Papa Leo XIV HIja ya Kichungaji Lampedusa: Ibada ya Misa Takatifu: Wakimbizi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 4 Julai 2026 amefanya hija ya kichungaji Kisiwani Lampedusa, Kusini mwa Italia kwa kutembelea Makaburi na kutoa heshima kwa Marehemu waliolazwa mahali hapa! Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, linasema tangu mwaka 2014 wakimbizi na wahamiaji zaidi ya 32, 700 wamefariki dunia wakijaribu kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora Barani Ulaya. Kunako mwezi Oktoba 2013 watu zaidi ya 368 walifariki dunia kwenye Kisiwa cha Lampedusa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV amepata nafasi ya kusali katika ukimya na kuweka shada la maua kwenye Makaburi; amekutana na kuzungumza na wakimbizi na wahamiaji kwenye Mlango wa Ulaya: “Porta d’Europa” baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa heshima yake kwa Sanamu ya Bikira Maria wa Bandari Salama “Portosalvo.” Amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, watoto wagonjwa pamoja na watu wa kujitolea. Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Barham Ahmed Salih, hivi karibuni ametoa pongezi kwa ujasiri na azma ya wakimbizi duniani kote, akisisitiza kwamba, ingawa mtu anaweza kuwa mkimbizi kwa kipindi fulani, hali hiyo haipaswi kufafanua maisha yake yote. Amebainisha kwamba wakimbizi na wahamiaji huchangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi wa jamii zinazowapokea, wakifanya kazi kama wafanyakazi, wanafunzi, wafanyabiashara, wasanii na viongozi. UNHCR inasema tangu mwaka 2014 wakimbizi na wahamiaji zaidi ya 32, 700 wamefariki dunia wakijaribu kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora Barani Ulaya.
Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Leo XIV Kisiwani Lampedusa inalenga kuikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji duniani inapaswa kushughulikiwa katika msingi wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Kisiwa cha Lampedusa ni mahali pa huzuni na masikitiko makubwa, lakini pia ni mahali bandari ya matumaini kwa watu waliopondeka na kuvunjika moyo. Baba Mtakatifu Leo XIV amefanya hija hii ya kichungaji akifuata nyayo za Mtangulizi wake Papa Francisko ambaye alitembelea Kisiwani hapa tarehe 8 Julai 2013 mara tu baada ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki. Injili ya Msamaria Mwema inaonesha kwamba, mshikamano, upendo na udugu wa kibinadamu ni njia ya uzima wa milele na inayowaokoa wale ambao wameangukia kati ya wanyang’anyi. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kujenga kwanza ujirani mwema, kwa kuwaonea huruma wale wanaoteseka pamoja na kujitahidi kuwahudumia kwa hali na mali.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, amekwenda Kisiwani Lampedusa kuwapongeza na kuwashukuru watu wa Mungu, ambao kwa kusukumwa na fadhila ya imani, au pasi na imani, wamejikita katika upendo wa kidugu kwa kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu amewakumbuka wakimbizi na wahamiaji waliohudhuria katika Ibada hii ya Misa Takatifu, walionja ukarimu na wao kwa upande wao wakawa wakarimu, kwa hawa ni kielelezo cha maskini wanaosaidiana katika umaskini wao, changamoto na mwaliko kwao kuendelea kujenga ujirani mwema, ili kuonesha upendo wa kweli katika uhuru kamili na uhuru kamili katika kutoa maamuzi. Watu waliofariki dunia kwenye Bahari ya Mediterrania ni matokeo ya maamuzi yaliyofanywa au maamuzi ambayo hayakufanyika, lakini yalipaswa kufanywa mintarafu: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, rushwa, mfumo wa uchumi wa dunia unaozalisha umaskini na utengano; hofu na woga unaozalisha maamuzi mbele, dharau na watu kutaka kujimwambafai. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni matokeo pia ya biashara haramu ya binadamu pamoja mifumo yote ya utumwa mamboleo mambo yanayoendelea kusigina na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu na kwamba, huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu unaotekelezwa na makundi ya kigaidi na magenge ya uhalifu wa Kitaifa na Kimataifa yanayotumia njia za wakimbizi na wahamiaji kujipatia fedha haramu; hali inayowafanya wapite kando kama ilivyokuwa kwenye Injili ya Msamaria mwema.
Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele na kwamba, Kristo Yesu amevunjilia mbali kuta za utengano, kumbe huu ni wakati wa: Kusimama na kuhurumia, kukaribia na kufunga jeraha kwa kuzitia mafuta na divai, kielelezo cha mwamini kuingia katika upendo wa Mungu uliofunuliwa na Kristo Yesu, ili kumwilisha Injili ya huruma na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji kama walivyofanya Mtakatifu Yohane XXIII, Mtakatifu Paulo VI pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II pamoja na umati wa Manabii wa Karne iliyopita. Huu ni mwaliko wa kutoa miundo mbinu inayokita mizizi yake katika tasaufi, tamaduni, sheria, siasa na uchumi ili kujenga utamaduni wa upendo unaopata chimbuko lake katika uaminifu wa matendo madogo madogo yanayokuza na kudumisha utu wa binadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya katika Bahari ya Mediterrania inapaswa kujielekeza zaidi katika kuishughulikia changamoto ya wakimbizi na wahamiaji; kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote; bila kusahau misingi ya haki na amani, kwa kuwa na uwajibikaji wa pamoja. Huu ni mwaliko wa kujikita katika sera na mbinu mkakati wa muda mrefu wa “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji.
Hii ni dhamana na wajibu wa Serikali, Jamii na Kanisa katika ujumla wake. Huu ni wakati wa kujenga utamaduni wa utalii, unaokita mizizi yake katika ugunduzi, kwa kutengeneza mazingira ya kiutu, ili kuwasaidia watalii kugundua tena maana ya maisha yao, kwa kuendelea kutunza mazingira nyumba ya wote sanjari na ujenzi wa urafiki wa kijamii. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Parokia iwe ni Jumuiya ambamo waamini wanajifunza shule ya Injili; wanajifunza kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji katika ushirika wa Parokia. Bikira Maria wa Bandari Salama “Madonna di Porto Salvo”, awaombee waamini ili waweze kushinda hofu na woga na badala yake wawe ni vyombo na mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya upendo na ukarimu. Iwe ni fursa ya kuimarisha na kumwilisha imani katika matendo sanjari na kuendelea kukuza Ibada kwa Bikira Maria. Waamini watambue kwamba, Mwenyezi Mungu ni bandari salama na kwamba, kila Jumuiya ya Kikristo inapaswa kuwa ni kielelezo cha bandari salama. Visiwa vya Lampeduda na Linosa viwe ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo.
Kwa upande wake Askofu mkuu Alessandro Damiano wa Jimbo kuu la Agrigento, lililoko Kusini mwa Italia, kwa niaba ya watu wa Mungu Jimbo kuu la Agrigento pamoja na waathirika wote, ametoa shukrani kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa uwepo na sala zake kwa wale wote waliopoteza maisha yao wakiwa safarini kuelekea Barani Ulaya. Uwepo wake ni ushuhuda wa heshima, unaotambua utu wao na hivyo kuwatakia maisha na uzima wa milele. Mlango wa Ulaya uliwekwa kwa heshima ya Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni mlango wa matumaini ya maisha mapya; udugu wa pamoja, unaosimikwa katika mtandao wa mshikamano, uhuru na ndoto ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Hija hii ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Leo XIV Kisiwani Lampedusa inawakumbusha umuhimu wa kuwa ni walinzi wa ndugu zao, waendelee kujikita katika huduma ya ukarimu inayotekelezwa na Majimbo ya Agrigento na Sicilia, kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika Injili ya upendo, katika ujenzi wa matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo!
Baba Mtakatifu Leo XIV alipowasili Kisiwani Lampedusa, kwenye Uwanja wa Michezo wa Arena, eneo la Salina: “Campo sportivo “Arena” in Località Salina” amewakumbusha watu wa Mungu wa Lampedusa na Linosa kwamba, amekuja kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, akawashukuru kwa mapokezi na ukarimu wao sanjari na mafungamano ya kijamii waliojenga na wakimbizi na wahamiaji, kumbukumbu endelevu na angavu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, aliyeonesha ukaribu kwao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, anaendeleza ule utume ulioanzishwa na Mtangulizi wake Papa Francisko, ili kuwasindikiza, kuwaenzi na kuwatia shime katika utume wao. Ekaristi Takatifu ni Ishara ya wazi inayoonesha uwepo wa Kristo Yesu kati pamoja nao. Kristo Yesu kwa kuumega mkate anadhihirisha ile sadaka ya kujitoa kwake ili aweze kuwa ni chakula na kinywaji safi kwa waja wake, chemchemi ya nguvu na ushirikiano. Lampedusa ni mahali ambapo panaposhuhudia matendo zaidi kuliko maneno. Lakini matendo ya binadamu yanahitaji moyo. Kumbe, adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu ni mahali pa kuchota upendo wa Kristo Yesu, kutoka katika Moyo wake Mtakatifu, ili kweli Ulimwengu uweze kusimikwa katika utu!
Dr. Filippo Mannino Meya wa Mji wa Lampedusa katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV mjini humo ameelezea sifa za Kisiwa cha Lampedusa, kilichoko kwenye Bahari ya Mediterrania kinachobeba maswali magumu na mazito; mateso na madonda ya watu; furaha na matumaini ya watu wa Mungu. Hapa ni mahali pa kusubiri, pa kutua nchi kavu; Lampedusa ni mahali pa huzuni na kumbukumbu. Ni mahali ambapo watu wengi wametafuta wokovu, heshima, na mustakabali. Wengine walipata mwanzo mpya, huku wengine hawakuwahi kufika; wote hawa wanabebwa nyoyoni mwa watu wa Lampedusa, kwani inaelewa thamani na uzito wa historia hii; hapa ni mahali ambapo taa ya matumaini inawashwa, kwa kutambua kwamba, maisha ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni matakatifu. Hapa ni mahali ambapo wakimbizi na wahamiaji wanapokelewa, wanalindwa, wanaendelezwa na kuwahusisha. Hapa ni mahali ambapo wakimbizi na wahamiaji wanasikilizwa, wanasaidiwa na kufarijiwa, Ujumbe wake kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kwamba, wanapaswa kusikiliza na kujibu kwa wakati kilio cha watu wa Lampedusa wenye majereha; Jumuiya ya Kimataifa ichague na kuishi Injili ya amani; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshuima na haki msingi za binadamu, huku wakioneshwa njia ya maisha yakufuatwa.
