Askofu Mkuu Gabriele Caccia, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye  Baraza la Umoja wa Mataifa. Askofu Mkuu Gabriele Caccia, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa. 

Vatican: UN: Achana na"mantiki ya uwongo"wa mbio za silaha

Askofu Mkuu Caccia,Mwakilishi wa kudumu wa Vatican katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,(UN)alikemea ongezeko la matumizi ya kijeshi duniani,ambayo mwaka 2024 yalifikia dola trilioni 2.7 "isiyokubalika:""Roho ya diplomasia na ushirikiano wa pande nyingi,iliyoundwa kwa uangalifu ili kulinda wanadamu dhidi ya janga la vita,inazidi kufichwa.

Vatican News

Ni muhimu kuachana na "mantiki potofu" ya mbio za silaha na kuzuia nyuklia na badala yake kukumbatia njia ya mazungumzo na kupokonya silaha. Hayo yalisisitizwa na Askofu Mkuu Gabriele Caccia, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Baraza la Umoja wa Mataifa ambaye kwa mara nyingine alitoa wito wa kusitishwa kwa "mbio za silaha" wakati wa hotuba yake tarehe 17 Oktoba 2025 kwenye mjadala mkuu wa Kamati ya kwanza ya kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kugundua tena Utamaduni mbalimbali

Askofu Mkuu huyo alibainisha kwamba, miaka 80 baada ya uharibifu wa Hiroshima na Nagasaki na kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, "roho ya diplomasia na ushirikiano wa pande nyingi, iliyobuniwa kwa uangalifu sana kulinda ubinadamu kutokana na janga la vita, inazidi kufichwa na kurudi kwa nguvu na hofu kama njia za kusuluhisha mizozo." Akinukuu maneno ya Papa Leo XIV  kwenye mkutano wa mashirika ya kutoa misaada kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki  mnamo Juni iliyopita, Askofu Mkuu Caccia auliza hivi: “Tunawezaje kuendelea kusaliti tamaa ya watu wa ulimwengu ya kutaka amani kwa propaganda kuhusu mkusanyiko wa silaha, kana kwamba ukuu wa kijeshi utasuluhisha matatizo badala ya kuchochea chuki zaidi na tamaa ya kulipiza kisasi?” Pesa zilizotumika kununua silaha, ambazo zilifikia dola trilioni 2.7 "zisizokubalika" mnamo 2024, zinaweza kutumika kujenga shule na hospitali mpya badala ya kuziharibu.

Kiungo hatari kati ya silaha na AI

Askofu Mkuu Caccia pia alionesha wasiwasi wake kuhusu "shindano jipya la silaha lililowekwa alama na ujumuishaji wa Akili Unde (AI) katika mifumo ya kijeshi yenye uwezo mkubwa wa uharibifu,"  na hivyo alitoa wito kwa mataifa yenye silaha za nyuklia kuheshimu wajibu wao chini ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), hasa kwa kuzingatia Mkutano ujao wa Mapitio.

Utumiaji wa Akili Unde AI, kwa silaha za kawaida, zaidi ya hayo, "huleta changamoto kubwa ambayo lazima iamshe ufahamu wa kimaadili wa jumuiya nzima ya kimataifa" kwani silaha hizi zinafanya kazi "bila udhibiti wowote wa kibinadamu" na kwa hiyo "kuvuka mipaka yote ya kisheria, usalama, kibinadamu, na zaidi ya yote, mipaka ya kimaadili."

Mabadiliko ya mtazamo inahitajika

"Cha  kusikitisha, watu wengi wasio na hatia wanaendelea kuteseka na matokeo mabaya ya silaha za milipuko, ambayo yanazidi kutumika kiholela katika maeneo yenye watu wengi, pamoja na tishio la mabomu ya kutegwa ardhini ambayo yanaendelea kulemaza na kuua kwa muda mrefu baada ya migogoro kumalizika,” aliendelea askofu mkuu na kukemea biashara haramu ya silaha ndogo ndogo. "Kinachohitajika," Askofu Mkuu Caccia alihitimisha, "ni mabadiliko ya kimsingi katika mtazamo: kuacha kutegemea silaha ili kujenga amani kwa njia ya mazungumzo, kwa kuzingatia mtazamo unaozingatia ubinadamu ambao umekita mizizi katika utu na heshima kamili kwa haki za binadamu, na kujitolea kwa maendeleo fungamani ya binadamu."

18 Oktoba 2025, 15:31