Mtakatifu Monica na Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa; ni watakatifu ambao waliunganishwa hapa duniani kwa vifungo vya kifamilia na mbinguni kwa hatima moja ya utukufu. Mtakatifu Monica na Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa; ni watakatifu ambao waliunganishwa hapa duniani kwa vifungo vya kifamilia na mbinguni kwa hatima moja ya utukufu.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Wakatifu Monica na Augustino: Waliunganishwa na Familia na Utukufu Mbinguni

Baba Mtakatifu Leo XIV: Tarehe 27 Agosti ni kumbukumbu ya Mtakatifu Monica na tarehe 28 Agosti ni kumbukumbu ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa; watakatifu ambao waliunganishwa hapa duniani kwa vifungo vya kifamilia na mbinguni kwa hatima moja ya utukufu. Mfano wao na uamshe ndani ya kila mwamini hamu ya dhati na ya shauku ya kutafuta ukweli wa Injili, ili waweze kuutangaza na kuushuhudia kwa furaha katika maisha yao ya kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV ana uhusiano wa karibu sana wa maisha ya kiroho na kihistoria na Mtakatifu Monica, Mama yake Mtakatifu Augustino Askofu wa Hippo, kutokana na yeye mwenyewe kuwa mtawa wa Shirika la Waagustino (Order of St. Augustine) kabla ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 26 Agosti 2026 imehitimisha Katekesi na tafakari juu ya: “Sacrosanctum concilium” yaani Katiba “Juu ya Liturujia” ambayo inaelezea kanuni za jumla za marekebisho na ukuzaji wa Liturujia Takatifu; Fumbo Takatifu la Ekaristi, Sakramenti nyingine na visakramenti; Liturujia ya Vipindi; Mwaka wa Liturujia wa Kanisa, Muziki Mtakatifu; na hatimaye, ni Sanaa Takatifu na Vifaa vitakatifu pamoja na kuelezea sababu zilizowafanya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kufanya mabadiliko makubwa katika Liturujia ya Kanisa, ili kuwawezesha waamini kuwa na ushiriki hai, mkamilifu na wenye tija kwa Taifa zima la Mungu katika adhimisho la Ekaristi Takatifu. Ushiriki huu unaambatana na ufahamu mkubwa wa Fumbo linaloadhimishwa na uhusiano wake na maisha ya kila siku. Kumbe, waamini hawapaswi kushiriki Liturujia ya Kanisa kama wageni au watazamaji bubu, bali washiriki hai na kwa uchaji. Rej. Sacramentum caritas, 52.

Tarehe 27 Mt. Monica & Tarehe 28 Mt. Augustino Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Tarehe 27 Mt. Monica & Tarehe 28 Mt. Augustino Askofu na Mwalimu wa Kanisa   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 27 Agosti, Mama Kanisa anafanya kumbukumbu ya Mtakatifu Monica na tarehe 28 Agosti ya kila mwaka ni kumbukumbu ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa; watakatifu ambao waliunganishwa hapa duniani kwa vifungo vya kifamilia na mbinguni kwa hatima moja ya utukufu. Mfano wao na uamshe ndani ya kila mwamini hamu ya dhati na ya shauku ya kutafuta ukweli wa Injili, ili waweze kuutangaza na kuushuhudia kwa furaha katika maisha yao ya kila siku. Itakumbukwa kwamba, Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 27 Agosti anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Monika, Mama yake Mtakatifu Augustino Askofu na Mwalimu wa Kanisa aliyekumbana na changamoto za maisha wakati wa ujana wake ambaye anaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 28 Agosti. Augustino alizaliwa na kulelewa katika familia ya Kikristo, lakini alipokuwa kijana mbichi kabisa alichagua kuishi mbali na Mwenyezi Mungu. Alijitumbukiza, akazama na hatimaye kumezwa katika maisha ya anasa, alifuata tamaa za dunia, na mara nyingi hakuyazingatia mafundisho aliyofundishwa na Mama yake Mzazi, Mtakatifu Monika. Augustino mwenyewe alikiri kwamba wakati wa ujana wake alifanya makosa mengi. Aliishi na mwanamke bila kufunga ndoa na akapata mtoto wa kiume aliyeitwa Adeodatus yaani “Zawadi ya Mungu.”

Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mt. Augostino
Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mt. Augostino   (@Vatican Media)

Ingawa alikuwa msomi mwenye maarifa na akili nyingi, moyo wake haukuwa na amani wala utulivu kwa sababu alikuwa bado anatafuta ukweli na furaha ya kweli. Mama yake Monica hakukata tamaa, alimlilia sana Mwanaye mpendwa, akamwombea na kumsindikiza kwa ushauri, usikivu mwanana, machozi na kwa mahangaiko makubwa. Na kwa sala za Mtakatifu Monika, Augustino akatubu na akamwongokea Mungu, akabatizwa, na hatimaye, kuachana na maisha yake ya zamani yaliyochakaa kama “jani la mgomba wa ndizi” na kuanza kumfuata na hatimaye kutembea katika mwanga wa Kristo Yesu Mfufuka kwa moyo wote. Baadaye akawa Padre, kisha Askofu wa Hippo, akabahatika kuwa ni Mwalimu wa Kanisa maarufu katika historia ya Kanisa. Yule kijana aliyekuwa anaishi mbali na Mungu akaja kuwa mtakatifu anayeheshimiwa na kuthaminiwa na watu wa Mungu sehemu mbalimbali za duni. Kwa sala na maombezi kwa mume wake, akabatizwa na hatimaye kufa kifo chema kunako mwaka 371.

Papa Leo XIV Hija ya Kitume Nchini Algeria
Papa Leo XIV Hija ya Kitume Nchini Algeria   (@Vatican Media)

Kumbukumbu hii ni fursa ya kujitahidi kunafsisha furaha ya Injili katika uhalisia wa maisha ya waamini, tayari kujitoa na kujisadaka ili kuwa ni chemchemi ya furaha kwa ndugu, jamaa na jirani; zawadi kubwa kwa Mama Kanisa na jamii katika ujumla wake. Pili, hii ni fursa ya kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa familia kama shule ya upendo, huruma, haki, amani na ukarimu. Kumbukumbu ya Mtakatifu Monica ni mwaliko kwa waamini kuwa na utulivu katika maisha ya sala; kuendelea kujikita katika wema na fadhila, silaha madhubuti katika mapambano dhidi ya nguvu za Ibilisi, Shetani. Mama Monica alipata heshima kubwa kutokana na uvumilivu wake, udumifu katika maisha ya sala na hivyo kuwa ni mfano bora wa kuigwa na wanawake wote katika maisha na utume wao ndani ya familia, jamii na Kanisa katika ujumla wake. Itakumbukwa kwamba, Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, uhai na upendo kielelezo cha ukomavu wa imani. Tatu, waamini wanakumbushwa kwamba, Sakramenti ya Ndoa inapyaisha upendo wa kibinadamu. Kumbe, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linaendelea kutambua dhamana, amana na mchango wa wanawake katika maisha na utume wake, huku likiendelea kutoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwa familia na vijana.

Mtakatifu Monica
27 Agosti 2026, 14:58