Papa Leo XIV:Upendo ni pambo zuri sana la binadamu,tujifunze kwa Mama Maria!

Tunaweza kukutana na uzuri wa Kupalizwa machoni pa wazazi wanaorudi nyumbani kwa watoto wao,wa babu na bibi wanaowatunza wajukuu zao,katika kujitolea kwa vijana na katika kazi ya wanaume na wanawake wanaoleta "kitu kidogo cha Mbingu duniani na dunia kuelekea Mbinguni."Ni katika mahubiri ya Papa wakati wa Misa iliyoadhimishwa katika Parokia ya kipapa ya Mtaakatifu Tommaso wa Villanova,huko Castel Gandolfo,kwa ajili ya sherehe ya Kupalizwa Bikira Maria mbinguni,Agosti 15.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mama Kanisa akiwa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, Baba Mtakatifu Leo XIV, aliongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Parokia ya Mtakatifu Thomas wa Villa Nuova huko Castel Gandolfo,  Jumamosi asubuhi tarehe 15 Agosti 2026. Katika mahubiri yake, Papa awali ya yote aionesha furaha kubwa kuadhimiha sherehe hiyo hata mwaka huu. "Majisterio ya Kanisa yanatufundisha kwamba "Maria, baada ya kukamilisha mwendo wa maisha yake ya kidunia, alichukuliwa mwili na roho katika utukufu wa mbinguni" (PIo XII, Katiba ya Kitume Munificentissimus Deus, Novemba 1, 1950) na inaelekeza kwenye Fumbo hili kama utimilifu wa ukamilifu wa neema ambayo Mungu alimpatia kwa usafi wa moyo.

Papa Leo alisisitiza kwamba "kwa sababu hiyo kazi nyingi za sanaa zinamwonesha, mwishoni mwa maisha yake ya kidunia, kama kijana mzuri,  akiinuliwa kimwili kutoka duniani kuelekea kwenye anga la mbingun," na hii ni kuongozwa na kifungu cha Kitabu cha Ufunuo cha  somo la kwanza: "Mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi chini ya miguu yake" (rej. Ufunuo 12:1), ikimaanisha kwamba katika moyo wa Maria, mbingu na dunia, wakati na umilele, vinakutana." Picha hii, juu juu, inapingana na uzoefu wetu wa kile ambacho tunapitia  kwa miaka. Kadri umri unavyosonga, miili yetu haizidi kuwa migumu, bali inakuwa nzito; Ngozi yetu haizidi kuwa mpya, bali inaonesha dalili za kuzeeka; nywele zetu hazipati tena rangi na kung'aa, bali hugeuka kijivu na kisha kuwa nyeupe.

Papa akihubiri
Papa akihubiri   (@Vatican Media)

Uhusiano wa mwanamke kijana wa ajabu tunayemkuta nyuma ya madhabahu?

Kwa hivyo, Papa aliuliza swali: "tuna uhusiano gani na mwanamke kijana wa ajabu tunayemkuta kachorwa nyuma ya madhabahu zetu? Ili kuelewa hili, ni lazima tuunganishe alama mbili ambazo: mwili usioharibika wa Mama wa Mungu na moyo wake safi. Ni usafi wa roho, ndani ya Maria, kama ilivyo ndani yetu, ambao, kwa neema ya Mungu, humwangazia na kumbadilisha mtu mzima, na kumleta kwenye utukufu wa Mbinguni. Utukufu wa Maria mwilini na rohoni unatufundisha kwamba uzuri wetu wa kweli haujumuishi kuficha ishara za kupita kwa wakati, bali katika kuonyesha, hata katika miili yetu, ishara za upendo usioisha (Rej. 1 Kor 13:8).

Papa Leo XIV alikazia kusema kuwa " Kwa hivyo inatualika kufikiria upya viwango vingi vya uzuri, hasa vya anasa na vya matumizi, ambavyo ulimwengu unatulazimisha, na ambavyo vinahatarisha kutufunga katika hali ngumu, na kutufanya tupoteze nguvu za thamani kwa kile ambacho hakina umuhimu wowote na kisichodumu milele. Kwa uzoefu wa kawaida, tunaweza kukutana na watu ambao nyuso zao zimetiwa alama ya uzee na mateso, lakini wenye uwezo wa kuakisi utulivu, wema, na amani; kama vile tunavyoweza kuwaona wengine, labda wenye kuvutia kwa nje, lakini wagumu na baridi ndani. Na ili kuwa rahisi kuelewa uzuri wa kweli upo wapi na wapi,  bado kuna haja ya uongofu, msamaha, na uponyaji.

Ikiwa tunataka kweli kugundua na kukuza uzuri wa kimungu unaotuzunguka na ambao tumeumbwa kwa ajili yake, na kuusambaza karibu nasi, lazima tujifunze kuusoma katika uso laini wa mtoto na pia katika mikunjo ya mzee, katika uchangamfu wa kijana na pia katika utulivu wa mtu mzima,  katika mapambo ya sherehe na pia katika nguo na vifaa vya kazi. Lazima tusikilize historia za kipekee za mapendo ambayo kila moja ya ukweli huu hutuambia, tukitambua ndani  midomo yake midogo ya mbinguni, Papa alifafanua.

Waamini katika Misa
Waamini katika Misa   (@Vatican Media)

Upendo ni pambo zuri la mwandamu

Papa Leo LXIV akidadvua sura ya Mama Kupalizwa alisema, "Upendo ni pambo zuri zaidi la mwanadamu: upendo unaobadilisha, unaogeuza, unaotukuza, na unaotuinua; ambao hutufanya tuwe wepesi, huru, karibu na Mungu, hata katika nyakati nzuri na mbaya za maisha. Mtakatifu Paulo VI, akitafakari fumbo la Kupalizwa kwa Bikira, alisema kwamba ili kuelewa maana yake, "lazima tufanye maneno tunayotumia katika lugha ya kidunia kuwa bora na kamili [...], kufikiria milele katika umbo dogo" (Mahubiri Agosti 15, 1969). Na kuhusu mkutano huu kati ya usio na mwisho na ulio na kikomo katika Mama wa Mungu, Papa Francisko aliandika: "Maria ndiye anayeweza kubadilisha zizi kuwa nyumba ya Yesu, akiwa na nguo chache za kitoto na mlima wa huruma" ( Evangelii Gaudium, 286).

Muujiza ambao Maria, msichana wa Nazareti, aliupata katika moyo wake usio na dhambi, na ambao ulimleta kwenye utukufu wa Mbinguni, ni mkutano wa mambo yaliyokithiri, kama yeye mwenyewe anavyoshuhudia katika maneno yaliyoongozwa na roho ya Magnificat, ( wimbo wa Sifa) ambao ulisikia katika Injili (taz.Lk 1:46-55). Katika wimbo huu, kupitia maneno ya unyenyekevu ya imani yake, Mama wa Mbinguni anatuzungumzia kuhusu mafumbo makubwa tu: ya Mungu ambaye ndani yake anakuwa mwanadamu ili kuokoa ubinadamu, ya Yule wa Milele anayejidhihirisha ndani yake kwa wakati ili kufungua tena njia ya umilele kwa ajili yetu pia, huku akituonesha, katika hali yake kama "mtumishi mnyenyekevu," "kipimo kidogo" ambacho, kama Mtakatifu Paulo VI alivyosema, sisi pia tunaweza kukutana na Bwana.

Je tunakutana na fumbo wapi?

Kwa hivyo, ukuu wa Fumbo tunalosherehekea Papa Leo XIV aliongeza "haupaswi kutafutwa mbali. Tunaweza kukutana nalo popote pale upendo wa kweli unapopatikana: machoni pa baba na mama wanaorudi nyumbani baada ya kazi ya siku, wakiwa wamechoka lakini wanafurahi kuwa na watoto wao; katika nyuso za babu na bibi ambao, licha ya magonjwa ya uzee, wanawashwa upya kwa nguvu zisizotarajiwa wanapowatunza wajukuu zao; au katika kujitolea kwa vijana wanaojitahidi kukua wakiwa safi na waaminifu, hata wakiwa tayari kwenda kinyume na "kile ambacho kila mtu mwingine hufanya"; hatimaye, katika kazi ya wanaume na wanawake wengi ambao kila siku, kwa imani na kujitolea, huchangia kuleta sehemu ndogo ya Mbingu duniani na duniani Mbinguni.

Misa huko Castel Gandolfo
Misa huko Castel Gandolfo   (@Vatican Media)

Sura nzuri ya Kupalizwa ni ya Kipekee:Matia mfano wa kwanza wa Kanisa

Papa Leo XIV kuwa, sura nzuri ya Kupalizwa ni ya kipekee, inapita kila uwakilishi unaowezekana, na bado, wakati huo huo, inajulikana kwetu: ni ile ya watu ambao wako karibu nasi, hata katika wakati huu, wa kaka na dada ambao tunashiriki nao, kwa imani, sadaka ya kila siku ya maisha yetu. Kwa sababu hiyo, katika mwanamke wa kwenye Ufunuo(Apocalypse),jumuiya ya waamini inajiona yenyewe, na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican  unamtaja Maria kuwa "mfano na mwanzo wa Kanisa, [...] ishara ya matumaini ya uhakika na faraja" (Rej. Lumen Gentium, 68).

Ndani ya Ubinadamu wa Maria, upo wa kwetu pia

Katika ubinadamu wake mtakatifu, kwa neema ya Mungu, kuna wetu pia, sisi pia tuko pale, tumeitwa kuishi utimilifu wa uzima sawa na yeye na kushiriki utukufu wake sawa. Mtakatifu Agostino, akizungumzia ufufuko wa Kristo, aliwaalika Wakristo wa wakati wake kuifanya dira na marejeo ya kuwepo kwao na kusema: "Kristo alifufuka tena asife tena [...]. Badili njia, fuata nuru! Anza kuinuka kutoka mahali pale alipofufuka" (Enarratio katika Zaburi 126, 7). Tufanye mwaliko wake uwe wetu. Tufuate nuru ya Mfufuka, tukibadilisha njia ikiwa ni lazima. Tufanye hivyo, hasa leo, kwa kumtazama Maria, ambaye Mungu alimvika taji ya utukufu mwilini na rohoni, na ambaye alitupa kama Mama, kiongozi, msafiri mwenza, na mlinzi katika njia ya Mbinguni", Papa alihitimisha.

Papa akifukiza ubani Picha ya Bikira Maria
Papa akifukiza ubani Picha ya Bikira Maria   (@Vatican Media)

Maadhimisho ya Misa

Katika adhimisho hilo kulikuwa na Askofu wa Albano Vincenzo Viva, Paroko wa Parokia hiyo Padre  Tadeusz Rozmus, Mkuu wa Kanda la  Shirika la wasalesiani Padre Fabio Attard, Mkuu wa Shirika la Wsalesinai Padre Pierfausto Frisoli na baadhi ya waalikwa, kwa sababu Parokia hiyo imekabidhiwa Shirika la Wasalesiani.

MAHUBIRI YA PAPA MISA CASTEL GANDOLFO AGOSTI 15

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

15 Agosti 2026, 11:15