Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi UNHCR linaadhimisha miaka 75 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Wakimbizi wa tarehe 28 Julai 1951 Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi UNHCR linaadhimisha miaka 75 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Wakimbizi wa tarehe 28 Julai 1951   (AFP or licensors)

UNHCR: Kumbukizi ya Miaka 75 ya Mkataba wa Wakimbizi wa Mwaka 1951

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi UNHCR linaadhimisha miaka 75 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Wakimbizi wa tarehe 28 Julai 1951 kwa kutoa wito wa mshikamano uliosainiwa na: Viongozi wa kidini, washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Wasanii, Wanariadha, Wafanyabiashara mashuhuri, viongozi wa wakimbizi na watetezi wa haki msingi za binadamu. Mkataba huu unapaswa kupyaishwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa kusoma alama za nyakati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anasema, kuna watu wanaokimbia nchi na makazi yao kwa sababu ya baa la njaa, vita, umaskini, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na hatari mbalimbali za maisha na hivyo wanatafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Kristo Yesu yuko kati pamoja na watu wote hawa kama hata ilivyo kwa wale wote wanaoteseka kwa kiu; walio uchi, wagonjwa, wafungwa na wageni. Waamini wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanauona Uso wa Kristo Yesu anayeteseka kati pamoja na watu wote hawa. Waamini waoneshe ujasiri wa kuwaendea ili kukutana nao, kuwapenda na kuwahudumia kwa niaba ya Kristo Yesu. Watu wasiokuwa na makazi maalum ni fursa nyingine tena ya kukutana na Kristo Yesu, tayari kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha katika maisha ya jumuiya inayowapatia ukarimu. Hii ndiyo sera na mkakati wa Kanisa katika kuwahudumia wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa sehemu mbalimbali za dunia. Kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau waliweza kumtambua Kristo Yesu kwa kuumega mkate.

Kisiwa cha Lampedusa ni mahali pa mateso na matumaini
Kisiwa cha Lampedusa ni mahali pa mateso na matumaini   (Afp or licensors)

Ni katika muktadha huu, Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Leo XIV Kisiwani Lampedusa tarehe 4 Julai 2026 ililenga kuikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji duniani inapaswa kushughulikiwa katika msingi wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Kisiwa cha Lampedusa ni mahali pa huzuni na masikitiko makubwa, lakini pia ni mahali pa bandari ya matumaini kwa watu waliopondeka na kuvunjika moyo. Baba Mtakatifu Leo XIV alifanya hija hii ya kichungaji akifuata nyayo za Mtangulizi wake Papa Francisko ambaye alitembelea Kisiwani hapa tarehe 8 Julai 2013 mara tu baada ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki. Injili ya Msamaria Mwema inaonesha kwamba, mshikamano, upendo na udugu wa kibinadamu ni njia ya uzima wa milele na inayowaokoa wale ambao wameangukia kati ya wanyang’anyi. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kujenga kwanza ujirani mwema, kwa kuwaonea huruma wale wanaoteseka pamoja na kujitahidi kuwahudumia kwa hali na mali.

Kumbukizi ya Miaka 75 ya Mkataba wa Wakimbizi wa Mwaka 1951
Kumbukizi ya Miaka 75 ya Mkataba wa Wakimbizi wa Mwaka 1951   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, alikwenda Kisiwani Lampedusa kuwapongeza na kuwashukuru watu wa Mungu, ambao kwa kusukumwa na fadhila ya imani, au pasi na imani, wamejikita katika upendo wa kidugu kwa kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu amewakumbuka wakimbizi na wahamiaji waliohudhuria katika Ibada hii ya Misa Takatifu, walionja ukarimu na wao kwa upande wao wakawa wakarimu, kwa hawa ni kielelezo cha maskini wanaosaidiana katika umaskini wao, changamoto na mwaliko kwao kuendelea kujenga ujirani mwema, ili kuonesha upendo wa kweli katika uhuru kamili na uhuru kamili katika kutoa maamuzi. Watu waliofariki dunia kwenye Bahari ya Mediterrania ni matokeo ya maamuzi yaliyofanywa au maamuzi ambayo hayakufanyika, lakini yalipaswa kufanywa mintarafu: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, dhidi ya rushwa, mfumo wa uchumi wa dunia unaozalisha umaskini na utengano; hofu na woga unaozalisha maamuzi mbele, dharau na watu kutaka kujimwambafai. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni matokeo pia ya biashara haramu ya binadamu pamoja mifumo yote ya utumwa mamboleo mambo yanayoendelea kusigina na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu na kwamba, huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu unaotekelezwa na makundi ya kigaidi na magenge ya uhalifu wa Kitaifa na Kimataifa yanayotumia njia za wakimbizi na wahamiaji kujipatia fedha haramu; hali inayowafanya wapite kando kama ilivyokuwa kwenye Injili ya Msamaria mwema.

Wakimbizi na wahamiaji ni watu wenye utu, heshima na haki zao msingi
Wakimbizi na wahamiaji ni watu wenye utu, heshima na haki zao msingi   (ANSA)

Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele na kwamba, Kristo Yesu amevunjilia mbali kuta za utengano, kumbe huu ni wakati wa: Kusimama na kuhurumia, kukaribia na kufunga jeraha kwa kuzitia mafuta na divai, kielelezo cha mwamini kuingia katika upendo wa Mungu uliofunuliwa na Kristo Yesu, ili kumwilisha Injili ya huruma na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji kama walivyofanya Mtakatifu Yohane XXIII, Mtakatifu Paulo VI pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II pamoja na umati wa Manabii wa Karne iliyopita. Huu ni mwaliko wa kutoa miundo mbinu inayokita mizizi yake katika tasaufi, tamaduni, sheria, siasa na uchumi ili kujenga utamaduni wa upendo unaopata chimbuko lake katika uaminifu wa matendo madogo madogo yanayokuza na kudumisha utu wa binadamu.

Kumbukizi  ya Miaka 75 ya Mkataba wa Wakimbizi wa Mwaka 1951
Kumbukizi ya Miaka 75 ya Mkataba wa Wakimbizi wa Mwaka 1951   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya katika Bahari ya Mediterrania inapaswa kujielekeza zaidi katika kuishughulikia changamoto ya wakimbizi na wahamiaji; kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote; bila kusahau misingi ya haki na amani, kwa kuwa na uwajibikaji wa pamoja. Huu ni mwaliko wa kujikita katika sera na mbinu mkakati wa muda mrefu wa “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, lililoanzishwa kunako mwaka 1950 lilipaswa kudumu kwa muda wa miaka mitatu tu. Lakini hadi mwaka 2026 bado lipo na hii ni kutokana na ukweli kwamba, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni sehemu ya changamoto tete kwa Jumuiya ya Kimataifa katika Ulimwengu mamboleo.

Waamini waoneshe mshikamana wa huruma na mapendo
Waamini waoneshe mshikamana wa huruma na mapendo   (@Vatican Media)

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi UNHCR linaadhimisha miaka 75 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Wakimbizi wa tarehe 28 Julai 1951 kwa kutoa wito wa mshikamano uliosainiwa na: Viongozi wa kidini, washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Wasanii, Wanariadha, Wafanyabiashara mashuhuri, viongozi wa wakimbizi na watetezi wa haki msingi za binadamu. Bwana António Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa nchi zote wanachama kupyaisha dhamira yao ya kutekeleza kwa dhati Mkataba wa Wakimbizi wa mwaka 1951, akisema haki ya watu wanaokimbia mateso kutafuta hifadhi inazidi kutiliwa shaka, kuwekewa vikwazo au kunyimwa. Katika ujumbe wake wa kuadhimisha miaka 75 tangu kupitishwa kwa mkataba huo, Guterres amesema migogoro inaongezeka, mateso yanaendelea na idadi kubwa zaidi ya watu inalazimika kukimbia makazi yao na nchi zao. “Mkataba wa Wakimbizi si masalia ya enzi nyingine. Ungali unahitajika hata leo kama ulivyohitajika wakati ulipopitishwa miaka 75 iliyopita” amesema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa. Mkataba huo ulipitishwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia wakati Mataifa yalipoahidi kuwa mtu anayekimbia mateso hatarudishwa mahali ambako maisha au uhuru wake unaweza kuwa hatarini kwa sababu ya rangi, dini, utaifa, uanachama wa kundi fulani la kijamii au maoni yake ya kisiasa.

Changamoto ya wakimbizi na wahamiaji ishughulikiwe kwa umoja
Changamoto ya wakimbizi na wahamiaji ishughulikiwe kwa umoja   (AFP or licensors)

Kwa mujibu wa Katibu mkuu, ahadi hiyo ilipopatiwa nguvu ya kisheria kupitia Mkataba wa mwaka 1951, iliokoa mamilioni ya maisha na kuwa moja ya vielelezo vya wazi zaidi vya ubinadamu wa pamoja. Amekaza kusema: “Mkataba huo si kikwazo cha kukwepwa, bali ni msingi unaopaswa kulindwa kwa kuhakikisha watu wanapata ulinzi, taratibu za hifadhi zinaendeshwa kwa haki na utu, na kanuni ya kutomrudisha mtu mahali ambako anaweza kukabiliwa na mateso inaheshimiwa bila ubaguzi.” Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka nchi wanachama kukataa sera zinazohamishia Mataifa mengine wajibu wa kuwalinda wakimbizi, kuwaadhibu watu kwa sababu ya kutafuta usalama au kuweka masharti ya ulinzi kwa kuzingatia utaifa, dini, kabila au njia waliyotumia kuwasili. Amekazia pia umuhimu wa ushirikiano wa kweli wa Kimataifa na kugawana wajibu, ikiwemo kuzisaidia nchi na jamii zinazohifadhi idadi kubwa zaidi ya wakimbizi, ambazo nyingi zina rasilimali kiduchu. “Mkataba wa Wakimbizi ulizaliwa kutokana na kushindwa kwa ubinadamu kuwalinda watu wakati walipohitaji msaada zaidi. Tunapoadhimisha miaka 75, hatupaswi kuhatarisha kurudia kushindwa huko,” amesisitiza Bwana António Guterres Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Onesheni mshikamano wa huruma na mapendo kwa wakimbizi
Onesheni mshikamano wa huruma na mapendo kwa wakimbizi

Barham Salih, Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya wakimbizi amesema mkataba huo umeyaokoa mamilioni ya maisha kwa miongo kadhaa na ni kiini cha ubinadamu wa pamoja. "Miaka sabini na tano iliyopita, ulimwengu ulitoa ahadi ya kuwalinda watu waliolazimika kuzikimbia nchi zao. Jukumu letu sasa ni kupyaisha ahadi hii kwa vizazi vyote vijavyo." Barham Salih amesema, "Mkataba huo wa kimataifa pia unahusu kutafuta suluhu, na hiyo ina maana kwamba sote tufanye kazi pamoja katika hatua za mwanzo za watu kuhama makwao, ili wakimbizi wasiachwe wakiteseka." Ameongeza kusema lazima tuziunge mkono nchi na jamii zinazowahifadhi, kutanua fursa kwa wakimbizi, na kuunda mazingira ya kurudi kwa hiari na suluhu nyingine za kudumu. Mkataba huo, ulioanzishwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia unasema kwamba kila mtu, bila kujali ni nani au anatoka wapi, ana haki ya kutafuta na kufurahia usalama kutokana na mateso. Katika kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 75, Shirika lakuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, limezindua taarifa ya umma ya mshikamano iliyopewa kichwa cha maneno “The Promise” yaani Ahadi. UNHCR imesema zaidi ya wakimbizi milioni 41 bado wanalazimika kuishi mbali na makwao duniani kote baada ya kulazimika kuyakimbia makazi yao.

75 Mkataba wa wakimbizi
29 Julai 2026, 15:35