Lengo la hija ye yote ni kuleta furaha ya ndani ya mhujaji. Ni Kitendo cha kujialika upya wa maisha. Lengo la hija ye yote ni kuleta furaha ya ndani ya mhujaji. Ni Kitendo cha kujialika upya wa maisha.   (@Vatican Media)

Hija ya Wawata Nchini Italia, Ufaransa na Ureno! Chemchemi ya Baraka na Neema

Lengo la hija ye yote ni kuleta furaha ya ndani ya mhujaji. Ni Kitendo cha kujialika upya wa maisha. Ni msukumo wa kuona mambo upya kulingana na jicho la Mungu. Na ndio maana wale walioenda kuhiji mji ya Daudi Yerusalemu; walipokuwa wanatokea bondeni Yeriko, na kukikabili kilima cha Yerusalemu waliimba kwa furaha: “Nalifurahi waliponiambia na twende nyumbani kwa Bwana. Miguu yetu imesimama ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.” (Zaburi 122:1-2

Na Padre Beno Michael Kikudo, - Jimbo kuu la Dar es Salaam.

UTANGULIZI: Waswahili husema: Safari hatua. Maana yake ni kuwa; safari ni kuenda mahali au sehemu ya mbali. Na kama ni mahali pa mbali; basi ni vizuri kujiandaa. Kila safari ina mahitaji yake. Kuna mahitaji ya kiakili, kisaikolojia, kisolojia (familia), kimwili na kiroho. Kwetu sisi, haya yote ni muhimu. Ila, kati ya yote kuajiandaa kiroho ni la muhimu zaidi. Baadhi yetu wanaweza kuwa wamekwishaenda hija nyingi. Ila, kila hija ya kiroho ina upekee wake. Kila hija ina maandalizi yake, ina malengo yake na makusudio yake ya pekee. Kwa yule anayejiandaa vizuri kiroho, huvuna chumo la kwake binafsi na wale aliowaacha nyumbani. Hata Waswahili walituambia: Kila mchuma janga hula na wa kwao. Sisi katika safari hii ya hija, hatuendi kuchuma janga; bali twalifuata na kulichuchumilia chumo la kiroho. Kuna waliotuomba tuwaombee tukiwa katika Madhabahu mbalimbali. Sisi ni miguu na mikono ni yao. Wewe ni balozi kwa niaba ya familia yako yote. Lengo la hija ye yote ni kuleta furaha ya ndani ya mhujaji. Ni Kitendo cha kujialika upya wa maisha. Ni msukumo wa kuona mambo upya kulingana na jicho la Mungu. Na ndio maana wale walioenda kuhiji mji wa Daudi Yerusalemu; walipokuwa wanatokea bondeni Yeriko, na kukikabili kilima cha Yerusalemu waliimba kwa furaha: “Nalifurahi waliponiambia na twende nyumbani kwa Bwana. Miguu yetu imesimama ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.” (Zaburi 122:1 – 2). Tunamshukuru Mungu aliyetuwezesha kimwili na kiakili kuwa na mipango ya safari nzima. Katika sehemu ya kwanza, tunawashukuru wenye kampuni (RAISSA) ambao ndio waliotuandalia safari nzima. Tunashukuru kwa mipango yote mizuri, kwa vile hatujasikia mkwamo wo wote ule hadi sasa. Tunawashukuru wao na ofisi yao kwa kuratibu kila kitu vizuri na kwa umakini hali ya juu kiasi ambacho tunajiona tupo katika mikono yao salama; ingawa tunaenda mbali kwenye nchi za kigeni. “Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana…" (Zaburi 122:1.)

Hija ni chemchemi ya neema na baraka
Hija ni chemchemi ya neema na baraka   (@Vatican Media)

Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women Of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika.” Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Taswira ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ni kuona kila mwanamke mkatoliki wa Tanzania anaelewa nafasi yake na wajibu wake wa Kikristo kuanzia ngazi ya Familia, Jumuiya, Kanisa, jamii na Taifa kwa ujumla. Pia wanawake wanakuwa na maendeleo fungamani ya kiuchumi ili kukidhi mahitaji msingi ya familia na hivyo kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na Jamii, na kufanya maisha ya hapa duniani kuwa taa na nuru katika Ulimwengu kama mawakili wa Kristo Yesu. Kumbe, kwa nafasi ya pili tunawashukuru uongozi mzima wa WAWATA Taifa kwa mawasiliano na uratibu katika ngazi ya kitaifa. Kazi ya kuwapata kina mama 47 kwa mara moja si jambo la mchezo. Na pia tumesikia hata idadi ilipindukia na kufikia akina mama 100. Hili ni jambo jema sana la maisha ya kiroho. Kila mama anayetoka kuenda nje na mbali hurudi na kitu cha kiakili, kiroho na kimwili. Na ndio maana Wahenga walisema: Mgaagaa na upwa, hali wali mkavu. Au, mtembea bure, sio sawa na mkaa bure. Tunawashukuru pia akina mama mmoja mmoja ambao wamevunja vibubu na akiba zao kwa ajili ya safari hii. Gharama ya hija ni kubwa sana.

WAWATA ilianzishwa kunako Mwaka 1972
WAWATA ilianzishwa kunako Mwaka 1972

Waswahili husema: Msafari Kafiri. Yaani, katika dini ya Kiislamu, kuna wale ambao huonekana kuwa hawana dini; yaani makafiri. Kwa wao, safari ni tukio ambalo cho chote chaweza kutokea. Kuna yale yasioyotarajiwa hutokea katika safari. Katika hili tunaweza kuharibikiwa na basi, au tukapata chakula pungufu, au wenyeji wengine huenda wasiwe wakarimu kama tulivyozoea katika Uafrika wetu. Katika hali zote hizi, tujiandae kwa mazuri au mabaya madogo madogo yatakayotokea. Shida ye yote isibomoe umoja na mshikamano wetu. Daima tubaki kama Watanzania, akina mama na Wakristo. Na kama Mtume Paulo, tujisikie furaha na kuwa na utulivu hata tukiingia katika changamoto ye yote ile: “Nayatimiliza katika mwili wangu, yale yaliyopungua katika mwili wa Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani kanisa.” (Wakolosai 1:24).

Hija ni chemchemi ya neema na baraka kwa familia, jamii na taifa
Hija ni chemchemi ya neema na baraka kwa familia, jamii na taifa   (@Vatican Media)

YEPI YA KUYAANGALIA KWA SAFARI YETU: Vitu hivi ni vya kuviangalia kwa safari yetu: KABLA YA KUONDOKA: Kabla ya kuondoka vitu hivi ni muhimu kuvingalia, Weka passport yako karibu na iwe daima salama. Hii ni hati muhimu ya kusafiria. Endapo ikidondoka na kutoonekana, itakuwa shida sana kuendelea na safari. Tunza tiketi yako ya ndege na boarding passes. Katika viambatanisho vya safari yako weka pia kadi ya homa ya Manjano. Kuna sehemu nyingine yaweza kuulizwa. Kwa ajili ya ukaguzi uwanja wa ndege, vimiminika vyote viwe katika mzigo wa kuingia ndani ya ndege. Katika mzigo wako wa mkononi (carry on bag) kama utakuwa na lotion au maji, vitatupwa katika kikapu cha taka taka. " Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana…" (Zaburi 122:1) Uwe na fedha yako binafsi ya kujikimu. Kwa nchi za Ulaya matumizi ni ya Euro. Ila, wakati mwingine wanapokea Dola ya Marekani. Na fedha yako ivunjevunje katika viwango vidogo vidogo ili isilete usumbufu wakati wa manunuzi ya vitu vidogo vidogo. Kuna wafanyibiashara wengine hutumia ujanja unapowapa fedha kubwa, wakadai yakuwa hawana chenji. Beba dawa zako za dharula. Tutakuwa na “First Aid Kit” ya pamoja. Ila, kwa wale wenye kisukari au presha, beba dawa zako za kutosha. Na usisahau kubeba vipimo vyako ili daima uwe unaangalia presha au sukari yako. Ni vizuri kuwa na dawa za tahadhali kwa maumivu pia au mafua ya ghafla. Na dawa hizi unapoingia kwa ndege ziweke katika begi lako la kuingia nalo ndani. Wakati mwingine bahati mbaya hutokea mizigo yetu hucheleweshwa hata kwa siku mbili kama imepelekwa sehemu nyingine.

Mambo ya kuzingatia wakati wa safari
Mambo ya kuzingatia wakati wa safari   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

UZITO WA MIZIGO: Ni vizuri kubeba mizigo kwa uzito wa kadiri kabla ya kuenda hija. Katika ndege ya kwenda Roma kutokea hapa Dar Es Salaam, tutakuwa na ruhusa walau ya kuwa na kilo 23 kg kwa mzigo mkubwa na ule mdogo wa mkononi ni kilo 10 Kgs. Kwa safari za ndani ya Bara Ulaya; mfano toka Roma Kwenda Lourdes ndege huwa ndogo. Hivyo uzito wa mizigo unayoruhusiwa ni walau kilo 20 kwa mzigo mkubwa, na kilo 10 kwa ule mdogo wa kuingia nao ndani. Katika manunuzi yetu tuwe na busara na uangalifu mkubwa. Unaweza kununua vitu vingi vikakugharimu sana kwa usafirishaji uwanja wa ndege kabla ya kupanda ndege. Tukumbuke ya kuwa kila mmoja wetu atakuwa na hamu ya kurudi nyumbani na zawadi kwa wapendwa wake; kishawishi ni kuomba kupima na mwingine ambaye naye atakuwa na mizigo mikubwa vile vile. HALI YA HEWA: Kwa ujumla miezi hii kati ya Mei na Juni ni kipindi cha joto kidogo kwa nchi zote za Ulaya. Ila, kwa tahadhali unaweza kubeba sweta jepesi. Au, kwa akina mama unaweza kuwa na mtandio wako mwepesi ili kujikinga na baridi itakapojitokeza. Katika safari zote za kutembea, vaa viatu vyepesi kama raba au “Sandles.” Na katika sehemu nyingi za makanisa huangalia sana uvaaji wa wana hija. Kuna vijana wetu wa sasa huingia makanisani na nguo zisizo na heshima.

Kila hujaji anapaswa kuangalia afya na stamina yake
Kila hujaji anapaswa kuangalia afya na stamina yake   (@Vatican Media)

AFYA YA KIMWILI, STAMINA: Kuna sehemu zitatulazimu kutembea umbali fulani kwa miguu ili kuzifikia sehemu za kuhiji. Tena kuna sehemu zina vilima au mipando mikali. Hapa kila mmoja awe vizuri katika “stamina” yake na afya. Na kama utakuwa na hali sio nzuri kwa changamoto ya afya; usijilazimishe. Ni vizuri kuwaambia viongozi wetu kabla ili waangalie uwe karibu au ubakie ndani ya basi. Katika mizunguko yako utahitajika kubeba chupa ndogo ya maji ya kunywa pale utakapokuwa na kiu. Vinginevyo, kwenye mabasi mengine maji huuzwa na dreva ndani ya basi. IBADA, NA MISA TAKATIFU: Katika hija na mizunguko yetu, kuna Makanisa ambayo tutakuwa na ruhusa ya kuadhimisha misa kwa lugha yetu ya Kiswahili. Kwa maandalizi ni vizuri kuwa na kitabu cha Misale ya Kirumi (Misale ndogo au Misale kubwa ya Altare) na pia kile kitabu kidogo cha masomo. Kama mmoja atakuwa na Biblia, itatosha kuwa na Shajara kwa siku husika.

Ushiriki mkamilifu katika Ibada mbalimbali ni muhimu
Ushiriki mkamilifu katika Ibada mbalimbali ni muhimu   (@Vatican Media)

MAANDALIZI YA KIROHO: Kabla ya kuondoka Jumatatu usiku; mchana wake tutakuwa na tafakari ya siku nzima. Kimsingi, tutakuwa na tafakari walau ya saa moja, kitubio na Adhimisho la Misa Takatifu. Kila mmoja wetu atumie fursa hii ya kujikusanya, kujihudhurisha na kujinyenyekeza mbele za Mungu wetu. Tukio la hija si la kila mwaka. Huenda kwa wengi wetu ni tukio la moja moja kwa maisha yako yote. Maandalizi ya kiroho ni muhimu sana. Hata Wana wa Israeli walipotaka kuvuka kikwazo kikubwa cha safari yao ya Nchi Takatifu (Mto Yordani) waliambiwa na Yoshua: “Yoshua akawaambia watu, Jitakaseni; maana kesho Bwana atatenda mambo ya ajabu kati yenu.” (Yoshua 3:5). Mpendwa, hakikisha unapata nafasi ya kitubio ili kukupa mazingira ya rehema kamili uwapo hija. Na Kitendo cha kujikabidhi kwa Mungu maana yake ni; kumuomba Mungu ili aweke mkono na baraka yake ili safari yote iwe na kibali chake. Tafakari yetu itaanza kuanzia saa 4:00 hadi saa 5:00 asubuhi. Baadaye, kabla ya misa Takatifu tutakuwa na zoezi la Sakramenti ya Kitubio. Tumeandaa mapadre wawili wa ziada ili kila mmoja awe huru kwenda kwa padre ye yote anayemtaka na kuomba msaada wa kiroho.

Jubilei ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi
Jubilei ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi   (ANSA)

HIJA NCHINI ITALIA: ROMA, ASISSI NA KASHIA: Tutaondoka Dar Es Salaam kulekea Roma, Italia usiku wa Jumatatu Mei 11, kuamkia Jumanne. Safari tutaianza saa 9:35 usiku kwa shirika la ndege ya Turkish, flight TK 604. Tutawasili Roma muda wa mchana karibu saa 8:10 mchana. Tutapokelewa na mwenyeji wetu Patrizia. Kwa siku ya kwanza na ya pili tukiwa Italia, yaani siku 3 na 4; yaani tarehe 13 Mei na 14 tutakuwa na haya yafuatayo: Kushiriki kutaniko na Baba Mtakatifu Leo XIV asubuhi wakati wa Katekesi yake juu ya Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kwa namna ya pekee, kuhusu Bikira Maria, sanjari na kumbukizi ya Miaka 45 tangu jaribio la kutaka kumuua Mtakatifu Yohane Paulo II lilipotokea kunako tarehe 13 Mei 1981. Hapa tutakuwa na mahujaji wenzetu kutoka kila pande za dunia mbele ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Ni tukio la kusisimua kwa vile tutaonana na kiongozi wetu Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani. Kama wahujaji kutoka Tanzania, nasi tutatengewa sehemu maalumu ambayo tutatakiwa kufika mapema. Baada ya kutaniko hili, tutatembelea Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu “Mary Major” Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran; Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta za Roma. Pia tutaona ngazi Takatifu (Sancta Sanctorum). Ngazi hizi zilichimbuliwa Yerusalem na Mtakatifu Helena, Mama Mzazi wa Mtakatifu Constantine. Alifanya kazi hii karne ya Nne. Na inasemekana ndizo ngazi alizopanda Kristo Yesu akienda “Priotorium ya Pontio Pilato” kabla ya kifo chake. Kulingana na mpango wa mwenyeji wetu, tutapata pia nafasi ya kuadhimisha misa katika Basilika la Santa Maria Maggiore, mahali alipozikwa Baba Mtakatifu Francisko.

Watanzania wengi wana Ibada kwa Mtakatifu Rita wa Cascia
Watanzania wengi wana Ibada kwa Mtakatifu Rita wa Cascia

Muda wa mchana tutaianza safari yetu ya kueleka Kashia na Assisi. Huko tutalala baada ya chakula cha jioni Assisi. Tukiwa Assisi na Kashia, asubuhi yake baada ya kifungua kinywa, tutatembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Klara, Kanisa la Mtakatifu Carlo Acutis na Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Wapendwa, Karne ya 12 ya historia ya kanisa, na historia ya dunia, ilikuwa ni kipindi cha kuibuka kwa mfumo wa ukabaila (feudalism). Watu wachache walihodhi ardhi kubwa na kufanya biashara kwa kiwango kikubwa. Tena sio biashara ya ndani, bali na sehemu za mbali. Kila familia ilijitahidi na kujibainisha kwa mafanikio yake kwa kibiashara na ukubwa wa ardhi walioyomiliki. Kipindi hicho kulikuwa na familia chache tajiri sana na wengi maskini wa kutupwa. Kuwa fukara; wakati huo, hata katika mtizamo wa kikanisa, ilikuwa ni kama laana au kutosikilizwa na Mungu. Na hata Kanisa lilijiingiza kuwa na umiliki wa maeneo au ardhi kubwa na kuwatumikisha watu katika mashamba yao. Ni katika karne hizi hizi, ambazo Kanisa lilizaa Mtakatifu muhimu sana; kijana Francisko wa Assisi. Kama vijana wengi wa wakati wake, aliyaanza maisha yake kwa anasa katika familia yake ya kitajiri. Baba yake alikuwa mfanyabiashara mkubwa na maarufu. Na Mtakatifu Francisko wa Assisi baada ya kuzingatia maisha yake kwa kina; alibadilika na kuwa maskini wa kutupwa kwa ajili ya Kristo. Na Mtakatifu Francisko kati ya mistari mingi ya Biblia iliyomgusa na kumfanya aache yote ni huu: “Yesu akamwambia, “kama ukitaka kuwa mkamilfu, nenda kauze vyote ulivyonavyo na fedha utakazopata, uwape maskini, nawe utakuwa umejiwekea hazina kubwa mbinguni.” (Mt 19:21)

Mtakatifu Carlo Acutis
Mtakatifu Carlo Acutis   (ANSA)

Maisha ya Mtakatifu Francisko wa Assisi yaliwavutia vijana wengine, kama Mtakatifu Klara ambao waliamua kufuata maisha ya mashauri ya kiinjili (Evangelical Counsels) mengi tutayasikia kupitia mwenyeji wetu. Kwa ujumla ni Francisko ni Mtakatifu aliyeacha alama kubwa sana katika Kanisa letu. Na ndio maana hata Papa aliyepita aliamua kuendeleza kile alichoanza Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa kuchagua jina la Baba Mtakatifu Francisko. Baada ya mizunguko yote ya mchana kutwa, jioni yake tutalala Kashia. Kesho yake siku ya 5 Ijumaa Mei 15, baada ya kifungua kinywa tutafanya adhimisho la Misa Takatifu. Baadaye tufanya mizunguko Kashia. Tutaona Kanisa kuu la Mtakatifu Rita. Baadaye tutaeleka Loreto. Hapa tutaona Madhabahu muhimu na maarufu duniani ambayo imetolewa kwa heshima ya Bikira Maria Mpashwa Habari. Na tutaona Sanamu ya Mama yetu Bikira Maria (Black Madona) ambayo ni chimbuko la Litania ya Loreto. Baadaye tutapelekwa San Giovanni Rotondo kwa chakula na mapumziko. Kashia ni mahali ambapo tutakutana na masimulizi ya Mtakatifu Rita wa Kashia kwa yale yaliyoshindikana. Mtakatifu huyu ni Mtakatifu pendwa sana na familia nyingi hapa Tanzania. Mtakatifu huyu ni wa karne ya 13. Rita hapo mwanzoni alikuwa mtu wa ndoa. Aliolewa na mume mkorofi aliyemuachia watoto wawili wa kiume. Maisha ya mtakatifu huyu ni kutaka kusema hata katika ndoa kuna chembe chembe za utakatifu. Katika maisha magumu yapo. Ila, anayevumilia hula baadaye mbivu. Mtakatifu huyu anatia moyo na shime kwa wana ndoa wengi. Na wengi wametendewa muujiza kwa maombezi yake. Na ndio maana kuna vikundi au vyama vya kitume parokia nyingi viitwavyo: Mtakatifu Rita wa Kashia. Kihistoria, tamanio la kwanza la Mt Rita wa Kashia, lilikuwa ni kuwa mtawa katika kanisa. Ila, wazazi wake walimlazimisha kuolewa na mtu mwenye uwezo na mali. Baada ya mume kufariki na watoto wake wawili pia, ilimpatia nafasi ya kuingia shirika la Kimonarki la Waaugustiniani. Na hapo ndipo alipozama katika maisha ya utakatifu.

Mtakatifu Padre Pio. Utuombee
Mtakatifu Padre Pio. Utuombee

Baada ya mizunguko ya siku nzima, kesho yake tukiwa San Giovanni Rotondo, tutatembelea sehemu muhimu ya Madhabahu ya Padre Pio. Na baadaye tutaenda Lanchiano kwenye eneo la Muujiza wa Ekaristi Takatifu. Mtakatifu Padre Pio ni Mtakatifu wa Karne ya 19 (1887 – 1968). Yeye alikuwa mtawa wa shirika la Wakapuchini. Maisha yake yanagusa sana. Tutaonana Mungu anayesema nasi katika nyakati zetu kwa njia ya upweke wetu, mateso na kusahaulika. Kuna vipindi ambavyo tutanuka na kutemewa mate kwa ajili ya Kristo Yesu. Na vipindi ambavyo lazima tuongee kwa ujasiri kama Ayubu mwenye madonda: “Lakini mimi najua ya kuwa mtetezi wangu yu hai, na ya kuwa atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, lakini pasipokuwa na mwili wangu nitamuona Mungu.” (Ayubu 19:25 - 261) Baada ya mizunguko yote ya upande wa Kaskazini mwa Italia kwa Mt Rita, Padre Pio na Mtakatifu Francisko wa Assisi, jioni yake tutarudi Roma kwa mapumziko na chakula.

Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes
Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes   (AFP or licensors)

NCHINI UFARANSA: LOURDES, KWA MTATAKATIFU BERNADETA WA SUBIRU: Jumatatu Mei 18 2026 baada ya kifungua kinywa, kundi letu la mahujaji litapelekwa kiwanja cha ndege kwa safari ya kuelekea nchini Ufaransa katika Kijiji cha Lourdes au Lurdi. Tunatarajia kufika jioni sana. Tutakutana na mwenyeji wetu Miguel. Na baada ya chakula ni mapumziko. Kesho yake asubuhi baada ya kifungua kinywa tutatembelea Kanisa kuu la Bibi yetu wa Lourdes; pamoja na Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili. Tukiwa hapo jioni yake tutashiriki maandamano makubwa ya Ekaristi Takatifu na wagonjwa. Wagonjwa mamia kwa mamia kutoka duniani kote hufika hapa. Na ni maandamano yanayovutia sana. Tukiwa njiani katika maandamano tunaweza kualikwa kusali fungu moja la Rozari kwa lugha ya Kiswahili. Na pia hata nyingi katika fungu letu tunaweza kuimba kwa Kiswahili. Hapa eneo la Lourdes au Lurdi ni mahali alipotokewa binti mdogo Bernadeta wa Subiru; na Mama Bikira Maria mwaka 1858. Kwa wale wanaopenda wataoga katika chemchem ambayo Bernadeta aliichimba kwa mikono yake huku akiongea na Mama Bikira Maria. Tutatembelea hata nyumba ya wazazi wa Mtakatifu Bernadeta na kupata masimulizi ya tukio zima. Jioni yake ni mapumziko na kulala.

Madhabahu ya Bikira Maria
Madhabahu ya Bikira Maria

HIJA NCHINI HISPANIA: ZARAGOZA NA BARCELONA: Jumanne ya tarehe 19 Mei 2026 tutaondoka na kuelekea Zaragoza nchi Hispania. Ni mwendo wa karibu masaa matatu (3). Ni urefu wa karibu kilometa 246. Tukifika huko, tutaliona Kanisa kuu la Bibi yetu wa Mnara (Pillar), makumbusho mbalimbali. Na jioni yake baada ya mizunguko yote; tutaenda katika hoteli tuliyopangiwa kwa kulala na chakula. Kesho yake Jumatano Mei 20, baada ya kifungua kinywa tutaianza safari ya kuelekea Barcelona. Kutoka Zaragosa hadi Barcelona ni karibu masaa matatu (3). Na ni umbali wa kilometa 309. Tukifika huko Barcelona cha pekee ni kuona Abasia ya Montserrat na Sanamu ya “Black Madona.” Jioni yake tutaelekea hotelini kwa chakula cha jioni na mapumziko.

Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima
Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima   (Reuters)

NCHINI URENO: LISBON HADI FATIMA: Alhamisi tarehe 21 Mei, baada ya kifungua kinywa, tutaianza safari ya kuelekea Ureno (Portugal). Tutatumia ndege kwa safari. Na umbali kutoka Barcelona hadi Lisbon ni kilometa 1,245. Ni sawa na umbali kama wa Dar Es Salaam hadi Bukoba. Tutafika jioni yake Fatima. Tutaadhimisha Ibada ya Misa katika kikanisa cha Apparitions (Matokeo ya Bikira Maria), baadaye ibada ya njia ya Msalaba, na tutatembelea Kanisa kuu la Utatu Mtakatifu (Holy Trinity Basilica). Jioni tutashiriki tukio kubwa na la kusisimua; la maandamano ya mishumaa. Tutaelekea hotelini kwa chakula cha jioni na kupumzika. Cha pekee hapa Fatima ni eneo ambalo watoto watatu: Francis, Lucia na Yasinta walipata maono ya Bikira Maria. Fatima ni sehemu muhimu sana ya hija kidunia. Mwaka 1917 yalitokea matukio ya kuonekana Ishara ya Mama yetu Bikira Maria kwa watoto hawa watatu ambao walikuwa wanachunga mbuzi kondeni. Na cha ajabu matokeo haya yalikuwa yanafanyika tarehe hiyo hiyo moja ya kila mwezi wa Mei na Oktoba. Na kila tokeo msisitizo ulikuwa ni kusali, kutubu, kuongoka na sadaka. Nchi ya Ureno itupe picha ya karne ile ya 13 – 15 ambapo safari za uvumbuzi wa ulimwengu zilifanyika kutokea hapa. Wareno walikuwa magwiji na wataalamu wa safari za Merikebu kwa kwenda mbali sana. Ni nchi ya kina Vasco Da dama na wenzake ambao walifika Pwani ya Afrika Magharibu, Afrika Kusini (Cape of Good Hope) baadaye Sofara (Pwani ya Msumbiji) na hata wakajenga Mnara wa “Fort Jesus” kati ya mwaka 1593.

Ijumaa tarehe 22 Mei 2026 ni Siku ya kurejea Tanzania
Ijumaa tarehe 22 Mei 2026 ni Siku ya kurejea Tanzania

MWISHO WA HIJA NA KURUDI NYUMBANI, TANZANIA: Ijumaa tarehe 22 Mei, 2026 baada ya kifungua kinywa (ambayo itawekwa kwenye kiboksi); tutaianza safari ya kuelekea Lisbon. Na tutanza safari yetu ya kurudi nyumbani Tanzania, na ndege yetu ni “TK 1756.” Na kila mmoja tunatarajia baada ya magumu ya hija yote; tutarudi na hadithi ya kumwambia Kristo: “Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme.” (Luka 10:17 - 18) Ila Yesu atatuambia kila mmoja wetu baada ya hija hii; licha ya mafanikio haya yote ya kuenda salama, kusali na kuvumilia; furaha yetu ni hii: “Lakini msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.” (Luka 10:20) Wapendwa mama zangu, wanandoa na mapadre, ninawatakia kila la heri kwa maandalizi ya Hija yetu.

Hija ya WAWATA 2026 OK
16 Mei 2026, 14:08