Msaada wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Waathirika wa Mafuriko Barani Asia
Na Sr. Christine Masivo, - Vatican
Dhoruba kali na mvua za masika, zimepiga maeneo ya Kusini Mashariki na Kusini mwa Asia katika kipindi cha Mwezi Desemba 2025 na hivyo kusababisha maporomoko ya ardhi na mafuriko. Kuna watu wengi wamepoteza maisha na wengine wengi wakiwa hawajulikani mahali walipo. Zaidi ya watu milioni moja wamepoteza makazi yao nchini Sri Lanka. Mvua kubwa na maporomoko ya ardhi Magharibi mwa Indonesia yamewajeruhi watu 5,000 na kuharibu miundombinu, ikiwemo shule na hospitali pamoja na makazi ya watu. Zaidi ya watu milioni mbili ambayo ni sawa na asilimia 10% ya idadi jumla ya watu nchini humo wameathiriwa na Kimbunga “Ditwah” kinachoelezwa kuwa kibaya zaidi kuwahi kutokea kisiwani humo katika karne hii ya sasa. Sri Lanka inatarajia kuendelea kupata mvua nyingi katika kipindi hiki.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika tarehe 7 Desemba 2025 alionesha kuguswa na maafa haya makubwa kwa watu na mali zao na hivyo kuliagiza Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo, kupeleka msaada wa dharura kwa nchi za: Sri Lanka, Indonesia, Vietnam, na Thailand. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuwahakikishia watu wa Mungu katika nchi hizi zilizokumbwa na majanga asilia uwepo wake wa karibu na hivyo kuhimiza Jumuiya ya Kimataifa kuonesha mshikamano na upendo wa kidugu kwa waathirika katika nchi hizi.