Papa Leo XIV Asikitishwa na Vita na Machafuko Nchi Takatifu, Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, Dominika tarehe 26 Julai 2026 alionesha masikitiko na wasiwasi mkubwa kutokana na vurugu na vita inayoendelea kupamba moto katika Nchi Takatifu na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Idadi ya vifo na majeruhi katika Ukingo wa Magharibi imezidi kuongezeka kutokana na operesheni za kijeshi na mashambulizi yanayofanywa na Israeli. Shirika la Kuratibu Misaada la Umoja wa Mataifa, OCHA linasema kuna vifo vya Wapalestina 68 tangu mwanzoni mwa mwaka 2026 hadi katikati ya mwezi Julai, huku ghasia zikiendelea kusababisha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu na vifo zaidi karibu na mji wa Nablus. Kuna idadi kubwa ya watu wanaendelea kupoteza maisha na kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara kwenye Ukanda wa Gaza na hivyo kusababisha uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na salama sanjari na huduma za afya. Watu wengi wamelazimika kuyakimbia makazi yao na kuishi katika kambi zenye msongamano mkubwa wa watu.
Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii kutoa wito kwa pande zote zinazohusika kufungua tena njia mpya majadiliano na diplomasia katika ukweli na uwazi, ili suluhu ya kisiasa iweze kupatikana, ili hatimaye, kukoleza na kudumisha: Utu, heshima na haki msingi za binadamu na hivyo kuepuka mashambulizi ya kijeshi, maamuzi yanayofanywa na upande mmoja peke yake, hususan yale yanayokiuka heshima na hali iliyopo ya maeneo matakatifu kwa dini mbalimbali. Lengo kuu ni kufikia kwa haraka amani ya kudumu inayotamaniwa sana katika eneo hili lote. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuwakumbuka na kuwaombea watu wote duniani wanaoteseka kutokana na vita. Mwenyezi Mungu aguse mioyo na kuangazia akili za wale wenye nyadhifa mbalimbali za uwajibikaji, ili upatanisho, haki na amani viweze kupatikana haraka. Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu nchini Ufaransa na Hispania ambao wameathirika kutokana na majanga ya moto. Ametumia fursa hii kuonesha mshikamano wake wa dhati na kwamba, waamini waendelee kuwaombea waathirika wa majanga haya ya moto na wale wote wanaoshughulikia dharura hii.
