Papa Leo XIV Apewa Medali ya Miaka 250 ya Uhuru wa Marekani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ilikuwa ni tarehe 4 Julai 1776, yaaani Miaka 250 iliyopita ya Uhuru wa Marekani (US Freedom 250) kundi la watu jasiri lilitangaza uhuru wao kutoka kwa utawala wa Waingereza na kuchukua hatua kubwa ya kuanzisha jaribio la kihistoria la kujitawala wenyewe. Maono yao yaliwekwa wazi katika Tamko la Uhuru, hati iliyosaidia kubadili dira na mwelekeo wa historia ya nchi ya Marekani. Kimsingi Marekani inaadhimisha Jubilei ya miaka 250 ya uhuru, kwa kusherehekea: urithi uliojengwa juu ya udadisi, ujasiri, na ubunifu. Marekani kwa mwaka huu inajivunia kuwa na Baba Mtakatifu Leo XIV kama Mtoto Mashuhuri kutoka Marekani. Hili ni taifa mashuhuri la watu maarufu waliokuwa na kiu ya kuwa huru, kuboresha maisha yao na ya watoto wao na kwamba, maadhimisho haya yasaidie kujenga na kudumisha: Umoja wa Kitaifa, haki na amani na kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa uwepo wa Mungu; utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Haki hizi ni pamoja na haki ya mtu kuishi, uhuru pamoja na kujitafutia furaha ya kweli mintarafu uelewa makini wa kazi ya uumbaji, ambapo Mwenyezi Mungu kadiri ya Maandiko Matakatifu: “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.” Mwa 1:27. Huu ndio msingi wa utu, heshima na haki msingi za binadamu zinazopaswa kulindwa na serikali husika. Kwa kipindi cha miaka 250 iliyopita, Wamarekani walijitahidi kujenga nchi yao katika msingi wa uhuru, wakafungua njia kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na watoto wao waliosaidia kupyaisha na kuboresha maisha ya watu wa Marekani. Lakini Karne iliyopita Marekani imeshuhudia nyakati za giza, uhuru wa watu wake ukitiwa giza; uhuru na haki ikaanza kuchechemea na hivyo kukabiliana na changamoto mamboleo.
Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV Ijumaa tarehe 3 Julai 2026 kama sehemu ya Mkesha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 250 ya Uhuru wa Marekani ambayo ni fursa na changamoto ya kutafakari ili hatimaye, kuendelea kuishi katika ndoto ya uhuru wa kweli, haki msingi za binadamu na kwamba, msingi wake ni haki ya mtu kuishi, kama ilivyotajwa na Waasisi wa nchi ya Marekani na kwamba, asiwepo mtu yeyeto anayepokonywa uhuru wa kutafuta furaha ya kweli. Utu na maisha ya kila mtu ni mambo yanayopaswa kulindwa na kuendelezwa, ili kuendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi ya uumbaji na hasa kwa zawadi ya Injili ya uhai: “Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana.” Zab 139:14. Kumbe, kanuni maadili na utu wema wa kila nchi ni mambo yanayofumbatwa kwa Serikali kulinda na kudumisha Injili ya uhai, hususan kwa watu wanyonge ndani ya jamii. Baba Mtakatifu Leo XIV amekubali kupokea Medali ya Uhuru iliyotolewa na Kituo Kikuu cha Katiba, nchini Marekani, huko Philadelphia. “Liberty Medal of the National Constitutional Center.” Kumbe, haki ya mtu kuishi na uhuru wa kweli ni mambo msingi katika matumaini ambayo yameendelea kulitegemeza Taifa la Marekani, lakini kwa bahati mbaya uhuru huu umetafsiriwa vibaya kwa watu kufanya yale wanayotaka kufanya. Lakini uhuru wa kweli unakita mizizi yake kwa mwanadamu kusimamia ukweli na kile kilicho chema, ili kutafuta na hatimaye kuambata furaha ya kweli katika maisha; hii ni sadaka safi sana kwa watu wa Marekani ambao wamesadaka maisha yao kwa ajili ya kusimamia ukweli wa Injili ya maisha na hatima yake, kumjua Mwenyezi Mungu na ukuu pamoja na utukufu wake na kwamba, kwa miaka mingi, Marekani imekuwa ikiongoza katika kutafuta na kudumisha uhuru wa kidini.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza rasmi kuwa kila mwanadamu anayo haki ya uhuru wa kidini. Haki hii inamlinda mtu asishurutishwe na mtu yeyote au mamlaka yoyote kutenda kinyume na dhamiri yake, na inatoa uhuru wa kuabudu faraghani au hadharani. Uhuru wa kidini ni nguzo msingi katika Katiba ya Marekani iliyofanyiwa marekebisho. Uhuru wa kuabudu unagusa na kutikisa undani wa mtu mwenyewe; kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; ushirika na mshikamano wa waamini wa dini mbalimbali, kwa kuragibisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; Kanuni maadili na utu wema; mambo msingi ambayo yameboresha maisha ya watu wa Marekani na historia yao. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, kanuni hizi zinaendelea kuzaa matunda katika hotuba za hadhara zinazopaswa kusimikwa katika: kiasi, kwa kuheshimu na kuthamini maoni ya watu wengine, ili kujenga mazingira yatakayosaidia kukuza na kudumisha: haki, amani na maridhiano ndani na nje ya Marekani.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Marekani inaundwa na kujengwa na watu kutoka katika dini, lugha na tamaduni mbalimbali, changamoto na mwaliko wa kutafuta na kudumisha ustawi na maendeleo ya wengi kwa siku za usoni, kwa kukita mizizi yake katika ukweli juu ya binadamu, umoja unaobubujika kutoka kwa Mungu, ili kujenga tena nchi ya Marekani, kwa kutambua kwamba, hata katika wingi, wao ni wamoja: “Pluribus unum.” Ili Taifa lolote liweze kuendelea na kusonga mbele, halina budi kusimikwa katika umoja wa tunu na mawazo yasiyopitwa na wakati mintarafu: Uhai, utu, heshima na haki msingi za binadamu; usawa na mambo msingi yaliyobainishwa katika Tamko la Uhuru wa Marekani, yawe ni chanzo cha umoja na mwanga unaoangaza sasa na kwa siku zijazo. Na kwa hotuba hii, Baba Mtakatifu Leo XIV amekubali kupokea Tuzo ya Jubilei ya Miaka 250 ya Uhuru wa Marekani. Hii iwe ni fursa ya kuendelea kujizatiti katika utekelezaji wa mambo yale ambayo yameiwezesha Marekani kuwa ni Taifa kubwa linaloheshimu: haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi; nchi inayosimikwa katika ukarimu na unyofu wa moyo na kwamba, anapenda kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu chanzo na chemchemi ya uhuru, amani ya kudumu na ambaye Jina lake ni Amani.
