Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico, kuanzia tarehe 15 hadi 16 Agosti 2026 limeadhimisha Siku ya Tatu ya Vijana Kitaifa nchini Mexico Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico, kuanzia tarehe 15 hadi 16 Agosti 2026 limeadhimisha Siku ya Tatu ya Vijana Kitaifa nchini Mexico   (ANSA)

Papa Leo XIV: Ujumbe: Maadhimisho Siku ya Tatu ya Vijana Nchini Mexico 2026

Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico, kuanzia tarehe 15 hadi 16 Agosti 2026 limeadhimisha Siku ya Tatu ya Vijana Kitaifa nchini Mexico katika Jimbo kuu la Monterrey kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami.” Yn 15:27. Huu ni mwaliko kwa vijana kuwa ni mashuhuda amini wa maisha, utume na kazi alizozitenda Kristo Yesu hapa ulimwenguni. Vijana wawe na ujasiri wa kusimama kidogo na kutafakari maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Mara baada ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa vijana yaliyonogeshwa na kauli mbiu: “Vijana mahujaji wa matumaini” Baba Mtakatifu Leo XIV alitangaza kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 Jimbo kuu la Seoul, Korea ya Kusini, yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 3 hadi 8 Agosti 2027 na kwamba, maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu; “Jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Yn 16:33. Matumaini yaliyomo ndani ya nyoyo za waamini ndiyo yanayowapatia nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia ushindi wa Kristo Mfufuka dhidi ya dhambi na mauti. Kwa hakika anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa matumaini hadi miisho ya dunia. Alitumia fursa hii kuwakaribisha vijana wengi zaidi huko Seoul, Korea ya Kusini, ili kwa pamoja waweze kuendeleza ndoto na matumaini. Kumbe, vijana pamoja na wachungaji wao watakaohudhuria maadhimisho haya wanazidi kuwa ni kiini cha maandalizi ya tukio hili muhimu la Kikanisa.

Papa Leo XIV amewaweka vijana nchini Mexico chini ya ulinzi wa B. Maria
Papa Leo XIV amewaweka vijana nchini Mexico chini ya ulinzi wa B. Maria

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico, kuanzia tarehe 15 hadi 16 Agosti 2026 limeadhimisha Siku ya Tatu ya Vijana Kitaifa nchini Mexico katika Jimbo kuu la Monterrey kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami.” Yn 15:27. Huu ni mwaliko kwa vijana kuwa ni mashuhuda amini wa maisha, utume na kazi alizozitenda Kristo Yesu hapa ulimwenguni. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa waandaaji na washiriki wa maadhimisho haya anasema, angetamani sana kushiriki pamoja nao tukio hili, ili kutembea pamoja nao katika hija hii ya maisha ya kiroho. Hii ni fursa ambayo imewakutanisha vijana pamoja na viongozi wa Kanisa kielelezo makini cha ujenzi wa ushirika pamoja na Kristo Yesu, ili kutangaza na kuwashuhudia walimwengu, lengo na maana ya maisha yao hapa ulimwenguni, yaani kushiriki pamoja na Kristo Yesu maisha na utakatifu wake, wito ambao kila mwamini anaitwa kuukumbatia katika hija ya maisha yake, kwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Vijana wa Mexico ni mashuhuda amini wa Kristo Yesu
Vijana wa Mexico ni mashuhuda amini wa Kristo Yesu   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kauli mbiu: “Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami.” Yn 15:27, ni mwaliko kwa vijana ndani na nje ya Mexico kuyakumbatia na kuyaambata maneno haya kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao yenye mvuto na mashiko, ili wakiwa wameungana na kushikamana na Kristo Yesu, wanaweza kuwafanya walimwengu wakamwamini Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele, licha ya matatizo na changamoto mbalimbali za maisha zinazowaandama katika maisha na utume wao yaani: Ukatili, uvunjifu wa misingi ya haki na amani; kwa baadhi ya watu kuwageuzia kisogo na hata wakati mwingine, kushindwa kufahamu maana ya maisha yao. Katika hali na mazingira kama haya, vijana wawe na ujasiri wa kusimama kidogo na kutafakari, yale mambo msingi katika maisha yanayoweza kuwajenga, huku wakifanya yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu. “Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vifaavyo. Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vijengavyo.” 1Kor 10:23. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka vijana wa Mexico kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema na kwa busara uhuru wao kwani baadhi ya mambo yanawezsa kudhuru maisha yao ya kiroho na kimwili. Wawe na busara ili wasiwakwaze jirani zao. Bali matendo yao yasaidie kuwajenga vijana wenzao kiroho na kimwili na waendelee kujitahidi kupendana na kusaidiana wao kwa wao! Na kwa jinsi hii, kwa hakika watakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu, na mashuhuda wa Injili ya matumaini. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa vijana wa Mexico kwa kuwatakia furaha na hivyo kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume!

Vijana Mexico 2026
18 Agosti 2026, 16:13