Mahubiri Kipindi cha Majilio 2025: Ujenzi wa Kanisa la Kristo Bila Upinzani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Majilio ni kipindi cha kumbukumbu na matumaini kwa Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake, ili kuweza kuinua utu na heshima yao, iliyokuwa imechakaa kutokana na dhambi, ili hatimaye, kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Hii ni hija ya maisha ya imani, matumaini na mapendo; inayowakumbusha waamini, Fumbo la Umwilisho na Siku ile ya mwisho, Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu; kama Kanisa linavyokiri na kufundisha kwenye Kanuni ya Imani. Kwa njia ya Kipindi cha Majilio, Mama Kanisa huwafungulia waamini utajiri wa uweza na mastahili ya Bwana wake Kristo Yesu na hivyo waamini huweza kuchota na kujazwa na neema ya wokovu. Mama Kanisa katika huruma na upendo wake wa daima anapenda kuwakomaza waamini kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; Mafundisho, Sala pamoja na Matendo ya toba na huruma. Rej. Sacrosanctum concilium, 102-111. Padre Roberto Pasolini, O.F.M. Cap. Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa anasema, tema inayoongoza Mahubiri ya Kipindi cha Majilio kwa Mwaka A wa Kanisa yaani Mwaka 2025 inachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu: “Kutazamia na Kuharakisha Kwa Ujio wa Siku ya Bwana. Tumaini la Maadhimisho ya Jubilei: Kati ya Matarajio ya Bwana na Ulimwengu wa Wokovu. Rej 2Pt 3:12. Mahubiri haya yanahudhuriwa na Baba Mtakatifu Leo XIV, Makardinali, Maaskofu, Wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican, Jimbo kuu la Roma pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yaliyoko mjini Roma. Mahubiri ya Pili ya Kipindi cha Majilio yamenogeshwa na kauli mbiu: "Kujenga Upya Nyumba ya Bwana: Kanisa Bila Upinzani.” Udanganyifu wa umoja; Kuchanganyikiwa kama tiba; Hekalu litajengwa upya; Kupyaishwa kwa Kanisa, pamoja na kufasiri ni kati ya mambo ambayo Padre Pasolini ameyapatia kipaumbele cha pekee katika mahubiri yake.
Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wamefanywa kuwa ni wafanyakazi pamoja na Mungu, shamba na jengo la Mungu. Rej 1Kor 3:9 na kwamba; “Katika Kristo Kanisa ni kama Sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote.” LG, 1. Huu ni umoja unaopaswa kuwaunganisha waamini wote, kiasi cha kujisikia kuwa ni ndugu wamoja, kwa kuaminiana na wala si katika kufanana kwa sababu waamini wana sura tofauti na wanatoka katika tamaduni mbalimbali, neema na baraka za Mungu zinazoweza kuzaa matunda, kinyume kabisa cha ujenzi wa Mnara wa Babeli: “Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote.” Mwa 11:4. Dhana ya ujenzi wa umoja unaosimikwa katika “ukomunisti” ni kishawishi ambacho hakiwezi kuliacha Kanisa salama hata katika masuala ya imani. Hii ni changamoto ya kujenga umoja wa Kanisa kwa kuzingatia tofauti zake msingi zinazoambata na kukumbatia upendo, uhuru, utu na heshima ya kila mmoja, kwani hakuna umoja pasi na tofauti. Hivi ndivyo ilivyotokea wakati wa Sherehe ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Rej Mdo 2:1-12. Pentekoste ni jibu kutoka kwa Mungu dhidi ya mahangaiko ya ujenzi wa Mnara wa Babeli, kielelezo cha umoja katika tofauti zake msingi.
Mwenyezi Mungu aliwachagua Waisraeli na kuwapatia upendeleo wa pekee katika historia nzima ya wokovu, akawaokoa kutoka utumwani Misri na kuwaongoza jangwani kwa muda wa miaka arobaini. Waisraeli walipotoka utumwani, Mfalme Daudi akatia nia ya kumjengea Mungu nyumba, hata katika muktadha huu, hawakukosekana watu waliogumisha mchakato wa ujenzi wa Hekalu la Mungu, lakini hatimaye wakafanikiwa kukamilisha ujenzi wa nyumba ya Mungu kwa kelele za shange na furaha kwa sauti ya machozi na maombolezo: “hata watu wasiweze kupambanua kelele za furaha, na kelele za vilio vya watu; maana watu walipiga kelele kwa sauti kuu, na kelele zao zikasikika mbali sana.” Ezr 3: 12-13. Hii anasema Padre Roberto Pasolini, O.F.M. Cap. Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa kwamba ni changamoto ya ujenzi na upyaishaji wa “Nyumba ya Mungu” kama alivyofanya Mtakatifu Francisko wa Assisi na kulisimika katika udugu wa Kiinjili na kama Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanavyosema: “Marekebisho yoyote ya Kanisa maana yake ni hasa ukuzaji wa uaminifu katika wito wake; bila shaka hiyo ndiyo asii ya jitihada kwa ujenzi wa umoja wa Kanisa.” Unitatis redintegratio, 6.
Hii ni changamoto kwa Kanisa kuendelea kuwa aminifu kwa tunu msingi za Kiinjili na utume wake; likiwa na uwezo wa kupokea kweli mbalimbali na hivyo kumwachia Roho Mtakatifu kutenda ndani ya Kanisa. Huu ni mwaliko wa kuendelea kupyaisha maisha ya kiroho, kwa kupambana kufa na kupona na yale mambo yanayokwenda kinyume na tunu msingi za Kiinjili, ili hatimaye, kujikita katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, tayari kuganga na kutibu majeraha yanayoendelea kulisibu Kanisa, ili kweli Kanisa liweze kuwa ni kwa ajili ya wengi.Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yalikuwa ni mapambazuko mapya ya Roho Mtakatifu, mwanzo wa matumaini mapya; kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa Neno la Mungu, maisha na utume wa waamini walei; umoja wa Kanisa la Kisinodi na kwamba, huu ni ushuhuda wa imani inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa. Kazi ya Roho Mtakatifu ni kuendelea kulisafisha na kulitakasa Kanisa, kwa kujikita katika mang’amuzi dhidi ya itikadi zinazopingana ndani ya Kanisa. Kipaumbele cha pekee ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linarejea kwenye kiini cha Injili. Kila mmoja anao wajibu na dhamana ya kulipyaisha Kanisa na kwamba, hii ni zawadi inayopaswa kupokelewa kila siku, kuihifadhi na kuimwilisha katika huduma.