Papa Leo XIV Akutana na Kusalimiana Na Wanawake Wakatoliki Tanzania Kundi la Pili
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV baada ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, anaendeleza Mzunguko wa Katekesi unaojikita katika Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Usomaji Mpya wa Nyaraka zake, ili kugundua tena uzuri na umuhimu wa tukio hili la Kikanisa, Kipindi cha neema ambacho kwa hakika, Mama Kanisa amekifaidi sana katika Karne ya ishirini. Kumbe, hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.” Katiba ya “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia” inaelezea kanuni za jumla za marekebisho na ukuzaji wa Liturujia Takatifu; Fumbo Takatifu la Ekaristi, Sakramenti nyingine na visakramenti; Liturujia ya Vipindi; Mwaka wa Liturujia wa Kanisa, Muziki Mtakatifu; na hatimaye, ni Sanaa Takatifu na Vifaa vitakatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanafafanua nafasi ya Liturujia katika fumbo la Kanisa kwa kusema kwamba, maana kwa njia ya Liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi wetu.” Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waoneshe katika maisha yao na kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo Yesu na pia maumbile halisi ya Kanisa la kweli. Kanisa kwa undani kabisa ni la kibinadamu na pia la kimungu, linaloonekana lakini lenye mambo yasiyoonekana ndani yake, lenye bidii kubwa katika matendo na uradhi katika kutafakari, lililopo ulimwenguni lakini kama mwenye kufanya hija. Hayo yote yamo ili yale ya kibinadamu ndani yake yaelekezwe kwa yale ya kimungu, yaonekanayo kwa yasiyoonekana, matendo kwenye kutafakari, yaliyopo yaelekee mji ujao tunakoelekea.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika Katekesi yake, Jumatano tarehe 24 Juni 2026, Sherehe ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Mbatizaji alikita mafundisho yake juu ya umuhimu wa Liturujia: Fumbo la Ekaristi Takatifu ni sadaka ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni karamu ya Bwana, kusanyiko la Kiekaristi, ukumbusho wa mateso kifo na ufufuko wa Bwana, Sadaka Takatifu ya Misa. Ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo, na ni karamu ya Pasaka. Ekaristi ni kitovu na kilele cha maisha ya Kanisa, kwa kuwa kwayo Kristo anachagamana na Kanisa lake na waamini wake wote! Katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, waamini wanaitwa na kualikwa kusikiliza Liturujia ya Neno la Mungu, kulishwa katika meza ya Bwana na kwamba, Liturujia ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu zimeunganika sana kati yake kiasi kwamba zinafanya ibada moja tu. Katekesi hii ya Baba Mtakatifu Leo XIV kuhusu Liturujia, imehudhuriwa na Kundi la Pili la Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women of Tanzania Association) ambacho ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika.”
Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Kundi hili la Pili linaundwa na wanawake 41 kutoka Tanzania chini ya uongozi wa Padre Alister Makubi, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Kichungaji Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. WAWATA kwa pamoja wameshuhudia mbele ya Baba Mtakatifu Leo XIV dhamana na mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Tanzania, katika mchakato wa kulitegemeza Kanisa, katika Malezi na Majiundo makini ya Makleri; katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili ya familia, uhai na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya ili wasitumbukie katika nyanyaso na ndoa za utotoni pamoja na kudumisha uhuru wa kuabudu ambao ni msingi wa umoja, udugu, haki na amani.
Kundi hili la Pili na WAWATA kutoka Tanzania, kuanzia tarehe 18 hadi 28 Juni 2026 linatembelea: Ufaransa, Hispania, Ureno na Italia. Hii ni fursa makini kupyaisha na kuimarisha imani, matumaini na mapendo yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kwa kukaza macho yao ya imani juu ya Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani, anayepanua mikono yake, tayari kuwapokea na kuwakumbatia katika huruma, msamaha na upendo wake wa daima. Huu ni mwaliko kwa waamini kujikita katika imani thabiti kwa kusali na kuombea haki, amani na utulivu. Utambuzi wa maisha kwa kawaida unafumbatwa katika msingi wa fasihi simulizi ya maisha ya mtu katika: huduma yake kwa Mungu na jirani; mchakato wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu; mambo msingi katika maisha bila kusahau mambo yanayoweza kuchefua roho na akili ya mtu.
Kumbe, ni jambo muhimu sana, mwamini akipata nafasi ya kutulia na kuanza kujichunguza mwenyewe tayari kuandika Kitabu cha historia ya maisha kutoka katika undani wa mtu mwenyewe. Utambuzi uwasaidie waamini kusoma maisha yao, kwa kutambua faraja, neema na baraka zinazobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bila kusahau upweke na ukiwa unaoweza kujikita katika sakafu ya nyoyo zao. Waamini wajitahidi kutambua ukweli wa maisha yao, mintarafu mwanga wa Injili. Hii inaweza kuwa ni fursa inayotolewa na Mwenyezi Mungu kwa mwamini kujifahamu vyema zaidi, tayari kuandika na kusimulia kitabu cha maisha yake kama mwamini. Waamini wajenge utamaduni wa kusoma na kutafakari Injili, ili hatimaye, waweze kuchota humo vigezo vitakavyowasaidia kupyaisha maisha yao binafsi na katika jamii. Wajenge utamaduni wa Kuabudu Ekaristi Takatifu, Kusali Rozari Takatifu sanjari na kufuata Njia ya Msalaba; yote haya yanapaswa kumwilishwa katika Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha imani tendaji.
