Papa Leo XIV amesikitishwa sana na taarifa za maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi katika eneo la East Nusa Tenggara, na anapenda kutumia fursa hii kuonesha mshikamano na watu wote wa Mungu nchini Indonesia Papa Leo XIV amesikitishwa sana na taarifa za maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi katika eneo la East Nusa Tenggara, na anapenda kutumia fursa hii kuonesha mshikamano na watu wote wa Mungu nchini Indonesia  

Mshikamano wa Papa Leo XIV Na Watu wa Mungu Nchini Indonesia

Tetemeko la ardhi lililotokea katika Jimbo la East Nusa Tenggara, nchini Indonesia, Jumamosi tarehe 15 Agosti 2026 limepelekea zaidi ya watu 68 kufariki dunia na wengine zaidi ya watu 213 kujeruhiwa vibaya na kwamba, nyumba zaidi ya 4,500 ziliharibiwa pamoja na vituo 122 vya afya, shule 252, maeneo 84 ya Ibada na kwamba watu 12, 800 hawana makazi ya kudumu kulingana na taarifa ya Shirika la Kitaifa la Kusimamia Maafa la Indonesia (BNPB). Papa Leo XIV asikitishwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Tetemeko la ardhi lililotokea katika Jimbo la East Nusa Tenggara, nchini Indonesia, Jumamosi tarehe 15 Agosti 2026 limepelekea zaidi ya watu 68 kufariki dunia na wengine zaidi ya watu 213 kujeruhiwa vibaya na kwamba, nyumba zaidi ya 4,500 ziliharibiwa pamoja na vituo 122 vya afya, shule 252, maeneo 84 ya Ibada na kwamba watu 12, 800 hawana makazi ya kudumu kulingana na taarifa ya Shirika la Kitaifa la Kusimamia Maafa la Indonesia (BNPB). Serikali ya Indonesia imesema kuwa zaidi ya maafisa 1,800 wa Jeshi na Polisi wametumwa katika maeneo yaliyoathirika ili kusambaza zaidi ya tani 100 za misaada kwa kutumia ndege na vyombo vya usafiri wa majini.

Madhara ya tetemeko la ardhi nchini Indonesia
Madhara ya tetemeko la ardhi nchini Indonesia   (AFP or licensors)

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Paulus Budi Kleden, SVD., wa Jimbo kuu la Ende, Indonesia, anasema, amesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi katika eneo la East Nusa Tenggara, na anapenda kutumia fursa hii kuonesha mshikamano na ukaribu wake wa maisha ya kiroho kwa watu wote wa Mungu nchini Indonesia walioguswa na kutikiswa na janga hili kubwa, kiasi cha kusababisha vifo, majeruhi na watu wengi kuyakimbia makazi yao.  Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuwatia moyo viongozi wa Kanisa na wa serikali wanapoendelea kutoa misaada ya kibinadamu, na anawaombea wafanyakazi wa dharura wanaoshiriki katika juhudi za uokoaji na urejeshaji wa hali ya kawaida katika maeneo yaliyoathirika.

Tetemeko la ardhi limesababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao
Tetemeko la ardhi limesababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV amewakabidhi marehemu wote chini ya huruma na upendo wa Mungu, Baba Mwenyezi; anawaombea baraka, faraja na nguvu za kimungu katika kipindi hiki kigumu cha maisha na historia yao. Kanisa nchini Indonesia linaendelea kuonesha ukaribu kwa watu walioathirika kwa tetemeko hili, kwa matumaini kwamba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, ataweza kuwaletea mapambazuko angavu katika kipindi hiki cha giza na majonzi makubwa anasema Askofu Siprianus Hormat wa Jimbo Katoliki la Ruteng. Tangu kutokea kwa tetemeko hili, Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Indonesia, Caritas Indonesia, limekuwa likiratibu misaada kutoka katika majimbo mbalimbali ya Indonesia, hili ni jibu la Kanisa moja, linatoa jibu moja katika kukabiliana na maafa haya. Hali ya mawasiliano na baadhi ya Parokia bado ni tete sana.

Tetemeko la ardhi Indonesia
18 Agosti 2026, 15:49