Vatican inasikitishwa na athari za vita na mdororo wa uchumi na matukio mabaya ya tabianchi!
Na Sr. Christine Masivo,CPS –Vatican.
Askofu Mkuu Fernando Chica Arellano, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya: Chakula na Kilimo (FAO, IFAD na WFP), alielezea wito wa Vatican wa ustahimilivu katika mifumo ya kilimo, ambayo imeona usumbufu mkubwa katika miaka ya hivi karibuni. Alizungumza hayo Jumanne tarehe 12 Mei 2026 katika Kikao cha 35 cha Mkutano wa kikanda wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Ulaya, uliofanyika huko Dushanbe, Tajikistan. Askofu Mkuu Arellano alielezea kuunga mkono lengo la mkutano huo la kuhamasisha mifumo ya kilimo, ili mtu yeyote asikose chakula kinachowawezesha kuishi maisha tulivu na kamili. Alisisitiza umuhimu wa hatua madhubuti za kukuza usalama wa chakula kufuatia migogoro ya hivi karibuni ya kimataifa. "Mchanganyiko wa vita visivyo na huruma, mdororo wa kiuchumi, matukio makubwa ya tabianchi, kutokuwa na utulivu wa kisiasa, na soko kuwa tete ambako kumesababisha mchanganyiko hatari kwa mifumo ya chakula duniani," alisema.
Migogoro imevuruga masoko ya chakula duniani
Katika miaka ya hivi karibuni, migogoro kadhaa imevuruga masoko ya chakula duniani, ikiwa ni pamoja na vita vya Urusi na Ukraine vilivyovuruga mauzo ya nje ya nafaka na usambazaji wa mbolea, pamoja na vita vinavyoendelea vya Iran na Marekani ambavyo tayari vimeongeza bei za mafuta na mbolea. Migogoro mingine imesababisha usumbufu mkubwa kwa mifumo ya chakula ya ndani, kama vile vita vya Sudan, ambavyo vimesababisha uhaba mkubwa wa chakula katika miji mikubwa na ongezeko la njaa kali. Katika hotuba yake, Askofu Mkuu Chica Arellano alitoa wito kwa mataifa kupambana na "mwenendo huu mbaya sana" kwa kuratibu hatua ili nchi ziweze kutembea pamoja "kwa maelewano ya kindugu." Lengo kuu, alisema, ni kwa watu wote kuwa na upatikanaji thabiti na wa kudumu wa chakula cha kutosha, chenye lishe, na salama.
Haki ya kijamii,uendelevu wa mazingirana heshima kwa binadamu
Katika hotuba yake Askofu Mkuu Arellano alizitaka nchi za Ulaya kutekeleza mifumo ya kisheria ili kuelekea mifumo ya chakula inayojumuisha "haki ya kijamii, uendelevu wa mazingira, na heshima kwa binadamu kama kanuni zinazoongoza hatua zote za umma na binafsi." Kujenga ustahimilivu katika mifumo ya kilimo duniani ni miongoni mwa vipaumbele vya dharura zaidi vya wakati wetu, alisema. Badala ya kutumia mbinu zile zile za uzalishaji, Askofu Mkuu Chica Arellano alitoa wito wa jinsi chakula kinavyozalishwa kubadilishwa, kuachana na unyonyaji wa uchoyo hadi uwekezaji ulioongezeka katika maeneo ya vijijini yaliyo hatarini zaidi na yaliyosahaulika.
"Sekta ya kilimo, inapaswa kuungwa mkono na maamuzi ya busara ya kiuchumi na kisiasa, kuwawezesha vijana kujitolea kwa shauku kwa kilimo na kutoacha mashambani kwa kukata tamaa ili kuhamia mijini." Hatimaye, Askofu Mkuu Chica Arellano alifafanua kwamba uzalishaji wa chakula cha kilimo lazima uendelee kuwa na heshima ya binadamu katikati, kukidhi mahitaji ya chakula bila kuhatarisha mustakabali, na kukuza kazi nzuri katika ngazi ya ndani.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.