kauli mbiu ya Ujumbe wa Pentekoste kwa Mwaka 2026: “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” kilichotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko. kauli mbiu ya Ujumbe wa Pentekoste kwa Mwaka 2026: “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” kilichotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko.  

Ujumbe wa Sherehe ya Pentekoste Kwa Mwaka 2026: Umoja, Ushiriki Na Utume

Roho Mtakatifu ni nguvu ya Mungu inayobadilisha mioyo na kupyaisha ulimwengu. Anapoingia ndani ya mwamini, huondoa kiburi na uchungu, akitoa uwezo wa kusamehe na kupenda. Kazi hii ya Roho Mtakatifu inaleta mwamko mpya unaofanya maisha ya watu binafsi na jamii kuwa vyombo vya haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na hivyo kuendelea na hija ya maisha ya kiroho kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu yuko pamoja nao hadi...

Na Kamati Tendaji ya Halmashauri ya Walei Taifa, - Dar Es Salaam, Tanzania.

Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka waamini kumwachia nafasi Roho Mtakatifu aweze kuwapyaisha kutoka katika undani wa maisha yao wanaposhiriki kikamilifu Liturujia ya Kanisa kwa njia ya Ibada, ishara, ukimya, lakini zaidi kwa njia ya uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu. Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa yawasaidie waamini kuzama katika Fumbo la maisha na utume wa Kanisa, kiasi kwamba, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa sanjari na Neno la Mungu linalotangazwa na kushuhudiwa linakuwa ni chemchemi ya mabadiliko ya ndani katika maisha. Wakiwa wameungana na Bikira Maria katika Sala, waendelee kumsubiri Roho Mtakatifu atakapolishukia Kanisa wakati wa Sherehe ya Pentekoste na kuwakirimia waamini Mapaji yake Saba. Roho Mtakatifu ni nguvu ya Mungu inayobadilisha mioyo ya waamini na kupyaisha ulimwengu. Anapoingia ndani ya mwamini, huondoa kiburi na uchungu, akitoa uwezo wa kusamehe na kupenda bila masharti. Kazi hii ya Roho Mtakatifu inaleta mwamko mpya unaofanya maisha ya watu binafsi na jamii kuwa vyombo vya haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na hivyo kuendelea na hija ya maisha ya kiroho kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahari. Ufuatao ni Jumbe kutoka Kamati Tendaji Halmashauri ya Walei Taifa!

Sherehe ya Pentekoste: Umoja, Ushiriki na Utume
Sherehe ya Pentekoste: Umoja, Ushiriki na Utume   (@Vatican Media)

Wapendwa katika Kristo Yesu, tunamshukuru Mungu kwamba Pentekoste ya mwaka huu imetukuta katika kipindi cha Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” kilichotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko. Kwa ajili hiyo tunawaalika kutafakari kwa namna ya pekee sana kauli mbiu yetu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Kanisa la Kisinodi linatuhimiza kila mmoja wetu kumpa nafasi Roho Mtakatifu na kuwa mshirika wa pamoja kuanzia ngazi ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo (JNNK); ambazo zimekuwa ni uti wa mgongo wa Utume wetu sisi Wakatoliki. Hapo ndipo mahali pekee pa kuweza kujenga maelewano na kuuishi Ukristo wetu; yaani hapo ndipo ushirika unapoanzia na kujieneza hatua kwa hatua hadi ngazi ya taifa. Tazama jinsi ilivyo vema, na kupendeza, ndugu wakae pamoja, kwa umoja (Zab 133:1). Ndani ya JNNK tunapata marafiki wa kusafiri pamoja, marafiki tunaoweza kutembea pamoja katika njia moja na marafiki wa kusikilizana na kusindikizana katika hija yetu ya hapa duniani.

Mtakuwa Mashuhuda wangu hadi miisho ya dunia
Mtakuwa Mashuhuda wangu hadi miisho ya dunia   (@Vatican Media)

Kanisa Takatifu Katoliki la Mitume linaishi katika upendo unaowezesha ushirika huu kukua na kudumu ambao Utatu Mtakatifu ni Kielelezo chake, yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Katika ngazi husika ya ushirika, watoto, vijana, wazee, wanawake kwa wanaume tunaweza kujiamini kuzungumza kwa uwazi, kusikilizwa tukiunganishwa kwa Uhuru, Upendo, Ukweli na bila kuwa ndumilakuwili. Nia yetu ikiwa kujitakatifuza wenyewe na kuyatakatifuza malimwengu. USHIRIKI: Kanisa la Kisinodi limeangalia mbali juu ya namna ya kujenga umoja katika Kanisa letu. Sote tunaalikwa, yaani Walei, Watawa wa kike na wa kiume na Waklero wote kwa pamoja tuwe kitu kimoja tukitenda kazi na majukumu yetu kwa umoja. Yesu Kristo Mkombozi wetu alituachia dhima ya umoja nasi ni wajibu wetu kuulinda na kuutetea umoja huo kwa vitendo kwa njia ya ushiriki wetu. Tukiwa watoto wa Mungu tulioumbwa kwa sura na mfano wake (Mwa 1:26a), tunatakiwa kuishi kwa umoja kama Utatu Mtakatifu, yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Wakristo wa Kanisa la mwanzo, waliishi wakiwa roho moja na moyo mmoja wakishirikishana mali zao kadri ya uhitaji wa kila mwanajumuiya. Hakuna hata mmoja aliyetindikiwa. Tunaona.

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari

Ndugu wapendwa katika Kristo, Katika maadhimisho haya ya Pentekoste mwaka 2026, tunasimama tena mbele ya Fumbo kuu la upendo wa Mungu lililofunuliwa kwa kushuka kwa Roho Mtakatifu juu ya Mitume (Mdo 2:1–11). Tukio hili si kumbukumbu ya historia, bali ni moto hai unaotaka kuwaka upya ndani ya mioyo yetu leo. Ni sauti ya Mungu inayotuita sisi sote—hasa walei tuamke, tubadilike, na tuanze kuishi kwa dhati wito wetu wa Kikristo. Katika mwanga wa Maandiko Matakatifu, mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na Mafundisho ya Papa Leo XIV kutoka mafundisho ya Papa Francisko akirejea katika Waraka wake wa Kitume wa Furaha ya Injili, “Evangelii gaudium” anasema tunaitwa kuingia katika maisha ya imani yaliyo hai, yanayoshuhudiwa kwa matendo, si kwa maneno pekee. Bwana wetu Yesu Kristo anatutuma kwa msisitizo usio na kificho: “Hubirini mkisema: Ufalme wa mbinguni umekaribia… mmepata bure, toeni bure” (Mt 10:7–8). Hili si ombi, bali ni agizo. Hili si jukumu la wachache, bali ni wito wa kila mbatizwa. Na bado, ukweli unaouma ni huu: mara nyingi tumenyamaza pale tulipotakiwa kunena, tumeficha imani yetu pale ilipotakiwa kung’aa, na tumeishi kama watu wa dunia hii badala ya kuwa mashahidi wa Ufalme wa Mungu. “Enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi…” (Mt 28:19–20) si maneno ya kupita, bali ni utume unaodai uhai wetu wote. Kama Kanisa linavyofundisha, walei si watazamaji, bali ni watendaji wakuu wa uinjilishaji hapa duniani (AA 2; LG 31, 33).

Karama mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa
Karama mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa

Ndiyo maana tunakumbushwa: “Tusichoke kutenda mema” (Gal 6:9). Lakini je, tunachoka kwa sababu gani? Je, si kwa sababu mioyo yetu imepoa? Je, si kwa sababu tumekubali kuishi nusu imani—imani ya Jumapili tu, bila mizizi katika maisha ya kila siku? Pentekoste ya mwaka huu iwe ni sauti ya kuamsha dhamiri: hatuwezi kuendelea kuwa Wakristo wa mazoea bila mageuzi ya kweli ya ndani. Habari Njema ya Ufalme wa Mungu huanza na toba ya kweli. “Msifananishwe na dunia hii, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu” (Rum 12:2). Uongofu si jambo la hiari, ni sharti la wokovu. Hatuwezi kumfuata Kristo huku tukishikilia dhambi kwa mkono mwingine. Hatuwezi kuwa mashahidi wa nuru huku tukiishi gizani. Tukizingatia mafundisho ya Kanisa Katoliki, tunakumbushwa kuwa maisha ya Kikristo yanahitaji nidhamu ya kiroho, sala ya kweli, toba ya dhati, na mshikamano na Sakramenti (KKK 1324; 2697). Hapo ndipo nguvu ya kubadilika hupatikana. Bila hivyo, imani hubaki tasa isiyozaa matunda. Nabii Hosea anatoa onyo kali lisilopaswa kupuuzwa: “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa” (Hos 4:6). Huu ni ukweli unaojidhihirisha hata leo. Wengi wanapotea si kwa sababu hawajui kusoma, bali kwa sababu hawamjui Mungu. Biblia ipo, mafundisho yapo, Kanisa lipo—lakini moyo wa kuyatafuta na kuyaishi umepungua. Hatuwezi kuendelea hivi. Neno la Mungu lazima lirudi katikati ya maisha yetu: katika familia, katika Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo, katika ratiba zetu za kila siku. Kama Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unavyosisitiza, Neno la Mungu ni chakula cha roho; bila chakula hiki, imani hufa polepole (Dei verbum 21).

Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo ni Jukwaa la Uinjilishaji
Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo ni Jukwaa la Uinjilishaji

Pentekoste inatukumbusha pia kuwa hatuko peke yetu. “Wote wakajazwa Roho Mtakatifu” (Mdo 2:4). Roho Mtakatifu ndiye nguvu ya Kanisa, ndiye anayewasha moto wa imani, ndiye anayetoa ujasiri wa kushuhudia pale tulipokuwa na hofu. Lakini swali la kujiuliza ni hili: je, tunamruhusu kweli Roho Mtakatifu atutawale? Au bado tunamzuia kwa ukaidi wetu, kwa dhambi zetu, na kwa uvuguvugu wetu wa kiroho? “Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote” (2 Kor 13:14). Ushirika huu si maneno ya baraka tu, bali ni maisha ya kweli ya kumtegemea Mungu kila siku. Katika mwanga wa Kanisa la kisinodi, tunaitwa kutembea pamoja kama watu wa Mungu, tukisikilizana, kushirikiana, na kubeba mizigo ya wengine kwa upendo. Hata hivyo, sinodi si mjadala wa maneno matupu, bali ni wito wa toba na mageuzi ya kweli ya moyo, tukiruhusu Roho Mtakatifu atuongoze katika maisha ya imani hai. Hivyo, tunahimizwa kuacha ubinafsi na kujenga umoja unaotokana na Kristo, tukishuhudia Injili kwa vitendo. Ndipo sisi walei tunapoitwa kung’aa katika familia, kazini na jamii, tukiwa kweli chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu. Ni kweli kwamba mara nyingi tunajitetea kwa kusema: “Roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu” (Mt 26:41). Lakini Je, hatujatumia maneno haya kama kisingizio cha kuendelea katika udhaifu? Kristo hakutuacha bila msaada. “Vaeni silaha zote za Mungu” (Efe 6:10–13). Hii ni vita ya kiroho, na ushindi wake unadai ujasiri, nidhamu, na imani thabiti. Mtume Paulo anathibitisha kuwa hata katikati ya mateso (2 Kor 11:23–27), neema ya Mungu inatosha. Hivyo basi, kukata tamaa si chaguo la Mkristo.

Neema na Baraka za Mwenyezi Mungu zinatosha
Neema na Baraka za Mwenyezi Mungu zinatosha

Ndugu wapendwa, pengine hali ya imani yetu imefika hapa ilipo kwa sababu sisi wenyewe tumezembea au tumekuwa waoga au tumekubali kuishi chini ya kiwango cha wito wetu. Lakini Pentekoste hii ni nafasi ya neema, nafasi ya kurudi, ya kuanza upya, ya kusema kwa unyenyekevu: “Wewe, Bwana, uko katikati yetu… usituache!” (Yer 14:9). Mungu hachoki kutuita, lakini Je, sisi tuko tayari kuitika? Huu ndio wakati wa kubadilika. Huu ndio wakati wa kuchoma mioyo yetu kwa moto wa Roho Mtakatifu. Huu ndio wakati wa kuacha imani ya juu juu na kuingia katika undani wa ufuasi wa Kristo. Tusonge mbele bila woga, tukishikilia ahadi yake: “Mimi nipo pamoja nanyi siku zote hata ukamilifu wa dahari” (Mt 28:20). Basi, kwa sauti moja, kwa moyo uliowaka moto wa imani, na kwa maisha yanayoshuhudia, tusimame na kutangaza kwa ujasiri: Roho Mtakatifu atujalie neema ya ujasiri, mageuzi ya kweli ya moyo, na upendo unaotenda kazi katika maisha yetu ya kila siku. Amina! Ni sisi watumishi wenu, Kamati Tendaji ya Halmashauri ya Walei Taifa.

Ujumbe wa Pentekoste 2026
21 Mei 2026, 17:58