2025.11.28 Piha ya Ziara ya Papa nchini Uturuki na Lebanon. Kituo cha maskini. 2025.11.28 Piha ya Ziara ya Papa nchini Uturuki na Lebanon. Kituo cha maskini.  (@Vatican Media)

Katika Dilexi Te:Tunataka kuwatangaza maskini kuwa Mungu anawapenda!

Baba Mtakatifu Fransisko alitambua kwamba utume wa Kanisa kwa wahamiaji na wakimbizi ni mpana zaidi na akisisitiza kwamba"mwitikio wetu kwa changamoto za uhamiaji wa kisasa zinaweza kufupishwa katika vitenzi vinne:kukaribisha,kulinda,kukuza na kuunganisha.”Hata hivyo vitenzi hivi havihusu wahamiaji na wakimbizi pekee bali vinaelezea utume wa Kanisa kwa wale wote wanaoishi pembezoni,ambao wanahitaji kukaribishwa,kulindwa, kuhamaishwa na kuunganishwa.”

Na  Padre Angelo Shikombe – Vatican.

Mpendwa Msomaji/msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya Wosia wa Kitume wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assis. Baba Mtakatifu Leo XIV alitoa Wosia huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tuendelee sura ya tatu inayoelezea Kanisa lililo kwa ajili ya maskini. 

Tukianza na kipengele cha kuwasindikiza wahamiaji, ndugu msikilizaji, urithi wa maisha ya uhamiaji unaambatana na historia ya wokovu wa taifa la Mungu. Abramu aliondoka bila kujua aendako; Musa aliwaongoza mahujaji jangwani; Mariamu, Yusufu, na mtoto Yesu walikimbilia Misri. Kristo mwenyewe, ambaye “alikuja kwa walio wake, na walio wake hawakumpokea” (Yn 1:11), aliishi kati yetu kama mgeni. Kwa sababu hii, Kanisa siku zote hutambua kwa wahamiaji uwepo hai wa Bwana ambaye, katika siku ya hukumu, atawaambia wale walioko upande wake wa kiume akisema; “Nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha” (Mt 25:35). Katika karne ya kumi na tisa, wakati mamilioni ya wazungu walihama ili kutafuta hali ya maisha bora, watakatifu wawili walitambulika katika utoaji wa huduma ya kichungaji: Mtakatifu Yohane Mbatizaji Scalabrini na Mtakatifu Fransisko Xavier Cabrini.

Scalabrini, alikuwa Askofu wa Piacenza, aliyeanzisha Shirika la Wamisionari wa Mtakatifu Kalori lililowasindikiza  wahamiaji kwenda mahali walikokwenda, huku wakiwapa mafundisho ya kiroho, kisheria, na misaada mbalimbali. Aliona wahamiaji kama wapokeaji wa injilishaji mpya, akionya juu ya hatari za unyonyaji na kupoteza imani katika nchi ya kigeni. Akifuata karama aliyopewa na Bwana, “Scalabrini alitazamia kwa hamu kuona ulimwengu na Kanisa lisilo na vizuizi, ambapo hakuna mtu anayejisikia mgeni”. Mtakatifu Fransisko Cabrini, mzaliwa wa Italia na mwenye asili ya kimarekani, alikuwa raia kutoka Marekani aliyetangazwa kuwa mtakatifu. Ili kutimiza dhamira yake ya kuwasaidia wahamiaji, alivuka mara kadhaa bahari ya Atlantiki. "Akiwa na ujasiri wa ajabu, alianzisha shule, hospitali na vituo vya watoto yatima bila kudai chochote kwa ajili ya umati wa maskini ambao walijitosa katika ulimwengu mpya kutafuta kazi. Kwa kutojua lugha na kukosa uwezo wa kupata mahali pa heshima huko Amerika, mara nyingi naye alikuwa muhanga wa upelelezi. Moyo wake wa kimama, ambao haukumruhusu kupumzika, ulimfanya afike kila mahali: katika mashimo, magereza na migodini walikopatikana wahamiaji”.

Ndugu msomaji/msikilizaji, tamaduni ya Kanisa ya kufanya kazi na wahamiaji inaendelea, na leo huduma hii inajipambanua katika mipango mikakati kama vile uwepo wa vituo vya kupokea wakimbizi, misheni za mpakani na juhudi za kimataifa za huduma ya karitas na taasisi nyingine ulimwenguni. Ufundishaji wa kisasa unathibitisha wazi utume huu. Baba Mtakatifu Fransisko alitambua kwamba utume wa Kanisa kwa wahamiaji na wakimbizi ni mpana zaidi, na akisisitiza kwamba "mwitikio wetu kwa changamoto za uhamiaji wa kisasa zinaweza kufupishwa katika vitenzi vinne: kukaribisha, kulinda, kukuza na kuunganisha.” Hata hivyo vitenzi hivi havihusu wahamiaji na wakimbizi pekee, bali vinaelezea utume wa Kanisa kwa wale wote wanaoishi pembezoni, ambao wanahitaji kukaribishwa, kulindwa, kukuzwa na kuunganishwa”.

Pia alisema: “Kila mwanadamu ni mtoto wa Mungu! Ana sura ya Kristo! Sisi wenyewe tunahitaji kuona, na kisha, tuwawezeshe wengine kuona, na hivyo wahamiaji na wakimbizi sio tatizo la kutatuliwa, bali ni kaka na dada wa kukaribishwa, kuheshimiwa na kupendwa”. Wao ni sababu inayotudsaidia kujenga haki zaidi za kijamii, demokrasia safi, nchi iliyoungana zaidi, ulimwengu wa kidugu na ulio wazi zaidi, na jumuiya za Kikristo”.  Kanisa, kama mama, hufuatana na wale wanaosafiri.  Mahali ambapo ulimwengu unaona vitisho, Kansia huona watoto; pale ambapo kuta zimejengwa, lenyewe hujenga madaraja. Kanisa linajua kwamba uinjilishaji unathaminika tu pale ambapo Kanisa linatafsiriwa katika ishara zake za ukaribu na kakaribisha. Na linajua kwamba katika kila mhamiaji anayekataliwa, ni Kristo mwenyewe ambaye anabisha mlangoni mwa jamii.

Ndugu msomaji/msikilizaji, kandokando ya kila aliye mdogo kati yetu yupo Kristo. Utakatifu wa kikristo mara nyingi hustawi katika sehemu ambapo utu wa mwanadamu umesahaulika na kujeruhiwa zaidi. Maskini zaidi ya maskini wengine ni wale ambao wanakosa si tu mali, bali pia sauti na kutambuliwa heshima na utu wao. Wana nafasi ya pekee katika moyo wa Mungu. Hao ndio wapendwa wa Injili, na warithi wa ufalme (rej. Lk 6:20). Ndani yao Kristo anaendelea kuteseka na kufufuka tena. Ni ndani yao, Kanisa huutambua tena wito wake wa ukweli na halali. Mtakatifu Teresa wa Calcutta, aliyetangazwa Mtakatifu mwaka wa 2016, amekuwa ishara ya kiulimwengu ya ukarimu hai unaotolewa kwa maskini zaidi, wale waliotupwa na jamii. Akiwa mwanzilishi wa Wamisionari wa upendo yaani “charity”, alijitolea maisha yake kwa walioachwa katika mitaa ya India. Alikusanya waliokataliwa, akawaoshwa majeraha yao, na kuandamana nao hadi wakati wa kufa kwao.

Upendo wake kwa maskini zaidi ulidhihirisha kwamba hakuwatunza tu maskini kwa kuwapa mahitaji yao, lakini aliwatangazia pia habari njema akisema: “Tunataka kuwatangaza maskini habari njema kwamba Mungu anawapenda, na kwamba tunawapenda, kwani wao ni watu muhimu kwetu, kwa kuwa pia wao wameumbwa kwa mkono uleule wa upendo wa Mungu, wana haki na wajibu wa kupenda na kupendwa. Watu wetu maskini ni wa mhimu sana, ni watu wa kupendwa sana. Hawahitaji huruma na upendeleo wetu, bali wanahitaji pendo letu la kuwatambua. Wanahitaji heshima yetu; wanahitaji tuwatendee kwa utu”. Haya yote yanatokana ya tafakari za kina za kiroho ambazo zinaiona huduma kwa maskini zaidi kama tunda la sala ya upendo, na chanzo cha amani ya kweli.

Papa Yohane Paulo II, aliwakumbusha mahujaji waliokuja Roma kwa ajili ya kutangazwa mama Teresa kuwa mwenye heri akisema: “Mama Teresa alipopata wapi nguvu ya kujiweka wakfu katika kutoa huduma kwa wengine? Aliipata nguvu hii katika sala na tafakari ya kimya kimya juu ya Yesu Kristo, uso wake mtakatifu, na moyo wake mtakatifu. Yeye mwenyewe alitamka kwamba: “Tunda la ukimya ni sala; tunda la sala ni imani; tunda la imani ni upendo; na tunda la upendo ni huduma”.  Ni sala iliyoujaza moyo wake amani ya Kristo mwenyewe na amani hiyo kuangazia wengine”. Mama Teresa hakujiona kuwa mfadhili au mwanaharakati, bali daraja analopita bibi-arusi wa Kristo Msulibiwa, akitumikia kwa upendo kamili kaka na dada zake wanaoteseka.

Ndugu msomaji/msikilizaji, nchini Brazil, Mtakatifu Dulce wa Maskini - anayejulikana kama "Malaika mwema wa Bahia" anajumuishwa pia katika sifa za uinjilishaji wenye tunu za utamaduni wa kibrazili. Kwake yeye na wanawake wengine wawili waliotangazwa kuwa watakatifu wakati wa adhimisho hilo, Papa Fransisiko alitambua upendo wao kwa waliotengwa zaidi na jamii akisema kwamba; “watakatifu wapya wanatufundisha kwamba maisha ya wakfu ni safari ya upendo kuzielekea jamii zilizo pembezoni mwa ulimwengu”. Dada Dulce alijibu hali ya hatari inayosababishwa na ubunifu, unaozuia huruma na hitaji la imani isiyotikisika. Alianza kwa kuwapoea wagonjwa na kuwalaza katika banda la kuku na kutoka hapo akaanzisha huduma kubwa zaidi ya kijamii nchini. Alisaidia maelfu ya watu kwa siku, bila kupoteza upole wake, akijifanya masikini miongoni mwa maskini ili kufikisha upendo kwa mnyonge. Aliishi na wadogo, aliomba kwa bidii na akitumikia kwa furaha. Imani yake haikumtenga na malimwengu, bali alizidi kuyakaribia malimwengu kwa undani zaidi ili kutibu maumivu ya anayeteseka kati yetu.

Tunaweza pia kutaja watu binafsi kama vile Mtakatifu Benedicto Menni na Masista Wahudumu wa hospitali Moyo Mtakatifu wa Yesu, anayefanya kazi pamoja na watu wenye ulemavu; Mtakatifu Kaloro de Foucauld ni miongoni mwa jamii za Sahara; Mtakatifu Katharina Drexel wa vikundi visivyo na uwezo zaidi huko Kaskazini mwa Amerika; Sista Emmanuelle, anayefanya kazi na wakusanya takataka katika kitongoji cha Ezbet El Nakhl cha Cairo; na wengine wengi. Kwa kila mmoja wao imegunduliwa kuwa maskini sio kitu cha sisi kuonesha huruma yetu, bali ni walimu wa Injili. Si suala la “kumleta” Mungu kwao, bali ni la kukutana naye kati yao. Mifano hii yote inatufundisha kuwa kuwatumikia maskini si ishara ishukayo “kutoka juu,” bali ni kusanyiko la watu walio sawa, ambapo Kristo anafunuliwa na kuabudiwa. Mtakatifu Yohane Paulo wa II, alitufundisha kwamba “kuna uwepo wa aina yake wa Kristo katika maskini unaolifanya kanisa kuwa na jicho la kipekee juu ya huduma kwa maskini. Kwa hiyo, wakati Kanisa linapoinama chini kumtunza maskini, linatoa ishara iliyo kuu zaidi ya uwepo wake. 

Ndugu msomaji/msikilizaji, katika harakati za kijamii, ni lazima pia tutambue kwamba, katika karne zote za historia ya kikristo, kuwasaidia maskini na kutetea haki zao hakukuhusisha tu watu binafsi, familia, taasisi na jumuiya za kidini. Kumekuwepo na, bado kunaendelea kuwepo kwa harakati mbalimbali maarufu zinazoundwa na walei au jamii ya watu wa kawaida na wanaoongozwa na viongozi maarufu, ambao mara nyingi wameshukiwa na hata kuteswa. Baba Mtakatifu Leo XIV, anarejelea kwa wasafiri wote, katika  jumuiya zao  zinazoungana na kuwa jamii moja ambayo haiwabagui na kuwaacha maskini na wanyonge nyuma... Viongozi ‘Maarufu’ wa halaiki, ni wale wanaomshirikisha kila mtu... Hawakwepeki wala hawaogopi, ni kundi la vijana walioumizwaa au kuzaliwa katika mazingira yenye uzito mkubwa wa msalaba”. Viongozi hawa maarufu wanajua kwamba mshikamano “pia unamaanisha kupinga dhidi ya mifumo za kimaskini na kandamizi; ukosefu wa kazi, ardhi na makazi; na kunyimwa haki za kijamii na kazi.

Hii inamaanisha kukabiliana na athari za uharibifu za himaya tajiri… Mshikamano, maana yake ya ndani kabisa, ni njia ya kutengeneza historia, na hivi ndivyo wanaharakati maarufu wanavyofanya". Kwa kwa sababu hiyo, wakati taasisi mbalimbali zinapofikiria kuhusu mahitaji ya maskini, ni muhimu “kujumuisha harakati maarufu za kijamii na kuimarisha miundo ya utawala wa ndani, kitaifa na kimataifa na hivyo kuwa na nguvu ya pamoja ya kiadili inayotokana na kujumuishwa harakati za pamoja ili kufikia hatima ya pamoja”. Ndugu msomaji/msikilizaji, harakati maarufu za kijamii, zinatualika kushinda "mtazamo wa sera za kijamii unaotoa sera kwa makundi ya maskini, lakini hauko na maskini na kamwe hauko kwa ajili ya maskini, bali kuendeleza miradi ambayo inawafanya watu kukaa pamoja”. Iwapo wanasiasa na wasomi hawajali maskini, "sera za demokrasia, hugeuka kuwa mbwembwe, na mitindo ya kimaisha, utaratibu huu hupoteza tabia ya uwakilishi na mwisho wake ni kusambaratika. Kwa sababu wamewasahau watu katika mapambano yao ya kila siku ya kupata utu, katika ujenzi wa maisha yao ya baadaye”. Na pia iko hivyo kwa taasisi za Kanisa.

Dilexi Te sehemu ya 11
03 Desemba 2025, 14:45