2025.11.23 Santa Messa per il Giubileo dei Cori e delle Corali

Katika Dilexi Te:Kanisa limeona ukombozi wa wanyonge kuwa ishara ya Pasaka

Hata leo,bado kuna mamilioni ya watu;watoto,wanaume kwa wanawake,wa karne zote,wanaonyimwa uhuru wao na kulazimishwa kuishi katika hali iliyo sawa na utumwa.Lakini kuna urithi wa utume kwa wenye kuhitaji unaoendelezwa na taasisi na mashirika mbalimbali yaliyoko vijijini,sehemu zenye migogoro na katika misafara ya uhamiaji.Kanisa linapovunja minyororo mipya inayowafunga maskini,linakuwa ishara ya Pasaka.

Padre Angelo Shikombe - Vatican.

Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya wosia wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assis. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tuendelee sura ya tatu inayoelezea Kanisa lililo kwa ajili ya maskini. 

Ndugu msomaji/msikilizaji, katika kuelezea kipengere cha kuteswaa kwa maskini, tangu nyakati za mitume, Kanisa limeona ukombozi wa wanyonge kuwa ishara ya ufalme wa Mungu. Yesu mwenyewe alitangaza hivyo mwanzoni mwa huduma yake ya halaiki pale aliposema: “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenipaka mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kutangaza kufunguliwa kwa wafungwa” (Lk 4:18).  Wakristo wa mwanzo, hata katika hali ngumu, walisali na kuwasaidia ndugu waliokuwa wafungwa, kama tunavyosoma katika kitabu cha Matendo ya Mitume (taz. 12:5; 24:23) na sehemu mbalimbali za maandishi ya Mababa. Dhamira hii ya ukombozi imeendelea kwa karne nyingi kupitia vitendo madhubuti, haswa wakati janga la utumwa na kifungo lilipoikumba jamii nzima.

Ndugu Msomaji/msikilizaji, kati ya mwishoni mwa karne ya kumi na mbili na mwanzoni mwa karne ya kumi na tatu, wakati wakristo wengi wakitekwa katika vita kwenye bahari ya Mediterania, mashirika mawili ya kidini yaliundwa: Shirika la ibada kwa Utatu Mtakatifu na lile shirika la wafungwa; yaani shirika la waamini wa Utatu lililoanzishwa na Mtakatifu Yohane wa Matha na Mtakatifu Felixi wa Valois, na shirika la Bikira Maria wa Huruma (Mercedarians), lililoanzishwa na Mtakatifu Peter Nolasco akisaidia na Mtakatifu Raymond mdomenikani wa Peñafort. Jumuiya hizi za wawekwa wakfu zilianzishwa zikiwa na karama mahususi ya kuwaweka huru wakristo waliokuwa watumwa, kuwagawana mali zao na wafungwa, na mara nyingi kutoa maisha yao wenyewe kuwa mbadala kwa wafungwa. Shirika la Utatu, wakiwa na kauli mbiu yao isemayo: “Gloria tibi Trinitas et captivis libertas” yaani “utukufu kwako, ee Utatu, na uhuru kwa wafungwa”, na Wamerkedari, walioongeza nadhiri ya nne katika mashauri ya Injili ya umaskini, usafi wa moyo na utii, walishuhudia kwamba upendo ni tendo la kishujaa. Ukombozi wa wafungwa ni mwonekano wa pendo la Utatu Mtakatifu: Mungu ambaye huwaseta huru sio tu kutoka utumwa wa kiroho bali pia kutoka ukandamizaji wa kijamii. Kitendo cha kumwokoa mtu kutoka utumwani na kifungoni kinaonekana kuwa mwendelezo wa sadaka ya ukombozi wa Kristo ambaye damu yake imegharimia ukombozi wetu (rej. 1Kor 6:20). Chimbuko la jumuiya hizi za maisha ya kiroho linatokana na tafakari za fumbo la msalaba, ambapo Kristo kwa hadhi yake ni mkombozi wa wafungwa, na Kanisa, lililo mwili wake, huendeleza fumbo hili kwa vizazi na vizazi.

Ndugu msomaji/msikilizaji, watawa hawautazami ukombozi kama sera ya kisiasa au kiuchumi, lakini kama tendo la kiliturujia, na kisakramenti cha kujitoa kwao wenyewe kuwa sadaka. Wengi walitoa maisha yao wenyewe kufidia nafasi za wafungwa, ili kutimiza amri ya Mungu inayosema: “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yh. 15:13). Mapokeo ya mashirika haya hayakufikia ukomo, kinyume chake, yalivuvia aina mpya za kupambana na utumwa mamboleo: biashara haramu ya binadamu, kazi za kushurutishwa, utumwa wa ngono na mifumo mbalimbali tegemezi. Upendo wa kikristo hukomboa unapomwilishwa. Vile vile, ni utume wa Kanisa hasa linapokuwa aminifu kwa Bwana wake, na wakati wote hutangaza ukombozi. Hata leo, bado kuna mamilioni ya watu; watoto, wanaume kwa wanawake, wa karne zote, wanaonyimwa uhuru wao na kulazimishwa kuishi katika hali iliyo sawa na utumwa”. 

Urithi wa utume huu unaendelezwa na taasisi na mashirika mbalimbali yaliyoko vijijini, sehemu zenye migogoro na katika misafara ya uhamiaji. Kanisa linapovunja minyororo mipya inayowafunga maskini, linakuwa ishara ya Pasaka. Hatuwezi kuhitimisha tafakari hii juu ya watu walionyimwa uhuru wao bila kuwataja hao walioko magerezani na mahabusu. Katika suala hili, tunakumbuka maneno ambayo Papa Francisko aliyoutubia kundi la wafungwa akisema: “Kwangu mimi, kuingia gerezani ni fursa muhimu, kwa sababu gereza ni mahali pa utu kamili... Utu unaojaribiwa, wakati mwingine umechakazwa na matatizo, hatia, hukumu, kutokuelewana, mateso, lakini wakati huo huo utu huo, umejaa nguvu, hamu ya msamaha, na tamaa ya ukombozi” Tamaa hii, miongoni mwa mambo mengine, imechukuliwa na mashirika yanayojitolea kutoa fidia ya wafungwa kama huduma ya upendeleo kwa Kanisa. Kama vile Mtakatifu Paulo alivyotangaza: “Kwa ajili ya uhuru Kristo ametuweka huru” (Wagalatia 5:1) Uhuru huu si wa ndani tu: unajidhihirisha katika historia kama upendo ambao anatujali na kutuweka huru kutoka katika kila kifungo cha utumwa.

Ndugu msomaji/msikilizaji, Kanisa ni shahidi wa kwanza wa umaskini wa kiinjili ambaye ndani yake anatimiza hutume huu kupitia utume wa mashirika mbalimbali. Tunapotafakari juu ya mashahidi wa umaskini wa kiinjili, ikumbukwe kuwa, katika karne ya kumi na tatu, wakati wa ukuaji wa miji na malimbuko ya mali huku zikiibuka aina mpya za umaskini, Roho Mtakatifu aliibua aina mpya ya wakfu katika Kanisa: Shirika la wamendicanti lilijihusisha na kusaidia ombaomba. Tofauti na mashirika tangulizi ya kimonaki, waandamizi waliazimia kuishi maisha ya kuzunguka, bila ya kumiliki mali binafsi au kijumuiya, wakijikabidhi wenyewe kwa uweza wa Mungu. Hawakuhudumia tu maskini, bali waliishi na masikini pamoja. Waliona miji kama jangwa jipya na waliotengwa kama walimu wapya wa kiroho. Mashirika haya, kama vile Wafransiskani, Wadominikani, Waagustiniani na Wakarmeli, waliwakilisha mapinduzi ya kiinjili, ambamo maisha ya kifukara yakiwa ishara ya utume wa kinabii, yakihuisha jumuyiya za kikristo zifanane na jumuiya ya kwanza ya kikristo (rej. Mdo 4:32). Ushahuda wa wamendikanti ulipinga utajiri wa makasisi na ubaridi wa jamii za mjini. Enzi hizo, Mtakatifu Fransisko wa Asizi alikuwa chipkizi la maisha ya kiroho. Kwa kukumbatia umaskini, yeye alitaka kumwiga Kristo, ambaye alikuwa maskini, mtupu, na msulibiwa. Katika kanuni zake, aliomba kuwa “ndugu haipaswi kumiliki kitu chochote; nyumba, wala mahali, wala kitu kingine chochote. Na kama mahujaji na wageni katika dunia hii, watawa wamtumikie Bwana katika umaskini na unyenyekevu, wazunguke huku na huko wakiomba kwa ujasiri, wala usiaibike, kwa sababu Bwana amejifanya maskini kwa ajili yetu katika ulimwengu huu”.

Maisha yake yalikuwa ya kujitoa: kutoka ikulu hadi kwa mwenye ukoma, kutoka kwa ufasaha hadi ukimya, kutoka milki hadi kujitoa zawadi iliyo timilifu. Francisko hakuanzisha mashirika ya utoaji wa huduma za kijamii, bali alianzisha udugu wa kiinjili.  Katika maskini, aliiona sura hai Bwana katika maisha ya kaka na dada. Utume wake ulikuwa kukaa nao kati yao, na alifanya hivyo kwa mshikamano ulioshinda utengano kwa upendo wa huruma. Utakatifu wake ulikuwa wa kimahusiano, uliomfanya kuwa jirani yao, aliye sawa na pengine mdogo kuliko wao. Utakatifu wake ulitokana na kusadiki kwamba Kristo anaweza kupokelewa kweli kwa kujitoa kwa ukarimu sadaka kwa ndugu.

Ndugu msomaji/msikilizaji, Mtakatifu Clara wa Assisi, alivutwa sana na mmfano wa Mtakatifu Francisko, alianzisha shirika la wanawake maskini, ambalo baadaye liliitwa masista wadogo, au “Masikini wa Klara. Mapambano yake ya kiroho yalihusisha uimara na uaminifu wa kanuni bora ya umaskini. Yeye alikataa upendeleo wa Papa ambao ungeweza kumhakikishia usalama wa mali kwa ajili ya monasteri yake. Kutokana na uhodari wake alitunukiwa na Papa Gregory IX kile kiitwacho Privilegium Paupertatis, hati inayothibitisha kuishi bila mali yeyote. Chaguo hili lilionesha imani yake kamili kwa Mungu na ufahamu thabiti wa kuishi umaskini kwa hiari ikiwa ni aina ya uhuru na unabii. Mtakatifu Clara aliwafundisha wafuasi wake kuwa; Kristo ndiye aliyekuwa urithi wao wa pekee na kwamba hakuna kitu ambacho kilipaswa kuficha ushirika wao pamoja naye. Sala na kilio chake cha ndani vilikuwa dhidi ya malimwengu na ulinzi wa kimya kimya wa maskini na waliosahaulika.

Kwa hiyo ndugu mpendwa msomaji/msikilizaji, kanuni za wamendicanti zilikuwa jibu hai la utengano na kutokujali. Hawakufanya mapinduzi ya kijamii, lakini ulikuwa uongofu wa mtu binafsi na wa ki-jumuiya katika kujenga ufalme wa Mungu. Kwao, umaskini haukuwa matokeo ya ufukara au uhaba wa vitu, bali lilikuwa chaguo huru kwa lengo la kujishusa ili waweze kuwakaribisha wadogo. Kama vile Thomas wa Celano alivyosema kuhusu Francisko kuwa: “Alionesha namna alivyowapenda sana maskini”. Aliwapenda maskini kiasi cha kuvua nguo zake na kuwavisha, alitafuta kufanana nao”.  Ombaomba wakawa ishara ya mahujaji, Kanisa nyenyekevu na la kidugu. Kuishi kati ya maskini haibadili maana ya fadhila ya umaskini, bali ni kielelezo cha utambulisho wao wa kweli. Wanatufundisha kwamba Kanisa ni nuru linapojivua kila kitu, na utakatifu wake huenea moyoni mwa wanyenyekevu walio wadogo kati yetu.

Ndugu msomaji/msikilizaji, tumefikia hapa kwa leo katika mwendelezo wa barua ya kitume, usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo.

Dilexi Te 9
27 Novemba 2025, 09:32