Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 13 Mei 2026 amekutana na kusalimiana na Wanawake Wakatoliki kutoka Tanzania waliohudhuria Katekesi yake. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 13 Mei 2026 amekutana na kusalimiana na Wanawake Wakatoliki kutoka Tanzania waliohudhuria Katekesi yake.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Akutana na Wanawake Wakatoliki Kutoka Tanzania

Kanisa linafanya kumbukizi ya Miaka 45 tangu Jaribio la kutaka Kumuua Mt. Yohane Paulo II lilipofanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tukio ambalo limekumbukwa na Papa Leo XIV wakati wa Katekesi yake na kuwazamisha mahujaji hata kutoka Tanzania, kuhusu: Bikira Maria na Kanisa kama mfano na kielelezo cha imani, upendo na umoja; aliyehifadhi muungano wake na Mwanaye mpendwa Kristo Yesu mpaka kufikia chini ya Msalaba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa tarehe 13 Mei ya kila mwaka anaadhimisha Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Fatima. Kwa mwaka 2026, Kanisa linafanya kumbukizi ya Miaka 45 tangu Jaribio la kutaka Kumuua Mtakatifu Yohane Paulo II lilipofanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tukio ambalo limekumbukwa na Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 13 Mei 2026 na kuwazamisha mahujaji hata kutoka Tanzania, kuhusu: Bikira Maria na Kanisa kama mfano na kielelezo cha imani, upendo na umoja; aliyehifadhi muungano wake na Mwanaye mpendwa Kristo Yesu mpaka kufikia kwenye Msalaba, akasimama imara. Baba Mtakatifu Leo XIV amepata nafasi ya kuzungumza, kuwapatia zawadi ya Rozari Takatifu pamoja na kupiga picha ya ukumbusho na mahujaji 49 kutoka Tanzania: Kati yao kuna Mapadre 3, Wanandoa 3 na wengine wote waliosalia ni Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women of Tanzania Association) ambacho ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika.” Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Papa Leo XIV akisalimiana na Mahujaji kutoka Tanzania
Papa Leo XIV akisalimiana na Mahujaji kutoka Tanzania   (@Vatican Media)

Bikira Maria aliyekingiwa dhambi ya asili, baada ya kumaliza mwendo wa maisha yake duniani, aliinuliwa katika utukufu wa mbinguni: mwili na roho; akatukuzwa kama Malkia. Kwa hakika Bikira Maria alishiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi ni Mama na Bikira: Ishara, tumaini thabiti na faraja kwa Taifa la Mungu linalosafiri huku bondeni kwenye machozi. Ilikuwa ni tarehe 13 Mei 1981, siku ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II alipouona mkono wa Bikira Maria katika maisha na utume wake, mwaliko kwa waamini kuendelea kujizatiti katika maisha ya sala, toba, wongofu wa ndani, msamaha na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa katika ulimwengu mamboleo ni Kanisa la mashuhuda ambalo linaendelea kujengwa kutokana na damu ya watoto wake inayomwagika sehemu mbalimbali za dunia. Kuna watu wanauwawa, wanayanyaswa na kudhulumiwa kutokana na chuki za kidini. Huu ndio ukweli uliokuwa umefumbatwa katika ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima, yaani Francis, Lucia na Yacinta. Ni Siri inayogusa matukio ya kihistoria, maisha na utume wa Kanisa. Hata leo hii, Kanisa linaendelea kujaribiwa, kwa baadhi ya watu kutaka kujenga hisia za chuki na uhasama dhidi ya Kanisa pamoja na kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo. Bikira Maria alipowatokea watoto wa Fatima, aliwapatia Siri kuu tatu ambazo zote zimekwisha fafanuliwa na viongozi wa Kanisa kwa nyakati tofauti. Ni siri ambazo zimejikita katika mwono wa vita, majanga asilia, kinzani na migawanyiko kati ya watu. Siri zote hizi ziliandikwa na Sr. Lucia. Siri ya tatu hakikuweza kufunuliwa kutokana na amri iliyotolewa na Askofu mahalia.

Papa Leo XIV akienda kuwasalimia mahujaji kutoka Tanzania
Papa Leo XIV akienda kuwasalimia mahujaji kutoka Tanzania   (@Vatican Media)

Mtakatifu Yohane Paulo II baada ya jaribio la kutaka kumuua kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican hapo tarehe 13 Mei 1981 aliamuru kwamba, siri ya tatu ifunuliwe na kuwekwa hadharani. Tafsiri ya siri hii ilitolewa kwa wakati huo na Kardinali Joseph Ratzinger, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na alisema kwamba, siri ya tatu ya Fatima ilikuwa ni mwaliko kwa Wakristo kusoma alama za nyakati na kutoa majibu muafaka kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo: kiroho na kimwili. Mtakatifu Yohane Paulo II anakiri kwamba, ni mkono na kinga ya Bikira Maria iliyomwezesha kusalimika katika jaribio la kutaka kumuua hapo tarehe 13 Mei 1981. Sala ni nguzo muhimu sana katika maisha dhidi ya wasi wasi wa kifo anasema Mtakatifu Yohane Paulo II.Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni mwamini hodari na shupavu katika maisha na utume wake. Taa ya imani ilikuwa ni dira na mwongozo wa maisha yake, hata pale alipoonekana yupo kwenye mahangaiko ya kuugua kwa muda mrefu, lakini bado aliendelea kuwa ni mtu mwenye amani, furaha na utulivu wa ndani. Ni mwamini ambaye alikuwa safarini kuelekea kwenye maisha na uzima wa milele. Hiyo ni changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiandaa kikamilifu ili kuweza kukabiliana na fumbo la kifo katika maisha yao. Ni mwaliko wa kuondokana na uchoyo na ubinafsi; kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hata baada ya jaribio la kutaka kumuua kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mnamo Mei 13 mwaka 1981, Mtakatifu Yohane Paulo II aliendelea na maisha na utume wake katika hali ya utulivu na amani ya ndani.

Mahujaji kutoka Tanzania wakisikiliza Katekesi ya Papa Leo XIV
Mahujaji kutoka Tanzania wakisikiliza Katekesi ya Papa Leo XIV

Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa na ibada ya pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kristo Yesu, kabla ya kukata roho, alipenda kuwakabidhi wanafunzi wake chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Ndiyo maana Mama huyu alikuwa na nafasi ya pekee sana katika maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II. Katika maisha kila mtu amekabidhiwa Msalaba wake, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Msalaba huu unakuwa ni chemchemi ya upendo na mwanga angavu wa maisha! Katika maisha na utume wake, aligusa medani mbalimbali za maisha ya binadamu; akaimarisha mafundisho msingi ya Kanisa yanayofumbatwa katika huruma ya Mungu, Roho Mtakatifu, Uhusiano kati ya imani na akili; Ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II, hata katika dakika zake za mwisho katika udhaifu wa mwili na magonjwa, aliendelea kuwa ni: Shuhuda, Nabii na Chombo cha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Akafanikiwa kuonesha ukuu, utakatifu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mahujaji wa Tanzania
13 Mei 2026, 17:09