Maamuzi ya vikundi vya Sinodi. Maamuzi ya vikundi vya Sinodi.  (@Vatican Media)

Sinodi yatoa ripoti kuhusu umaskini,mazingira na mitala

Sekretarieti Kuu ya Sinodi ilichapisha hivi karibuni Ripoti za Mwisho za Kundi la la Utafiti kifungu II:'Kusikia kilio cha maskini na dunia,'na ile ya Tume ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar(SECAM) kuhusu 'changamoto ya kichungaji ya mitala.'

Vatican News

Sekretarieti Kuu ya Sinodi hivi karibuni tarehe 24 Machi 2026 ilichapisha Ripoti ya Mwisho ya Kundi la Utafiti sehemu II kuhusu:"Kusikia kilio cha maskini na dunia," na ile ya Tume ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar (SECAM) kuhusu "Changamoto ya kichungaji ya mitala." Ripoti zote mbili, katika utofauti wao wa mada, zinashuhudia safari ya Sinodi ya Kanisa: Kanisa linalosikiliza, linalotambua, linalosindikiza, na, lenye mizizi katika Injili, haliachi kamwe kumkaribia kila mwanamume na mwanamke, likijibu changamoto za wakati wetu. Ripoti za Mwisho na muhtasari mfupi katika lugha tano zinapatikana kwenye tovuti ya Sekretarieti Kuu ya Sinodi: www.synod.va.

Papa Leo XIV aliagiza uchapishaji wa Ripoti hizi za Mwisho ili kushirikisha Watu wote wa Mungu, matunda ya tafakari na utambuzi uliofanywa wakati wa Sinodi, kwa roho ya uwazi na uwajibikaji. Hizi zinachukuliwa kuwa hati za kufanyia kazi. Kwa kuwasilisha Ripoti za Mwisho kwa Sekretarieti Kuu ya Sinodi, Vikundi vya Utafiti ambavyo vimewasilisha vinakamilisha jukumu lililokabidhiwa kwao na kwa hivyo vinachukuliwa kuwa vimevunjwa.

Ripoti ya Mwisho ya Kikundi cha Utafiti kifungu cha Pili

Ripoti ya Mwisho ya Kikundi cha Utafiti kufungu cha Pili kuhusu "Kusikia kilio cha maskini na dunia" imeandaliwa katika sehemu kadhaa.   Ikitanguliwa na tafakari kutoka kwa Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Binadamu, Ripoti hiyo ilitafuta kujibu maswali matano ya msingi yaliyokabidhiwa kwa Kundi kuhusu jinsi Kanisa linavyoweza kusikia vyema kilio cha maskini na cha dunia. Hati hiyo inatokana na imani ya Kitaalimungu kwamba kuwasikiliza maskini na dunia si chaguo la kichungaji, bali ni tendo la imani linalounda utume wa Kanisa, unaotokana na amri mbili za upendo na mfano wa Msamaria Mwema.

Kama Kardinali Czerny alivyokumbuka katika utangulizi wake, neno "kusikiliza" linaashiria mchakato mzima unaojumuisha kukutana, kuelewa tatizo, kitendo, tathmini, na msaada wa kiroho, na linamhusu kila Mkristo, ikiwa ni pamoja na wale ambao wenyewe wanahisi maskini. Swali lililoongoza kazi ya Kundi hivyo lilikuwa: Kanisa linawezaje kusikiliza vyema vilio hivi viwili vilivyounganishwa, likijua kwamba kujibu kilio cha maskini pia kunamaanisha kujibu kilio cha dunia, na kinyume chake?

Ripoti inaelezea mbinu za kazi zilizotumika, mapungufu yaliyopatikana, na mafunzo iliyopata kujifunza. Ilibainisha zana zilizopo tayari ndani ya Kanisa, ikiwa ni pamoja na parokia, jumuiya msingi, harakati, Mihili ya Caritas, mitandao ya kiekumeni na kimataifa, na inaakisi utajiri wake, huku ikitoa wito wa kushinda kishawishi cha kukabidhi vibaya miundo maalum, ikimrudisha kila mtu aliyebatizwa kwenye uwajibikaji kwa mwingine. Miongoni mwa mapendekezo halisi ni kuanzishwa kwa Uchunguzi wa Kanisa kuhusu Ulemavu, uliopendekezwa na kikundi kidogo kilichoundwa kwa kiasi kikubwa na watu wenye ulemavu, kama kielelezo ambacho kinaweza kuigwa katika ngazi mahalia na kikanda ili kutoa sauti kwa makundi yote yaliyotengwa.

Katika ngazi ya kitaalimungu, Ripoti ilisisitiza hitaji la Taalimungu inayotokana na kuwasikiliza maskini na dunia kama eneo halisi la Kitaalimungu, na likiwataka Wataalimungu kutoka jamii zilizo katika mazingira magumu zaidi kushiriki kikamilifu katika uandishi wa hati za kimafundisho ya Kanisa. Uangalifu hasa unatolewa kwa malezi, ukizingatia programu za mafunzo kwa walei, watawa, na waseminari, ukizingatia kwamba lazima ziunganishe kukutana moja kwa moja na pembezoni mwa maisha, uwezo wa kusikiliza kama nidhamu ya kiroho, si tu kama mbinu na uchambuzi wa kijamii. Ripoti inahitimisha kwa maono ya Kanisa la kisinodi linaloweza kuwa chombo cha kusikiliza, si tu kuwa na miundo ya kusikiliza, bali kubadilisha kila mmoja wa washiriki wake kuwa uwepo wa kimisionari pamoja na walio hatarini zaidi.

Historia ya Tume ya SECAM kuhusu mitala

Tume ya SECAM iliyozingatia changamoto ya mitala ilitokana na ombi la Kikao cha Kwanza cha Mkutano Mkuu wa Kawaida wa 16 wa Sinodi ya Maaskofu mnamo Oktoba 2023, ambacho kilihimiza SECAM kuhamasisha utambuzi wa Kitaalimungu na kichungaji kuhusu mitala(yaani ndoa za wake wengi) na kuwasindikiza watu walio katika muungano wa wake wengi ili waweze kuingia  katika imani. Kwa hivyo, Kanisa barani Afrika, kupitia chombo chake cha bara, cha Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagacar(SECAM) lilianzisha Timu ya Wataalamu waliojitolea. Timu ya Wataalamu, iliyojumuisha wataalamu 12 kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika na visiwa vyake na inayowakilisha nyanja mbalimbali kama vile Taalimungu ya kidogma na ya msingi, mafunzo ya Biblia, utunzaji wa kichungaji, sheria ya Kanisa, na anthropolojia, ilikusanyika ana kwa ana na kwa njia ya mtandaoni.

Rasimu ya Hati ilishirikishwa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya  Kanisa kupitia Sekretarieti Kuu ya Sinodi. SECAM ilipokea maoni ya kutia moyo kutoka kwa Baraza la Kipapa hilo, pamoja na mambo maalum ya kushughulikiwa na maandishi hayo yalirudishwa kwenye Timu ya Wataalamu kwa ajili ya uboreshaji zaidi. Maandishi ya muda yaliwasilishwa na kujadiliwa na Maaskofu na Wataalimungu wakati wa Mkutano Mkuu wa  Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madgascar(SECAM,) uliofanyika huko Kigali, nchini Rwanda, kuanzia tarehe 30 Julai hadi 4 Agosti 2025. Maarifa kutoka katika mkutano huo yalichangia toleo la mwisho la Hati hiyo. Kufuatia majadiliano katika Mkutano Mkuu, maandishi ya mwisho yaliwasilishwa kwa Sekretarieti Kuu ya Sinodi na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kwa mwongozo zaidi na Ripoti ya Mwisho ilichapishwa tarehe 24 Machi 2026.

Mhutasari wa Ripoti ya SECAM

Kwa hivyo, SECAM imeunda tafakari nzima  kuhusu changamoto ya kichungaji ya mitala, yenye mizizi katika muktadha wa kiutamaduni, anthropolojia, na kitaalimungu kwa bara la Afrika. Ripoti inaanza na utambuzi wa thamani takatifu ya familia ya Kiafrika, iliyoanzishwa juu ya agano kati ya makundi ya wanadamu, na mababu, na Mungu, ambapo mtoto anachukuliwa kuwa baraka ya kimungu na hamu ya watoto wengi huunda sehemu muhimu ya utambulisho wa kijamii. Ni ndani ya  muktadha  huo ambapo uwepo wa kihistoria wa mitala upo, jambo ambalo si la Afrika pekee,  bali hasa limejikita humo na ni la dharura kichungaji. Uchambuzi wa kibiblia unaonesha utata wake: ukivumiliwa katika Agano la Kale, unazidi hatua kwa hatua na ufunuo wa Agano Jipya, ambapo Yesu, akikumbuka mpango wa awali wa Muumba, anathibitisha waziwazi umoja na kutovunjika kwa ndoa. Waraka huo unarudia kwa uthabiti mafundisho ya Kanisa: Ndoa ya Kikristo ni ya mke mmoja kwa asili ya kitaalimungu na si kwa kulazimishwa kwa kiutamaduni.

Katika ngazi ya uchungaji, SECAM haijumuishi aina yoyote ya utambuzi wa mitala na inapendekeza kwamba wakatekumeni wenye wake wengi wasikubali kubatizwa kabla ya kukubali kwa uhuru ahadi ya ndoa ya mke mmoja. Hili si suala la kutengwa au unyanyapaa, bali ni suala la kusindikiza  kwa uvumilivu na heshima, lililoongozwa na huruma ya Kristo. Heshima ya wanawake imewekwa katikati ya mbinu hii ya uchungaji, huku Maria, Mama wa Yesu, akitolewa kama mfano wa uinjilishaji uliojidhihirisha ndani ya utamaduni. Hitimisho linafunguka kuelekea "utunzaji wa uchungaji wa ukaribu" unaoweza kufungua milango ya Kanisa kwa wale wanaoishi pembezoni mwa kiroho na kuwepo, wakitambua katika kila mtu mtoto wa Mungu aliyeitwa kwa upendo mwaminifu na kwa Agano.

Hitimisho la ripoti ya mitala

Ripoti inahitimisha, ikitambua kwamba mitala inaendelea kuwa ukweli katika jamii za Kiafrika leo, lakini uwepo na kuenea kwake hutofautiana kulingana na sera za kila jimbo, dini kuu, na ushawishi wa kiutamaduni wa kitamaduni. "Katika muktadha huu, tangazo la Injili na pendekezo lake la kuzingatia uhusiano wa ndoa ya mke mmoja wakati mwingine hukutana na upinzani fulani unaothibitishwa na sababu za kitamaduni. Wanakubali kwamba katika historia yote ya uinjilishaji, kumekuwa na majaribio ya kuwakubali watu wanaoishi katika mahusiano ya wake wengi katika jumuiya ya Kikristo ambayo yamekuwa na mifumo tofauti, wakati mwingine hutofautiana kutoka jimbo  moja hadi lingine, kutoka Baraza mmoja la Maaskofu hadi lingine, lakini ndani ya nafasi moja ya kijamii na kiutamaduni. "Wakati ambapo Kanisa linakusudia kuishi kikamilifu tabia yake ya Kisinodi, katika ushirika na ushiriki wa wote, inakuwa muhimu kwa Kanisa barani Afrika," ripoti inabainisha, "kushiriki mifano hii na kuitathmini kimafundisho na kichungaji, na inapobidi, kupendekeza njia zingine, kwa lengo la kutoa kwa wote uwezekano wa kukutana na Kristo na Injili yake."

Kitendo cha kichungaji cha Kanisa barani Afrika katika kusindikizana na wanafamilia wenye wake wengi, ambacho kinaomba kukaribishwa Kanisani, kinaonekana kama jaribio la kuwa waaminifu kwa uelewa wa Kanisa kuhusu ndoa na ule wa familia ya Kikristo."Haja ya kuwakaribisha na kusindikizana na watu binafsi na familia inazidi kuwa dhahiri," Maaskofu wa Afrika wanasisitiza, "ili waweze kuitikia kwa uwazi zaidi,  wito unaotolewa kwao na ukweli uliofunuliwa na Injili kuhusu wito na utume wa familia katika Kanisa na katika jamii." "Kwa hivyo, ni  umuhimu wa kuwa na mbinu ya kichungaji ya ukaribu na umakini ili kusaidia kuelewa sakramenti ya ndoa si kama mkutano wa kijamii, bali kama zawadi kwa ajili ya utakaso na wokovu wa wanandoa," wakibainisha, "Kama wito na utume, hupokelewa kama zawadi," wanahitimisha.

SINODI NA SECAM

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.

 

08 Aprili 2026, 14:10