Jumatatu tarehe 18 Mei 2026 amekutana, amezungumza na kusali pamoja na Mheshimiwa Sana Aram I wa Wakatoliki wa Kanisa la Kitume la Armenia. Akiwa mjini Roma, Mheshimiwa Sana Aram 1 Jumatatu tarehe 18 Mei 2026 amekutana, amezungumza na kusali pamoja na Mheshimiwa Sana Aram I wa Wakatoliki wa Kanisa la Kitume la Armenia. Akiwa mjini Roma, Mheshimiwa Sana Aram 1   (ANSA)

Papa Leo XIV: Kumbukizi ya Mwaka Mmoja Tangu Aanze Utume Wake!

Umegota Mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Leo XIV alipoanza utume wake wa kuongoza, kufundisha na kutakatifuza watu wa Mungu, Jumatatu tarehe 18 Mei 2026 amekutana, amezungumza na kusali pamoja na Mheshimiwa Sana Aram I wa Wakatoliki wa Kanisa la Kitume la Armenia. Akiwa mjini Roma, Mheshimiwa Sana Aram 1 Jumanne tarehe 19 Mei 2026 anatembelea Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki na hapa anategemewa kutoa mhadhara kuhusu changamoto zinazo yakabili Makanisa katika Ulimwengu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV aliuanza utume wake Dominika tarehe 18 Mei 2025 kama Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 267 na Askofu wa Roma. Katika mahubiri yake aligusia kifo cha Papa Francisko; Umoja na Mshikamano wa Baraza la Makardinali pamoja na sala za waamini; Ujenzi wa Kanisa linalosimikwa katika upendo wa Mungu; Kwa kukuza na kudumisha: Umoja na mshikamano wa Kanisa, chachu ya upatanisho, tayari kujikita katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Baba Mtakatifu Leo XIV alitambua uwepo wa umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliofika kushuhudia alipokuwa anauanza utume wake rasmi kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa kifo cha Papa Francisko, waamini waligubikwa na huzuni na majonzi makubwa, wakawa kama kondoo wasio na mchungaji. Rej. Mt 9:36. Waamini wakajikita zaidi katika imani kwa Kristo Mfufuka kwa kutambua kwamba, kamwe Kristo hawezi kuwaacha kondoo wake wapotee, atawakusanya, na kuwalinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake.Rej. Yer 31:10. Ni katika roho ya Pasaka, Baraza la Makardinali lilikutanika kufanya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu, Askofu wa Roma, Mchungaji mwenye uwezo wa kulinda na kudumisha amana na utajiri wa imani ya Kikristo, akiwa na mwelekeo mpana zaidi, ili kuweza kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali katika ulimwengu mamboleo. Makardinali wakasindikizwa na Sala za waamini, wakashirikiana na kushikamana na matokeo yake wakampata Papa Leo XIV anayekuja mbele ya Kanisa kama ndugu anayetaka kujisadaka katika huduma ya imani, ili aweze kuwa kweli ni chemchemi ya furaha, huku wakitembea kwa pamoja katika njia ya upendo wa Mungu, anayetaka watu wote wawe wamoja kama familia moja.

Baraza la Makardinali ni Chombo Cha Ushauri kwa Papa
Baraza la Makardinali ni Chombo Cha Ushauri kwa Papa   (@Vatican Media)

Dhamana na utume wa Baba Mtakatifu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na Askofu mkuu wa Roma ni kuwa ni msingi wa umoja na mchungaji mkuu wa Kanisa la Kiulimwengu. Ametwikwa mamlaka ya kulinda imani, kuhimiza mshikamano wa udugu wa kibinadamu, na kuongoza utume wa Kanisa ulimwenguni kote. Utume na dhamana hii ya kiulimwengu inajumuisha mambo makuu yafuatayo: Mhimili wa Umoja: Yeye ndiye mwamba na ishara inayoonekana ya umoja wa Kanisa lote. Anahakikisha ushirika kati ya Makanisa yote mahalia sehemu mbalimbali za dunia na anafanya kazi ya kuunganisha waamini katika umoja na utofauti zao. Ni Kiongozi wa Mafundisho, Maadili na Utu wema. Kama Mwalimu mkuu wa Kanisa, anawajibika kulinda na kufundisha ukweli wa Injili, akitoa mwongozo thabiti wa kiroho, kimaadili na utu wema. Ni Mlinzi wa Haki na Amani: Katika maisha ya Kanisa la Kiulimwengu, Baba Mtakatifu anasisitiza umuhimu wa huduma ya upendo na utetezi wa haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Ni Mkuu wa utume na maisha ya Kanisa lote ambalo lina wajibu wa kimisionari wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu hadi miisho ya dunia. Ni katika muktadha wa kumbukizi ya Mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Leo XIV alipoanza utume wake wa kuongoza, kufundisha na kutakatifuza watu wa Mungu, Jumatatu tarehe 18 Mei 2026 amekutana, amezungumza na kusali pamoja na Mheshimiwa Sana Aram I wa Wakatoliki wa Kanisa la Kitume la Armenia. Akiwa mjini Roma, Mheshimiwa Sana Aram 1 Jumanne tarehe 19 Mei 2026 anatembelea Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki na hapa anategemewa kutoa mhadhara kuhusu changamoto zinazo yakabili Makanisa katika Ulimwengu mambo leo. Hii ni fursa pia ya kutembelea Taasisi na Mabaraza mbalimbai ya Kipapa.

Rais Sergio Mattarella wa Italia amempongeza Papa Leo XIV
Rais Sergio Mattarella wa Italia amempongeza Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Rais Sergio Mattarella wa Italia, kama sehemu ya kumbukizi ya mwaka mmoja tangu Baba Mtakatifu Leo XIV aanze utume wake, amemwandikia ujumbe heri na matashi mema, huko akimpongeza kwa Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” yanayotoa mwaliko wa kusimama kidete kutafuta na kudumisha haki, kwa kuondokana na uchoyo pamoja na ubinafsi; kwa kujiepusha na kinzani migogoro na vita, ili haki, amani na majadiliano yaweze kushika kasi, ili hatimaye, kuepuka majanga pamoja na athari kubwa za vita. Hija yake ya kwanza ya Kitume Barani Afrika, imeonesha umuhimu wa viongozi wa Kanisa kuwa karibu na watu wao; umuhimu wa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, haki, amani, utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza. Mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni muhimu sana katika kupambana na umaskini wa maisha ya kiroho na kimwili. Hatimaye, Rais Sergio Mattarela amemshukuru Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kuonesha ukaribu kwa watu wa Mungu nchini Italia na kwamba anamtakia heri na baraka katika hija zake za kichungaji nchini Italia.

Rais Sergio alipotembelea Vatican
Rais Sergio alipotembelea Vatican   (@Vatican Media)

Mama Kanisa katika maisha na utume wake anakazia kuhusu: Uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma. Anasema uekumene wa damu na ule wa utakatifu wa maisha ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo sehemu mbalimbali za dunia katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni Ufalme wa ukweli na uzima, ufalme wa haki na amani, ufalme wa mapendo na ni ufalme ambao Mwenyezi Mungu anatawala katika mioyo ya watu wake sanjari na ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu ya Ukristo. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume.

Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa
Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake, amekazia kuhusu: Ushirika wa maisha ya kiroho kati ya Makanisa na hasa Kanisa la Cilicia, mahali alipozaliwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa; Kanisa la Roma, mahali alipomshuhudia Kristo Yesu kwa kuyamimina maisha yake na kwamba, kuna idadi kubwa ya watakatifu na mashuhuda wa imani, ambao wameandikwa kwenye Kitabu cha Orodha ya Majina ya Wafiadini wa Kirumi “Roman Martyrology”: Martirologio Romano.” Huu ni ushuhuda wa umoja wa watakatifu wa Kanisa, kiini cha umoja wa Kanisa. Umoja huu ulikuwa na nguvu katika Kipindi cha Kati cha Maisha ya Kanisa “Middle Ages” na maendeleo mapya yakaibuka katika Karne ya 20 na hasa wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Itakumbukwa kwamba, Mheshimiwa sana Khoren wa Kwanza wa Makanisa ya Mashariki ndiye aliyekuwa Kiongozi mkuu wa kwanza kutoka Mashariki kutembelea Roma kunako mwaka 1967 na kwamba, Mheshimiwa Sana Aram I wa Wakatoliki wa Kanisa la Kitume la Armenia anaendelea kutangaza na kushuhudia mwamko huu wa majadiliano ya kiekumene na katika medani za Kimataifa, kwa ushiriki wake kwenye Baraza la Makanisa Ulimwenguni, ambako amewahi kushikilia nafasi za uongozi wa juu. Katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene, viongozi wakuu Wakatoliki wa Kanisa la Kitume la Armenia walitembelea Roma, mwezi Januari 1997 wakati wa Maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo.

Umoja wa Imani ni msingi wa Umoja wa Kanisa
Umoja wa Imani ni msingi wa Umoja wa Kanisa   (@Vatican Media)

Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki iliundwa kunako mwaka 2003 na tangu wakati huo kuna nyaraka kadhaa ambazo zimetolewa kuhusu: Asili na Utume wa Kanisa; Ushirika katika Kanisa la Mwanzo na kuhusu Sakramenti za Kanisa. Licha ya magumu na changamoto ambazo zimejitokeza hivi karibuni, lakini ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, majadiliano ya kiekumene yatasonga mbele, kwani umoja katika imani ndiyo nguzo ya umoja wa Kanisa.Baba Mtakatifu amekumbusha hija yake ya Kitume alipotembelea Lebanon, Mwezi Desemba 2025, hapa ni mahali ambapo watu wa tamaduni na dini mbalimbali wanaweza kuishi kwa umoja, changamoto na mwaliko kwa Makanisa kuonesha mshikamano huu pamoja na waamini wa dini mbalimbali na kwamba, anapenda kumhakikishia sala na sadaka yake ya daima. Mama Kanisa katika kipindi hiki anajiandaa kuadhimisha Sherehe ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Mwanzo. Baba Mtakatifu baada ya hotuba hii, wamesali pamoja ili kuombea umoja, amani ya kudumu na upyaisho wa sura ya dunia.

Majadiliano ya Kiekumene

 

18 Mei 2026, 14:47