Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2026 unanogeshwa na kaulimbiu: “Ndugu, Msichoke Kutenda Mema.” Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2026 unanogeshwa na kaulimbiu: “Ndugu, Msichoke Kutenda Mema.”  

Baraza La Maaskofu Katoliki Tanzania: Ujumbe wa Kwaresima 2026: Msichoke Kutenda Mema

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2026 unanogeshwa na kaulimbiu: “Ndugu, Msichoke Kutenda Mema.” Rej. 2The 3:13 na kwamba, katika kipindi hiki cha Kwaresima, waamini wanahimizwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini kwa kuendelea kutendeana mema na kusameheana bila kuchoka. Waamini watambue kwamba Mwenyezi Mungu ndiye asili ya wema na utakatifu wote wa maisha!

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, - Dar es Salaam, Tanzania.

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2026 unanogeshwa na kaulimbiu: “Ndugu, Msichoke Kutenda Mema.” Rej. 2The 3:13 na kwamba, katika kipindi hiki cha Kwaresima, waamini wanahimizwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini kwa kuendelea kutendeana mema na kusameheana bila kuchoka. Kauli mbiu hii inachota amana na utajiri wake kutoka katika Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike anayewataka waamini kutenda mema na kuachana na tabia ya uvivu inayowakatisha wengine kutenda mema, wadumu katika kutenda mema, wakitambua kwamba, wao ni ndugu katika Kristo Yesu, kumbe wanapaswa kusaidiana, huku wakiendelea kumkazia macho Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini kujibidiisha kuwa wema na watakatifu kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye asili ya wema na utakatifu wote. Kwa vile ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, hivyo anaitwa kuwa mkamilifu zaidi kwa kutumia vyema akili na utashi ili kupambanua na kuchagua mema. Mwamini anawajibika kikamilifu kumtendea wema jirani yake kwa sababu ya udugu wa kibinadamu. Matendo mema yanafumbatwa katika kutekeleza mahitaji msingi kiroho na kimwili; kwa mwamini kutekeleza dhamana na majukumu yake kwa uaminifu na ukarimu. Mtume Paulo anatoa Amri kwa waamini wasichoke kutenda mema maana watavuna kwa wakati wake, maisha na uzima wa milele. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linasema kuna sababu zinazoweza kumfanya mwamini kujisikia kuchoka na hivyo kushindwa kutenda mema: Maelekeo binafasi ya kutenda dhambi; Ushawishi mbaya kutoka katika jamii inayo mzunguka; pale waamini wanapoishi katika jamii iliyojaa uchafu: Kwa kutoheshimu Amri za Mungu, Kazi ya Uumbaji, Kutoheshimu na kufuata sheria, kanuni na miongozi ya kijamii. Waamini wachague kumpendezesha Mungu na wala si watu! Kutenda wema ni wito endelevu unaodai sadakam kwa kujikana, kujitwika Msalaba na kuanza kumfuata Kristo Yesu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani; kwa imani na ustahimilivu, kwa kutumaini kwamba, bidii yao haitakuwa bure. Kudumu katika kutenda mema, ni kazi ya Roho Mtakatifu anaye waimarisha waamini wasitikisike, bali wadumu katika imani inayosimikwa katika utii.

Watanzania tusichole kutenda mema
Watanzania tusichole kutenda mema   (© Elena Galeotti)

Maaskofu Katoliki Tanzania wanasema Matendo Mema ni Nafasi ya Kumweka Kristo Katika Maisha; Matendo mema ni kuzishika Amri na Maagizo ya Kristo Yesu. Matendo mema ni ushuhuda wa imani tendaji na ushuhuda wa wokovu na kwamba, kila mtu atahukumiwa kwa matendo yake mwenyewe. Kumbe kumpenda Mungu na jirani ni njia inayowaelekeza waamini kwenye maisha na uzima wa milele. Waamini kamwe wasiache kutenda mema na kusamehe na kwamba, ukarimu wao ni muhimu, bila kujali ukubwa wa zawadi wanayotoa kama ilivyokuwa ile sadaka ya mwanamke mjane, au yule kijana aliyekuwa ni samaki wawili na mikate mitano. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanatumia vipaji vyao ili kuwasaidia wengine. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linasema matendo mema ni mwendelezo Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yaliyonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini“ kwa kukazia upyaisho wa maisha ya kiroho; msamaha na upendo; matumaini na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, bila kusahau wajibu wa kiikolojia, yaani utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko wa kukuza jumuiya na kutunza mazingira pamoja na kuendelea kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili, bila kusahau hija na maisha ya sala. Malango ya Jubilei ya Matumaini yamefungwa lakini amana na utajiri wa Mama Kanisa unaobubujika kutoka katika huruma na upendo wa Mungu bado unaendelea kubaki wazi. Kwa waamini ambao hawakupata fursa ya kushiriki matukio mbalimbali ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Kipindi cha Kwaresima ni nafasi yao kwa kujitathmini nafsi yao mbele ya Mungu kwa kutafuta wasaa wa kushiriki tukio la kibinafsi na kwamba, kamwe wasichoke kutenda mema, kwani hii ni safari ya imani na kwamba, maisha daima yana changamoto zake, hivyo inabidi waamini kuwa wastahimilivu kupitia imani, matumaini na furaha katikati ya magumu, ili kuwatumikia wengine na hivyo kutimiza mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo
Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo   (AFP or licensors)

Waamini wanakumbushwa kwamba, kazi ya imani inapaswa kuendelea, uchovu wa maisha ya kiroho ni neno la kweli na wala si nadharia inayoelea kwenye ombwe na kwamba, uvumilivu unalipa, daima waamini wajitahidi kutembea pamoja kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Kumbe, waamini wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika Jumuiya ndogondogo za Kikristo, vyama vya Kitume, wawajibike katika maisha na utume ndani ya familia, kanisa na jamii katika ujumla wake. Haya ni maeneo yanayoonesha umoja, ushiriki na ujenzi wa mafungamano muhimu sana kwa waamini wanapoonesha dalili za kukata tamaa! Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wake kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2026 linawahimiza waamini kutenda mema daima kama ushuhuda wa imani wanayosadiki, kuikiri na kuishuhudia hadharani. Hii ni imani inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Imani yenye nguvu inahusisha uelewa na kuikiri hadharani, kuishuhudia katika matendo ya kila siku. Kutenda mema ni mchakato wa kila siku unaofumbatwa katika maisha ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu; Kwa kuenenda katika Roho Mtakatifu: kwa kutenda haki, kupenda rehema na kujivika fadhila ya unyenyekevu bila kuchoka kusamehe, bila kulipa kisasi na wala kukata tamaa. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linawahimiza waamini kuyatakeleza mambo haya ili yawasaidie kuwa watu wema, waadilifu na watakatifu. Ujumbe wa Kwaresima uwakirimie watu wa Mungu nchini Tanzania matumaini, waishi kadiri ya mapenzi ya Mungu kwa kutenda mema na kusamehe; kamwe wasitake kulipiza kisasi wala kushindsana na mtu mwovu. Rej. Mt 5:38-39. Waendelee kukesha na wala wasichoke kwani wanaweza kuacha kutenda mema na kuzama katika kutenda mabaya. Waamini waendelee kutenda mema kwa imani, kwa upendo na nguvu inayopata chimbuko lake katika Jina la Kristo Yesu. Waamini wasichoke kumwomba Mwenyezi Mungu kuzitia moyo roho zao, hasa pale wanapokutana na: vikwazo na changamoto mbalimbali za: kiuchumi, migogoro katika maisha ya ndoa na familia; changamoto za mahusiano na afya, yote haya yasiwafanye wachoke kutenda mema!

Waamini wasichoke kutemda mema
Waamini wasichoke kutemda mema

Ufuatao ni ujumbe mzima wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Ujumbe wa Kwaresima 2026

1. Kwa neema ya Mwenyezi Mungu tunaanza kipindi kingine cha Mwaka wa Kanisa, kipindi kitakatifu cha Kwaresima. Kwaresima inatupatia fursa ya kujitengenezea mazingira mazuri ya kuwa karibu zaidi na Mungu na jirani. Ni kipindi cha siku arobaini ambazo kwazo msingi na maana yake inapatikana katika Maandiko Matakatifu. 

2. Maandiko Matakatifu yanasema mtumishi wa Mungu Musa kwa siku arobaini alikuwa mlimani akimsikiliza Mwenyezi Mungu na kuandika. Katika kipindi hicho alifunga kula na kunywa (rej. Kut 24:12-18). Hii inatufundisha kuwa hizi siku arobaini zina mchango mkubwa katika kurekebisha mwenendo wa maisha yetu tukiongozwa na Maandiko Matakatifu.  

3. Kwa siku arobaini tunaalikwa vilevile kutembea na nabii Eliya aliyetembea siku arobaini akielekea Mlima Horeb akimtafuta Mwenyezi Mungu; na baada ya siku hizo akawa amempata (rej. 1Fal 19:8). Sisi pia tuko katika safari ya kiroho kuelekea kuonana na Mungu mbinguni kama nabii Eliya alivyoelekea Mlima Horeb. Katika safari yetu ya kumtafuta Mungu tutakutana na milima na mabonde lakini tusikate tamaa tubaki tukiwa tumejizatiti kumtafuta Bwana. 

4. Haya yote yanapata mwanga kamili toka kwa Mwalimu wetu Bwana wetu Yesu Kristo aliyefunga siku arobaini akijiandaa kuanza kazi ya kuhubiri Habari Njema ya wokovu (rej. Mt 4:1-11). Ndani ya siku hizi arobaini tunatafuta nguvu ya kuishi maisha yetu kama wakristo imara wenye kulinda, kuthamini na kuishi ahadi zetu za ubatizo. 

5. Katika Kwaresima hii ya mwaka 2026, sisi Maaskofu wenu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, tukiongozwa na Wazo kuu la Mwaka wa Jubilei 2025 la Mahujaji wa Matumaini, tumeona ni vyema kuja na ujumbe unaosema “Ndugu, Msichoke Kutenda Mema” (rej. 2The 3:13). Wakati wa maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei 2025 tulijiwekea malengo mbalimbali ya kutusaidia kukua kiroho. Baada ya kufunga Mwaka wa Jubilei hatupaswi kurudi tena katika maisha ya kale. Tudumu katika kutenda mema haijalishi tunapitia katika majaribu gani tukitambua kuwa sisi ni Mahujaji wa Matumaini. Wazo hili linatualika pia kuendelea kutenda mema hata baada ya kipindi cha Kwaresima kwani wengi wetu kipindi cha Kwaresma tunaweka mikakati mizuri sana ya kuwa karibu zaidi na Mungu na jirani kwa kusali, kufunga na kufanya matendo ya upendo lakini baada ya Kwaresima tunarudi katika maisha ya giza. 

6. Katika Kwaresima hii tunaalikwa kuendelea kuwa mahujaji wa matumaini kwa kuendelea kutendeana mema na kusameheana bila kuchoka. Tunawatakia tafakari njema na mfungo mwema wa Kwaresima.   

Matendo mema ni ushuhuda wa imani tendaji
Matendo mema ni ushuhuda wa imani tendaji

 SURA YA KWANZA: KUTENDA WEMA: WITO KUTOKA KWA MUNGU UNAODAI BIDII YA BINADAMU 

Muktadha wa nukuu kadiri ya Maandiko Matakatifu 

7. Katika Kwaresima ya Mwaka huu 2026, ujumbe wetu Maaskofu unaongozwa na Kauli Mbiu isemayo: Ndugu, msichoke kutenda mema (rej. 2The 3:13). Nukuu hii ni sehemu ya ujumbe wa Mtume Paulo kwa Waamini wa Thesalonike. Pamoja na ukweli kwamba katika jamii hii watu wengi walijibidisha kutenda mema, lakini walikuwepo wengine ambao kwa bahati mbaya walikuwa ni wavivu na wala hawakuwa tayari kufuata mfano mwema wa Mtume Paulo; badala yake walijishughulisha tu na mambo ya watu wengine (vv.6-12). Mbaya zaidi, kwa tabia yao ya uvivu waliwakatisha tamaa wale ambao walikuwa na bidii ya kutenda mema. 

8. Katika muktadha huu, Mtume Paulo anawaandikia ujumbe wa matumaini na kuwatia moyo kwamba wasichoke kutenda mema. Hali kadhalika, anawahimiza kwamba hata katikati ya changamoto na kukatishwa tamaa, kamwe wasirudi nyuma bali wadumu katika maisha yanayompendeza Mungu. Zaidi sana, anawaalika wajione kuwa wao ni ndugu na kila mmoja amsaidie mwenzake kutenda mema. Daima wamkazie macho Kristo kupitia mfano mwema wa Mtume Paulo na wanajumuiya wengine wanaojibidisha kutenda mema.

Msingi wa Wito wa Kutenda Mema 

9. Mwaliko wa kutenda mema waweza kutafsiriwa kwa namna nyingine kuwa ni mwaliko wa kuwa watu wema au watakatifu. Wito huu wa kutenda mema una chimbuko lake kama maelezo yafuatayo yanavyotanabahisha: 

Mwenyezi Mungu ndiye chimbuko la wito huo wa kutenda mema kwani Yeye ni Mtakatifu na ubaya hauna nafasi kwake. Hata baada ya kazi ya uumbaji, kila kitu alichoumba kilikuwa chema sana (rej. Mwa 1:31). Ndio maana, katika liturujia ya Kanisa Katoliki, hususani katika Misa Takatifu, inasemwa hivi juu ya Mungu: “Ee Bwana, kweli u Mtakatifu na chemchemi ya utakatifu wote” na mahali pengine huelezwa hivi: “Ee Mungu, uliye makimbilio na nguvu yetu, uliye asili ya wema wote…” Hivyo, ubaya wote uliopo duniani hata sasa si kazi ya Mungu bali shetani.  

10. Maandiko Matakatifu yanashuhudia kuwa mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (rej. Mwa 1:26-27). Hivyo, ameitwa kuakisi sifa ya Mungu ya kuwa MWEMA, yaani kudumu katika kutenda mema. Kwa tafsiri pana zaidi, mwanadamu anaitwa kuwa mtakatifu au mkamilifu kama alivyo Muumba wake (rej. Mt 5:48). Hivyo, kuwa mwema au kutenda mema ni kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu. 

Uhuru wa mwanadamu wa kuchagua kutenda mema au mabaya 

11. Pamoja na kwamba wito wa kutenda mema una msingi wake katika Mungu mwenyewe, bado Mwenyezi Mungu katika mpango wake wa uumbaji amemkirimia mwanadamu akili na utashi vinavyompa uhuru wa kuweza kutambua mema na mabaya na kufanya uchaguzi wa lipi alitende kati ya jema au baya. (rej. KKK 1705, GS 17) 

12. Katika kulichuchumilia lililo jema, akili na utashi hutenda kwa ushirikiano. Kwa upande mmoja kazi ya akili ni kupambanua kati ya mema na mabaya ilhali utashi, kwa upande mwingine, humsukuma mtu kuchagua yaliyo mema na kuepa yaliyo mabaya. Mwanadamu hutenda hivi kwa kusukumwa na sheria ya maumbile (natural law) ambayo ni sauti ya Mungu ndani yake inayomsihi kutenda mema na kughairi mabaya. 

13. Hata hivyo, asili ya mwanadamu imejeruhiwa kwa dhambi ya asili. Hali hii humfanya mwanadamu awe na maelekeo ya ubaya na dhambi. Ili aweze kudumu katika kutenda mema lazima ategemee Neema za Mungu – ambazo ni msaada wake kwetu usiostahilika (KKK 1996) na kuweka jitihada, yaani, kutochoka kutenda mema. Ni kwa nini tunapaswa kutenda mema? 

Waamini wawe ni mashuhuda wa matendo ya huruma
Waamini wawe ni mashuhuda wa matendo ya huruma

a. Wajibu kwa Jirani  

14. Katika mpango wake wa uumbaji, Mwenyezi Mungu anampa kila mwanadamu dhamana ya kujishughulisha ustawi, uhai, haki, amani na wokovu wa mwenzake (rej. Mwa 4:9). Ndio maana, Kristo ametupatia kanuni ya dhahabu inayotudai kumpenda jirani yetu kama tunavyojipenda wenyewe (rej. Mt 7:12), yaani kudumu katika kutenda mema kwa wengine bila ubaguzi wowote ule. Na jirani ni yeyote yule anayehitaji msaada wako (rej. Lk 10:30 – 37). Kwa kuwa ni mwaliko wa Mungu kuwa kila mwanadamu anapaswa kujali ustawi wa mwenzake, na kwa kufuata kanuni ya dhahabu tuliyoitaja hapo juu, mwanadamu hapaswi kumtendea ubaya mwanadamu mwenzake ambaye kimsingi ni ndugu yake kwani sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.   

15. Katekisimu ya Kanisa Katoliki (KKK 360) inafundisha kuwa: “Kwa sababu ya kuwa na chanzo kimoja, yaani Mungu, kizazi cha mwanadamu kinafanya umoja, kwani ‘naye Mungu alifanya kila taifa la mwanadamu kutoka umoja’. (Mdo 17:26)”; “Sheria hii ya mshikamano wa wanadamu na ya upendo, bila kuacha utajiri wa tofauti za watu, za tamaduni za mataifa inatuhakikishia kuwa watu wote ni kweli ndugu” (KKK 361). Kwa msingi wa undugu huu, tunaalikwa tusichoke kutendeana mema. 

16. Lakini ni kwa nani tunapaswa kutenda mema? Mtume Paulo anafuata maagizo yake: "Kwa hivyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, na hasa jamaa ya waaminio." (Gal 6:10).  Kwa furaha, Mtume Paulo hazuii mwito wetu wa kuzaa matunda kwa nyanja moja ya ushawishi au kikundi cha watu. Ingawa anatufundisha kuwatanguliza ndugu na dada zetu katika Kristo (hasa nyumba ya Imani), anapanua wigo wa matendo mema na kujumuisha kila mtu (rej. 1The 5:15). Matendo mema yanaweza kuchukua namna ya kutoa mahitaji ya haraka ya kimwili (rej. Tit 3:14), kulea watoto, kuhudumia waamini, kutunza walio na taabu, na kuonyesha ukarimu (rej. 1 Tim 5:10). Tunafanya mema kwa kufanya kazi bora kwa mwajiri wetu, kwa umma na serikali (rej. Efe 6:5-9), tukionyesha ukarimu (rej. 1 Tim 6:18) na maelfu ya njia nyinginezo (rej. Efe 2:10; Tit 2:14).  

b. Tamanio la Kufika Mbinguni 

17. Katika moja ya mafundisho msingi ya Kanisa Katoliki, tunafundishwa ni kwa nini Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu. Lengo lenyewe ni kusudi mwanadamu amjue, ampende, amtumikie na hatimaye afike kwake mbinguni (rej. KKK 1). Ndio maana Mtume Paulo anahimiza kuwa hapa duniani tunapita na wenyeji wetu uko mbinguni (rej. Fil 3:20). Tena Mtakatifu Agustino anahimiza kuwa tuwapo hapa duniani roho zetu hazitatulia, hadi zitakapotulia mkononi mwa Mungu.

18. Kitabu cha kwanza sura ya kwanza). Hivyo, tunaalikwa kudumu katika kutenda matendo mema ili kujiwekea hazina mbinguni (rej. 1Tim 6:17-19) hali tukitambua kuwa Mwana wa Adamu ajapo, atamlipa kila mtu kadiri ya matendo yake (rej. Mt 16:27).  

19. Amri, "Tena tusichoke katika kutenda mema, maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho” (Gal 6:9). Maneno “maana” yanaonesha kwamba Mtume Paulo anatupa sababu ya kutia moyo kwa nini ni lazima tutii himizo lililotangulia. Katika muktadha huu, motisha katika ahadi ya masharti ya baadaye ni kwamba tutavuna endapo tutatekeleza agizo hilo la kutenda mema. Pia, Mtume Paulo anatuambia: “maana yeye apandaye kwa mwli wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele” (Gal 6:8). Asiyekata tamaa katika kutenda mema atavuna uzima wa milele. Lakini anayeacha kutenda mema atavuna ufisadi au uharibifu (rej. Lk 12:33; Rum 8:21; 1Kor 15:42,50; Kol 2:22; 2 Pet 2:12).  

Waamini wawe ni mashuhuda wa imani tendaji
Waamini wawe ni mashuhuda wa imani tendaji

Sababu za kujisikia kuchoka kutenda wema 

20. Katika maisha ya mwanadamu, ziko sababu nyingi ambazo zinaweza kumfanya ashindwe kutenda mema. Miongoni mwa sababu hizo ni hizi zifuatazo: 

a. Maelekeo binafsi ya dhambi 

21. Kama ilivyodokezwa tayari, asili ya mwanadamu imedhoofishwa na kujeruhiwa kwa dhambi ya asili na hivyo kumfanya awe na maelekeo ya dhambi (KKK 405, 418).  

Lazima mwanadamu aendelee na mapambano dhidi ya maelekeo haya mabaya (KKK 2520) huku akitegemea neema za Mungu. 

b. Ushawishi mbaya kutoka katika jamii inayomzunguka (jirani zake)   

22. Mwanadamu haishi kama kisiwa, bali ni mwanajamii. Katika kuhusiana na wengine, ziko nyakati kabisa ambapo mwenendo usiofaa wa wengine waweza pia kumuathiri. Kama Nabii Isaya alivyojieleza kuwa anaishi kati ya watu wenye midomo michafu na kuathiriwa binafsi, kadhalika yaweza kuwa hivyo kwa yeyote (rej. Is 6:5).    

23. Pale tunapoishi katika jamii iliyojaa ‘uchafu’ wa aina mbalimbali kama vile lugha mbaya, kutoheshimu amri za Mungu, kutothamini utu wa wenzetu na nafasi ya maumbile (creation), kutoheshimu sheria na miongozo mizuri ya kijamii, tukitaja kwa uchache; hayo yaweza kuathiri tabia zetu tusipokuwa makini. Endapo katika jamii, dhambi na ubaya vinachukuliwa kuwa ndio mtindo wa maisha, iko hatari ya kutekwa na maelekeo hayo na kushindwa kudumu katika kutenda wema. 

24. Hivyo, tuchague kumpendeza Mungu sio wanadamu! Mithili ya Mt. Veronica (kama tunavyotafakari katika Kituo cha Sita cha Njia ya Msalaba), nasi tumuombe Mungu atujalie kujua jema tunalopaswa kutenda na kulitenda bila kujali au kuogopa macho na maneno ya watu waovu. Tena, atujalie ushupavu na ujasiri wake wa kutenda mema (rej. Misale ya Waamini uk.1119). 

Kutenda wema ni wito endelevu unaodai sadaka
Kutenda wema ni wito endelevu unaodai sadaka

Kutenda Wema ni Wito Endelevu Unaodai Sadaka 

25. Wito wa kudumu katika kutenda mema unaweza kutafsiriwa kwa lugha nyingine kuwa ni wito wa kudumu katika kutimiza mapenzi ya Mungu, yaani, kudumu katika maisha ya utakatifu. Ni wito wa kumpa Mungu nafasi ya kwanza katika maisha yetu na kuwatanguliza wengine kabla ya kujifikiria kwanza sisi wenyewe. Yeyote yule anayezingatia wito huu kwa vipimo hivi ana kila haki ya kuitwa mfuasi wa Kristo.   Kristo Mwenyewe anatoa masharti mahususi kwa yeyote yule anayetaka kuwa mfuasi wake: “mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate” (Mt 16:24). Sharti hilo la mtu kujikana, na kuwa tayari kujisahau mwenyewe kwa faida ya mwingine, ni tendo la kujitoa sadaka. Kama Kristo alivyokuwa tayari kupitia mateso na hatimaye kifo cha aibu msalabani kwa faida yetu sisi wadhambi, ni wito wa kila mmoja wetu kuwa tayari kuteseka kwa kutenda mema kwa faida ya jirani (rej. Mt 25:40).  

26. Mafundisho ya ulimwengu wa leo yamejikita katika injili ya mafanikio zaidi bila ya kuhusisha dhana ya Msalaba na maisha yajayo. Pamoja na kuhitaji mafanikio ya kiinjili kwa ulimwengu huu, waamini wote tunaalikwa kutafakari umuhimu wa Msalaba na Mateso yatokanayo na Msalaba huo, bila kusahau kushikilia tumaini la thawabu ya wakati ujao ambalo Mungu amewaahidi wale wanaodumu katika kutenda mema. Kimsingi, aya hii “Ndugu, msichoke kutenda mema” inawatia moyo waamini kuendelea kwa imani na ustahimilivu wakitumaini kwamba bidii yao katika Bwana haitakuwa bure. 

27. Kwa hiyo, hatupaswi kukata tamaa katika kutenda mema kwa sababu kukata tamaa ni dalili kwamba hatuelekei uzima wa milele. Tunaporuhusu magumu na majaribu ya maisha yatufanye tuache kuhudumia wengine na kumezwa na sisi wenyewe, tunapanda kwa mwili. Mtu ambaye ana sifa ya kujitolea kwa nafsi yake mwenyewe anatoa uthibitisho kwamba hajakaliwa na Roho anayezaa matunda ambaye kipaumbele chake cha kwanza ni kutengeneza upendo unaolenga katika maisha ya muamini (rej. Gal 5:22-23; taz. 2 Tim 3:2). 

28. Kudumu katika kutenda mema kunawezeshwa na Roho Mtakatifu kwa sababu tutavuna urithi wa milele ambao utafanya shida zote kuwa na thamani yake (rej. 2 Kor 4:16-18). Paulo Mtume anamalizia sura yake juu ya ufufuo kwa maonyo haya: “Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana siku zote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana” (1Kor 15:58). Imani katika urithi usioharibika inatualika kuendelea katika njia ya utii na kuzaa matunda. 

Matendo mema ni nafasi ya kumweka Kristo katika maisha
Matendo mema ni nafasi ya kumweka Kristo katika maisha

SURA YA PILI: MATENDO MEMA KATIKA MAANDIKO MATAKATIFU KAMA USHUHUDAWA IMANI: Matendo Mema ni Nafasi ya Kumweka Kristo Katika Maisha 

29. Dunia inapositawi sana katika maendeleo huzaa mambo mazuri na mabaya pia. Katika mabaya, ustawi husababisha miongoni mwa wanajamii kumsahau Mungu na kuanza kutenda maovu, kuwakandamiza, kuwanyonya na kuwaonea wengine. Katika hali kama hiyo wajibu wa Kanisa ni kupaza sauti ya kinabii na kuiamsha jamii na kuhimiza watu watende mema na kuzingatia haki. 

30. Neno la Mungu, iwe katika Agano la Kale au Agano Jipya, linamkataza kila mwanadamu kufanya matendo mabaya na linamtaka kutenda mema siku zote. Ni agizo la Mungu kwamba kila mwanadamu aache mabaya na atende mema, kwani matendo mabaya yote yanatuingiza kwenye dhambi na kumuasi Mungu na matokeo yake tunakosa nafasi katika uzima wa milele (rej. Zab 34:14; Amo 5:15). 

31. Ni kusudi la Mungu kwamba wanadamu wote wawatendee wengine jinsi ambavyo wao wenyewe wangetaka watendewe. Aliweka kielelezo kizuri sana cha kuonyesha anajali maslahi ya wengine kwa jinsi alivyowaumba wanadamu. “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba; mwanaume na mwanamke aliwaumba” (Mwa. 1:27). Hiyo inamaanisha kwamba, kwa upendo Mungu aliwapa wanadamu dhamiri, ambayo inapozoezwa vizuri, ingesaidia kuwatendea wengine jinsi ambavyo wao wenyewe wangetaka watendewe.   

32. Katika Agano Jipya tunahimizwa sana pia kutenda mema. “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema na hasa jamaa ya waaminio” (Gal. 6:9-10). Kwa sababu hii, mkristo unaalikwa usiache kufanya matendo mema, kwani ndio nafasi ya kumweka karibu Yesu Kristo katika maisha yako. 

33. Katika kipindi hiki cha Kwaresima, kwa namna ya pekee zaidi, kila mmoja anaalikwa kutenda mema. Mwaliko huu wa Mtume Paulo unamtaka kila mmoja kuwa tayari kutoa mali zake, ashirikiane na wengine kwa moyo kama akiba ya msingi mzuri na imara kwa wakati ujao na kujipatia uzima ulio kweli (rej. 1Tim 6:18). Ili mwanafunzi wa Kristo awe kamili yampasa kutenda kila tendo jema katika mwito wake. 

34. Nyakati zetu hizi pengine kuliko nyakati nyingine zote za maisha na utume wake, Kanisa linashuhudia hitaji kubwa la maisha ya ushuhuda wa kiimani katika kutafuta mambo mawili yanayosimama pamoja ambayo ni haki na kutenda mema. Kwa mambo haya, Kwaresima hii sisi wachungaji wenu wakuu tunawahimiza na kuwaalika ninyi nyote kujenga msingi wa uwiano wa ongezeko la wanaomwamini Kristo na ongezeko la matendo mema, matendo ya huruma na kukua kwa upatikanaji na utoaji wa haki. 

Matendo mema ni Amri na Maagizo ya Kristo Yesu
Matendo mema ni Amri na Maagizo ya Kristo Yesu

Matendo Mema ni Kushika Amri na Maagizo ya Kristo Yesu.

35. Ni dhahiri kwamba kumwamini Kristo ni kushika amri na maagizo yake; na agizo kuu analotupatia ni kupendana. Tusisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu (rej. Ebr 13:16). Matendo mema ni moja ya vigezo vya mwamini kukubalika na Kristo mwenyewe.  Mfano wa mtumwa wa Akida aliyekuwa hawezi na yu karibu na kufa, naye ni mtu aliyempenda sana. Lakini aliposikia kwamba Yesu yupo katika mji huo aliwatuma wazee wamwendee na kumsihi Yesu amponye mtumwa wake. Wazee mbele ya Yesu walimnadi Akida kwa kueleza wema wake mbele za Bwana na kwa wenzake, kwamba mtumwa wake alistahili kuponywa kutokana na matendo mema ya Akida yule, na Bwana akakubali kumponya (rej. Lk 7: 2- 6). Hivyo ndugu tusichoke kutenda mema. 

36. Kumuamini kwetu Kristo kuambatane kikamilifu na matendo mema na kushika amri zake (rej. Yn. 14:15). Matendo mema yasisimame peke yake, mfano mtu akajitolea sana kwa watu kwa ajili ya matatizo yao, akasaidia sana yatima, wajane, akasaidia sana wasiojiweza na wazee, yote hayo yatakosa ukamilifu bila kumkiri Bwana Yesu kwamba ni Bwana na Mwokozi wa ulimwengu. Mtume Yohane katika Barua yake ya kwanza kwa watu wote anasema “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?” (1 Yoh 3:17-18).  

Matendo Mema Yanatoa Ushuhuda wa Imani 

37. Katika Maandiko Matakatifu, Bwana anatuonya na kutufundisha kwa maneno na mifano mbalimbali kama mfano wa tajiri na maskini (rej. Lk 16:19-31) na kama ilivyo pia kwa mfano wa hukumu ya mwisho - nalikuwa na njaa, ukanilisha, nalikuwa uchi ukanivika, nalikuwa na kiu ukaninywesha, nalikuwa mgonjwa ukaja kunitazama, nalikuwa mgeni ukanikaribisha, nalikuwa kifungoni ukanijia (rej. Mt 25:31-46).  

38. Matendo mema yanapofuata mwongozo wa Kristo ni dhahiri kwamba yatatoa ushuhuda wa imani yako kwa Kristo mwenyewe. Yakobo Mtume anasisitiza na kutuasa kwa maneno mazito: “Ndugu zangu, yafaa nini mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je, ile imani yaweza kkumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kapungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akamwambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaaa ini?  Vivyo hivyo na imani isipokuwa ina matendo, imefufa nafsini mwake” (Yak 2:14-17).  

39. Yakobo Mtume hasemi kwamba matendo yetu hutufanya kuwa waadilifu mbele za Mungu bali kwamba imani ya kweli yenye kuokoa inaonyeshwa kwa matendo mema. Imani katika Kristo daima husababisha matendo mema. Matendo mema ni ushahidi wa wokovu. Mtu anayedai kuwa mkristo lakini hamtii Kristo kwa makusudi ana imani ya uongo au iliyokufa. Mtume Yakobo anabainisha aina mbili tofauti za imani - imani ya kweli iokoayo na imani potofu ambayo imekufa (rej. Yak 2:17).  

Kila Mtu Atahukumiwa Kwa Matendo Yake Mwenyewe 

40. Matendo ya mtu, yawe mema au mabaya, ndiyo kipimo cha mastahili yake, kila mtu atahukumiwa kwa matendo yake mwenyewe. Ujumbe huu wa Kwaresima unatualika kuchagua kutenda mema, kwa sababu Bwana atamlipa kila mtu kulingana na matendo yake (rej. Mt 25:31-46). Na kibali cha kuingia katika ufalme wa mbinguni ni kuyafanya mapenzi ya Mungu. Yesu anasema, “vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mt 5:16). Ujumbe katika kipindi hiki cha Kwaresima unatualika sote kamwe tusichoke kufanya matendo mema. 

41. Pamoja na ukweli kwamba leo hii tunashuhudia ongezeko la watu, makundi ya watu na taasisi zinazojishughulisha na kuwasaidia wahitaji, lakini pia tunashuhudia wengi wa watu hao na taasisi hizo zikiwatumia wahitaji ili kujinufaisha wao zaidi ya walengwa. Upendo na matendo mema kwa wenzetu haupatani na ubinafsi unaopelekea kujilimbikizia mali na matumizi yake ya choyo. 

42. Matendo mema yanapokosekana huzaliwa ubinafsi na uchoyo ndani ya jamii. Hali hii inapokithiri huathiri sana jamii yetu kiasi cha kubadili hata mifumo ya kiutendaji ili kuwalinda wachache wenye mali na nguvu ya madaraka. Mwelekeo huu umeshusha thamani ya utu na kupumbaza fikra za wengi kiasi cha kuelekea kuamini kuwa walionacho kingi hata kama hawajakipata kwa njia halali ndio wenye haki ya kufanya chochote wapendacho dhidi ya wengine.  Jinsi hii ya kuendeleza ubinafsi na uchoyo badala ya kutenda wema kwa wengine inaelekea kumeza malengo makuu ya maisha ya mwanadamu wa leo kama Mungu alivyoyakusudia. Hivyo, kila mmoja atambue kuwa matendo yake ndiyo yatakayomuhukumu siku ya mwisho mbele ya Mungu (rej. Mt 25:31-46).  

43. Tunaalikwa wanafamilia ya Mungu kuziepuka nyakati ambazo ukatili na kutothaminiana vinachukua nafasi kubwa ya maisha ya binadamu kuliko wito tulioitiwa wa kutenda mema. Tukumbuke kuwa tutahukumiwa kadiri ya matendo yetu. Haitoshi kuwa umebatizwa tu ili kuingia mbinguni, matendo yako mema yashuhudie imani yako katika Kristo. Sio kila anayesema Bwana Bwana ataingia katika ufalme wa Mungu bali ni yule anayetimiza mapenzi ya Baba yetu wa mbinguni (rej. Mt 7:21). Kuingia mbinguni au motoni unachagua wewe mwenyewe kwa namna ya maisha yako ya sasa. Mpende Mungu na jirani uingie uzimani. Matendo mema hayaozi, hata kama hakuna aliyeona, Mungu huona na kuyahesabu na kuyawekea akiba.  

Waamini  msichoke kutenda mema
Waamini msichoke kutenda mema

 Msiache Kutenda Mema na Kusamehe 

44. Tunapoalikwa kuzingatia haki na kutenda mema, wakati huo huo, tunaalikwa pia kutafuta upatanisho kati yetu na Muumba wetu na kati yetu sisi wenyewe kwa kuwa tayari kusamehe na kuomba msamaha pale tulipokosea. Ni dhahiri kuwa Mungu ndiye asili na chimbuko la msamaha na kwamba ni vigumu kwa hulka yake, binadamu kuweza kusamehe kirahisi. Familia nyingi zinasambaratika kutokana na wanandoa kushindwa kutoa au kupokea msamaha.  

45. Kuzingatia haki na kusamehe ni kutenda mema. Tusipokuwa tayari kuwasamehe waliotukosea, tunajifungia milango ya kupokea msamaha wa dhambi zetu kutoka kwa Mungu Mwenyezi (rej. Mt. 6:12, 14-15). Mara nyingi mioyo yetu imekuwa migumu ikijitwika chuki, kinyongo na roho ya kisasi kwa waliotukosea pamoja na kwamba hata sisi wenyewe si wenye haki mbele ya Mungu.  

46. Katika Maandiko Matakatifu tunapata mifano mingi ya ukarimu na kuwatendea wengine mema yalifanywa na wale walioshika na kushuhudia imani yao kwa Mungu. Kwa uchache tunaweza kutaja vifungu vifuatavyo kama mfano wa namna tunavyoweza nasi kuwatendea wenzetu mema; 

47. Ukarimu wa Ibrahimu (rej. Mwa 18:1-8): Fungua nyumba na moyo wako kwa wengine, hata wakati unahisi usumbufu. Karibisha na uwajali watu wanaokutembelea, ukiwafanya wajisikie kuwa wa thamani na kupendwa. Huwezi kujua kuna wakati unaweza kuwakaribisha malaika pia. 

48. Mjane wa Sarepta aliyeaminiwa (rej. 1 Fal 17:7-16): Usiruhusu visingizio vyako vikuzuie kutoa kwa ukarimu na hivi kupata baraka zinazotokana na kutoa kwako kwa ukarimu. 

49. Wema wa mwanamke Mshunami kwa mjumbe wa Mungu (rej. 2 Fal 4:8-37): Fanya mapinduzi ya namna unavyotoa kwa kupanga utoaji wako kwa watu kama zawadi inayotolewa kwa Mungu. 

Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote
Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote

Sadaka ya mwanamke mjane (rej. Mk 12:41-44): Ukarimu wako ni muhimu, bila kujali ukubwa wa zawadi yako. 

50. Kijana aliyetoa mikate mitano ya shayiri na samaki wawili (rej. Yn 6:5-13): Kuwa tayari kushirikisha kile ulicho nacho, hata kama kinaonekana kuwa kidogo, ukijua kwamba Mungu ni mzidishi wa karama.  Wema wa Dorkasi aliyetumia kipaji chake cha ushonaji katika kusaidia wahitaji (rej. Mdo 9:36-42): Tumia kipaji chako kwa kusaidia wengine. 

 

SURA YA TATU: MATENDO MEMA KAMA MUENDELEZO WA MWAKA MTAKATIFU: Yatokanayo na Mwaka Mtakatifu 2025 

51. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei Kuu 2025, yenye mada Mahujaji wa Matumaini, yanahimiza masuala kadhaa muhimu: 

·        Upyaisho wa Kiroho

Wakatoliki tunaalikwa kuiishi upya imani yetu na kueneza tumaini kwa ulimwengu mzima. Tuendelee kujihusisha na maandiko, maombi, na sakramenti, tukiimarisha uhusiano wetu na Mungu.  

·        Msamaha na Upendo

Mwaka wa Jubilei Kuu 2025 ulitilia mkazo upokeaji wa sakramenti ya Upatanisho na kurudisha uhusiano mwema na Mungu pamoja na jirani. 

·        Matumaini na Mshikamano

Jubilei Kuu ya 2025 ilitupatia matumaini mapya katika kuishi imani yetu licha ya changamoto mbalimbali za ulimwengu wa leo. Aidha, ilituhimiza kuishi katika upendo, umoja na mshikamano. Mwaka wa Jubilei 2025, ulihimiza sio tu Wakatoliki bali pia Wakristo wote kutumainia maongozi ya Mungu, kutoa tumaini kwa wengine, na kuimarisha imani yao. Vile vile, baraka za kiroho za baada ya Jubilei hutoa ujumbe wenye nguvu wa amani, kuwakumbusha waamini kwamba amani ya kweli inatoka kwa Bwana mwenyewe ambayo kwa upande wetu tunapaswa kuidumisha.  

·        Wajibu wa Kiikolojia

Jubilei Kuu 2025 ilisisitiza utunzaji wa uumbaji ili kudumisha mahusiano mazuri kati yetu sisi na mazingira yanayotuzunguka kwa faida yetu na ya vizazi vijavyo. 

·        Kukuza Jumuiya

Waamini waendelee kujenga jumuiya imara, zinazosaidiana na zinazohimizana katika kutenda mema na kuishi kwa imani yao. Mwaka wa Jubilei sio mwisho wa kuzingatia uhusiano wetu na mazingira na sisi kwa sisi, bali ni kuendelea kuishi kwa njia inayozingatia yote mawili, kukuza jamii na kutunza dunia yetu.  

·        Msaada kwa Wahitaji

Jubilei Kuu 2025 ilitualika waamini kushiriki katika matendo ya upendo wa kiinjili kwa wahitaji ambayo ni: 

Ya kimwili: kulisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwavika walio uchi, kuwakaribisha wageni, kuwaponya wagonjwa, kuwatembelea wafungwa na kuwazika wafu. 

Ya kiroho: kuwashauri walio mashakani, kuwafunza wajinga, kuwaonya wadhambi, kuwafariji waliojeruhiwa, kusamehe maovu, kuchukuliana kwa saburi na wale waliotutendea maovu na kuombea walio hai na wafu. 

Aidha, kila muamini anahimizwa kushiriki katika vitendo vya huduma, hasa kujitoa talanta zake na kuunga mkono mashirika ya kutoa misaada hasa yale yaliyo chini ya Kanisa kama vile Caritas. 

·        Hija na Sala

Mahujaji walihimizwa kutembelea maeneo matakatifu yaliyotengwa, kushiriki katika shughuli za kiroho, na kuomba rehema na huruma ya Mungu kwa lengo la kukuza maisha ya sala ya mtu binafsi na vikundi na kutafakari Maandiko ili kuimarisha uhusiano wa mwanadamu na Mungu. Kwaresima hii iwe nafasi kwa kila mmoja wetu ya kutafakari juu ya safari ya imani, akitafuta uhusiano wa ndani zaidi na Mungu na kujitahidi kuendelea kuishi katika matumaini. 

Huduma kwa wafungwa ni ushuhuda wa upendo na mshikamano
Huduma kwa wafungwa ni ushuhuda wa upendo na mshikamano

Matukio Makuu ya Mwaka Mtakatifu 2025 

52. Katika kuadhimisha Jubilei Kuu ya Mwaka 2025, yalifanyika mazoezi mbalimbali ya kiroho, zikiwemo hija kwa makundi mbalimbali. Je, wewe binafsi ulishiriki kikamilifu katika moja ya makundi yaliyokuwepo? Na kama ulishiriki kikamilifu, je, unahisi ulivuna kitu chochote? Kufungwa kwa Jubilei 2025 hakumaanishi kumalizika kwa safari ya kiroho ya kuutafuta utakatifu bali ni mwanzo wa maisha mapya.  Na kama hukushiriki tukio lolote, mwaka huu uwe fursa mpya ya kujitathmini nafasi yako mbele ya Mungu, na kujitahidi kutafuta wasaa wa tukio la kibinafsi linalofanana na hilo.  

Ndugu, Msichoke Kutenda Mema 

53. Kauli mbiu Ndugu, msichoke kutenda mema (rej. 2 The 3:13) inatukumbusha umuhimu wa kudumu katika huduma za kikristo hata baada ya kipindi cha sherehe za maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei 2025. Inatuangazia pamoja wakristo wote tusipoteze motisha na shauku ya kutenda mema, na kututia moyo kubaki imara katika kujitolea kwetu kumtumikia Mungu na jirani. Ustahimilivu huu unahusishwa na ahadi na thawabu ya wakati ujao, na kuwahakikishia waamini na watu wote kwamba kutenda mema si kazi bure. 

54. Sisi Maaskofu wenu tunapenda mzingatie kwamba, sehemu hii ya Maandiko Matakatifu, “Ndugu, msichoke kutenda mema” ni mwito wa kutenda unaojikita katika kuelewa kwamba maisha ya imani katika Kristo ni safari, si marudio. Ingawa maadhimisho ya Jubilei yaliweza kutuletea hali ya upyaisho na msisimko mpya wa maisha ya imani, hali halisi ya maisha ya imani ni ya kila siku, pamoja na changamoto na matokeo yake kiasi kwamba uchovu na kuvunjika moyo daima kupo. Hii ni kweli hasa katika muktadha wa kuwahudumia wengine. Maisha ndani ya Kristo ni kutokuchoka tukitambua kwamba maisha daima yana changamoto, lakini lazima tuwe na ustahimilivu kupitia imani na matumaini, furaha katikati ya magumu, kusudi la kuwatumikia wengine na kutimiza mpango wa Mungu. 

55. Maisha ndani ya Kristo yanatoa msingi wa kukabiliana na matatizo ya maisha kwa imani, matumaini na mapendo. Ushauri wa Mtume Paulo katika Wagalatia 6:9, na vifungu sawa katika 2 Wathesalonike 3:13, ni ukumbusho kwamba: 

·        Kazi ya Imani inaendelea   

Hata baada ya kupata hali ya juu ya kiroho, maisha ya kikristo yanahitaji jitihada thabiti na kujitolea kwa kazi nzuri. 

·        Uchovu wa Kiroho ni Neno la Kweli  

Wanadamu, hata wale wanaosukumwa na imani, kuna kukata tamaa na kuchoka katika kutenda mema. 

·        Umilivu hulipa   

Mungu anaahidi mavuno kwa wale wasiokata tamaa, akiwatia moyo waamini kuendelea kuvumilia kwa bidii. (rej. Mt.24:13) 

56. Hivyo basi, baada ya Jubilei, waamini wote wanaalikwa kutafakari kile kilichochochea shauku yao wakati wa Jubilei na jinsi wanavyoweza kuunganisha nguvu na shauku hiyo katika maisha yao sasa na ya siku zijazo. Jubilei ilikuwa ni mwaka wa kujitolea katika kutoa huduma mbalimbali hasa kwa wahitaji; ni vema kutambua kwamba, wito wa kutenda mema kikomo chake sio mwisho wa Mwaka wa Jubilei, ila unaendelea zaidi ya kipindi cha sherehe za Jubilei na hata kuongeza jitihada zaidi za majitoleo hayo matakatifu. 

Umuhimu wa Kutembea Pamoja  

57. Sinodi ya Maaskofu juu ya Kanisa la kisinodi inatuhimiza sisi waamini kutembea pamoja katika safari ya imani. Mwenye imani thabiti ndiye apataye majaribu zaidi ya kukatisha tamaa na kuvunja moyo. Wewe mtu wa imani, wategemee waamini wenzako kwa ajili ya kutiwa moyo na kuwajibika, ukitambua kwamba safari ya imani ni bora zaidi katika kutembea pamoja. Zingatia kwa makini ushiriki wako katika Jumuiya Ndogondogo za Kikristo, Vyama vya Kitume; wajibu wako wa uongozi ndani ya familia, Kanisa, kwenye jamii, na mahali pengine popote unapokabidhiwa majukumu. Ndani yake sehemu hizo, utapata usaidizi wa kukutia moyo pale unapoelekea kukata tamaa. 

Basi Ndugu Tutende mema daima
Basi Ndugu Tutende mema daima

           SURA YA NNE: BASI, NDUGU TUTENDE MEMA DAIMA

58. Wapendwa, baada ya kusoma hizi sura tatu za mwanzo, sura hii ya nne inakuwa ni kujibu nini tufanye ili katika mfungo wetu huu wa Kwaresma, hata baada yake, tuwe mashahidi wa Injili ya Kristo, sio tu kwa kuitangaza imani yetu kwa maneno lakini pia kwa kuiweka katika matendo yetu ya kila siku. Kwa maneno mengine, tuwe mashahidi kweli wa Kristo kwa kuwa sio wanenaji tu bali watendaji pia. Hili litadhihirika, pamoja na mengine, kwa kuwatendea watu mema daima.  Kabla ya kuona tufanye nini ili tuweze kuwa mashahidi wa matendo mema pasipo kukata tamaa ni vyema tukatafakari kidogo uhusiano uliopo katika ya imani tunayosadiki (maneno) na imani tunayoishi (matendo). 

59. Dhana ya "imani tunayosadiki" (maneno) na "imani tunayoishi" (matendo) inakazia tofauti kati ya imani ya kutamka kwa maneno na imani ya ushuhuda wa matendo mema. Kuna tofauti kati ya kudai imani katika jambo fulani (mfano dini) na kutekeleza imani hiyo katika maisha ya kila siku. Hivyo, kuna tofauti kati ya Imani ambayo kwayo tunatamka na Imani ambayo kwayo tunayoishi ingawa haya mawili yanakamilishana. 

Imani Tunayosadiki 

60. Hii inajidhihirisha katika kukiri na kutangaza kwa maneno au kuthibitisha hadharani kuyaamini mafundisho fulani hususani ya dini. Ni tamko la hadharani la imani ya mtu hasa kuhusu mambo ya dini. Hii inajitokeza hasa katika kukariri mafundisho fulani ya dini, kushiriki katika sherehe za dini hiyo, au kujiambatanisha na kikundi fulani cha kidini. Ni imani inayoonekana katika kutamka, kuikiri na katika kushiriki taratibu na sheria za kiibada ya imani hiyo.  Kwa Nini Kukiri Imani Hadharani? 

61. Katika ya changamoto kubwa katika karne hii tunayoishi ni swala la ulazima na umuhimu wa kukiri imani hadharani. Wapo ambao wanadai ni wakristo lakini hawaonekani katika mazoezi yoyote ya kiroho na mbaya zaidi hawafiki hata kwa maadhimisho ya Misa siku za Dominika au kushiriki Jumuiya Ndogondogo za Kikristo kwa maelezo kwamba wanasali kwa namna yao nyumbani. Swali moja la kujiuliza hapa, je ni lazima kukiri imani hadharani?  Kwa kifupi ni kwamba kukiri imani hadharani ni kitu ambacho sio tu muhimu, bali ni lazima katika maisha ya ufuasi ya mbatizwa. Ni lazima kufikia wakati ambapo mtu anapaswa kutangaza wazi na kibinafsi kile anachoamini. Haitoshi kuwa na jina lako limeandikwa kwenye kitabu cha Ubatizo katika parokia mahali fulani wakati hauwezi kukiri imani hiyo hadharani. Haitoshi kwa kila mtu kudhani kuwa wewe ni mfuasi kwa kuwa tu ulibatizwa wakati fulani. 

62. Wale ambao wamezaliwa upya katika Ubatizo na wanaomcha Mungu na hasa wale ambao wamepokea sakramenti ya Ubatizo wakiwa watoto wachanga, wanapaswa kuonyesha kwamba wameifanya imani ya kikristo kuwa yao ikizingatiwa kuwa walibatizwa wakiwa hawana uwezo wa kukiri imani wao wenyewe. Ni kwa msingi huu, Maandiko Matakatifu yanatuambia, “Na tushike kwa uthabiti imani tunayokiri” (Ebr 4:14) na, “Tushike bila kuyumba tumaini tunalokiri” (Ebr 10:23). 

63. Sasa, kwa kujibu wale ambao wanasisitiza kuwa kwa nini suala la imani haliwezi kubaki kuwa jambo la kibinafsi au kwa nini ni lazima lifanywe hadharani? Jibu la hili liko katika maneno ya Bwana Yesu yanayopatikana katika Luka 12:8-10. Hapo anazungumza kuhusu “Yeyote anayenikiri mbele ya watu” nami nitamkiri mbele ya Malaika wa mbinguni (rej. Lk 12:8;). Kristo anatuasa kukiri imani yetu mbele ya Kanisa na mbele ya watu. 

Imani tunayoishi (matendo) 

64. Changamoto ya pili inayojitokeza kwa kasi katika zama zetu hizi ni pale mmoja anapoacha kukiri imani yake na kuacha shughuli nyingine zote za kiibada akieleza kuwa hana shida ya kushikamana na imani yoyote kwani kwake yeye ni matendo tu ndiyo muhimu. Je, kwa ajili ya wokovu wetu, matendo mema peke yake yanatosha au tunahitaji kuwa na imani pia? Jibu ni kwamba matendo peke yake bila imani hayatuokoi.  

65. Ingawa matendo mema mara nyingi huonekana kama dhihirisho la imani na matokeo chanya ya maisha ya kiroho, sio njia pekee ambayo mtu anaokolewa nayo. Wokovu kwa ujumla hueleweka kuwa ni zawadi inayopokelewa kwa njia ya imani katika nguvu ya juu zaidi (neema ya Mungu), isiyopatikana kwa matendo peke yake. Paulo Mtume anatuambia “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu” (Efe 2:8-9). 

66. Dhana hii ya kusadiki na kutenda inatuonyesha jinsi imani ya mtu inavyoongoza matendo yake, machaguo yake na tabia yake katika maisha ya kila siku. Ni imani ndiyo inatuongoza katika mahusiano yetu kama wanadamu, maamuzi tunayofanya, na mtindo wa maisha kwa ujumla kwa mfano kuwahurumia wengine, kutenda kwa uadilifu, kutenda mema au kufanya chaguzi kadiri ya sheria na kanuni za Kanisa. Imani ni muongozo, ni taa, ni dira inayotuangazia ili tuweze kutenda matendo mema. 

Kuwepo na uhusiano kati ya imani tunayokiri na imani tunayoishi
Kuwepo na uhusiano kati ya imani tunayokiri na imani tunayoishi

Uhusiano kati ya Imani tunayokiri na Imani tunayoishi: 

67. Kimsingi, imani tunayokiri na imani tunayoishi vinapaswa kuwiana kwa karibu. Yakobo Mtume anasema, “Kwa maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa” (Yak 2:26). Imani bila matendo ni imani iliyokufa kwa sababu ukosefu wa matendo hudhihirisha maisha yasiyobadilika au nafsi iliyokufa kiroho. Kuna aya nyingi za Biblia zinazosema kwamba imani ya kweli inatupelekea kwenye ushuhuda wa maisha mapya yanayodhihirisha maisha yetu ndani ya Kristo. Kwa maneno mengine, imani inaonyeshwa kwa kazi njema tunazofanya.  Jinsi tunavyoishi hudhihirisha kile tunachoamini na kinyume chake ni kweli pia kuwa tunachoamini kina akisi tunachotenda. 

68. Biblia inakazia umuhimu wa kuungama imani na kutenda matendo mema, ikionyesha kwamba imani inapaswa kudhihirika kwa njia zinazoonekana. Mtume Yohane anatuambia kuwa “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akimwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je, upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?” (1 Yoh 3:17). Kristo mwenyewe anasema “Si kila aniambiaye: Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.” (Mt 7:21). Kiuhalisia, “imani tunayokiri” ndiyo msingi, huku “imani tunayoishi” ndiyo jengo lililojengwa juu yake. Imani yenye nguvu inahusisha uelewa na kukiri hadharani imani hiyo na kuishuhudia kwa uthabiti kwa matendo katika maisha ya kila. 

Mambo ya Kutusaidia ili Kuishi Ipasavyo Kauli Mbiu hii “Ndugu, Msichoke Kutenda Mema”   

69. Kutenda mema ni safari ambayo inapaswa kukua siku kwa siku kwa nguvu zake Mungu mwenyewe. Si suala la siku moja bali ni mchakato unaopaswa kukua siku kwa siku katika kuelekea ukamilifu. Hivyo, katika safari hiyo ya kukua katika kutenda mema bila kuchoka tunapaswa kuzingatia yafuatayo: 

Sala: Jambo la kwanza kabisa katika kukua kwenye kutenda mema ni kusali. Tunasali kwa kuwa tunatambua jambo hili ni la kimungu na hivyo sisi wenyewe hatuwezi kulitekeleza kwa nguvu zetu. Tunahitaji neema ya Mungu ili itubadilishe na kutufanya kuwa watu wema na hivi kuakisi sura ya Mungu ambaye ndiye Wema wenyewe. Mzaburi anasema; “Bwana asipoijenga nyumba waijengao wanafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji yeye aulindaye akesha bure” (Zab 127:1). Lengo la Zaburi hii sio kutaka watu wasijibidishe bali anatufundisha kuwa juhudi yetu pasipo Mungu ni kazi bure. Hivyo wapendwa tunawaasa kuwa msichoke kusali kwani ni katika sala ndiyo tunapata neema ya Mungu yakutubadilisha na kuwa watu wema.

Neno la Mungu: Neno la Mungu ndiyo dira yetu, Neno la Mungu ndiyo mwongozo wetu, Neno la Mungu ni taa ya miguu yetu na mwanga wa njia yetu (rej. Zab 119:105). Kusoma Neno la Mungu ni kusikiliza anachosema Mungu. Ni kukaa karibu Naye, ni kuutafuta uwepo Wake. Hivyo, tujibidishe kusoma Neno la Mungu ili tupate kuchota humo hekima na ufahamu wa kujua Mungu anataka nini kwetu.  Katika simulizi la tukio la Yesu kugeuka sura tunasikia pia sauti ya Baba ikisema huyu ni “Mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye” (Mk 9:7). Kristo anatuambia “Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata” (Yoh 10:27). Tunapaswa kuisikia sauti ya Mungu ili kujua mapenzi yake. Na kama alivyotuambia Mama Bikira Maria, “Lolote atakalowaambia fanyeni” (Yoh 2:5). Hali kadhalika nasi wafuasi wa Kristo, lolote analotuambia Mungu katika Neno lake tulifanye. 

Kuenenda katika Roho: Mtume Paulo anatuambia; “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria” (Gal 5:22-23). Vipengele hivi vyote vitakuwa sehemu ya maisha yetu endapo tutaruhusu kuongozwa na Roho. 

Imani inapaswa kumwilishwa katika matendo adili na matakatifu
Imani inapaswa kumwilishwa katika matendo adili na matakatifu

Tenda Haki: Neno la Mungu linatuasa pia kuwatendea mema wenzetu kama anavyotuambia Paulo Mtume; “Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, na hasa jamaa ya waaminio” (Gal 6:10). Nabii Mika anasema; “Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema: na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!” (Mik 6:8). 

Kusamehe: Kuhusu umuhimu wa kusamehe, Neno la Mungu linatufundisha yafuatayo: “Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia. Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe nyinyi makosa yenu” (Mt 6:14-15). “Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe nyinyi” (Kol 3:13). “Mnaposimama kusali, msameheni kila mtu aliyewakosea chochote, ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe nyinyi makosa yenu” (Mk 11:25). Basi wapendwa katika kutenda mema, msisahau kusameheana pia kwani pasipo kusamehe sadaka yako mbele ya Bwana ni bure.  

Usilipe kisasi: Mtume Paulo anatukumbusha kuwa tusimlipe mtu ovu kwa ovu. Tuangalie yaliyo mema machoni pa watu wote. Lakini, adui yako akiwa na njaa, mlishe na akiwa na kiu mnyweshe. Anaongeza kwa kusema maana kwa kufanya hivyo utampalia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema (rej. Rum 12:17,20-21). Wabarikini wanaowaudhi; barikini wala msilaani (rej. Rum 12:14). Iweni watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mlioitiwa ili mrithi Baraka (rej. 1Pet 3:9).  

Usikate Tamaa: “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni dhiki, au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?” (Rum 8:35). Wapendwa, hatupaswi kukata tamaa kwani kukata tamaa ni dhambi. Ni kumkufuru Roho Mtakatifu kwa maana kukata tamaa ni kushindwa kuona nguvu ya Mungu dhidi ya changamoto unazopitia. Nguvu ya Mungu ni kubwa kuliko changamoto zetu. Neno la Mungu linatualika kumtumainia Mungu daima. Mungu anatuambia kuwa tusiogope kwa maana yeye yu pamoja nasi; tusifadhaike, kwa maana yeye ni Mungu wetu (rej. Is 41:10). Pia Mwenyezi Mungu anatuambia kwa kinywa cha nabii Yeremia; “Tazama, mimi ni Bwana, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lolote nisiloweza?” (Yer 32:27) 

70. Wapendwa, tujitahidini kuyatekeleza hayo ili yatusaidie katika safari ya kuelekea kwenye utakatifu. Katika mfungo wetu wa Kwaresma tunawaalika kuyaweka haya katika mazoezi yetu ya kiroho nanyi mtaona matunda yake. 

Huduma kwa wagonjwa ni ushuhuda wa imani tendaji
Huduma kwa wagonjwa ni ushuhuda wa imani tendaji

HITIMISHO 

71. Kwa kuhitimisha ujumbe huu wa Kwaresima, sisi Maaskofu wenu tunawaasa waamini wote na taifa zima la Mungu; “Ndugu, msichoke kutenda mema” (rej. 2The 3:13). Ulimwengu wetu unapitia changamoto mbalimbali kama vile vita, magonjwa, usaliti, mafarakano, umaskini, mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ukame unaoleta baa la njaa, mafuriko, vifo, uharibifu wa mazingira na kuwaacha wengi bila makazi kwa kutaja machache, mambo haya yanaweza kumfanya mfuasi wa Kristo kukata tamaa na kujiuliza kuna faida gani ya kuishi na zaidi sana kuna faida gani ya kusali na kutenda mema kama tunapitia magumu ya namna hii.  

72. Ujumbe huu wa Kwaresima utupatie matumaini kuwa pamoja na changamoto zozote tunazoweza kupitia hapa duniani, tumaini letu ni Mungu mwenyewe kwani hapa duniani sisi ni wasafiri na makazi yetu ni mbinguni. Lakini tutambue kwamba ili kufika mbinguni ambapo ndiyo lengo letu kuu, kila mmoja anapaswa kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu ni kutenda mema na kusamehe. Hivyo ndugu usichoke kutenda mema. 

73. Pamoja na changamoto hizo zilizotajwa hapo juu, pia kuna changamoto ya kutendewa ubaya na wenzetu pamoja na mema tunayoweza kuwa tunajitahidi kuwatendea. Wewe ndugu usichoke kutenda mema na acha kulipiza kisasi kwa yule aliyekutendea ubaya kwani ubaya upaswa kulipwa kwa wema. Maandiko Matakatifu yanatuasa kutolipiza kisasi na kutoshindana na mtu mwovu (rej. Mt 5:38-39). 

74. Katika ujumbe huu tumeelezea ni kwa nini tunapaswa kutenda mema. Moja ya sababu zinazotusukuma kutenda mema ni Mungu mwenyewe kwani Yeye ndiye Wema wenyewe. Mwaliko ni kuwa “Iweni watakatifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo Mtakatifu” (Mt. 5:48). Pia kwa kuwa Mungu alituumba kwa sura na mfano wake, basi hatuna budi kuwa sura na mfano wa Mungu katika maisha yetu ili watu wanapoona matendo yetu mema waweze kumtukuza Baba yetu aliye mbinguni (rej. Mt 5:16). 

Waamini msichoke kutenda mema kwani ni chemchemi ya neema na baraka
Waamini msichoke kutenda mema kwani ni chemchemi ya neema na baraka

75. Tukeshe daima huku viuno vyetu vikiwa vimefungwa na taa zetu zinawaka wakati tukimsubiri Bwana harusi ili atakapokuja kutoka harusini tumfungulie mara (rej. Lk 12: 35-36). Huu ni mwaliko wa kutenda mema bila kuchoka maana hatujui muda atakapokuja Bwana harusi. Maisha ya ufuasi hayana kupumzika. Ndugu, msichoke kutenda mema maana tutavuna kwa wakati wake. Katika kusisitiza uvumilivu katika kutenda mema mpaka atakapokuja Bwana, Maandiko Matakatifu yanatuambia tena; “Basi, ndugu zangu, muwe na subira mpaka Bwana atakapokuja. Tazameni mkulima anavyongoja kwa subira mimea yake itoe mavuno ya thamani. Yeye hungojea kwa subira mvua za masika na za vuli. Nanyi pia mnapaswa kuwa na subira; imarisheni mioyo yenu, maana siku ya kuja kwake Bwana inakaribia” (Yak 5: 7-8) 

76. Neno “kuchoka” linalotumika hapa halizungumzii kuchoka kwa mwili ambako kunaweza kukarabatiwa kwa kula, kunywa maji ya kutosha, kupumzika, au kuoga maji ya baridi ambako kitaalamu kunaweza kuwa tiba ya kuchoka kwa mwili. Kuchoka katika muktadha huu inamaanisha kuchoka kwa nafsi, kukata tamaa, ni hali ya kutokuendelea au hali ya kuvunjika moyo. Hali hii inatokana na kukosekana kwa mwamko wa moyo na sio kuchoka mwili. Hali ya kukosa muamko inaweza kupelekea mtu kuchoka katika nafsi mwili na roho. Huku ndiko kuchoka ambao ujumbe wetu unaongelea na kimsingi ndiyo kuchoka kunakoweza kuleta madhara makubwa kama vile kuchoma moto mali za watu, maandamano yasiyo ya amani na kuiba na kuharibu vitu kama inavyotokea sehemu mbalimbali duniani leo hii. Watu wanapokata tamaa huweza kuacha kutenda mema na kutenda mabaya. 

Mahujaji na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo
Mahujaji na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo

77. Msichoke kutenda mema, hili ni suala ambalo Neno la Mungu linatutia moyo, kwamba tuendelee kutenda mema kwa imani, kwa upendo, na nguvu tuliyonayo katika jina la Yesu. Hii ni kanuni ambayo ina mavuno ndani yake, lakini sio hivyo tu, ni jambo lenye kumpendeza Mungu pia. Hatupaswi kuchoka kutenda mema hata kidogo na hivyo tunamuomba Mungu azitie moyo roho zetu na nia zetu hata tunapokutana na vikwazo vya namna mbalimbali kama vile mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, migogoro ndani ya ndoa, ndani ya familia, changamoto za mahusiano, changamoto za afya, kupoteza maswala kadhaa katika ulimwengu huu, kukosekana kwa shukrani au kupongezwa au hata kutiwa moyo, nk. Biblia inatuasa: “Ndugu, msichoke kutenda mema”.  

  Ni sisi Maaskofu wenu.

TEC: Ujumbe wa Kwaresima 2026
17 Februari 2026, 14:41