Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria Akutana na Papa Leo XIV
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 24 Julai 2025 amekutana na kuzungumza na Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria ambaye baadaye, alibahatika kukutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Monsinyo Daniel Pacho Katibu mkuu msaidizi wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu Leo XIV na mgeni wake, wameridhishwa na uhusiano mwema wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili sanjari na mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Algeria.
Baadaye, viongozi hawa wawili wamejielekeza zaidi katika masuala ya siasa za ndani na hasa zaidi umuhimu wa majadiliano ya kidini katika kujenga na kukuza haki, amani na maridhiano kati ya watu. Wamekazia pia ushirikiano wa kitamaduni kama nyenzo msingi ya kukuza na kujenga amani na udugu wa kibinadamu sehemu mbalimbali za dunia.