Papa Leo XIV Mashindano ya Michezo ya 20 ya Mediterania: Amani na Udugu
Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo wa XIV katika Waraka wake wa Kitume kuhusu Michezo anaonesha kwa namna ya pekee: Thamani ya michezo: Michezo na ujenzi wa amani; tunu msingi za michezo katika majiundo; Michezo kama shule ya maisha na ya kisasa; Michezo na maendeleo binafsi; Mambo yanayohatarisha tunu msingi za michezo; Mashindano na utamaduni wa watu kukutana; Michezo, Mahusiano na mang’amuzi; sanjari na Mpango mkakati wa michezo kwa ajili ya kuwa na maisha tele! Kipindi chote cha mashindano ya Olimpiki, vita na misigano yote ya kisiasa na kijamii ilisitishwa ili kutoa fursa kwa wananchi kufurahia michezo na hivyo michezo ikawa ni fursa ya kujenga na kudumisha amani; ukuaji wa udugu wa kibinadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, vita, kinzani na mipasuko ni dalili za kushindwa kwa ubinadamu. Dunia ina kiu ya amani kumbe, kuna haja ya kutumia nyenzo zitakazo saidia kusitisha matumizi mabaya ya madaraka na hivyo kujikita katika utawala wa haki na sheria. Tunu msingi za michezo katika majiundo ili kuweza kuwa na maisha tele pamoja na utimilifu wake. Rej. Yn 10:10.
Mama Kanisa hana budi kutekeleza dhamana na utume wake hapa ulimwenguni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu katika michezo kama anavyosema Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa kuhusu utaratibu kwa wanariadha: “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate. Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika.” 1Kor 9:24-25. Hiki ni kielelezo cha mashindano ya kiroho; na kwamba Binadamu ni umoja wa mwili, roho na nafsi na hivyo Mama Kanisa anakazia umuhimu wa michezo katika maisha ya mwanadamu kama mambo muhimu sana katika kuhubiri na kufundisha. Ni katika muktadha wa Mashindano ya Michezo ya 20 ya Mediterania, ambayo yatafanyika mjini Taranto, Kaskazini mwa Italia kuanzia tarehe 21 Agosti hadi tarehe 3 Septemba 2026, kwa kuhusisha nchi mbalimbali kutoka Afrika, Asia, na Ulaya zilizoko katika eneo la Mediterania yananogeshwa na kauli mbiu: “Yakumbatie Maisha ya Baadaye."
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, tukio hili la Michezo ya 20 ya Mediterania litakuwa ni ishara ya amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu miongoni mwa watu wa Mataifa. Michezo hii itafunguliwa kwa Ibada ya Misa takatifu pamoja na kusimika Msalaba wa Wanamichezo, Jumatano tarehe 19 Agosti 2026, majira ya jioni, kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Taranto. Ibada hii ya Misa Takatifu itaadhimishwa na Askofu mkuu Ciro Miniero wa Jimbo kuu la Taranto kwa ushiriki wa Askofu mkuu Paul Tighe, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu. Kwa upande wake Kardinali José Tolentino de Mendonça Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu anasema, Kikundi cha Wanamichezo kutoka Vatican kinashiriki kama kielelezo cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu katika michezo, kama kielelezo makini cha mchakato wa ujenzi wa amani na udugu wa kibinadamu kati ya watu wa Mataifa. Ni kipindi cha kushirikishana tunu ya maisha na matumaini na kwamba, Msalaba wa Wanamichezo ni alama ya wazi ya ushiriki wa Kanisa katika michezo hii na kwamba, wanamichezo katika mashindano haya, wanapoteseka na kutoka jasho, wanapaswa kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa.
Kwa upande wake Askofu mkuu Ciro Miniero wa Jimbo kuu la Taranto, anapenda kuchukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Leo XIV kwa wosia wake mintarafu michezo na kwamba, sasa ni dhamana na wajibu wa wanamichezo kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ujenzi haki na amani; mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Kikundi cha Wanamichezo kutoka Vatican kilianzishwa kunako mwaka 2018 chini ya usimamizi wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu. Hii ni kuonesha kwamba, hata michezo inaweza kuwa ni ushuhuda wa huduma ya Kanisa hasa miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kumbe, michezo ni kwa ajili ya ujenzi wa ujirani mwema, usindikizaji na hija shirikishi kwa wanamichezo.
