2026.08.14 Abasia ya Mount Angel Abbey, ya Kibenediktini huko Oregon,Marekani (©Mount Angel Abbey) 2026.08.14 Abasia ya Mount Angel Abbey, ya Kibenediktini huko Oregon,Marekani (©Mount Angel Abbey) 

Papa Leo XIV:Kuelimisha Watu wa Mungu&maandalizi ya mapadre ni kipaumbele

Katika Barua kutoka kwa Papa Leo XIV kwa Kardinali Roche,Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada Takatifu na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa,katika hafla ya mkutano unaofanyika kuanzia Agosti 14 hadi 19 katika Abasia ya Kibenediktini ya Mount Angel,Oregon(Marekani),wakitafakari njia zilizofunguliwa na Barua ya Kitume ya Papa Francisko "Desiderio desideravi”amehimiza:"Malezi bora ya kiliturujia kwa wote kwa kuzingatia maandiko yaliyoidhinishwa.”

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV amemtumia mwakilishi wake Kardinali Arthur Roche, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Ibada Takatifu na Nidhamu za Sakramenti za Kanisa ujumbe ambao pamoja na kuwatakia washiriki heri ya kazi, alitoa baadhi ya mada muhimu ili kufikia lengo la mkutano huo ulioanza tarehe 14 hadi 19 Agosti 2026, katika Abasia ya Kibenediktini ya Mlima Angel, huko Oregon, Nchini Marekani. Papa Leo XIV anatoa salamu za dhati kwake yeye na kwa wote waliokusanyika katika Abasia hiyo  kutafakari mada muhimu ya malezi ya kiliturujia ya Watu wa Mungu. Papa anabainisha kwamba katika Barua yake ya Kitume, 'Desiderio Desideravi', ambapo alielezea uzuri wa kina cha kitaalimungu na kiroho cha liturujia, Papa Francisko alisisitiza hitaji la malezi makini na endelevu ya mapadre na walei ili kufufua maisha ya kiliturujia ya Kanisa la ulimwengu wote(Rej. n. 38).

Kipaumbele katika malezi

Baadaye alitukumbusha kwamba aina hii ya malezi "sio utaalamu kwa wataalamu wachache, bali ni mtazamo wa ndani wa Watu wote wa Mungu"(Hotuba kwa Washiriki katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Kipapa la Ibada ya na Nidhamu ya Sakramenti, Februari 8, 2024). Kwa hivyo Papa Leo XIV aliwahimiza, “kuchunguza njia halisi za malezi ya kiliturujia katika kila ngazi ya Mwili wa Kristo. Wakati huo huo, hatupaswi "kuondoa kipaumbele katika malezi ya wale ambao, kwa nguvu ya sakramenti ya Daraja, wameitwa kuwa mafumbo, yaani, kuwashika mkono waamini na kuwasindikiza katika ujuzi wa mafumbo matakatifu."

Baba Mtakatifu aliendelea kudadavua kuwa, fursa za kwanza halisi za malezi ya liturujia hutokea katika desturi yetu ya kukusanyika kila Dominika kusherehekea Misa. Sherehe hizi ni sehemu ya mdundo wa kila mwaka wa liturujia, huku Fumbo la Pasaka likiwa katikati yao. Kwa sababu hii, ni muhimu kwamba nazo ziwe za kina, zikikuza uelewa wa kina zaidi waadhimishaji, unaooneshwa, si tu na mshereheshaji wa liturujia bali pia na kusanyiko lote (taz. Desiderio Desideravi, na 54).

Mafumbo ya Kimungu

Kwa njia hiyo, "kupitia elimu inayofaa na ibada inayoadhimishwa kwa heshima, Wakatoliki wataundwa katika liturujia na kwa liturujia(taz. ibid, n. 34). Zaidi ya hayo, ili kukuza sherehe inayostahili ya mafumbo matakatifu, ni lazima tusisitize hitaji la uaminifu kwa maandiko na vifungu vilivyoidhinishwa. Papa Leo amejikita kutazama Katekesi zake za hivi karibuni zinazoendelea ambazo zinatazama Katiba ya Mtaguso ya Sacrosanctum Concilium kuhusu Liturujia Takatifu,  kwamba “nilielekeza umakini kwenye heshima ambayo wale wote walioitwa kuandaa maadhimisho ya mafumbo ya Kimungu, na hasa mapadre, lazima waoneshe kwa ibada zilizotangazwa na Papa Mtakatifu Paulo VI na Papa Mtakatifu Yohane Paulo II.

Papa amekazia kusema "ni muhimu kwamba heshima hii "ichochee kutoka kwa mtazamo wa ndani wa uwazi na uaminifu kwa Mungu, kuonyesha unyenyekevu mbele ya ukuu wake na uaminifu wa dhati kwa ushirika wa kikanisa"(Katekesi, Mei 27, 2026). Kwa hisia hizi, Papa Leo XIV aliongeza, “ninakabidhi tafakari zenu kwa Maria, Kikao cha Hekima, na kwa hiari yangu nawapatia  wote waliohudhuria mkutano huu Baraka yangu ya Kitume, kama ahadi ya hekima na amani katika Bwana.”

Barua ya Desideri Desideravi

Ikumbukwe, kufuatia na Barua ya Kitume ya Papa Francisko  Desiderio desideravi kuhusu mafunzo ya kiliturujia  kwa watu wa Mungu, iliyochapishwa tarehe 29 Juni 2022, Baraza la Kipapa Ibada, Sakramenti na Nidhamu  za Kanisa ilifanya Mkutano wake mkuu kuanzia tarehe 6-9 Februari 2024, na kutafakari katika kutatufa kung’amua michakato ya mafunzo ya kiliturujia kwa ajili ya wahudumu wa daraja na waamini Walei. Katika kuendeleza tafakari hiyo, Baraza la Kipapa  liliandaa Mkutano kuanzia tarehe 14 hadi 19 Agosti 2026 katika Abasia  ya Kibenediktini ya Mlima Angel, huko Oregon(https://www.mountangelabbey.org) ambapo baadhi ya Makardinali, Maaskofu na Walei, kutoka sehemu mbali mbali na uzoefu wa kikanisa, walialikwa kutafakari pamoja kwa lengo la kufikia mwisho wa mapendekezo shirikishi, ya dhati na ya kiutendaji.

Uchaguzi wa Kimonaki

Kwa mujibu wa waandaaji wanabainisha kuwa “uchaguzi wa Jumuiya ya kimonaki ni kuelezea zaidi juu ya nia ya kutaka kukabiliana katika muktadha wa sala, kuacha nafasi ya kufundwa na liturujia(Desiderio desideravi 55-60). Zaidi ya kuwa Warsha ya mafunzo, itakuwa kipindi cha utambuzi wa kiroho kuhusu mada ya mafunzo ya kiliturujia, kwa ajili ya kuendeleza safari ya mchakato wa  Sacrosanctum Concilium.

BARUA YA PAPA KWA KARD.ROCHE

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

 

14 Agosti 2026, 13:01