2026.06.05 "Namsubiri Papa Leo XIV katika kisiwa kikubwa cha Kanari." 2026.06.05 "Namsubiri Papa Leo XIV katika kisiwa kikubwa cha Kanari." 

Ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV:Ousseynou,“namsubiri Papa Leo”

Kijana wa Senegal alinusurika ajali ya meli mwaka 2020 ambapo alishuhudia kifo cha kaka yake na wengine wengi.Baada ya kufika bandari ya Arguineguín kwenye Kisiwa kikubwa cha Kanari,alikaribishwa na familia mahalia na sasa anafanya kazi kama mpishi.Mnamo 2023,alimwandikia barua Papa Francisko akimwalika kutembelea visiwa hivyo.Mnamo tarehe 11 Juni,badala yake atamkaribisha Papa Leo XIV:"Ningependa kumwomba atusaidie hasa wale wahamiaji wanaokufa safarini.”

Na Salvatore Cernuzio – Madrid.

Upepo, kiu, CAYUCO, mashua ya kiutamaduni ya mbao, ikichukua maji kwa kasi, mawimbi, giza, watu waliokufa baharini, miongoni mwao kaka yake mwenyewe. Kisha kukaja mwanzo mpya, makaribisho mazuri, kazi kama mpishi, na mwaliko wa kutembelea Visiwa vya Kanari, pamoja na fursa ya  kumsindikiza Papa binafsi kupitia bandari ya Arguineguín. Kwa miaka mingi, bandari hiyo ilijulikana kama el muelle de la vergüenza “gati la aibu” kwa sababu ya msongamano na hali hatarishi ambapo maelfu ya wahamiaji walilazimika kuishi. Papa Francisko aliguswa sana aliposoma maneno yaliyoandikwa na Ousseynou Fall, mvuvi wa zamani aliyekimbia Senegal na sasa anaishi Kisiwa cha Kanari. Katika barua, Ousseynou alisimulia historia yake ya kuondoka Afrika, nchi yake ya asili, na kuanza maisha mapya katika Visiwa vya Kanari. Ni historia ambayo mkasa ulikutana na ukarimu na mshikamano usio na ubinafsi, historia iliyosimuliwa na wahamiaji wengi walionusurika ya njia  mbaya ya Atlantiki na kufika ufukwe wa Visiwa vya Kanari, tofauti na wengine wengi ambao hawakuwahi kufika.

Mapenzi ya Papa Francisko yanatimizwa na Papa Leo XIV

Ousseynou na wahamiaji wengine kadhaa vijana walikuwa wamemwandikia Papa Francisko ambaye alifanya suala la uhamiaji kuwa moja ya vipaumbele vya upapa wake, akimwalika kutembelea maeneo yaliyowawezesha kuanza maisha mapya. Katika barua yake, iliyowasilishwa kwa Papa Francisko wakati wa Ziara yake ya Kitume  huko Luxembourg na Ubelgiji na Eva Fernández, mwandishi wa habari wa Radio ya Hispania COPE, Ousseynou aliandika kwamba ziara kama hiyo itakuwa "faraja kubwa" kwake na kwa wenzake. Akiguswa na historia zao, Papa Francisko aliamua kutembelea visiwa hivyo, akikiona kama hatua ya tatu ya ziara iliyojitolea kwa uhamiaji baada ya Lampedusa na Lesbos. Lakini ugonjwa na, baadaye, kifo chake vilizuia ziara hiyo kutokea. Sasa, Papa Leo XIV amechukua matashi mema ya mtangulizi wake na atatembelea Visiwa vya Kanari  mnamo tarehe 11 na 12 Juni 2026  mwishoni mwa ziara yake ya Kitume nchini Hispania. Ousseynou atakuwepo kumkaribisha Papa Leo XIV, pamoja na wahamiaji wengine, jamaa za wale waliotoweka baharini, timu za uokoaji na watu wa kujitolea. Itakuwa mahali pale pale ambapo, miaka sita iliyopita, alifika akiwa mwenye baridi, amechoka na mwenye kiu, akilala kando ya mfereji wa maji kwenye gati, kabla ya kupata joto, zaidi ya makaribisho mema na watu mahalia.

Kuvuka kutoka Senegal

"Kama ningeweza kuzungumza na Papa, jambo la kwanza ningeomba ni kwamba atusaidie kufanya mengi zaidi kwa wahamiaji wanaokufa njiani," Ousseynou alitoa kauli hiyo kwa  Vatican News. "Watu waliotaka kuja hapa lakini hawakufika. Kaka yangu pia alikufa safarini. Na wengine wengi pia." Alipatikana kwa simu wakati wa mapumziko kutoka kazini jikoni mwa hoteli, ambapo ameajiriwa kwa muda mrefu kama mpishi. Kwa furaha alichukua muda mfupi kushirikisha kumbukumbu ya maisha yake. Asili ya Ousseynou ni kutoka mji wa pwani wa Mtakatifu Louis nchini Senegal, na alifanya kazi kama mvuvi kabla ya kuamua kuondoka, pamoja na kaka yake, kwa sababu ya mgogoro ulioathiri tasnia ya uvuvi ya eneo hilo. Alifika katika kisiwa kikubwa cha Kanari tarehe 12 Novemba 2020 ndani ya CAYUCO, yaani mashua ndogo ya kiutamaduni ya mbao, baada ya safari ya kutisha wakiwa na kiu kali, hofu, vilio na machozi, na kupotea kwa wasafiri wenzake baharini.

Kuwasili Hispania

"Ilikuwa asubuhi na mapema nilipofika," Ousseynou alikumbuka. "saa chache zilipita na mashua yetu ilikuwa ina maji mengi. Kisha ikaanza kuzama. Timu ya uokoaji ya Salvamar Menkalinan, ilituona kwa mbali baharini. Walituokoa hapo na kutuhamisha kwenye chombo kidogo kilichotupeleka Arguineguín." Asubuhi hiyo gati ilikuwa tayari imejaa watu. Karibu wanaume na wanawake 2,000 walikuwa wamelala hapo kwa siku kadhaa chini ya mahema na blanketi, kujikinga kutokana na jua na mvua. Katika mwezi huo pekee, zaidi ya wahamiaji 6,300 walipitia bandari ndogo kwenye pwani ya kusini-magharibi ya kisiwa kikubwa cha Kanari.

Kumsubiri Papa

"Siku chache baadaye, Shirika la Msalaba Mwekundu lilituhamisha hadi hoteli," aliendelea kusimulia. Alipokuwa akitafuta chakula na nguo pamoja na binamu yake, alikutana na Fermina na Cristobál. Leo hii anawaita mama na baba. Walimkaribisha nyumbani kwao na kuhakikisha hakukosa chochote. "Wao ndio walionikaribisha. Hapa ndipo ninapoishi sasa," Ousseynou alielezea. Kwa msaada wa kikundi cha usaidizi cha wenyeji na Parokia ya Arguineguín, alijifunza Kihispania kwani alipofika, hakuwa anajua kusoma na kuandika.  Kwa miaka mingi alijifunza lugha hiyo, akijifundisha taaluma na kupata kazi. Leo ameunganishwa kikamilifu na maisha ya kisiwa kikubwa cha Kanari. Bado anatembelea bandari mara kwa mara, na tarehe 11 Juni asubuhi  anatumaini  kumkaribisha Papa Leo XIV. Sio tu kama mhamiaji, bali kama raia wa kawaida, mtu huru ambaye maisha yake yaliokolewa na ambaye heshima yake ilirejeshwa.

Imesassishwa tarehe 7 Juni 2026, saa 3.40 asubuhi na Angella Rwezaula.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

07 Juni 2026, 09:00