Ukumbi  Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana, Roma Ukumbi Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana, Roma 

Wamisionari wa matumaini watakutana katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana

Ulimwengu wa Kimisionari unaadhimisha Jubilei yake, tarehe 4-5 Oktoba 2025 katika Mkutano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana,Roma.“Utume wa Watu leo hii” ndiyo mada ya tafakari ya Mkutano ambapo Kardinali Tagle,Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Kwanza na Makanisa Maalumu na Chansela wa Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana,atafungua rasmi mkutano huo.

Sr. Christine Masivo CPS

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari FIDES), limebainishwa kwamba, Roma inakaribisha wamisionari kutoka ulimwenguni kote ambao watakusanyika katika mji wa Vatican kusherehekea Jubile yao tarehe 4 na 5 Oktoba 2025. Katika kuadhimisha Dominika ya Kimisionari Ulimwenguni, Papa Francisko alichagua kauli mbiu:  “Wamisionari wa matumaini kati ya watu,” sambamba na Jubilei ya Matumaini kwa mwaka 2025. Tukio hili la siku mbili, ambalo limetayarishwa kwa muda mrefu katika majimbo mbalimbali duniani, limetolewa kwa ajili ya wamisionari, ambao ni “watu wa majira yakuchipuka, wakiwa na mtazamo  daima wenye matumaini ya kuwashirikisha wote,” kama sala iliyotungwa kwa ajili ya Jubilei yao inavyosema.

Kushiriki Katekesi ya Papa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro: saa 4.00

Ratiba ya tukio kwa njia hiyo inabainisha kwamba: Jumamosi, asubuhi tarehe 4 Oktoba 2025, Papa Leo XIV atafungua Jubilei kwa Katekesi yake saa 4.00 kamili masaa ya Ulaya na ambapo itafuatiwa na hija kwenye Mlango Mtakatifu wa Basilika ya Mtakatifu Petro.

Nyimbo, ngoma na hotuba

Katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, cha kihistoria katika malezi ya wakleri wamisionari na wanafunzi kutoka Makanisa mahalia, alasiri, kitaandaa Mkutano wa Kimataifa wa Kimisionari katika Ukumbi Mkuu kuanzia saa 11:00 hadi 12:45 jioni. Hata hivyo Mkutano huo utatanguliwa na wakati wa nyimbo na ngoma za  kutumbuiza zilizoandaliwa na Watawa kutoka Mashirika tofauti wa Chuo cha Mater Ecclesiae na wanaseminari wa Chuo cha Kipapa cha Urbaniana, saa 10.30 jioni.

Kardinali Tagle: Utume wa Watu Leo hii

“Utume wa Watu leo hii," ndiyo mada ya tafakari ya Mkutano ambayo Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Kwanza na Makanisa Maalumu na Chansela Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, ambaye atafungua rasmi mkutano huo.

Kardinali Marengo: Kunong'oneza Injili zaidi ya mipaka na vizuizi

Baada ya hotuba hiyo atafuata Kardinali Giorgio Marengo, Mmisionari wa Consolata na Msimamizi wa Kitume wa Ulaan Baatar, huko Mongolia, atazungumza. Kardinali Marengo atawasilisha mada yenye kichwa: “Kunong’oneza Injili zaidi ya mipaka na vizuizi,” ambayo inabeba mada,  ya mpendwa wake, katika kutangaza Injili kama “minong’ono” katika nchi hizi anazofanyia utume wake

Ushuhuda wa Sr Djeba: Furaha na matumaini miongoni mwa watu

Baada ya mapumziko mafupi ya muziki, Watakaoshiriki kwenye Ukumbi Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana watasikiliza ushuhuda wenye nguvu wa Sista Suzanne Djebba, Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Immakulata(PIME) kuhusu mada "Furaha na Matumaini katika Utume Miongoni mwa Watu. Kushirikishana."

Padre Albanesi:Changamoto za Utume leo hii

Baadaye Padre Giulio Albanese, Mmisionari wa Comboni, na mwandishi wa habari, na Mkurugenzi wa Ofisi ya Mawasiliano ya Kijamii na Ofisi ya Ushirikiano wa Kimisionari ya Vicariate ya Roma, atatoa hotuba ya kufunga inayohusu: "Changamoto za Utume Leo hii." Wakati Padre Anh Nhue Nguyen (OFMConv,) Katibu Mkuu wa Umoja wa Wamisionari wa Kipapa atasimamia mkutano huo. Kufuatia mawasilisho hayo, ataacha muda wa maswali na majadiliano na washiriki wa Mkutano huo.

Mkutano pia kwa njia ya Zoom

Mkutano utaweza kufuatiliwa moja kwa moja kupita mtandaoni katika jukwaa la Zoom, ambalo pia litatoa tafsiri kwa wakati mmoja katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kihispania. Kwa Kurugenzi za Kitaifa za Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa yatakayoshiriki Jubilei hiyo yenye wajumbe wengi siku ya Jumamosi, tarehe 4 Oktoba 2025, baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Kimataifa, Misa za kimisionari/mikesha ya sala inapangwa kati ya saa 1:15 jioni na 8:45 usiku, ikigawanyika kufuatia na vikundi vya lugha, katika  vikanisa  kadhaa vya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro.

Jumuiya zote za kitaza katika majimbo yote ulimwengini zinaalikwa kushiriki  na Parokia

Jumuiya zote za Kitawa za kimisionari zilizopo katika majimbo, jumuiya na parokia mbalimbali duniani zinaalikwa kujumuika kiroho katika mikesha hii ya maombi ya umisionari, kwa ushirika na vikundi vilivyopo mjini Roma, ili kuadhimisha Jubilei ya Ulimwengu wa Kimisionari kwa kiwango cha kimataifa.

Jumamos 4 Oktoba saa 3.00 usiku masaa ya Ulaya,Rozari Takatifu katika Uwanja wa Mtakatifu Petro

Programu rasmi itaendelea Jumamosi, Oktoba 4, saa 3:00 usiku masaa ya Ulaya ambapo ni saa 4.00 masaa ya Afrika Mashariki na Kati, kwa Rozari ya kimisionari ya Kimataifa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro. Siku inayofuata, Dominika tarehe 5 Oktoba 2025, itaadhimishwa Misa Takatifu, itakayoongozwa na Papa Leo XIV, saa 4.30 asubuhi masaa ya Ulaya. Alasiri ya Dominika tarehe 5 Oktoba, kati ya Saa 8:30 mchana na Saa 1:00 jioni, itafanyika Siku kuu ya Watu "Wahamiaji na Wamisionari wa Matumaini Miongoni mwa Watu," iliyoandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika bustani za Castel Sant'Angelo, kuhitimisha Jubilei ya Ulimwengu wa Kimisionari.

02 Oktoba 2025, 17:14