Malawi:Jiwe la Msingi kwa ajili ya Ujenzi wa Ubalozi wa Vatican lilibarikiwa huko Lilongwe
Vatican News
Jiwe la msingi la Ubalozi wa Vatican wa baadaye nchini Malawi uliwekwa Septemba 22, 2025, katika mji mkuu, Lilongwe. Askofu mkuu Gian Luca Perici ambaye ni Balozi wa Vatican nchini Zambia na Malawi alibariki jiwe la msingi la Makao Makuu mapya ya Uwakilishi wa Kipapa. Hadi sasa, ujumbe wa kidiplomasia wa Vatican nchini Malawi ulikuwa na makao yake mjini Lusaka, Zambia. Kwa hiyo ujenzi wa Ubalozi wa Vatican katika moyo wa nchi unawakilisha hatua muhimu, inayolenga kuimarisha uhusiano kati ya Vatican na Malawi. "Nyumba ya Papa" haitakuwa kitovu cha shughuli za kidiplomasia tu, bali pia ni ishara halisi ya ushirika na ukaribu, mahali pa kukutana na mazungumzo katika huduma ya amani na maendeleo.
Sherehe hiyo ilihudhuriwa na wawakilishi wengi wa kikanisa na mamlaka za kiraia. Waliowakilisha Kanisa Katoliki ni Monsinyo Martin Anwel Mtumbuka, Askofu wa Karonga na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi (MCCB), Askofu Mkuu George Desmond Tambala wa Lilongwe, na Monsinyo Peter Sababu, Askofu wa Dedza. Wawakilishi wa taasisi hizo walihudhuria hafla hiyo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Halmashauri ya Manispaa ya Lilongwe, Kamisheni Kuu ya Tanzania, Baraza la Taifa la Sekta ya Ujenzi, na Kampuni ya Terrastone Limited inayohusika na ujenzi wa jengo hilo.