Papa Leo XIV: Changamoto ya Matumizi ya Teknolojia ya Akili Unde Maishani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2026 yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kuhifadhi Sauti na Nyuso za Binadamu.” Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia mintarafu matumizi ya teknolojia ya akili unde “Artificial Intelligence” anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika kukuza na kudumisha mawasiliano yanayoheshimu, kulinda na kudumisha: Utu, heshima, haki msingi za binadamu na ukweli ambao kimsingi ni kanuni elekezi ya kila uvumbuzi wa kiteknolojia unaofanywa na mwanadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuhakikisha kwamba, uvumbuzi wa teknolojia, hasa matumizi ya teknolojia ya akili unde, inamhudumia binadamu badala ya kuchukua nafasi au kupunguza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake anasema, nyuso na sauti za binadamu ni za kipekee, sifa bainifu za kila mtu; zinafichua utambulisho wa mtu mwenyewe usioweza kurudiwa na ni vipengele vinavyobainisha vya kila kukutana na wengine. Waraka wa kwanza wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” utazinduliwa rasmi tarehe 25 Mei 2026 kwenye Ukumbi wa Sinodi ya Maaskofu, kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Leo XIV na hitimisho litatolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu, Alhamisi tarehe 21 Mei 2026 limeadhimisha Kongamano la Kimataifa ambalo limenogeshwa na kauli mbiu:“Kuhifadhi Sauti na Nyuso za Binadamu” fursa kwa washiriki wa Kongamano hili kushirikisha karama na mapaji waliokirimiwa na Roho Mtakatifu sanjari na kuweza kuhifadhi akili zao dhidi ya athari za matumizi makubwa ya teknolojia ya akili unde; kuhifadhi ndani mwao namna ya kuchagua yale mema na kuyaendeleza na mabaya kuachana nayo; kutambua ukweli na kukwepa ulaghai na jinsi ya kuweza kuwasiliana na wengine katika ulimwengu mamboleo. Huu kwa hakika ni mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa.
Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu anasema Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii, kujikita katika kuhifadhi tunu msingi za kijamii kama vile: Ukweli na uwazi; Uwajibikaji wa kijamii na kwamba, wadau wa tasnia ya mawasiliano wanawajibika kikamilifu kulinda utambulisho wao sanjari na mabadiliko yanayoendelea kuletwa na matumizi makubwa ya teknolojia ya akili unde. Mawasiliano ya jamii hayana budi kusimikwa katika uhuru wa mawazo, uwajibikaji wa kijamii; uhuru wa kupanga na kuchagua; kiu na kuwa na jamii ambayo inasimikwa katika ukweli, uwazi sanjari na hifadhi ya kumbukumbu hai, kwamba, wao ni nani katika Ulimwengu mamboleo! Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii yamefungua fursa kubwa ya mawasiliano, kwa kuwawezesha watu kuwasiliana kwa ufasaha zaidi; watu kufahamu mambo kwa kina na mapana pamoja na kujenga ujirani mwema; lakini kwa bahati mbaya haya ni mambo yanaweza kubadilisha mihimili msingi ya ustaarabu wa mwanadamu kiasi cha kugusa na kutikisa undani wa maisha ya mtu; uhusiano wake na jirani zake na matokeo yake ni ukosefu wa usawa sanjari na kuibuka kwa ukosefu wa haki jamii anasema Kardinali José Tolentino Calaça de Mendonça Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu. Kumbe changamoto katika maendeleo ya teknolojia ya matumizi ya akili unde si kuzuia na kuweka vikwazo, bali ni kujenga ufahamu wa matumizi sahihi; kulinda, kudumisha na kuhifadhi sauti na sura za binadamu halisi, kwa kutoa nafasi ya mtu kuweza kufikiri kikamilifu. Ni katika muktadha huu, Taasisi za Elimu ya Juu pamoja na Vyuo Vikukuu vya Kikatoliki vinapaswa kuwa ni mahali pa kuchukua maamuzi ya ujasiri kwa kufanya tafiti makini, ili kuongoza maendeleo makubwa ya teknolojia, ili yaweze kuwa ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kamwe yasimfanye mwanadamu kuwa ni mtumwa wa mabadiliko ya teknolojia, bali teknolojia iwe ni kwa ajili ya huduma ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Kongamano la Kimataifa ambalo limenogeshwa na kauli mbiu: “Kuhifadhi Sauti na Nyuso za Binadamu.”
Baba Mtakatifu Leo XIV Ijumaa tarehe 22 Mei 2026 amekutana na kuzungumza na washiriki wa Kongamano hili. Katika hotuba yake amekazia zaidi kuhusu: Wasomi, wataalam na wabobezi katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kidijitali, waliofika mjini Roma ili kutafakari kwa kina na mapana juu ya vyombo vya upashanaji habari na ujuzi wa kidijitali sanjari na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, mambo muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa katika Ulimwengu mamboleo. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati yao” Inter mirifica” Yaani “Kati ya Mambo ya Ajabu ya Kiteknolojia ambayo akili ya mwanadamu, ikiongozwa na Mungu, imevumbua kutoka kwa vitu vilivyoumbwa ni vyombo vya upashanaji habari. Mtaguso wa Pili wa Vatican ndio ulioanzisha Maadhimisho ya Siku ya Upashanaji Ulimwenguni na kwamba, Kanisa ambalo ni Sakramenti ya Wokovu linasukumwa na wajibu wa kutangaza na kuhubiri Habari Njema ya Wokovu: “Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.” Yn 17:3. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema watu wana kiu ya kuufahamu ukweli, ili wapate kuokoka. Huu ni mwaliko kwa wataalam na mabingwa wa matumizi ya teknolojia, na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya kidigitali sanjari na matumizi ya sayansi ya akili unde kuhakikisha kwamba, yote haya yanakuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu kwa kulinda na kutunza utu na heshima yake. Lakini kwa bahati mbaya, maendeleo haya makubwa ya sayansi na teknolojia yamekuwa yakimong’onyoa utu, heshima na haki msingi za binadamu na hivyo kuathiri mahusiano na mafungamano thabiti ya binadamu, changamoto kubwa ni kwa watu wa Mataifa kuona na kutambua ukuu wa mwanadamu, wenye chapa ya sura ya Mungu na wanadamu.
Waraka wa kwanza wa Kitume wa Papa Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Ubinadamu wa ajabu" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” unazinduliwa rasmi Jumatatu tarehe 25 Mei 2026 Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa ili awe ni faraja na matumaini kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wanahimizwa kufanya hija ya maisha ya kiroho pamoja na Bikira Maria, aliyethubutu kumfuasa Kristo Yesu katika Njia ya Msalaba, ili kuambata huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Maria ni Bikira na Mama kwa sababu yeye ni ishara na utimilifu kamili wa Kanisa. Kanisa kwa kupokea Neno la Mungu kiaminifu linakuwa pia ni Mama na Mwalimu kwani kwa mahubiri na ubatizo linazaa watoto waliotungwa na Roho Mtakatifu na kuzaliwa na Mungu kwa uzima mpya usiokufa.Baba Mtakatifu Leo XIV anasema ni katika mwanga wa kumtafakari Kristo Yesu, Neno aliyefanyika mwili, ndipo mwanadamu anaweza kuufahamu ukweli wa ubinadamu ulivyo na kumjulisha wito wake mkuu, thamani na hadhi yake kuu, ndiyo maana kwa sababu hii, uhifadhi wa kweli wa uso na sauti ya kila mtu ni lazima uhusishe kukutana naye ambaye ni “mfano wa Mungu asiyeonekana,” na wakati huohuo yeye mwenyewe akiwa mtu mkamilifu (Kol 1:15.) Kwa kawaida, haya yote lazima yazingatiwe wakati wa kujadili athari za teknolojia ya kidijitali na dhamana na jukumu la Kanisa katika matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii na kwamba, jukumu hili si rahisi, lakini Kanisa linaitwa na kutumwa kuwaletea binadamu nuru ya Kristo Yesu ulimwenguni mintarafu shughuli za wanadamu. Rej. Yn 8:12; Mt 5:14-16. Matokeo yake, Kanisa linajikuta likilazimika kuchangia katika juhudi za kupanga na kutekeleza vyombo vya upashanaji habari, na ujuzi wa kusoma na kuandika wa teknolojia ya akili unde ndani ya mifumo ya elimu, lengo maalum likiwa ni watu kupata ujuzi wa kufikiri kwa kina na kwamba, teknolojia inachangia kwa kiasi kikubwa wokovu wa wale wanaoitumia.
Baba Mtakatifu Leo XIV anataadharisha kuhusu athari za matumizi ya teknolojia ya kidigitali na akili unde kwa kukazia wajibu wa watoto, vijana, wazazi na walezi kwa kujizoesha kutumia kwa kiasi na kwa nidhamu vyombo vya upashanaji habari, wakiwa na lengo lakufahamu sawasawa kila wakionacho, wakisikiacho na kile wanachosoma. Haya ni mambo wanayopaswa kujadili pamoja na walezi na wataalam wa mambo haya. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, kwa kuzingatia dhamana na utume wa Kanisa katika Ulimwengu mamboleo sanjari na imani potofu za sasa kuhusu Mungu na mwanadamu, ujuzi na maarifa ya kidijitali lazima ujumuishe elimu katika ukweli kuhusu Mungu na ubinadamu. Vijana wasaidiwe kugundua maana ya maisha, waelimishwe namna bora zaidi ya kukutana na Kristo Yesu aliye hai sanjari na kuwafundisha kujumuisha matumizi ya teknolojia katika mtindo wa maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu Leo XIV anakiri kwamba, maendeleo na matumizi ya teknolojia ya akili unde ni kati ya vipaumbele katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na kipaumbele cha Mama Kanisa kwa sasa. Hakika, kama Mama na Mwalimu, Kanisa linapendezwa na maisha adili na matakatifu ya watoto wake, likitamani kuwaongoza kwenye ukomavu kamili. Rej Ef 4:13. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, tafakari hizi zitaleta imani inayopyaishwa katika teknolojia kama tunda la fikra za mwanadamu mintarafu mpango wa kazi ya uumbaji kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwishoni, amewapatia baraka zake za kitume, furaha na amani ya kweli.
