Papa Leo XIV Ushuhuda wa Umasiha wa Yesu! Kashfa ya Fumbo la Msalaba

Papa Leo XIV anasema, Miujiza na ishara mbalimbali alizozifanya kristo Yesu katika maisha na utume wake, zilimtambulisha kuwa ni Masiha wa Bwana, Mwana wa Mungu aliye hai, chemchemi ya imani na matumaini ya wafuasi wa Kristo Yesu. Lakini ilikuwa ni vigumu sana kwa Mitume wa Yesu na wafuasi wengine kukubali na kupokea Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa wafu uletao maisha na uzima wa milele. Petro ilimbidi kujifunza, kupokea na hatimaye kulishuhudia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 22 ya Mwaka A wa Kanisa inaorodhesha Masharti ya kumfuasa Kristo Yesu yanayojikita kwa namna ya pekee: Katika kujikana nafsi, kujitwika vyema Msalaba wako kila siku na kumfuasa Yesu kwa: njia ya imani, mapendo, utii na unyenyekevu; kwa kujifunga nira yale iliyo laini na nyepesi, tayari kuendelea kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu ambaye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo! Kumkiri Yesu Kristo kama Masiha ni mwaliko wa kutembea kila siku katika njia yake. Si njia rahisi, kwa kuwa ni Njia ya Msalaba, inayowadai wafuasi wake kujikana nafsi, kuchukua Misalaba yao kila siku na kwenda katika njia yake kwa ajili ya ukombozi wao na ule wa jirani zao. Waamini wanapata faraja na matumaini kwa kuwa baada ya hayo yote upo ushindi na thawabu, yaani kupata maisha na uzima wa milele. Miujiza na ishara mbalimbali alizozifanya kristo Yesu katika maisha na utume wake, zilimtambulisha kuwa ni Masiha wa Bwana, Mwana wa Mungu aliye hai, chemchemi ya imani na matumaini ya wafuasi wa Kristo Yesu. Lakini ilikuwa ni vigumu sana kwa Mitume wa Yesu na wafuasi wengine kukubali na kupokea Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa wafu uletao maisha na uzima wa milele. Kwa ufupi, ilikuwa ni vigumu sana kwa Mitume na Wafuasi wa Yesu kukubali na kupokea kwa imani Kashfa ya Fumbo la Msalaba. Kristo Yesu anachukua fursa hii: kutangaza na kuwafafanulia wanafunzi maana ya Kimasiha kwa ishara na miujiza yote hii aliyotenda na hatimaye anawatangazia wazi kwamba imempasa, kuteswa, kufa na kufufuka kwa wafu: “Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka.” Mt 16:21.

Ushuhuda wa Umasiha wa Kristo na Kashfa ya Fumbo la Msalaba
Ushuhuda wa Umasiha wa Kristo na Kashfa ya Fumbo la Msalaba   (vincenzo livieri)

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 30 Agosti 2026. Anasema, maneno haya ya Kristo Yesu yalikwenda kinyume sana na matumaini pamoja na matarajio ya Mitume na Wafuasi wake, kwani wao walimtegemea Masiha wa kisiasa, mwenye nguvu na ushindi, ambaye kwa msaada wake wangewashinda na kuwagalagaza maadui wao. Rej. Zab 108:14). Lakini katika muda wote waliokuwa naye, walikuwa tayari wameshangazwa na matendo na maneno yake mengi. Hata hivyo, ujumbe huu wa hivi punde unazidi kabisa yale yote waliloweza kutarajia. Hasa, Mtume Petro anaonesha kutokubaliana kwake na kumkemea Yesu, akisema: “Hasha, Bwana! Hili halitakupata kamwe.” Mt 16:22. Ni Mtakatifu Petro, Mtume, muda mfupi tu alitangaza kiri kuu ya imani akisema Wewe ni “Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”  Mt 16: 16. Mtume Petro akiwa ameshangazwa na pengine kukata tamaa na yale aliyoyasikia, na kinyume kabisa cha ungamo lake la imani alilokuwa amelitoa hivi punde anamkea Kristo Yesu, akimaanisha kwamba, “Ndiyo, naamini wewe ni Masihi, lakini si kwa namna hii ambavyo ulimwengu unaokolewa.” Mwitikio wake unatokana na ari ambayo bila shaka inatokana na upendo wa kweli lakini unatoa jambo ambalo waamini wanapaswa kulifanyia tafakari. 

Waamini waendelee kubaki waaminifu na watii kwa Baba wa Milele
Waamini waendelee kubaki waaminifu na watii kwa Baba wa Milele   (@Vatican Media)

Kwani kwa hakika, anasema Baba Mtakatifu Leo XIV “si rahisi kwetu sisi pia kuelewa na kukubali njia za Mungu, hasa zinapofautiana sana na njia zetu. Katika nyakati kama hizo, hutokea jaribu kinyume na mantiki ya imani, kiasi cha kufikiri kwamba Kristo Yesu amekosea, au mbaya zaidi, kwamba hawasikilizi au hawajali hata kidogo, anawaangalia kama “nyanya mbichi.” Tunapokabiliwa na hali hii ya kutokuwa na uhakika, Petro Mtume ingawa anaweza kuwa mtu wa kuchukua hatua za haraka bila kutafakari sana Baba Mtakatifu Leo XIV anasema anatufundisha mambo mawili muhimu: Jambo la kwanza ni kutokatiza kamwe sala na mazungumzo na Kristo Yesu hata katika nyakati kama hizi, na badala yake waamini wawe ujasiri wa kumwelezea Kristo Yesu ugumu wanaokumbana nao wa kuelewa yale anayowataka kutenda. Jambo la pili, kwa waamini ni kutohukumu kamwe matendo ya Mungu, bali kusikiliza kwa unyenyekevu, katika sala na tafakari ya kina yale anayowafunulia kupitia matendo yake, hata pale yanapokwenda kinyume na matarajio yao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Petro Mtume, anaonesha ukuu wake kama Kiongozi mkuu wa Mitume kwa majibu kutoka kwa Kristo Yesu: "Nenda nyuma yangu, Shetani!" Mt 16:23.

Waamini wakisalimiana na Papa Leo XIV mjini Castel Gandolfo
Waamini wakisalimiana na Papa Leo XIV mjini Castel Gandolfo   (@Vatican Media)

Kristo Yesu anatumia fursa hii kumwelezea Mtakatifu Petro pamoja na Mitume wengine kwamba, ili kufuata nyayo zake, ni lazima wajikane wenyewe, wachukue Msalaba wao, na kumfuata.” Mt 16: 24. Mtakatifu Petro alifanya hivyo hasa: baada ya kumsikiliza, alikubali changamoto hiyo na kubaki mwaminifu kwa maneno ya Kristo Yesu ambaye alikuwa amemtambua kama Mkombozi wake katika maisha yake yote, hata kufikia hatua ya kuuawa kwa ajili ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Kristo Yesu awajalie katika maisha yao imani na sala pamoja na unyofu uleule ambao Mtakatifu Petro aliuonesha kwa kumwelezea kwa unyenyekevu na upole, hisia zao za kweli, hata pale mioyo yao ikiwa na mkanganyiko; wakati huo huo, wafuasi wa Kristo Yesu, wajaliwe utayari ule ule wa kukubali yale ambayo Kristo Yesu anawataka kutenda, hata pale yanapozidi matarajio yao. Bikira Maria aliyebaki mwaminifu na mtiifu kwa mipango ya Mungu katika maisha yake, kiasi hata cha kuthubutu kusimama chini ya Msalaba wa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu awasaidie waamini.

Kashfa ya Msalaba
30 Agosti 2026, 12:40

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >