisi ya Kifalme ya Kristo Yesu, inayopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo. Hii ni huduma kwa ajili ya waamini wengine na ujenzi wa maisha ya ushirika na huduma hii ni tunda la uchaguzi huru, ambao lazima ueleweke kuwa ni kielelezo cha utambuzi wa pamoja unaoruhusu sauti ya kila mtu kuoneshwa kwa uhuru zaidi. Kumbe, uongozi ni karama ya Roho Mtakatifu inayotambulikana kuwa ni zao la imani kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi; ni kwa ajili ya kuendeleza mema ya jumuiya, ushirika na Kanisa katika ujumla wake. Kumbe, uongozi kamwe hauwezi kutumika kwa ajili ya masilahi ya mtu binafsi, ufahari pamoja na hali ya mtu kutaka kujimwambafai na kwamba, uongozi hauwezi kamwe kulazimishwa kutoka juu, lazime uwe ni zawadi inayotambulika na kukubalika katika jamii na kwamba, zawadi hii inatokana na uchaguzi huru, ili kuleta ufanisi. Uongozi lazima utambuliwe na wachungaji wa Kanisa ambao husimamia uhalisi na matumizi sahihi ya karama za waamini.

Safa kuu za uongozi: Hii ni karama ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa
Safa kuu za uongozi: Hii ni karama ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anataja sifa muhimu katika uongozi: Kusikiza na uwajibikaji wa pamoja; ukweli na uwazi; Ukaribu wa kindugu; na utambuzi wa Jumuiya. Uongozi bora ni ule unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa ushiriki na uwajibikaji wa wanajumuiya wake; mambo msingi yanayopaswa kuzamishwa akilini kila wakati kiongozi anapotaka kutumia mamlaka yake. Ikumbukwe kwamba, watu wanaasili na historia tofauti; utambulisho wao sanjari na kanuni maadili na utu wema. Kumbe, viongozi wanaitwa kujivika jukumu la Kinabii, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza mahitaji ya sasa ya shughuli za kichungaji, ili kufahamu jinsi ya kukabiliana na changamoto mpya sanjari na hisia za kitamaduni, kijamii na za kiroho katika Ulimwengu mamboleo. Ni kwa njia hii, kiongozi anaweza kuwa ni Mkristo, mwanafunzi na mmisionari katika ulimwengu mamboleo na ndani ya Kanisa. Dhamana ya Unabii ndani ya Kanisa ni kukuza: Ukweli na Uwazi; Kusoma alama za nyakati; kujitamadunisha pamoja na kuangalia maisha na utume wa Kanisa, mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, viongozi wanapaswa kujenga na kudumisha ushrika kwa kuwa ni wasikivu hasa kwa kuhifadhi, kukua, na uimarishaji wa umoja na ushirika. Karama hii ni muhimu kwa ujenzi wa chama cha kitume na Kanisa katika ujumla wake,  kwa kujifunza kusikiliza na kukumbatia maoni mbalimbali, mwelekeo tofauti wa kitamaduni, maisha ya kiroho, tabia mbalimbali za kibinafsi, daima viongozi wajibidiishe kutafuta na kuhifadhi maamuzi ya wengi, ustawi, maendeleo na mafao makubwa ya ushirika. Hili jambo linahitaji ushuhuda wa upole, kujitenga, na upendo usio na ubinafsi kwa wote, ambao hutumika kama mfano kwa wote. Uaminifu kwa karama ni muhimu sana kama rejea kwa uongozi wa taasisi au wa Kikanisa.

Viongozi wanaalikwa kujivika jukumu la kinabii
Viongozi wanaalikwa kujivika jukumu la kinabii   (@Vatican Media)

Kila karama halisi tayari inajumuisha uaminifu na uwazi kwa Kanisa. Kuongoza kwa uaminifu na ukweli ni kwa kufuata mifano chanya iliyopita, kukumbatia changamoto za wakati kwa kusoma alama za nyakati. Vyama vya kitume, mashirika na jumuiya mpya ni zawadi kubwa kwa Mama Kanisa, ni chemchemi ya amana na utajiri mkubwa, wa elimu na ujuzi wa kueneza Habari Njema ya Wokovu, sanjari na kukuza miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Kumbe, tofauti za karama, mapaji ya Roho Mtakatifu; sera na mbinu mkakati wa shughuli za kitume zinazoendelezwa kwa muda mrefu zinachota amana na utajiri wake kutoka katika tamaduni, sanaa, jamii, maeneo ya kazi na hivyo kubeba ndani mwake mwanga wa Injili; mambo yanayopaswa kuhifadhiwa kwa neema ya Mungu na kwamba, hili ni jukumu lao kuhakikisha kwamba, wanasaidia kukuza karama na zawadi mbalimbali za Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa.

Uongozi wa waamini walei
21 Mei 2026, 16:59