Baba Mtakatifu Leo XIV amepokea kwa huzuni na majonzi makubwa taarifa ya msiba huu mkubwa nchini Zimbabwe. Baba Mtakatifu Leo XIV amepokea kwa huzuni na majonzi makubwa taarifa ya msiba huu mkubwa nchini Zimbabwe.   (AFP or licensors)

Boti ya Abria Mbuya Nehanda Yazama na Kusababisha Vifo vya Watu 92 Zimbabwe

Boti ya abiria ya Mbuya Nehanda ilizama katika Ziwa Kariba nchini Zimbabwe Jumanne, tarehe 11 Agosti 2026 na kusababisha vifo vya watu 92, wakiwemo watoto wadogo. Watu 77 waliweza kuokolewa. Boti hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka mji wa Kariba kwenda vijiji vya pembezoni mwa ziwa hilo. Boti ilikuwa imebeba abiria pamoja na wafanyakazi wapatao 153, ingawa uwezo wa Boti hii ni kubeba watu 90. Ilizama baada ya kupigwa na wimbi kubwa, ikapoteza mwelekeo wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Boti ya abiria ya Mbuya Nehanda ilizama katika Ziwa Kariba nchini Zimbabwe Jumanne, tarehe 11 Agosti 2026 na kusababisha vifo vya watu 92, wakiwemo watoto wadogo. Watu 77 waliweza kuokolewa. Boti hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka mji wa Kariba kwenda vijiji vya pembezoni mwa ziwa hilo. Taarifa zinaonesha kwamba, Boti hii ilikuwa imebeba abiria 153, wakiwemo wafanyakazi wa Boti hii kabla ya ajali na kwamba, uwezo wa Boti hii ni watu 90. Boti hii ilizama baada ya kupigwa na mawimbi makubwa yaliyopelekea injili kuzima, kukosa uelekeo na hatimaye kuzama. Abiria walikuwa wameelezea wasiwasi kuhusu hali mbaya ya hewa kabla ya kuondoka, na walionusurika baadaye walisema kwamba maombi ya kukatiza safari hayakusikilizwa na wafanyakazi wa Boti hii.

Watu 92 wamefariki dunia baada ya Boti kuzama katika Ziwa Kariba
Watu 92 wamefariki dunia baada ya Boti kuzama katika Ziwa Kariba   (AFP or licensors)

Ni kwa takribani dakika 30 baada ya safari, mawimbi yalianza kuifunika Boti hiyo iliyokuwa ikifanya kazi kwa injini moja tu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV amepokea kwa huzuni na majonzi makubwa taarifa ya msiba huu mkubwa nchini Zimbabwe. Katika ujumbe ulioandikwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuchukua fursa hii, kuzikabidhi roho za marehemu kwa huruma na upendo wa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapenda kutoa salam zake za rambirambi kwa wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito. Baba Mtakatifu anawaombea viongozi wa Serikali na wafanyakazi wa dharura katika juhudi zao zinazoendelea kukabiliana na janga hili ambalo limeacha kurasa chungu katika maisha ya watu wengi nchini Zimbabwe. Kwa wote walioathirika, Baba Mtakatifu anawaombea baraka, faraja, uponyaji na nguvu za Kimungu katika kipindi hiki cha majonzi makubwa.

Papa Leo XIV atuma salam za rambirambi nchini Zimbabwe
Papa Leo XIV atuma salam za rambirambi nchini Zimbabwe   (AFP or licensors)

Kwa upande wake, Rais Emmerson Mnangagwa alitangaza hali ya janga na kukiri mapungufu katika uwezo wa safari za majini nchini Zimbabwe. Kuzama kwa boti hii kulivuruga usafiri na biashara katika jamii zilizo kando ya njia ya Chalala, na Serikali imeahidi kutoa chombo kingine na kurekebisha barabara zinazounganisha maeneo haya.

Kariba Zimbabwe
18 Agosti 2026, 16:49