Papa Leo XIV Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Ushirika!

Neema ya Bwana wetu Kristo Yesu, na pendo la Mungu na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote! Baada ya Sherehe ya Pentekoste, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Utatu Mtakatifu, msingi wa Mafumbo yote yanayosherehekewa na Kanisa. Hili ni Fumbo la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake Mwenyewe. Mwenyezi Mungu katika historia na Mpango wa ukombozi amejifunua kuwa ni Mungu mmoja katika Nafsi Tatu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Neema ya Bwana wetu Kristo Yesu, na pendo la Mungu na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote! Baada ya Sherehe ya Pentekoste, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, msingi wa Mafumbo yote yanayosherehekewa na Kanisa kwa nyakati mbalimbali. Hili ni Fumbo la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake Mwenyewe. Mwenyezi Mungu katika historia na Mpango wa ukombozi amejifunua kuwa ni Mungu mmoja katika Nafsi Tatu. Baba Mungu Mwenyezi Mwumba mbingu na nchi, na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Kanisa linasadiki kwa Kristo Yesu, Mwana wa pekee, wa Mungu aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Ni Mungu aliyetoka kwa Mungu, Mwanga kwa mwanga. Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, Mwenye umungu mmoja na Baba. Ndiye aliyeshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kanisa linasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana na mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa na Baba na Mwana: Aliyenena kwa vinywa vya Manabii.

Fumbo la Utatu Mtakatifu
Fumbo la Utatu Mtakatifu

Mababa wa Kanisa wanasema, Mwenyezi Mungu amejifunua jina lake linaloelezea: Uwapo, Umoja wa Nafsi, na Maana ya maisha yake na kwamba, jina lake ni kielelezo cha nguvu. Mungu amejifunua jina lake, amejijulisha na kujionesha ili aweze kukaribiwa, kujulikana na kutajwa kwa Nafsi yake. Fumbo la Utatu Mtakatifu ni msingi wa imani na maisha ya Kikristo. Fumbo la Umwilisho linafunua kwamba, Mungu ni Baba wa milele, na Mwana ni uwamo wa pamoja na Baba, yaani ndani yake, na pamoja Naye, ni Mungu mmoja tu. Roho Mtakatifu anatumwa na Baba na Mwana ni uwamo wa pamoja, anaabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana. Kwa neema ya Ubatizo, waamini wanaitwa kushiriki Uzima wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, hapa duniani katika giza la imani, na baada ya kifo katika Mwanga wa milele.  Mababa wa Kanisa wanasema, Imani Katoliki mintarafu Fumbo la Utatu Mtakatifu ndiyo hii: “Tunamwabudu Mungu Mmoja katika Utatu na Utatu katika Umoja, bila kugawanyika nafsi, wala kutenganisha uwamo; kwani ni Nafsi ya Baba, ya Mwana na Roho Mtakatifu. Ni umungu mmoja wa Baba, na wa Mwana na wa Roho Mtakatifu, utukufu ulio sawa, ukuu wa pamoja wa milele.” KKK 266.

Tunamwabudu Mungu Mmoja Katika Utatu
Tunamwabudu Mungu Mmoja Katika Utatu

Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Dominika 31 Mei 2026, amesema, Mama Kanisa anawakirimia watoto wake fursa ya kutafakari tena safari ya maisha yao ya kiroho; maisha yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Maisha haya ni ushirika wenye nguvu na wa milele yote na ni ushirika wenye kuzaa matunda kwa kumshirikisha Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba aliyemimininwa ndani ya waamini, ili kwa njia hii, Kanisa Ulimwenguni lichukue sura ya Sakramenti ya ushirika; fursa ya waamini kukutana; kielelezo cha upendo na maisha ambayo yanagusa mbingu na dunia. Baba Mtakatifu Leo XIV anaendelea kusema: Injili ya Liturujia, Sherehe ya Utatu Mtakatifu Mwaka A wa Kanisa: Yn 3:16-18, inamtambulisha Nikodemo, mtu mashuhuri sana katika Israeli ambaye katika maisha yake, alivutwa sana na Kristo Yesu. Alikwenda kumtembelea usiku ili asionekane na watu, ili kuzima shauku yake ya ndani ya kutaka kumfahamu vyema Mwalimu huyu wa ajabu, na hatimaye, kupata fursa ya kumuuliza maswali. Kwaa kumkaribisha Kristo Yesu katika maisha yake, alitoa mwanya wa pekee katika mchakato wa utafutaji wake, alimshangaa kwa kudokeza kwamba, hata mtu mzima anaweza kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu na kwamba, huu ni mwanga ambao huleta mabadiliko makubwa katika maisha. Kristo Yesu anazungumza na Nikodemu kuhusu Roho Mtakatifu kiasi cha kumwangazia usiku ule kuhusu ukweli ambao Mama Kanisa kwa Sherehe ya Utatu Mtakatifu, unasikika kwenye Makanisa yote: “Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.” Yn 3: 17.

Nafsi tatu Katika Mungu Mmoja!
Nafsi tatu Katika Mungu Mmoja!   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika Fumbo la Utatu Mtakatifu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu, waamini wanajisikia wako nyumbani kabisa pamoja na Kristo Yesu, kwani maisha ya Mungu ni ya ajabu kabisa, yanavutia pamoja na kuleta amani katika nyoyo za watu ambazo kwa kweli haziwezi kutulia na hatimaye, huwaleta pamoja kama ndugu katika furaha ya Roho Mtakatifu. Fumbo la Utatu Mtakatifu huwasukuma waamini kuwapenda wote na kugundua kwamba, kila kiumbe ni kwa ajili ya kujenga ushirika, husiano sanjari na kutoa fursa ya watu kukutana. Na kwa kulinganisha waamini wanaelewa kwanini kuna migawanyiko na vita na kwamba, dharau na kutozingatia utafiti wa kina, ni mambo yanayoweza kuleta ubadhirifu, huzun na ubaridi ulmwenguni. Nikodemo alikuwa mjumbe wa Sanhedrini, yaani Baraza la viongozi wa Israeli. Na aliposikilia maneno ya dharau na kejeli kutoka katika Sanhedrin aliwaalika kumsikiliza kwanza kabla ya kumhukumu. Nikodemo alikuwa amepokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa njia ya Kristo Yesu, Roho wa ushirika, ambayo inafungua moyo kwa ukweli mpya na upya wa kweli. Wale wasiomkaribisha Roho Mtakatifu wanazeeka haraka katika majungu; na katika upweke na hawaweze kamwe kuwa katika roho ya Sherehe. Leo ni Sherehe kubwa na ndiyo maana Mtakatifu Paulo anawaandikia  Wakorintho akisema: “Hatimaye, ndugu, kwaherini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.”  2 Kor 13:11. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumgeukia Bikira Maria, aliyekubali kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake anawasaidie hata waamini “Ndiyo” yao isaidie kuchipusha upendo kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Papa Leo XIV Utatu Mtakatifu 2026
31 Mei 2026, 15:06

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >