Papa Leo XIV Asikitishwa na Hali Tete Huko El-Obeid, Sudan
Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.
Tarehe 9 Julai 2026, Sudan Kusini imeadhimisha kumbukizi ya miaka 15 ya uhuru wake tangu ilipojitenga rasmi na Sudan Kongwe tarehe 9 Julai 2011. Sherehe hizo zimeongozwa na Rais Salva Kiir katika mji mkuu Juba, kwa kunogeshwa na kauli mbiu "15 Years of Freedom - A Better Future Together" yaani "Miaka 15 ya Uhuru Kuelekea Wakati Bora Ujao kwa Pamoja.” Sudan Kusini imeadhimisha miaka 15 ya uhuru wake tangu taifa hilo lilipojitenga na Sudan Kongwe mwaka 2011, huku ikikabiliwa na changamoto kubwa za: kibinadamu, umaskini uliokithiri miongoni mwa wananchi wake; hali tete ya kisiasa, kiuchumi, athari za vita ya wenyewe kwa wenyewe mambo yanayotia mashaka kuhusu kutimia kwa ndoto ya matumaini yaliyokuwepo hapo awali.
Katika kura ya maoni ya mwaka 2011, karibu asilimia 99% ya wananchi waliunga mkono kujitenga na Sudan, wakiamini uhuru ungefungua ukurasa mpya wa maisha na maendeleo. Hata hivyo, matumaini hayo kwa kiasi kikubwa hayajatimia kutokana na migogoro ya ndani na changamoto za kiuchumi. Leo, Sudan Kusini ni miongoni mwa mataifa maskini na dhaifu zaidi duniani. Takribani watu milioni 10, sawa na karibu theluthi nne ya idadi ya watu wake, wanahitaji msaada wa kibinadamu kwa mwaka 2026. Mbali na changamoto za kibinadamu, nchi hiyo bado inakabiliwa na hali ngumu ya maisha, ambapo wastani wa umri wa kuishi uko chini ya miaka 58 na ni asilimia 8% pekee ya wananchi wa Sudan ya Kusini wanaopata huduma ya nishati ya umeme.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika baa la njaa, umaskini na maafa makubwa, changamoto na mwaliko kwa watu wote kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani; kwa kuwafariji wale wanaoteseka kwa vita, kuna haja ya kukomesha vita, ili kukijengea kizazi cha sasa na kile kijacho amani, ustawi na maendeleo, kwa kukazia tunu msingi za maisha ya kijamii kwa kujikita katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na uhakika wa usalama wa chakula sehemu mbalimbali za dunia; watu wawe na uwezekano wa kupata rasilimali zitakazo saidia kuchochea maendeleo endelevu hasa vijijini.
Hali ya Usalama na Utulivu Sudan Kongwe pia inatisha. Ni katika muktadha huu wa ukosefu wa uhakika wa usalama, amani na utulivu, Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 9 Agosti 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema anaendelea kufuatilia kwa hofu na wasiwasi mkubwa wa hali ya kutisha nchini Sudan na hasa katika mji wa El-Obeid: “Al-Ubayyid” ambao kwa sasa unakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula; maji safi na salama; ongezeko kubwa la watu wasiokuwa na makazi ya kudumu kutokana na wengi wao kukimbia vita eneo la Kordofan, Kaskazini mwa Sudan Kongwe. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha ukaribu wake wa maisha ya kiroho kwa wananchi wote wa Sudan, huku akikazia tena wito wake kwa viongozi wa Serikali na wale wenye madaraka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na njia salama za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya raia. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuunga mkono juhudi zinazolenga kufikia makubaliano ya kusitisha vita mara moja. Baba Mtakatifu amewaombea waathirika wote wa vita, ili waweze kupata faraja na kwamba, Mwenyezi Mungu abadilishe mioyo ya wale wanaochochea vita, vurugu na mipasuko ya kijamii na azime kiu ya amani kwa wananchi wa Sudan, amani wanayo isubiri kwa muda mrefu.
