Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ametoa tamko zito kuhusu Kikundi cha Pio wa X Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ametoa tamko zito kuhusu Kikundi cha Pio wa X   (ANSA)

Tamko la Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi: Jumuiya ya SSPX

Askofu mkuu Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anatamka kwamba: Kikundi cha Pio wa X hakitambuliki wala kukubalika katika Kanisa Katoliki ndani ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Waamini Wakatoliki waepuke kabisa kufungamana na kikundi hicho, wala wasihudhurie ibada zao kwani wakifungamana nao, watambue kwamba hao wamejitenga na Kanisa Katoliki. Izingatiwe kwamba Baba Mtakatifu ndiye Wakili wa Kristo na kumtii ni moja ya vibainishi vya mkatoliki halis

Na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi OFM Cap., - Dar es Salaam

Wapendwa katika Bwana: Yah: "THE SOCIETY OF SAINT PIUS X": Ninawasalimuni nikiwatakia neema, amani na baraka ya Bwana wetu Yesu Kristo. Tafadhali zingatieni kichwa cha habari kilichodokezwa hapo juu. Ninapenda kuwakumbusha kwamba Kanisa Katoliki linayo tabia, mwelekeo na miongozo inayowaongoza na kuwatanabaisha waamini wake. Ninasikitika kuwatahadharisha kuhusu ukweli kwamba wako watu wanaojidai kuwa wakatoliki lakini ambao hawazingatii wala kuheshimu miongozo, mwono na maelekezo ya Kanisa Katoliki. Tambueni na kumbukeni kwamba Kanisa Katoliki katika historia yake, limekuwa na vipindi vya kujitathmini na kujipanga ipasavyo. Tathmini hizo mara nyingi zimechukua sura ya Mitaguso. Mathalan, tunasoma kuhusu Mtaguso wa kwanza wa Kanisa Katoliki huko Yerusalem. Mtaguso huo wa kwanza ulitafakari, kumsikiliza Roho Mtakatifu na kupambanua namna sahihi ya kukabili na kushugulikia changamoto zilizotokana na kukua na kuenea kwa Kanisa katika tamaduni na maeneo mapya - tazama Matendo ya Mitume 15:5-21.

Askofu mkuu Ruwaichi atoa Tamko zito kuhusu: SSPX
Askofu mkuu Ruwaichi atoa Tamko zito kuhusu: SSPX

Kwa kifupi, Mtaguso ni fursa ya Kanisa kujitathmini, kumsikiliza Roho Mtakatifu, kupyaishwa na kujipanga upya huku likidumisha tabia na uhalisia wake. Kanisa Katoliki la zama zetu linaongozwa na mang'amuzi ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mtaguso huo ulioadhimishwa kuanzia mwaka 1962 na kuhitimishwa mwaka 1965 ndilo chimbuko la dira na upyaisho wa Kanisa leo. Kwa bahati mbaya, wapo watu au vikundi wanaoona shida kukumbatia dira mpya ambayo haivurugi hulka ya Kanisa. Moja ya vikundi hivyo ni lile kundi linalojiita: "The Society of St. Pius X". Inasemekana kwamba wafuasi wa kundi hili wapo hapa Dar es Salaam na hukusanyika na kusali katika maeneo ya Parokia ya Mtakatifu Yohana Muzeeyi, Tegeta A, eneo linalobainishwa kama la kwa MADAWA, Dar es Salaam. Kikundi hiki hutembelewa na kuratibiwa na "Padre" kutoka Kenya. Siku za hivi karibuni "Askofu" wa kikundi hiki bila kibali au ruhusa ya Baba Mtakatifu Leo XIV, alifanya tendo la uasi kwa kuwaweka wakfu "Maaskofu" wanne wasio halali. Kitendo hicho ni mwendelezo wa vitendo vya kushupaa na kutoheshimu mamlaka halali na sahihi ya Kanisa Katoliki.

Maaskofu wapya wa Jumuiya ya SSPX
Maaskofu wapya wa Jumuiya ya SSPX   (ANSA)

Anayefanya hivyo ni mwasi ambaye kwa tabia na tendo lake anakuwa anajitenga na kujiengua kutoka katika ushirika na Kanisa Katoliki. Kwa kuzingatia maelezo hayo, ninapenda kutamka kama ifuatavyo: a) Kikundi cha Pio wa X hakitambuliki wala kukubalika katika Kanisa Katoliki ndani ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam. b) Waamini Wakatoliki waepuke kabisa kufungamana na kikundi hicho, wala wasihudhurie ibada zao kwani wakifungamana nao, watambue kwamba hao wamejitenga na Kanisa Katoliki. c) Izingatiwe kwamba Baba Mtakatifu ndiye Wakili wa Kristo na kumtii ni moja ya vibainishi vya mkatoliki halisi. Asiyemtii Baba Mtakatifu hana ushirika na Kanisa. Ninawasihi na kuwashauri waamini wote kuzidi kumwomba Mungu ili awasaidie watu kama hao kwa mwanga wa Roho Mtakatifu na kupenda kutunza na kuhifadhi umoja wa Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki la Mitume.

Waamini Jimbo kuu la Dar wameonywa kutojifungamanisha na SSPX
Waamini Jimbo kuu la Dar wameonywa kutojifungamanisha na SSPX

Waraka wa Papa Leo XIV kwa Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio X: Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na ni chombo cha upatanisho, umoja na mshikamano wa Kitaifa na Kimataifa. Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio X (kwa Kilatini: Fraternitas Sacerdotalis Sancti Pii X - FSSPX), “The Priestly Society of Saint Pius X (SSPX)” ilianzishwa na Askofu Marcel Lefebvre kunako mwaka 1970. Jumuiya hii inajulikana kwa kusimamia Mapokeo ya Kikatoliki, kuheshimu Ibada Misa Takatifu katika lugha ya Kilatini, na kukataa mabadiliko yaliyoletwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kumekuwepo na juhudi za makusudi za kutaka kuirudisha Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio X katika ushirika kamili na Kanisa Katoliki, tangu wakati wa uongozi wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI, hadi wakati huu wa uongozi wa Baba Mtakatifu Leo XIV, juhudi zote hizi bado zinagonga mwamba na kwamba, Jumuiya imetanga mpango mkakati wa kuwaweka wakfu mapadre wanne kuwa Maaskofu, tarehe 1 Julai 2026 bila idhini ya Khalifa wa Mtakatifu Petro ambaye kwa wakati huu yuko katika nafsi ya Baba Mtakatifu Leo XIV huko Écône, nchini Uswissi. Kitendo hiki kitapelekea Jumuiya hii kujitenga moja kwa moja na Kanisa Katoliki na hivyo kuzidisha kinzani na mivutano ya miaka mingi isiyokuwa ya lazima.

Papa Leo XIV aliwaandikia waraka Jumuiya SSPX akiwaonya wakakaidi
Papa Leo XIV aliwaandikia waraka Jumuiya SSPX akiwaonya wakakaidi   (@Vatican Media)

Ni katika jitihada hizi, Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 29 Juni 2026 alimwandikia ujumbe Mheshimiwa Padre Davide Pagliarani, Mkuu wa Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio X na kwa njia yake, Maaskofu, Mapadre, Majandokasisi na waamini walei wanaovutwa kufuata mtindo wa maisha ya Jumuiya hii. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, anamwadikia ujumbe huu, akifahamu fika dhamana na wajibu wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mama Kanisa anatambua na kuthamini maisha ya kiliturujia, malezi na majiundo ya Mapadre, ari na mwamko wa shughuli za kichungaji pamoja na shauku ya kutaka kuendelea kuwa waaminifu kwa Mapokeo ya Kanisa, hali inayohitaji uelewa mpana, jambo ambalo watangulizi wake walilipatia kipaumbele cha pekee. Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa amefungwa na upendo wa Kikristo, anasali na kuwaomba kwa moyo wake wote, kurejea katika mapito yao! Waangalie kwa umakini mkubwa mafao ya kiroho kwa ajili ya waamini kwa sababu utengano na Kanisa, utakuwa ni kuzuizi cha waamini wao kupokea kwa halali Sakramenti za Kanisa, wanazopenda kupokea kama njia ya kujitakatifuza. Mama Kanisa yuko tayari kuanza mchakato wa majadiliano ya kina yanayowezeshwa na kufanikishwa na Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasali na kuwaomba kwamba, “wasichane nguo ya Kristo Yesu” kwani hii ni dhambi nzito. Kristo Yesu apende kuziangazia dhamiri zenu, aamshe nyoyo zenu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kwa uchungu mkubwa kwamba, kwa mamlaka aliyopewa na Kristo Yesu, na kwa moyo uliosheheni machungu, lakini bado akiwa na matumaini anahisi ndani mwake, kuwaomba kuachana na nia ya kuwawekwa wakfu Maaskofu wapya; anaweka nia zote hizi chini ya Moyo Safi wa Bikira Maria, Mama wa Shauri Jema.

Wote waliohusika wamejitenga na ushirika wa Kanisa Katoliki
Wote waliohusika wamejitenga na ushirika wa Kanisa Katoliki   (ANSA)

Wakati huo huo, Jumuiya ya Mapadre wa Mtakatifu Pio X (SSPX) ilijitenga rasmi na Kanisa Katoliki tarehe Mosi Julai 2026, baada ya viongozi wake kuwaweka wakfu maaskofu wanne bila kibali cha Papa Leo XIV, katika mji wa Econe, Uswisi bila idhini ya Baba Mtakatifu, hatua inayokiuka: Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa Katolik. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa likatangaza rasmi kuwa Maaskofu, mapadre, na wote waliohusika na tukio la kuwekwa wakfu Maaskofu hao wametengwa rasmi na Kanisa Katoliki. Onyo hili pia lilitolewa kwa waamini walei wanaoendelea kuhudhuria Ibada sanjari na kuunga mkono Jumuiya hii kwamba nao wanakabiliwa na adhabu ya kutengwa na Kanisa Katoliki. Askofu Alfonso de Galarreta Genua, SSPX ndiye aliyeongoza Ibada ya kuwaweka wakfu Maaskofu hao wane wa Jumuiya ya Mtakatifu Pio X, tarehe Mosi, Julai 2026 bila idhini ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Itakumbukwa kwamba, Askofu Alfonso de Galarreta Genua, SSPX aliwekwa wakfu kuwa Askofu kunako mwaka 1998 na Askofu mkuu Marcel Lefebvre bila idhini ya Mtakatifu Yohane Paulo II, tukio ambalo lilipelekea kujitenga na ushirika wa Kanisa Katoliki. Kunako mwaka 2009, Baba Mtakatifu Benedikto XVI akawaondolea adhabu ya kutengwa na Kanisa Katoliki, ili kuanzisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili hatimaye kurejesha ushirika kamili na Kanisa Katoliki.

Tamko Jimbo Kuu la Dar es Salaam
17 Julai 2026, 17:01