Papa Leo XIV:Tunawezaje kulinda zawadi ya Bwana aliyokabidhi Kanisa lake?
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kabla ya kutoa tafakari ya mwisho katika Mkutano Mkuu Maalum wa Makardinali kutoka ulimwenguni kote uliofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 26 hadi 27 Juni 2026 mjini Vatican, Baba Mtakatifu Leo XIV alionesha ukaribu wake, pamoja na Baraza zima la Makardinali na kuwakumbuka watu wa Venezuela, walioathiriwa: "Tunawahakikishia maombi yetu kwa ajili ya waathiriwa, familia zao, na wote wanaoteseka kutokana na matokeo ya janga hili. Pia tunawakabidhi kwa Bwana wale wote wanaohusika katika shughuli za uokoaji, na tunaomba kwamba mshikamano wa jumuiya ya kimataifa kuelekea taifa hilo pendwa usipungue," Papa aliongeza.
Kutafuta mapenzi ya Mungu
Kutoka Ukumbi Mpya wa Sinodi Jumamosi tarehe 27 Juni 2026 jioni, Baba Mtakatifu Leo XIV alitoa hotuba yake ndefu ambapo alianza kusema kwamba: “Sasa tunafikia mwisho wa siku hizi tukiwa na hisia kubwa ya shukrani. Ninawashukuru kwa uhuru, udugu, na roho ya Kanisa ambayo mlishiriki nayo katika kazi yetu. Ninabeba sio tu maudhui ya tafakari zenu, bali pia uzoefu mliowezesha.
Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa: “Tumetafuta pamoja mapenzi ya Bwana, tukiwa na uhakika kwamba Kristo anaendelea kutenda katika Kanisa lake: ni Yeye anayetutangulia, anatukusanya, anazungumza kupitia ndugu zetu, na anatuongoza katika utume. Kila kitu hutoka kwake na kila kitu kinamrudia. Kwa sababu hiyo, alisema kwamba kuwaona Makardinali kutoka Makanisa, tamaduni, na hali mbalimbali wakisikilizana na kutafuta pamoja kile kinachofaa zaidi Injili kumekuwa chanzo cha faraja na matumaini kwangu.”
Kukuza uelewa halisi wa Sinodi
Katika kiini cha tafakari yake, Papa Leo XIV alisisitiza kwamba Sinodi haipaswi kueleweka kama njia ya shirika au mfuatano wa mikutano, bali kama njia ya kuwa Kanisa. Swali halisi la sinodi si nani aliye na mamlaka ya kuamua, bali tunawezaje kulinda pamoja zawadi ambayo Bwana ameikabidhi Kanisa lake? Kulingana na Papa, safari hii huzaliwa kutokana na kukutana, hukua kupitia kusikilizana kwa pamoja, na kukomaa kupitia utambuzi unaoongozwa na Roho Mtakatifu. Kwa hivyo aliwaomba makardinali kukuza utekelezaji wa mchakato wa sinodi katika Makanisa yao maalum, na kukuza uelewa halisi wa hilo.
Makardinali walishirikisha wasi wasi kuhusu vita,umaskini na dhuluma
Papa Leo XIV pia alibainisha kuwa wakati wa Mkutano Mkuu, Makardinali walishirikisha wasiwasi wao kuhusu vita, umaskini, dhuluma, na vurugu zinazowaathiri watu wengi ulimwenguni kote. Hata hivyo, alisema kwamba nyuma ya mikasa hii kuna mgogoro mkubwa zaidi: upweke, mgogoro wa mahusiano, kupoteza matumaini, na ugumu wa kutambuana kama kaka na dada. Papa aliakisi hasa hali ya vijana, ambao utafutaji wao wa maana na uhalisi na, katika baadhi ya matukio, mateso ambayo hata husababisha kujiua, yanawakilisha moja ya majeraha makubwa zaidi ya wakati wetu." Pia alisisitiza umuhimu wa familia kama shule ya mahusiano, mshikamano, na matumaini. Katika muktadha huu, alitangaza mkutano mnamo Oktoba na viongozi wa Makanisa ya Mashariki na marais wa Mabaraza ya maaskofu ili kutathmini mapokezi ya Waraka wa Amoris Laetitia, ambapo familia pia zitashiriki.
Kifungu cha amani
Kifungu kimoja katika mkutano kilijikita juu ya amani. Ndani yake, Papa Leo XIV alisema kwamba Makardinali walielewa wazi moja ya ufahamu wa waraka wa Waraka wa Magnifica humanitas kuwa: Vita havitokani na migogoro kati ya nchi tu, bali pia na utamaduni wa madaraka unaoenea katika mahusiano ya kibinadamu, uchumi, siasa, teknolojia, na hata dini. Katika kujibu, alipendekeza kujenga upya utamaduni wa ushirikiano na mazungumzo, kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi, na kukuza ushiriki wa watu wa kawaida katika maisha ya umma yaliyoongozwa na mafundisho jamii ya Kanisa.
Papa Leo XIV pia alitetea majibu yasiyo ya vurugu kama chaguo la kiinjili lenye kina, akifafanua kwamba haimaanishi kutojali, bali kukabiliana na migogoro bila kuiga mantiki ya chuki. Katika muktadha huo, alifichua kwamba vikundi kadhaa vya kazi vilikuwa vimeomba tafakari ya kina ya kitaalimungu na kichungaji kuhusu ulinzi halali kutokana na mabadiliko yanayoathiri migogoro ya kisasa. Papa Leo alisisitiza kwamba ufufuko wa Kanisa hautegemei mageuzi ya kimuundo tu, bali zaidi ya yote ushuhuda wa jamii zinazoweza kuishi Injili kwa uaminifu. Kanisa limeitwa kuwa kikamilifu zaidi kwa kile anachotangaza, alibainisha Papap huku akisisitiza kwamba mageuzi yote ya kitaasisi yatazaa matunda ikiwa tu yatatokana na kukutana na Kristo na maisha ya kisakramenti. Baba Mtakatifu Leo XIV pia alisisitiza nia yake ya kuendelea na mkutano huo wa kila mwaka kuanzia mwaka ujao. Papa alifafanua kwamba tarehe bado haijapangwa, lakini anatumaini kuitangaza ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Tuna Jukumu la kutembea kwa ujasiri
Mwishoni mwa hotuba yake, Papa Leo XIV alikubali kikamilifu wito wa pamoja uliotoka katika Mkutano Mkuu huo na kuwaalika Makardinali kuupitisha kwa makanisa na watu wote wa dunia.“Mungu anaendelea kufungua njia za upatanisho na amani katika historia. Tuna jukumu la kutembea kwa ujasiri na kusaidia ulimwengu kuzitambua," alisema. Pia aliwashukuru wote kwa mchango wao, pamoja na Waratatibu, Wasimamizi, na wale wote ambao, kwa ukarimu na busara, walifanya siku hizi za kazi na udugu ziwezekane. “Asante kwa kunisaidia, tena, kutambua kazi ambayo Kristo anaendelea kuitimiza miongoni mwa watu wake na duniani. Tunakabidhi matunda ya Mkutano Mkuu huu kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Atufundishe kuhifadhi umoja katika utofauti na kutumikia Injili ya amani kwa unyenyekevu, ujasiri, na matumaini. Asante! Papa alihitimisha.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here.
