Malengo makuu ya Mkutano wa Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi ya Utawala yalikuwa ni kujadili mabadiliko ya kiutawala, matumizi ya teknolojia ya akili unde na akili ya binadamu katika utendaji wa umma. Malengo makuu ya Mkutano wa Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi ya Utawala yalikuwa ni kujadili mabadiliko ya kiutawala, matumizi ya teknolojia ya akili unde na akili ya binadamu katika utendaji wa umma.  (@Vatican Media)

Hotuba ya Papa Leo XIV Kwa Wajumbe Wa Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi ya Uongozi

Malengo makuu ya Mkutano wa Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi ya Utawala yalikuwa ni kujadili mabadiliko ya kiutawala, matumizi ya teknolojia ya akili unde na akili ya binadamu katika utendaji wa umma, na kuimarisha taasisi za Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo endelevu na mafao ya wengi. Wajumbe wa mkutano huu, Ijumaa tarehe 28 Agosti, wamekutana na kuzungumza na Papa Leo XIV mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, hata Vatican ni mwanachama wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi ya Uongozi (International Institute of Administrative Sciences - IIAS) ni chama cha usimamizi wa shughuli za umma kinachojumuisha wizara, taasisi za mafunzo ya uongozi wa serikali, vyama vya kitaifa, vyuo vikuu na watu binafsi. Ilianzishwa kunako mwaka 1930 na makao yake makuu yako huko Brussels nchini Ubelgiji. Taasisi hii huandaa mikutano ya kitaaluma, huchapisha machapisho ya kitaaluma na kutoa huduma za uhakiki wa ubora katika elimu: Mkutano wa Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi ya Uongozi unalenga hadhira ya Kimataifa ya wataalamu wa usimamizi wa umma na sera;  Mkutano wa Chama cha Kimataifa cha Shule na Taasisi za Utawala (IASIA) unalenga hadhira ya kimataifa ya wasomi wa fani ya usimamizi wa umma. Mkutano wa 51 wa Kundi la Ulaya la Utawala wa Umma (EGPA), ambalo ni tawi la Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi ya Uongozi “International Institute of Administrative Sciences (IIAS), ulifanyika mjini Roma, nchini Italia kuanzia tarehe 24 hadi 27 Agosti 2026 Kwenye Chuo Kikuu cha “Sapienza” kilichoko mjini Roma. Mkutano huu umenogeshwa na kauli mbiu: "Public Governance for the Common Good: Human Intelligence Serving the Global Community" Yaani: “Utawala wa Umma kwa Ajili ya Manufaa ya Wote: Akili ya Binadamu Inayohudumia Jamii ya Kimataifa.” Mkutano huu umewahusisha wataalamu, watafiti na viongozi zaidi ya 900 kutoka katika nchi zaidi ya 70 duniani kutoa na kujadili masuala ya uongozi. Malengo makuu ya mkutano huu yalikuwa ni kujadili mabadiliko ya kiutawala, matumizi ya teknolojia ya akili unde na akili ya binadamu katika utendaji wa umma, na kuimarisha taasisi za Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo endelevu na mafao ya wengi. Wajumbe wa mkutano huu, Ijumaa tarehe 28 Agosti, Kumbukumbu ya Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, hata Vatican ni mwanachama wa Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi ya Utawala.

Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi ya Uongozi wakiwa na Papa Leo XIV
Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi ya Uongozi wakiwa na Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Taasisi hii ilianzishwa kunako mwaka 1930 kufuatia mgogoro mkubwa wa kiuchumi duniani, na ikapewa: "Wito wa kudumu kwa dhamiri ya mamlaka za kisiasa ili kurekebisha maisha ya kijamii kulingana na hali zinazobadilika kila mara, ili yaweze kutimiza makusudi na mipango ya Hekima ya Mwenyezi Mungu, Muumba." Rej. Pius XII, Hotuba kwa washiriki wa Kongamano la VIII la Kimataifa la Sayansi ya Utawala, Agosti 5, 1950. Utawala wa Umma kwa Ajili ya Manufaa ya Wote: Akili ya Binadamu Inayohudumia Jamii ya Kimataifa ni wito wenye nguvu kwa ulimwengu mamboleo katika zama hizi za  kidijitali. Huu ni wito wa kudumisha uwiano katika matumizi ya teknolojia za kidijitali. Wito huu unaendana na ule uliotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV Katika Waraka wake wa kwanza “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde.” Baba Mtakatifu katika Waraka huu, anakazia umuhimu wa kulinda na kudumisha utu wa mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Anasema: “Leo hii, hatuwezi kuepuka kukabiliana na uhalisia unaoathiri sana namna yetu ya kuishi na kupenya katika kila ngazi ya maisha ya kijamii. Kasi kubwa ya uvumbuzi wa teknolojia ya akili unde inatulazimu kujiuliza iwapo tutaweza kudhibiti mashine hizi hapo baadaye, na iwapo wanadamu wako katika hatari ya kuwa wahanga wa uvumbuzi wao wenyewe. Moja ya masuala mazito ya leo ni ukweli kwamba maamuzi yanayohusu maisha ya binadamu yanaachiwa mashine.”

Wajumbe wakipokea baraka za kipapa
Wajumbe wakipokea baraka za kipapa   (@Vatican Media)

Kwa kuzingatia hali hii ya kutia wasiwasi, Baba Mtakatifu Leo XIV amewakaribisha wajumbe wa mkutano huu, ambao unalenga kutilia mkazo tena umuhimu usiobadilika wa akili ya mwanadamu mbele ya zana hizi za kiteknolojia. Tafakari na upembuzi wao unaweza kusaidia mamlaka katika kufanya maamuzi katika nyanja hii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu wengi.  Kutoa wito wa tahadhari, udhibiti madhubuti, na wakati mwingine hata kupunguza kasi ya kupitisha matumizi ya teknolojia ya Akili Unde, AI, hakumaanishi kupinga maendeleo, bali ni kuonesha kujali kwa uwajibikaji familia ya wanadamu. Rej. Magnifica humanitas, 106. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuandaa mfumo wa kimaadili utakaongoza matumizi ya zana hizi muhimu ambazo kwa bahati mbaya zimejikita mikononi mwa wadau wakubwa wa uchumi na teknolojia ambao serikali inahangaika kuwadhibiti. Lazima kuhakikisha kwamba, ustawi wa familia ya wanadamu hautolewi kafara kwa ajili ya maslahi binafsi.

Wajumbe wakisikiliza hotuba ya Papa Leo XIV.
Wajumbe wakisikiliza hotuba ya Papa Leo XIV.   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii, kuwatia shime wajumbe wa Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi ya Uongozi (International Institute of Administrative Sciences, IIAS, kuendeleza utafiti wao ili kutafuta njia za kuchangia katika utawala wa umma kwa kuzifanya teknolojia za kidijitali ziwe na sura ya kibinadamu, kwa ajili ya kuragibisha na kuhudumia Injili ya uhai na amani. Papa Francisko katika Ujumbe wake wa Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2024 ulinogeshwa na kauli mbiu: “Teknolojia ya Akili Unde na Amani”: “Artificial Intelligence and Peace”: Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu anagusia kuhusu: Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kuelekea ujenzi wa amani; Wakati ujao wa teknolojia ya Akili Unde: kati ya ahadi na hatari; Teknolojia ya siku zijazo: mashine ambazo "hujifunza" peke yake; Hisia ya kikomo katika dhana ya kiteknolojia; Masuala motomoto kwa maadili; Je, tugeuze panga ziwe majembe? Changamoto za kielimu na hatimaye ni changamoto za maendeleo ya Sheria za Kimataifa. Jumuiya ya Kimataifa inalo jukumu la kupanua mtazamo wao na hivyo kuelekeza utafiti wa kiteknolojia na kisayansi kwenye ujenzi wa amani, ustawi na maendeleo ya wengi, katika huduma ya maendeleo kamili ya mtu binafsi na jamii. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema anafahamu kuwa dhamira yao si rahisi na kwamba wakati mwingine hali ya kukata tamaa inaweza kujitokeza. Anamwomba Mwenyezi Mungu awaimarishe, na kuwawezesha kutekeleza kazi hii tukufu kwa azimio thabiti. Mwishoni amewaombea baraka tele za Mwenyezi Mungu na kuwashukuru tena.

Sayansi ya uongozi
28 Agosti 2026, 15:36