Papa Leo XIV:Watu wanaotafuta haki ni kwa sababu wanaitamani kama mkate wa kila siku!

“Utume ninao wakabidhi ni hasa:muwe binadamu.Wanawake na wanawaume wa nyama na mfupa.Si kijujuu,bali sura za kuaminika.Watu wanaotafuta haki kwa sababu wananjaa kama ile ya mkate wa kila siku.”Ni wito wa Papa Leo XIV kwa vijana wa Hispania,wakati wa mkesha wa usiku,Juni 6,2026,katika Uwanja wa Lima,Madrid na akijibu maswali ya vijana,kisha kuhitimisha kwa kuabudu Ekaristi."Mnaweza kubadilisha historia,"Papa aliwatia moyo.

Na Angella Rwezaula- Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV alishiriki Mkesha wa sala na Vijana katika Uwanja wa Lima huko Madrid, Jumamosi tarehe 6 Juni 2026 akiwa katika Ziara yake ya 4 ya Kitume nchini Hispania. Uwanja huo uliwaona waamini wapatao 600,000, mwishoni mwa siku nzima ya Ziara ya Papa yenye matukio mbali mbali ambapo Baba Mtakatifu alijibu maswali kutoka kwa vijana wa kike na kiume wakiwakilisha vijana wa rika na shughuli mbali mbali. Majibu yalikuwa ya kukumbusha miaka yake kama mmisionari huko Peru na ushuhuda wa imani iliyo na matatizo mengi lakini iliyojaa matumaini. Mwisho Papa aliwaomba vijana wawe na nyuso za kibinadamu, kikamilifu, zinazoaminika na si sura za kijujuu,  bali pia wafurahie maisha bila kutarajia utajiri, raha, au nguvu. Yafuatayo ni maswali na majibu kamili ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwa vijana hao.

Kila mmoja na Papa katika mkutano na vijana
Kila mmoja na Papa katika mkutano na vijana   (@Vatican Media)

Tunajua kuwa Mtakatifu Agostino ni muhimu sana kwako, lakini ni watakatifu wapi na wengine ambao walikusaidia kukua kama Mkristo(Marina Cabrero García, wa Parokia ya Yesu na Maria Vicaria 6, mwenye umri wa miaka  15).

Ninataka kukuuliza juu ya miaka yako ukiwa kama mmisionari wa Peru. Ni kumbukumbu gani au uzoefu gani unahifadhi kama tunu ya miaka ile?(Maria José Secada,kijana wa Peru Peru (kijana wa Peru aliyefika Hispania miaka 3 iliyopita,mwenye umri wa miaka 21).

Baba Mtakatifu Leo XIV alianza kujibu, ni vema, kwanza kabisa, salamu kwenu nyote. Asante kwa kuwa hapa na asante kwa kushiriki maisha yenu na Madrid yote na Hispania yote. Kwanza kabisa mliuliza kuhusu baadhi ya watakatifu ambao wamekuwa watu walioniongoza, wakati wa ukuaji wangu, ujana wangu, lakini pia kama mtazamaji, kama Papa. Nitataja Mtakatifu Agostino na sote tunajua kwamba Mtakatifu Agostino ni mtu muhimu sana kwa Kanisa lote, lakini pia nilimfikiria kama mmoja wa Baba wa Kanisa la Mashariki ambaye aliitwa Mtakatifu Yohane Chrysóstomo. Jina lake linamaanisha "mdomo wa dhahabu," jina ambalo Baba huyu wa Kanisa alipata kwa ufasaha wake. Kabla ya kubatizwa mwaka 368 BK, alisoma falsafa. Baadaye, alijitolea kwa ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu, pamoja na vijana wengine kutoka Antiokia, mji wake wa asili. Baada ya kipindi kama mtawa pweke, alijitolea kwa ajili ya huduma ya Kanisa kama Padre na baadaye kama Askofu.

Wakati wa kujibu maswali
Wakati wa kujibu maswali   (@Vatican Media)

Na hapa ninachukua fursa hii kuwaambia nyote: msiogope kamwe kufikiria wito wa ukuhani, maisha ya kitawa, au huduma zingine katika Kanisa! Kwa maana Yohane Chrysostom, ambaye alibeba moyoni mwake upendo huo kwa Neno la Mungu, baada ya kuwa Padre na askofu, alitoa ushuhuda wenye nguvu, zaidi ya yote kupitia uthabiti wa maisha yake. Ikiwa alihubiri, ilikuwa kwa sababu aliishi ujumbe huo. Kwa hivyo, binafsi, nilivutiwa sana na katekesi yake, mahubiri yake, maandishi yake yaliyochanganya upendo kiukweli na unyofu wa maisha yake. Lakini pia alikuwa na ujasiri mkubwa; hakuogopa kuzungumza mbele ya Mfalme, kusema mambo ambayo yalipendelea haki na si tu kuwafurahisha wengine. Alikuwa mtu wa neno lake. 

Mtakatifu mwingine niliyemfikiria ni Mtakatifu Thomas wa Villanova, Muagostino, ambaye pia aliitwa kuwa mchungaji wa Kanisa. Alikuwa Mhispania. Alisoma katika Chuo Kikuu cha Alcalá na, kwa sababu ya hekima yake, alipata heshima ya Mfalme Charles V. Baadaye, aliteuliwa kuwa Askofu wa Valencia, na akaanza kazi kubwa ya kurekebisha Kanisa, hasa mapadre, akiwahimiza ndugu zake kudumu katika maombi, katika maisha ya usafi wa moyo, na katika utii. Upendo wake wa dhati, anajulikana hadi leo kama “askofu wa maskini” umenitia moyo wakati wa majaribu na wakati wa huduma.  Mwenzake mwingine katika safari hiyo ni Mtakatifu Toribio de Mogrovejo, ambaye pia ni Mhispania. Katika karne ya 16, alikuwa mmisionari huko Peru, ambapo alijitolea kwa bidii kubwa ya uinjilishaji wa watu wa kiasili, akisoma lugha za kijamii za wenyeji. Mtakatifu Toribio alichanganya maisha ya dhati  ya maombi na kujitolea kwa haki, hasa katika kukabiliana na dhuluma na ufisadi wa wakati wake. Kwa sababu hiyo, yeye ni mfano wa kujitolea kwa watu, hasa maskini zaidi, kwa jina la Kristo.

Vijana wote wanataka kumuona Papa Leo XIV
Vijana wote wanataka kumuona Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Peru:Ushuhuda wa imani ya watu iliyojaa matatizo mengi lakini pia matumaini

Nikitafakari maisha ya watakatifu hawa, kama Mtakatifu Agostino, (maungamo VIII, 27). Jambo ambalo ninawakabidhi nyote pia kwa furaha, nikiwaalika kuchagua mifano ya maisha mazuri ambayo yanavutia kwenu na kwa wengine. Kuhusu miaka niliyotumia huko Peru, kwanza kama mmisionari na kisha kama askofu, nakumbuka zaidi ya yote ushuhuda wa imani ya watu, uliojaa matatizo mengi, lakini umejaa matumaini. Ilikuwa hasa kukutana na majeraha na furaha ya watu ndiko kulikonisaidia kukua katika njia ya kumfuata Yesu. Nilipotangaza, mimi pia nilibadilishwa na Injili, nikabadilishwa na maisha na imani ya watu hawa, mara nyingi maskini sana kimwili, lakini tajiri wa imani, na kupata imani hii kupitia Neno la Bwana, kwani nimeona jinsi Neno la Mungu linavyoweza kubadilisha migogoro kuwa amani, linaweza kuwa chanzo cha upatanisho, amani, na haki.

Swali la Tatu: Je wewe unafikiri nini kinaweza kutusaidia kujua sauti ya Mungu katikati ya sauti nyingine nyingi?( Myriam Más, wa Parokia ya Mtakatifu Theresa wa Yesu huko Tres Cantos, Vikarieti ya 8, wa kujitolea kawaida katika Uwakilishi wa Vijana,mwenye umeri wa miaka 20).

Swali la Nne: Jinsi gani sisi tunaweza, licha ya kwamba tunatafuta, kusindikiza wengine katika mchakato wa kugundua uzuri wa imani?(Manuel Martín, wa Parokia ya Mama Yetu wa Mafanikio Mazuri, Vikarieti ya 7, mwenye umri wa miaka 26).

Vema, kwanza, tunaweza kuzungumzia kidogo jinsi ya kusikia sauti hii ya Mungu, jinsi ya kutambua kama ni Mungu anayezungumza au kitu kingine, mvuto mwingine, ugumu mwingine. Ili kutambua sauti ya Mungu, ukimya unaweza kutusaidia zaidi ya yote, nadhani ni muhimu sana kila mmoja wetu kutafuta kukuza uwezo wa kukaa kimya. Mara nyingi tunatembea huku tumevaa vipokea sauti vya masikioni, tukisikiliza muziki, tukiwa tumevurugwa na mambo mengine, lakini hatujui jinsi ya kunyamaza. Na naamini kwamba mara nyingi ni katika uzoefu huu wa ukimya ambapo Mungu anaweza kuzungumza nasi au ndipo tunaweza kutambua sauti ya Mungu.

Tunapotafuta ukimya, tunaamua kile ambacho hatutaki kusikiliza na kile ambacho hatutaki kuruhusu kituvuruge. Kwa kujikomboa kutoka katika kelele za sauti nyingi sana, tunatambua kwamba baadhi hudanganya tamaa zetu, wengine hutununua bila kutulisha, na bado wengine huzungumza kwa maslahi yao binafsi. Tukiwa kimya, tunaelewa kwamba itikadi hupita, huku ukweli ukibaki.  Na hapa pia ningependa kusisitiza umuhimu wa kutafuta Ukweli kwa sababu sauti nyingi, mambo mengi kwenye mitandao ya kijamii hutudanganya na kutuambia uongo. Tafuteni Ukweli kila wakati. Na Mungu ndiye Ukweli, na ikiwa unawaelekeza mbali na Mungu, si ukweli. Msisahau hilo.

Wakati muhimu katika kuhitimisha siku ya kwanza ya Papa nchini Hispania
Wakati muhimu katika kuhitimisha siku ya kwanza ya Papa nchini Hispania   (@Vatican Media)

Pili, nawakikishieni kwamba Mungu anaijua sauti yenu vizuri, sauti yenu! Anawasikia na atawajibu. Msiogope kuelezea mnachohisi moyoni mwenu. Kuna zaburi inayosema: "Yeye aliyeumba sikio, je, hasikii?"(Zab 94:9). Mazungumzo yetu ya ndani huwa sala, sifa, na maombi yanapokabidhiwa kwa yule pekee anayeweza kuisikia. Sala ni sauti huru kwa sababu haizungumzi kutoa hesabu, kuonesha kwamba tuko tayari, au kujifanya tujisikie muhimu. Tunapojifanya kuwa maombi, Bwana anatujibu kwa Neno lake, ambaye alifanyika mwanadamu kwa ajili yetu, akithibitisha kwamba anatupenda kwa nafsi yake yote.

Tatu, ili kutambua sauti ya Mungu, ni muhimu kusikiliza Neno. Neno la Mungu liko hai kwa sababu ni Kristo, ambaye sauti yake inaendelea kusikika katika Kanisa, ambalo ni Mwili wake. Anatimiza Maandiko yote, agano la kale na jipya lililotolewa kwa wanadamu kama ahadi ya wokovu. Ibada ya Ekaristi, ambayo tutashiriki usiku wa leo, pia ni mahali sahihi pa kukaa kimya, kuweka huru mioyo yetu, na kuwapo mbele za Bwana, tukizungumza naye ili upendo wake, uliofanywa chakula kwa wanadamu wote, uweze kuwa fasaha. Zaidi ya hayo, wapendwa vijana, ili kuawasindikiza wengine katika kugundua uzuri wa imani yetu, kumbukeni kwamba hakuna hata mmoja wetu aliyezaliwa mwalimu na kwamba, mbele ya Bwana, sisi sote ni wanafunzi. Shirikisheni safari yenu ya kiroho, mkiishuhudia kwa uthabiti wa maisha: nia ya kumfuata Yesu itawafanya upya kila mara, hasa wakati wa ugumu. Ni muhimu kuona kwamba hakuna mtu aliye peke yake anayemwamini Yesu. Tazameni  ni wangapi kati yenu mko hapa!

Wakati muhimu wa kusikiliza Papa anajibu nini
Wakati muhimu wa kusikiliza Papa anajibu nini   (@Vatican Media)

Na vivyo hivyo, katika jamii, katika vikundi vya vijana, katika familia zetu, sote tunaweza kujifunza uzuri wa imani yetu. Kwa kushirikisha safari yenu ya kiroho, nia ya kumfuata Yesu itawafanya upya kila mara. Anatembea pamoja nasi na kuangazia njia yetu. Kwa kufuata mfano wa Bwana, ninawaalika kutenda kama wachungaji, waelimishaji, na marafiki. Mkiomba kwa upendo, vijana watathamini umuhimu wa sala. Mkiungua kwa imani, mtasambaza moto wake ulio hai. Tafuteni moto huu wa upendo wa Mungu mioyoni mwenu! Kwa maana kuna uwepo wa Yesu, na uwepo wake wa karibu unahisiwa hata wakati wa kujikwaa kwetu kwa sababu Yesu hatuachi. Pia, tunapokuwa mkono ulionyooshwa, kukumbatiana kwa kidugu, tunapotafuta fursa za kuwahudumia wengine, kufanya matendo ya upendo, kutafuta njia za kugusa maisha ya wengine kupitia majeraha yao, huzuni yao, na magumu yao. Hapo, imani katika Yesu Kristo inakuwa hai, na hapo, Yesu atatusaidia sote kusaidiana katika safari.

Swali ya tano: Tunawezaje kuishi vijana wa Kikristo wanaojishughulisha na jamii hii? (María Azargui, de la JOC,wa chama cha Vijana wakristo Wafanyakazi, miaka 21.)

Na swali la sita: Ni utume gani wa dhati ambao wewe unawakabidhi vijana wa Kanisa?(Fernando Conde-Pumpido:Kutoka Parokia ya Bikira Maria wa Fuensanta, vikarieti 5, umri miaka 30.

Hongera kwa ndoa yako, Fernando! Pia nimewaona wachumba  wengine hapa watakaofunga ndoa. Hongereni na baraka! Kwa sababu kama nilivyosema hapo awali, "Msiogope kufikiria wito," ndoa pia ni wito. Msiogope ndoa na kuanzisha familia! Katika karne nyingi za historia ya Kanisa, sisi Wakristo tumeishi katika jamii za kila aina, tukipitia mabadiliko katika tamaduni ambazo tumeshiriki na kusaidia kuziunda. Kuna maandishi ya kale, Barua kwa Diognetus, ambayo yanatupatia ufahamu mzuri katika suala hili: "Wakristo ni kwa ulimwengu kama roho ilivyo kwa mwili" (VI). Hii ndiyo njia yetu ya maisha: wanafunzi wa Yesu daima ni wa kisasa, lakini kamwe hawafungwi na muda unaopita. Tuko huru katika Kristo! Na Kristo ametuweka huru kwa upendo wake.

Shukrani kwa upendo huu, sisi daima tuko huru dhidi ya kulazimishwa na udanganyifu wote. Tuko huru kutokana na mitindo kwa sababu sisi ni wanafunzi wa ukweli; tuko wazi kwa wakati ujao kwa sababu tunajua kwamba kifo hakitungojei. Kinyume chake, maana ya historia inafikia kilele katika ushirika wa milele wa uzima ambao Mungu anaandaa kwa ajili ya wote. Kwa mtazamo huu, nyinyi vijana, hasa, mmeitwa kutoa mwelekeo mpya kwa jamii, mkiwa mawakala wa mabadiliko kupitia mahusiano yenu ya kila siku, uzoefu mlio nao katika familia zenu, chuo kikuu, na kazini. Kwa kuwatazama nyinyi vijana wapendwa, mkiwa mmejawa shauku hii inayochochewa na imani, kunanijaza matumaini kwa uwezo wenu wa kumshuhudia Kristo duniani, ikiwa ni pamoja na uhalisia wa kidijitali, ili kuwasilisha maadili na uzuri wa Injili (taz. Christus vivit, 105; Salamu za Jubilei ya Wamisionari wa Kidijitali ,Julai 29, 2025).

Kuweni Chumvi ya dunia na nuru ya Ulimwengu

Kwa hivyo ninawaalika nyote kuwa pamoja chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu (taz. Mt 5:13). Ili kuishi hivi, ni muhimu kwanza kabisa kutafsiri jamii ya leo, kuishi kwa hekima, ili tuweze kuibadilisha kama mashahidi wa Injili. Kiukweli, Mkristo kijana anang'aa katika furaha na majaribu, akitoa ladha kwa ukweli kwa sababu anaishi ndani yake kama mtu anayefurahia maisha kutoka ndani, bila kutarajia furaha hiyo itokee kutokana na utajiri, raha, au nguvu. Huu ndio uhuru wetu, ambao chanzo chake ni imani, ambayo ina uwezo wa kutoa mwanga na maana kwa kila jamii, kwa kila uzoefu wa mwanadamu. Kwa upande mwingine, maisha yanapokosa ladha, ni kana kwamba yananyakuliwa kutoka kwetu: hatuhisi tena kuwa ni yetu. Mkikabiliwa na utupu wa kutojali na kufuata sheria, mkikabiliwa na vurugu za vita na uongo, iweni cheche ya ubinadamu mpya.

Mkutano wa Papa katika mkesha na vijana
Mkutano wa Papa katika mkesha na vijana   (@Vatican Media)

Na kwa hivyo ninataka niwakabidhi nyote jambo moja: kuweni binadamu. Ndiyo, kuwa binadamu! Wanaume na wanawake wa nyama na mfupa. Sio tu sura, bali nyuso za kuaminika. Watu wanaotafuta haki kwa sababu wanaitamani, kama mkate wa kila siku. Watu wanaotamani maisha ya uaminifu na unyofu kwa sababu wanafurahi kuwafanyia wengine kile ambacho wangependa wengine wawafanyie. Kuweni binadamu kama Kristo alivyo, mtu mkamilifu, Mfufuka anayeshirikisha historia nasi katika kila kizazi. Kwa kukuza kujitolea huku, watazameni Mitume, Wakristo wa kwanza, wakazi wa ulimwengu wa kipagani. Kwa kufuata mfano wao, kuweni wamisionari wa Injili katika kukabiliana na umaskini wa kimwili na kiroho wa wakati wetu, mkijua vyema kwamba imani yetu ni njia ya maisha iliyotimizwa katika upendo (taz. Gal 5:6). Vijana wapendwa, hii ndiyo fadhila inayobadilisha historia zaidi kuliko nyingine yoyote. Mnaweza kubadilisha historia. Ifanyeni kwa upendo. Asanteni sana.

Kuabudu ndiyo njia muafaka wa kuzungumza na Bwana
Kuabudu ndiyo njia muafaka wa kuzungumza na Bwana   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu alihitimisha. Kisha ilifuatia ibada ya kuabudu ekaristi, wakati muafaka wa kukaa kimya na Bwana, kama Baba Mtakatifu alivyokuwa amewashauri hapo awali.

Hatimaye: Iñigo Blanco, mwenye umri wa miaka 14 (aliomba Papa asaini katika msalaba wa vijana).

Papa Leo XIV mara baada ya Mkesha na vijana
Papa Leo XIV mara baada ya Mkesha na vijana   (@Vatican Media)
MKESHA WA PAPA NA VIJANA MADRID

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

06 Juni 2026, 22:45