Padre Daleng,Muagostinian ni Makamu Mpya wa Nyumba ya Kipapa
Vatican News
Papa Leo XIV amemteua Padre Edward Daniang Daleng,(O.S.A), kuwa Makamu Mkuu Nyumba ya Kipapa. Kabla ya Uteuzi alikuwa ni mshauri mkuu na Msimamizi mkuu(Procuratore) wa Shirika la Mtakatifu Agostino.
Wasifu wa Padre Daleng
Alizaliwa tarehe 4 Aprili 1977, huko Yitla'ar, Kwalla, Jimbo la Plateau (Nigeria), alifunga nadhiri za kwanza katika Shirika la Mtakatifu Agostino mnamo tarehe 9 Novemba 2001, na nadhiri za daima mnamo tarehe 13 Novemba 2004. Alipewa daraja la Upadre mnamo tarehe 10 Septemba 2005 na akapata Shahada ya Uzamivu katika Taalimungu ya Maadili kutoka Chuo Kikuu Kipapa cha Alphonsian, Roma mnamo 2012.
Mahojiano
Katika mahojiano na vyombo vya habari vya Vatican, siku chache baada ya kuchaguliwa kwa Papa Leo XIV kwenye kiti cha Mtume Petro, alizungumzia uhusiano maalum wa Prevost na Afrika. "Afrika iko moyoni mwake,"Padre Daleng alisema. "Alitembelea misheni zetu zote za Kiafrika mara kadhaa na akafika nchini mwangu, Nigeria, angalau mara kumi na mbili, ikiwa ni pamoja na ile ya mwaka 2016 tulipoadhimisha Mkutano Mkuu wa kati kwa mara ya kwanza."
"Ili kuelewa jinsi alivyojali nchi yangu,"Padre huyo aliendelea, "inatosha kukumbuka kwamba baada ya kuwa Mkuu wa Shirika katika siku yake ya kuzaliwa ya miaka 46, kunako Septemba 14, alikuwa tayari nasi nchini Nigeria mwezi Novemba. Hakukosa hata mkutano mmoja; alikuwepo kila wakati."