Katika Dilexi Te:Ugawanaji wa mahitaji hutokana na pendo la kimungu
Na Padre Angelo Shikombe – Vatican.
Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya wosia wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assis. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “Nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tuendelee sura ya tatu inayoelezea Kanisa lililo kwa ajili ya maskini.
Tukianza na mafundisho ya Mtakatifu Augustine, Mtakatifu Ambrose, alikuwa kiongozi wa kiroho wa Mtakatifu Augustine ambaye alisisitiza juu ya hitaji la kushirikishana mali. “Unachowapa maskini si mali yako, bali ni mali yao. Kwa nini umiliki mali ya umma iliyo kwa matumizi ya kawaida kwa wote?" Kwa Askofu wa Milano, anafundisha kuwa “Ukarimu ni haki ya kurejesha, siyo ishara ya ubaba”. Katika mahubiri yake, anasisitiza kuwa “Rehema ina tabia ya kinabii: anashutumu miundo ambayo inajirimbikizia vitu na kusisitiza ushirika kama wito wa Kanisa. Kwa tamaduni hii, Askofu wa Hippo kwa upande wake alifundisha juu ya upendo kwa maskini. Mchungaji makini na mwanatalimungu mwenye ufahamu adimu, anatambua kwamba umoja wa kweli wa kikanisa ni ule unaoshirikisha matumizi ya pamoja ya vitu. Anatukumbusha wakristo kuwa ukristo wa kweli hauwabagui wale wanaoishi katika taabu na mahangaaiko, kwa kuwa Kristo anaishi ndani yako inakupasa kuwapa msaada wegeni. Ugawanaji huu wa mahitaji hutokana na pendo la kimungu na lengo lake kuu ni upendo wa Kristo. Kulingana na mafundisho ya Mtakatifu Augustine, “Maskini si watu wa kusaidiwa tu, bali ni uwepo wa kisakramenti wa Bwana”.
Ndugu msomaji/ msikilizaji, daktari wa neema analiona jukumu la kuwajali maskini kama uthibitisho thabiti wa uaminifu wa imani. Mtu yeyote ambaye anasema wanampenda Mungu na hana huruma kwa wahitaji ni muongo (rej. 1 Yoh 4:20). Mtakatifu Augustine akiomwongelea kijana tajiri na suala zima la kujiwekea “hazina mbinguni” kwa wale wanaotoa mali zao kwa maskini (rej. Mt 19:21), anasema kwa nafsi ya Yesu kuwa; “nimeipokea dunia, nikaipa mbingu; nilipokea mali ya kuharibika, nitarudisha mali ya milele; nilipokea mkate, nitauhuisha na kuupa uhai; nimepewa ukarimu, nami nitawafikisha nyumbani; Nilitembelewa wakati nikiwa mgonjwa; nami nitawapa afya njema; nilitembelewa gerezani, nami nitawapa uhuru. Mkate uliompa maskini wangu ameula, lakini mkate nitakaowapa hautawaburudisha ninyi tu, bali ni chemichemi inayotiririka kamwe”. Mwenyezi Mungu hatapungukiwa ukarimu kwa wale wanaotumikia watu wahitaji: kadiri unavyokuwa na upendo mkubwa kwa maskini, ndivyo thawabu inavyokuwa kubwa kutoka kwa Mungu.
Ndugu msomaji/msikilizaji, mtazamo huu wa kina wa kikristo na wa kikanisa hutuongoza kuthibitisha kwamba majitoleo yanapotokana na upendo, si tu hupunguza mahitaji ya ndugu, bali pia hutakasa moyo wa mtoaji ikiwa yuko tayari kubadilika. Kwa maneno ya mwandishi mmoja juu ya maisha ya Mtakatifu Augustine yanasema: “kutoa sadaka kunaweza kuwa na manufaa kwako katika kufuta malipizi ya dhambi zako za zamani, ikiwa umezirekebisha njia zako”. Kwani hii ni njia ya kawaida ya uongofu kwa wale wanaotaka kumfuata Kristo kwa moyo usiogawanyika. Ndani ya Kanisa linaloutambua uso wa Kristo katika maskini na katika kushirikishana mali kwa njia ya upendo, wazo la Mtakatifu Augustine linabaki kuwa nuru. Leo, uaminifu kwa mafundisho ya Mtakatifu Augustine unahitaji si tu kufanya utafiti wa kazi zake, bali pia utayari wa kuishi kwa kiasi kikubwa wito wake wa uongofu, ambao unajumuisha huduma ya upendo. Mababa wengine wengi wa Kanisa, kutoka mashariki na magharibi, wamezungumza juu ya ukuu wa umakini kwa maskini katika maisha na utume wa kila mkristo. Kutokana na mtazamo huu, kwa muhtasari, mafundisho na malezi ya mababa wa Kanisa yalikuwa ya vitendo, yakilenga Kanisa ambalo lilikuwa makini na kwa ajili ya maskini. wakifuasa mfano wa Injili iliyotangazwa kwa usahihi wanatufundisha kuwa inatupasa kugusa uhalisia wa maisha ya walio wadogo zaidi miongoni mwetu; na kuonya kwamba ukali wa mafundisho bila huruma ni kupiga porojo tupu.
Ndugu msomaji/msikilizaji, huruma ya kikristo imejidhihirisha kwa namna ya pekee katika utunzaji wa wagonjwa na wanaoteseka. Kulingana na ishara zilizopo katika huduma ya uponyaji wa vipofu, wenye ukoma na waliopooza kama ilivyotolewa na Yesu hadharani, Kanisa linaipa kipaumbele katika utume wake kana kwamba kuwatunza wagonjwa, ni tendo ambao ndani yake tunamtambua kwa urahisi Bwana aliyesulubiwa. Wakati wa tauni katika mji wa Carthage, alipoishi Askofu, Mtakatifu Cyprian aliwakumbusha wakristo umuhimu wa kuwatunza wagonjwa: “Tauni ni ugonjwa ambayo ulionekana wa kutisha sana na wenye kuua. Lakini uwepo wa ugonjwa huchunguza haki ya kila mmoja, na huchunguza mawazo ya wanadamu, ni kipimo kwa wenye afya kama wanawatumikia wagonjwa; kama jamaa wanapendana kwa uaminifu; ikiwa mabwana wanawahurumia watumwa wao wagonjwa; kama madaktari hawawaachi wagonjwa wanaoomba msaada”. Tamaduni ya kikristo ya kuwatembelea wagonjwa, kuwaosha majeraha na kuwafariji wanaoteseka si tu jitihada za hisani, bali ni tendo la kikanisa ambalo ndani yake Kanisa huugusa mwili wa Kristo mteseka.
Ndugu msomaji/msikilizaji, katika karne ya kumi na sita, Mtakatifu Yohana wa Mungu alianzisha shirika la Hospitaller ambalo linaitwa kwa jina lake, ili kujenga hospitali za mfano ambazo zilikaribisha kila mtu, bila kujali hali ya kijamii au kiuchumi. Inakumbukwa kauli yake maarufu isemayo; “Fanyeni mema, ndugu zangu!” ambayo ilikuwa kauli mbiu ya upendo hai kwa wagonjwa. Wakati huo huo Mtakatifu Camillus de Lellis alianzisha Utume wa wagonjwa ili kuwahudumia wagonjwa kwa kujitolea kikamilifu. Mwongozo wake unaamuru hivi: “Kila mtu na amuombe Bwana kuwa na upendo wa kimama kwa jirani ili tuwatumikie kwa mapendo yote, katika roho na mwili, kwa sababu tunatamani, kwa neema ya Mungu, kuwahudumia wagonjwa wote kwa upendo wa ukaribu wa ki-mama mwenye mtoto wake wa pekee aliye mgonjwa”. Utume huu wa ki-kamilliano unamwilisha huruma ya Kristo-Tabibu katika ma-hospitali, kwenye viwanja vya vita, magerezani, na mitaani.
Ndugu Msomaji/msikilizaji, kuwatunza wagonjwa kwa upendo wa ki-mama, kama mzazi anavyomtunza mtoto wake, umevutia akina mama wengi katika maisha ya wakfu huku wakichukua nafasi kubwa zaidi katika kutoa huduma za afya kwa maskini. Mabinti wa Upendo wa shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo, Masista wa huduma ya wagongwa, Masista wadogo wa maongozi ya Mungu, na mashirika ya mengi ya kike yamekuwa uwepo wa uuguzi wa akina mama wenye busara katika hospitali, vituo vya uuguzi na nyumba za wastaafu. Hawa wameleta faraja, sikio lenye kusikiliza, uwepo, na zaidi ya yote, huruma. Wamejenga, mara nyingi kwa mikono yao wenyewe, vituo vya huduma za afya katika maeneo yasiyo na msaada wa matibabu. Wanafundisha usafi, wanasaidia katika katika huduma ya uzazi na utoaji wa dawa kwa hekima ya asili na imani ya kina. Nyumba zao zimekuwa chemchemi za hadhi ambapo hakuna mtu aliyetengwa. Uwepo wa huruma hii umekuwa dawa na huduma ya kwanza. Mtakatifu Louise wa Marillac aliwaandikia dada zake, Mabinti wa Upendo, akiwakumbusha kwamba “wamebarikiwa ki-pekee na Mungu kwa ajili ya huduma ya maskini kwa wagonjwa Hospitalini”. Leo, urithi huu unaendelea katika hospitali za kikatoliki, vituo vya huduma za afya katika maeneo ya mbali, zahanati vijijini, katika makazi ya waraibu wa dawa za kulevya na katika hospitali za maeneo ya vita.
Ndugu msomaji/msikilizaji, uwepo wa ukristo miongoni mwa wagonjwa unafunua wokovu kana kwamba si wazo la kufikirika, bali ni tendo halisi. Katika kutibu jeraha, Kanisa linatangaza kwamba ufalme wa Mungu unaanza kati ya walio hatarini zaidi. Kwa kufanya hivyo, Kanisa linabaki aminifu kwake aliyesema, “Nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama” (Mt 25:36). Wakati Kanisa linapiga magoti kandokando ya mwenye ukoma, mtoto mwenye utapiamlo au mtu anayekufa asiyejulikana, linatimiza wito wake wa ndani kabisa wa kumpenda Bwana mahali ambapo amejerhiwa sana.
Ndugu msikilizaji, tumefikia hapa kwa leo katika mwendelezo wa barua ya kitume, usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo.