Askofu Bernardin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa, kilichotokea tarehe 14 Aprili 2026 Askofu Bernardin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa, kilichotokea tarehe 14 Aprili 2026  

Askofu Bernardin Francis Mfumbusa Amefariki Dunia! Pigo Kwa Tasnia ya Mawasiliano

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC linasikitika kutangaza kifo cha Askofu Bernardin F. Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa, kilichotokea tarehe 14 Aprili 2026 Majira ya Saa 11:45 asubuhi kwenye Hospitali ya Benjamin Mkapa, BMH alikokuwa amepelekwa kwa matibabu ya dharura. Mipango ya mazishi inaendelea kufanyika. Alizaliwa tarehe 1 Aprili 1962, Akapadrishwa tarehe14 Juni 1992 na kuteuliwa kuwa Askofu wa Kondoa tarehe 12 Machi 2011. Gwiji wa mawasiliano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC linasikitika kutangaza kifo cha Askofu Bernardin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa, kilichotokea tarehe 14 Aprili 2026 Majira ya Saa 11:45 asubuhi kwenye Hospitali ya Benjamin Mkapa, BMH alikokuwa amepelekwa kwa matibabu ya dharura. Askofu Mfumbusa anatarajiwa kuzikwa Jumatano tarehe 22 Aprili 2026 Jimboni Kondoa. Itakumbukwa kwamba, tarehe 9 Aprili 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV alikuwa amemteua Askofu Bernardin Francis Mfumbusa, Rais wa Kamati ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar, “Pan African Episcopal Conference For Social Communication, CEPACS,” kuwa ni Mjumbe wa Baraza la Kipapa la Mawasilianiano ya Jamii. Kanisa limempoteza Askofu na mtaalam mbobezi wa Mawasiliano ya Jamii. Itakumbukwa kwamba, Hayati Askofu Bernardin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa, alizaliwa tarehe Mosi Aprili 1962 mjini Kondoa na ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 64 tangu alipozaliwa. Baada ya malezi na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 14 Juni 1992 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre mikononi mwa Askofu Matthias Joseph Isuja, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma. Baba Mtakatifu Benedikto XVI tarehe 12 Machi 2011 akaanzisha Jimbo Katoliki la Kondoa na kumteuwa Askofu Bernardin Francis Mfumbusa kuwa Askofu wake wa kwanza, na hivyo kuwekwa wakfu na Kardinali Polycarp Pengo, aliyekuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, tarehe 15 Mei 2011, akisaidiana na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi aliyekuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza pamoja na Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, C.S.Sp., wa Jimbo Katoliki la Zanzibar. Kumbe Askofu Bernardin Francis Mfumbusa amefariki dunia akiwa amelitumia Kanisa kama Padre kwa Miaka 33 na kama Askofu mwenye dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa miaka 14.

Marehemu Askofu Bernardini Mfumbusa wa Jimbo la Kondoa
Marehemu Askofu Bernardini Mfumbusa wa Jimbo la Kondoa

Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Mzaburi anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima.” Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo! 

Askofu Bernardin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa
Askofu Bernardin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa

Kristo Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini. Mbele ya Fumbo la Kifo binadamu ni mnyonge na ni “mdogo sana kama kidonge cha piliton”. Lakini, neema katika hali na mazingira kama haya, inaweza tena kuamsha imani na Yesu mwenyewe kuwashika mkono watu wake na kuwaambia “Talitha kum” tafsiri yake “Msichana, nakuambia, inuka.” Haya ni maneno ambayo Yesu anapenda kumwambia kila mtu, simama na fufuka tena! Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ndiyo matumaini ya Kikristo mbele ya Fumbo la Kifo. Kwa mwamini hili ni lango ambalo liko wazi; lakini kwa mwenye mashaka, ni giza linalomwandama na kumtumbukiza mtu katika majonzi na msiba mkuu. Kwa kila mwamini, hii itakuwa ni neema siku ile mwanga huu utakapoangaza.Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, kifo ni sehemu ya matukio ya maisha ya mwanadamu, ni urithi na kumbukumbu. Tangu pale mwanadamu anapozaliwa, anaanza safari ya kuelekea katika Fumbo la kifo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia kufa kifo chema badala ya kujifungia katika muda na ubinafsi wao! Mama Kanisa anawataka watoto wake kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo katika maisha yao. Kifo ni urithi unaofumbatwa katika ushuhuda ambao unapaswa kutolewa kwa wale wanaobaki. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wakristo kujiuliza swali la msingi, Je, wewe leo ukifa utaacha ushuhuda gani nyuma yako? Swali hili liwasaidie waamini kujiandaa kufa vyema. Lakini, kabla ya kuitupa mkono dunia Je, kuna jambo gani ambalo ningependa kulifanya leo hii? Fumbo la kifo liwasaidie waamini kufikiri na kutenda kila siku wakitambua kwamba, daima wako safarini kuelekea kufani! Maswali haya ni muhimu kwa waamini wote, ili kuweza kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo!

Askofu Mfumbusa atakumbukwa sana kwa mchango wake katika elimu
Askofu Mfumbusa atakumbukwa sana kwa mchango wake katika elimu

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi anasema, Mwili wa Hayati Askofu Mfumbusa utapelekwa kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo kuu la Dodoma, Jumanne tarehe 21 Aprili 2026 saa mbili asubuhi kwa ajili ya Misa Takatifu na Majira ya Saa 6: 00 Mchana mwili utapelekwa Jimboni Kondoa na baadaye kufuatiwa na Ibada ya Misa Takatifu itakayoanza majira ya Saa 10:00 Jioni sanjari na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kupata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho na kuuaga mwili wa Hayati Askofu Mfumbusa. Jumatano tarehe 22 Aprili majira ya Saa 4:00 Asubuhi itaanza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Askofu Bernardin Mfumbusa.

Askofu Mfumbusa

 

14 Aprili 2026, 10:21