Papa Leo XIV Katekesi Kuhusu Liturujia: Akutana na Mahujaji Kutoka Tanzania
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katiba ya “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia” inaelezea kanuni za jumla za marekebisho na ukuzaji wa Liturujia Takatifu; Fumbo Takatifu la Ekaristi, Sakramenti nyingine na visakramenti; Liturujia ya Vipindi; Mwaka wa Liturujia wa Kanisa, Muziki Mtakatifu; na hatimaye, ni Sanaa Takatifu na Vifaa vitakatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanafafanua nafasi ya Liturujia katika fumbo la Kanisa kwa kusema kwamba, maana kwa njia ya Liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi wetu.” Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waoneshe katika maisha yao na kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo Yesu na pia maumbile halisi ya Kanisa la kweli. Kanisa kwa undani kabisa ni la kibinadamu na pia la kimungu, linaloonekana lakini lenye mambo yasiyoonekana ndani yake, lenye bidii kubwa katika matendo na uradhi katika kutafakari, lililopo ulimwenguni lakini kama mwenye kufanya hija.
Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 20 Mei 2026 imekita mizizi yake katika Liturujia katika Fumbo la Kanisa. Baba Mtakatifu ametambua uwepo na ushiriki wa Kundi la Pili la Mahujaji 35 kutoka Tanzania. Hili ni kundi ambalo limeandaliwa na Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu katika nafsi ya Padre John Greyson C.PP.S., Dekano wa Dekania ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Jimbo Kuu la Dodoma, Tanzania. Hili ni kundi linalowahusisha watu wa Mungu kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jimbo kuu la Dodoma, Jimbo la Moshi, Iringa na Bukoba na Kayanga. Lina watawa wawili, waamini walei ishirini na sita na mapadre saba. Kati ya hawa Mapadre kuna Mapadre wanne kutoka Jimbo Katoliki la Moshi, wanaomwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre. Hawa ni Padre Emmanuel Ndekusara, Padre Gregory Bahati, Padre Peter Asantebwana pamoja na Padre Victorine Salema wote ni kutoka Jimbo Katoliki la Moshi, Tanzania.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre ni muda muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema, upendo na ukarimu wake. Ni kipindi cha kuwashukuru kwa wale wote walijiojisadaka bila ya kujibakiza, kiasi cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya huduma kwa Habari Njema ya Wokovu na leo hii wamekuwa hivi jinsi walivyo. Hawa ni viongozi wa Kanisa waliobeba madonda ya watu wa Mungu wakachangia kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu na kwamba, mateso na mahangaiko ni kielelezo cha uaminifu wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi.
Baba Mtakatifu Leo XIV anawaka waamini kumwachia nafasi Roho Mtakatifu aweze kuwapyaisha kutoka katika undani wa maisha yao wanaposhiriki kikamilifu Liturujia ya Kanisa kwa njia ya Ibada, ishara, ukimya, lakini zaidi kwa njia ya uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu. Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa yawasaidie waamini kuzama katika Fumbo la maisha na utume wa Kanisa, kiasi kwamba, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa sanjari na Neno la Mungu linalotangazwa na kushuhudiwa linakuwa ni chemchemi ya mabadiliko ya ndani katika maisha. Wakiwa wameungana na Bikira Maria katika Sala, waendelee kumsubiri Roho Mtakatifu atakapolishukia Kanisa wakati wa Sherehe ya Pentekoste na kuwakirimia waamini Mapaji yake Saba. Roho Mtakatifu ni nguvu ya Mungu inayobadilisha mioyo ya waamini na kupyaisha ulimwengu. Anapoingia ndani ya mwamini, huondoa kiburi na uchungu, akitoa uwezo wa kusamehe na kupenda bila masharti. Kazi hii ya Roho Mtakatifu inaleta mwamko mpya unaofanya maisha ya watu binafsi na jamii kuwa vyombo vya haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na hivyo kuendelea na hija ya maisha ya kiroho kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahari.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, tarehe 18 Mei 1986, Miaka 40 iliyopita Mtakatifu Yohane Paulo II alichapisha Waraka wake wa Kitume: “Dominum et Vivificantem” Yaani "Bwana Mleta Uzima.” Waraka huu unahusu hasa Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu sanjari na kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya Kanisa na ulimwengu. Katika Waraka huu, Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Roho Mtakatifu ni “Jicho la moyo” anayewapatia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, ujasiri wa kutaka mema na mabaya kwa majina yao halisi. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu aweze kuziamsha nyoyo na dhamiri nyofu za waamini kwa karama na mapaji yake saba, ili waamini waweze kujikita kikamilifu katika mapambano dhidi ya ukosefu wa haki, amani na maridhiano; aweze kusaidia kusitisha vita sehemu mbalimbali za dunia, vita inayoendelea kusababisha maafa na majanga makubwa katika maisha ya watu. Waamini wasichoke kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kulipyaisha Kanisa la Kristo Yesu.
