Pasaka ya Bwana ni fursa nyingine kwa waamini kuweza kuonja upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya msamaha wa dhambi. Pasaka ya Bwana ni fursa nyingine kwa waamini kuweza kuonja upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya msamaha wa dhambi.   (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Huruma ya Mungu: Sifa Kuu ya Mungu na Kiini Cha Mafundisho ya Kanisa

Kristo Mfufuka analipatia Kanisa dhamana ya kuwatangazia watu huruma na msamaha wa Mungu, unaowakirimia waamini amani, utulivu wa ndani na furaha inayobubujika kwa kukutana na Kristo Mfufuka. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia kuwa ni watoto wapendwa wa Baba wa milele. Huruma ni Utambulisho wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na haki” anasema, huruma ya Mungu inapaswa kuendelezwa katika medani mbalimbali za maisha ya watu kama utimilifu wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Huruma ya Mungu inajionesha katika maadhimisho ya Sakramenti mbalimbali za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee kabisa, Sakrameti ya Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa. Huruma ya Mungu inaendelea kujifunua katika historia na maisha ya watu kwa njia ya Neno la Mungu, ikikumbukwa kwamba, Biblia ni muhtasari wa ufunuo wa huruma ya Mungu kwa binadamu! Huruma ya Mungu katika mwanga wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana ni kielelezo cha ufahamu ambao unaweza kuchukua mitindo mbalimbali katika maisha ya mwanadamu yaani: kwa kutumia milango ya fahamu, kwa kufundishwa, lakini kubwa zaidi ni kwa njia ya mang’amuzi ya huruma ya Mungu inayofungua akili na nyoyo za watu ili kuweza kufahamu kwa kina na mapana zaidi Fumbo la maisha ya Mungu na maisha ya mtu binafsi. Huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba: vita, chuki, uhasama na ubaya wa moyo ni mambo ambayo hayana msingi kabisa na kwamba, waathirika wakubwa ni wale watu wanaofungwa katika hali kama hizi, kwani ni mambo yanayowapokonya utu wao, heshima na haki msingi. Kumbe, Pasaka ya Bwana ni fursa nyingine kwa waamini kuweza kuonja upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya msamaha wa dhambi. “Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.” Yn 20:21-22.

Dominika ya Huruma ya Mungu: Chemchemi ya upendo, msamaha na maisha
Dominika ya Huruma ya Mungu: Chemchemi ya upendo, msamaha na maisha   (Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumatatu tarehe 13 hadi 23 Aprili 2026 anafanya hija ya kitume ya Siku 10 kwa kutembelea: Algeria, Cameroon, Angola pamoja na Guinea ya Ikweta. Baba Mtakatifu Leo XIV anatembelea Barani Afrika kama shuhuda wa matumaini, amani na upatanisho, mkazo ni kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inajikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho, ili kweli Afrika iwe ni mahali pazuri pa kuishi! Kristo Yesu Mfufuka analipatia Kanisa dhamana ya kuwatangazia watu huruma na msamaha wa Mungu, unaowakirimia waamini amani, utulivu wa ndani na furaha inayobubujika kwa kukutana na Kristo Mfufuka. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia kuwa ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Huruma ya Mungu anasema Hayati Baba Mtakatifu Francisko inawasha moto wa upendo mioyoni mwa watu, kwa kuguswa na mahitaji yao pamoja na kuwashirikisha. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuishi kwa furaha yote haya kama walivyokuwa Wakristo wa Kanisa la Mwanzo.

Huruma ya Mungu ni chemchemi ya upendo, ukarimu na sadaka
Huruma ya Mungu ni chemchemi ya upendo, ukarimu na sadaka

Dominika ya Pili ya Pasaka kadiri ya Mapokeo ya Kanisa na mwendelezo wake kama Dominika ya huruma ya Mungu, ambamo Mama Kanisa anatumwa na Kristo Yesu kuwa ni chombo cha huruma na upatanisho kwa kuwaondolea watu dhambi zao! Dominika ya Pili ya Pasaka inajulikana pia kama “In Albis” yaani “Dominika nyeupe”, siku ambayo Wakristo waliobatizwa kwenye mkesha wa Pasaka walikuwa wanavua mavazi yao meupe, yaliyokuwa yana maanisha utu mpya wa watoto wa Mungu waliozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Mavazi haya meupe wakati huo yalivaliwa kwa muda wa juma zima, kumbe, Jumapili Nyeupe ilikuwa ni mwanzo wa maisha mapya ndani ya Kristo Mfufuka na Kanisa lake! Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000 wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo aliamua kuipatia Dominika hii umuhimu wa pekee na kuitangaza kuwa ni Dominika ya huruma ya Mungu. Hii ni changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kujichotea nguvu, rehema na neema zinazobubujika kutoka katika huruma ya Mungu. Mtakatifu Maria Faustina Kowalska wa Huruma ya Mungu, mtawa, ndiye aliyepata maono na kuidhihirisha kwetu huruma ya Mungu.

amani ni zawadi kutoka kwa Kristo Mfufuka
amani ni zawadi kutoka kwa Kristo Mfufuka   (Vatican Media)

Katika maono hayo aliona miali ya mwanga iliyotoka kifuani pa Bwana wetu Yesu Kristo mwali wa rangi nyekundu ukiwakilisha Damu yake Azizi na rangi ya bluu hafifu ikiwakilisha Maji ya ubatizo. Dominika ya Huruma ya Mungu kimsingi inakazia zaidi: Saa ya Huruma Kuu; Umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, ili kulipyaisha Kanisa la Kristo Yesu kwa chachu ya utakatifu wa maisha. Waamini wajitahidi kushiriki Ibada ya Misa Takatifu kwa uchaji na ibada; wakimbilie daima huruma ya Mungu kwa Sakramenti ya Upatanisho; wajenge utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu na maisha ya sala sanjari na kudumisha Ibada ya Njia ya Msalaba katika uhalisia wa maisha yao. Mtakatifu Maria Faustina Kowalska ni kati ya watakatifu waliotangaza, wakashuhudia na hatimaye, kueneza Ibada ya huruma ya Mungu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu ni kinga na kimbilio la maskini na wadhambi. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao, ili waweze kupata msamaha na maondoleo ya dhambi. Huruma ya Mungu inazidi uelewa, maarifa na ufahamu wa akili ya binadamu.Kwa Njia ya Picha ya Yesu wa Huruma inayomwonesha Yesu akibariki na miale miwili ikitoka katika ubavu wake uliochomwa na chini imeandikwa Yesu Nakutumainia, ikimwalika mwanadamu kuitumainia daima Huruma kuu ya Mungu katika maisha yake.

Dominika ya Huruma ya Mungu: Huruma ni utambulisho wa Mungu
Dominika ya Huruma ya Mungu: Huruma ni utambulisho wa Mungu   (Vatican Media)

Njia ya Rosari ya Huruma inayomwalika mwanadamu kutakafakari Mateso makali ya Yesu aliyoyapata kwa ajili ya kumkomboa Mwanadamu na kumwalika kumtolea Baba wa milele kwa ajili ya dunia nzima. Njia ya Saa ya Huruma, yaani kujizamisha katika Huruma ya Mungu saa ya huruma kuu, saa 9 alasiri ambapo Kristo Yesu alidhihirisha upeo wa Huruma yake na kujitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Njia ya Sherehe ya Huruma ya Mungu tunayoadhimsha Dominika ya Pili ya Pasaka yaani Dominika ya Huruma ya Mungu ambapo Kristo Yesu alitaka picha yake Ibarikiwe kwa ibada na waamini wapokee Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi wapate maondoleo ya dhambi na adhabu zake. Injili ya Siku inaonesha jinsi ambavyo Yesu alivyowapatia Mitume wake dhamana ya kuwaondolea watu dhambi zao kwa kuwapatia Roho Mtakatifu.“Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaokubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Yesu, daima furaha inazaliwa upya na huo unakuwa ni mwanzo wa uinjilishaji mpya unaosimikwa kwa Kristo Mfufuka.” Evangelii gaudium, 1.

Huruma ya Mungu ni muhtasari wa mafundisho ya Papa Francisko
Huruma ya Mungu ni muhtasari wa mafundisho ya Papa Francisko   (Vatican Media)

Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya Huruma ya Mungu, muhtasari wa mafundisho makuu ya Baba Mtakatifu Francisko, aliyetaka kuwaona Wakristo wakijizatiti katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Huruma ya Mungu si dhana ya kufikirika inayoelea kwenye ombwe anasema Hayati Baba Mtakatifu Francisko, bali ni sifa kuu ya Mungu na mafundisho ya Kanisa. Yesu alikuja ulimwenguni ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa kumjalia maisha mapya na uzima wa milele.Ni mganga wa kweli anayewatafuta wagonjwa na wala si wenye haki ambao hawahitaji kutubu na kumwongokea Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Toma, aliyekiri udhaifu wake na kuungama imani yake kwa Kristo Yesu, Mtu kweli na Mungu kweli. Huu ni mwaliko kwa waamini kujitahidi kukutana na Kristo Mfufuka katika maisha yao kwa njia ya: Neno, Sakramenti za Kanisa, Sala, Huduma na Maisha ya Kijumuiya kama ushuhuda wa Kanisa la Mwanzo unavyoonesha, kwani Wakristo hawa, walisimika maisha yao katika msingi wa imani, matumaini na mapendo. Hii ni nguvu iliyopata chimbuko lake katika Neno, Kuumega Mkate pamoja na Maisha ya Sala iliyomwilishwa katika huduma. Ikumbukwe kwamba, Mama Kanisa anachota amana na utajiri wa mafundisho yake katika: Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa.

Liturujia ya Huruma ya Mungu 2026
11 Aprili 2026, 18:51