Rais Gabriel Boric Font wa Chile Akutana na Papa Leo XIV Mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 13 Oktoba 2025 alikutana na kuzungumza na Rais Gabriel Boric Font wa Chile, ambaye baadaye alibahatika kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa.
Katika mazungumzo yao ya faragha, viongozi hawa wawili wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Chile. Wamegusia pia kuhusu mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Chile katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Baba Mtakatifu Leo XIV pamoja na mgeni wake, wamegusia pia hali ya kisiasa na kijamii nchini Chile mintarafu mapambano dhidi ya baa la umaskini, wimbi la wakimbizi na wahamiaji; kanuni maadili na utu wema.