Ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli Jumanne tarehe 30 Juni 2026 umekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV  mjini Vatican. Ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli Jumanne tarehe 30 Juni 2026 umekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Hotuba Kwa Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa Kwanza: Ushuhuda

Ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza Jumanne tarehe 30 Juni 2026 umekutana na Papa Leo XIV ambaye katika hotuba yake amegusia kuhusu: Hija yake ya Kitume nchini Uturuki, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso Mkuu wa Nicea uliofanyika Asia Ndogo kunako Mwaka 325. Katika zama zenye vita, kinzani na migawanyiko inayozidi kukua na kupanuka: kitamaduni na kijamii, Wakristo waliopatanishwa, wakaungana wawe ishala ya amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, katika Sherehe ya Watakatifu Petro aliyeteuliwa na Kristo Yesu kuwa Mchungaji mkuu wa Kondoo wake na Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa; wote wawili ni Miamba wa imani ya Kanisa, Jumatatu tarehe 29 Juni 2026, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, akabariki Pallio Takatifu na kuwavisha Maaskofu wakuu wapya 35 walioteuliwa katika kipindi cha Mwaka 2025-2026. Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake ametaja sifa kuu na udhaifu wa watakatifu Petro na Paulo katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto na mwaliko kwa wakristo kuwa ni wajenzi wa umoja wa Kanisa, huku upendo wa Mungu na jirani zao ukipewa kipaumbele cha kwanza, kama njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa Pallio Takatifu waamini pia wawe tayari kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu kuubeba Msalaba ambao mwili na ulimwengu “Caro et mundus” huwatwisha mebegani mwao wote watafutao haki na amani. Waamini wanahimizwa na Mama Kanisa kusadaka nguvu, muda, mateso na hata maisha yao, ili Injili iweze kuwafikia watu wote na ndani mwake waweze kupata amani na utulivu. Ametambua uwepo wa ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ukiongozwa na Askofu mkuu Emmanuel Adamakis wa Jimbo kuu la Calcedonia.

Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza: Sherehe ya Miamba ya Imani
Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza: Sherehe ya Miamba ya Imani   (@Vatican Media)

Ujumbe huu, Jumanne tarehe 30 Juni 2026 umekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye katika hotuba yake amegusia kuhusu: Hija yake ya Kitume nchini Uturuki kuanzia tarehe 27 hadi tarehe 30 Novemba 2025 iliyonogeshwa na kauli mbiu: “Bwana mmoja, Imani na Ubatizo Mmoja,” Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso Mkuu wa Nicea uliofanyika Asia Ndogo kunako Mwaka 325. Katika zama zenye vita, kinzani na migawanyiko inayozidi kukua na kupanuka: kitamaduni na kijamii, Wakristo waliopatanishwa wao kwa wao, wakaungana na kukiri imani yao moja, wanaitwa kuwa ni ishara ya kuaminika ya amani, kwa kuchangia juhudi kubwa za watu wa Mungu katika ujenzi wa amani.

Umoja wa Wakristo ni hitaji muhimu la Wakristo katika Ulimwengu mamboleo
Umoja wa Wakristo ni hitaji muhimu la Wakristo katika Ulimwengu mamboleo   (@Vatican Media)

Hija ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uturuki kuanzia tarehe 27 hadi tarehe 30 Novemba 2025 iliyonogeshwa na kauli mbiu: “Bwana mmoja, Imani na Ubatizo Mmoja.” Baba Mtakatifu Leo XIV alikazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa uinjilishaji, Utangazaji na ushuhuda wa Injili yaani “Kerygma” kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya wokovu. Utengano kati ya Wakristo ni kikwazo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kutembea kwa pamoja katika hija ya maisha ya kiroho kuelekea Maadhimisho ya Mwaka wa Ukombozi, yaani miaka 2033 ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, huko mjini Yerusalemu. Hapa ni mahali ambapo Kristo Yesu aliadhimisha Karamu ya Mwisho, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, Siku ile ya Pentekoste, ili kujenga na kuimarisha umoja wa Wakristo huku akirejea kwenye kauli mbiu yake ya Kiaskofu: "In illo Uno Unum" yaani "Ingawa Sisi Wakristo ni Wengi, Katika Kristo Mmoja Sisi ni Wamoja.” Hili ni tukio la kihistoria, ambalo litawakusanya Wakristo kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Hadi sasa hakuna tarehe maalum ambayo imekwisha kupangwa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika hija hii ya kitume, ilikuwa ni fursa ya kukazia urafiki wao, kushirikishana mang’amuzi mbalimbali, lakini zaidi kuonesha ile nia ya pamoja ya kujenga umoja wa Kanisa.

Ujumbe kutoka kwa Patriaki ukiwa pamoja na Papa Leo XIV
Ujumbe kutoka kwa Patriaki ukiwa pamoja na Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso Mkuu wa Nicea uliofanyika Asia Ndogo kunako Mwaka 325. Huu ulikuwa ni Mtaguso wa kwanza wa Kiekumene kufanyika katika historia ya Kanisa na hivyo ukaibua imani ambayo ilikamilishwa na Mtaguso wa Kwanza wa Costantinopol ulioadhimishwa Mwaka 381 na hivyo kutoa dira na mwongozo wa imani ya Kanisa kwa Kristo Yesu. Maadhimisho haya yamefanyika ndani ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Kristo Tumaini Letu” na imeambatanishwa na maadhimisho ya Sherehe ya pamoja ya Pasaka ya Bwana kwa Wakristo wa Makanisa ya Mashariki na Magharibi. Hii ilikuwa ni fursa ya kupyaisha tena Kanuni ya Imani ya Nicea-Costantinopoli ambayo ni tafakari ya mchakato wa tafsiri rasmi wa imani ya Kanisa kwa Mungu aliye hai. Yaani Mungu Baba Muumbaji; Mungu Mwana Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu anayetakatifuza, kulitegemeza na kulielekeza Kanisa katika ukweli wote, yaani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huu ni ushuhuda uliotolewa na viongozi hawa kwa pamoja na kwamba, Kanuni ya Imani ya Nicea inapaswa kuwa ni msingi, dira na mwongozo wa safari ya Kiekumene, ili kujenga umoja katika utofauti yaani: Umoja katika Utatu Mtakatifu na Utatu Mtakatifu katika Umoja. Huu ni mwaliko kwa Wakristo wote kujizatiti katika maandalizi na hatimaye Maadhimisho ya Millenia ya Pili ya Ukristo, kunako mwaka 2033. Hii iwe ni hija ya pamoja ya Wakristo wote kwa pamoja, ili kugundua zawadi na wito wa kuwa mashuhuda wa Kristo Mfufuka.

Ushuhuda wa imani ni muhimu kwa sasa
Ushuhuda wa imani ni muhimu kwa sasa   (@Vatican Media)

Katika zama zenye vita, kinzani na mipasuko na migawanyiko inayozidi kukua na kupanuka: kitamaduni na kijamii, Wakristo waliopatanishwa wao kwa wao, wakaungana na kukiri imani yao moja, wanaitwa kuwa ni ishara ya kuaminika ya amani, kwa kuchangia juhudi kubwa za watu wa Mungu katika ujenzi wa amani. Baba Mtakatifu Leo XVI anasema, si tu katika muktadha wa hali halisi ya maisha ya binadamu. Leo hii kuna haja ya kujenga na kudumisha ushirikiano mkubwa kati ya Wakristo, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo ambazo ni pamoja na haki, amani sanjari na matumizi sahihi ya sayansi na teknolojia mintarafu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, mambo ambayo yanapata chanzo na hitimisho lake kutoka katika Injili ya Kristo Yesu mwenyewe. Kwa hakika wajibu wa maisha na hadhi ya kila mwanadamu ni kigezo kinachoamua hatima ya binadamu kwa sasa na kwa milele yote. Rej. Mt 25:31-46. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru na kuwapongeza wajumbe hawa kwa kuendeleza kazi hii takatifu ya ujenzi wa umoja wa Wakristo. Amewahakikishia sala na sadaka yake, ili kufikia umoja kamili; Umoja unaoonekana. Kwa maombezi ya watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, wasindikizwe na Mungu katika hija hii ya ujenzi wa umoja wa Wakristo.

Ujumbe wa Patriach
30 Juni 2026, 14:44