Kuanzia tarehe 4 Juni hadi tarehe 7 Juni 2026 Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, Taifa inaadhimisha mkutano wake mkuu wa 47 wa WAWATA, huko Jimbo Katoliki la Singida. Kuanzia tarehe 4 Juni hadi tarehe 7 Juni 2026 Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, Taifa inaadhimisha mkutano wake mkuu wa 47 wa WAWATA, huko Jimbo Katoliki la Singida.  

Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 47 wa WAWATA, Taifa, Singida

Kuanzia tarehe 4 Juni hadi tarehe 7 Juni 2026 Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, Taifa inaadhimisha mkutano wake mkuu wa 47 wa WAWATA, huko Jimbo Katoliki la Singida. Mkutano huu umefunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Waraka wa Papa Leo XIV: "Magnifica humanitas" Utu!

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, Jimbo Katoliki la Singida, Tanzania.

Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women Of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika.” Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Taswira ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ni kuona kila mwanamke mkatoliki wa Tanzania anaelewa nafasi yake na wajibu wake wa Kikristo kuanzia ngazi ya Familia, Jumuiya, Kanisa, jamii na Taifa kwa ujumla, pia wanawake wanakuwa na maendeleo fungamani ya kiuchumi ili kukidhi mahitaji msingi ya familia na hivyo kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na Jamii kwa ujumla, na kufanya maisha ya hapa duniani kuwa ni taa na nuru katika Ulimwengu kama mawakili wa Kristo Yesu. Kuanzia tarehe 4 Juni hadi tarehe 7 Juni 2026 Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, Taifa inaadhimisha mkutano wake mkuu wa 47 wa WAWATA, huko Jimbo Katoliki la Singida. Mkutano huu umefunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC.

WAWATA katika ubora wao
WAWATA katika ubora wao   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Ifuatayo ni hotuba ya Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa WAWATA Taifa anayemaliza muda wake na Rais wa Umoja wa Wanawake Barani Afrika.  Napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Uhai na kwa zawadi ya Utume wa Wanawake Wakatoliki Tanzania. Ninatoa pole kwenu nyote kwa safari na kwa masumbufu yote ya njiani. Tunatambua sadaka yenu ya muda na majitoleo ya mali, ahsanteni. Kwa namna ya pekee na kwa moyo wa unyenyekevu niwashukuru sana wenyeji wetu Jimbo Katoliki Singida kwa maandalizi yote na mapokezi. Ahsanteni sana. Mpendwa Mhashamu sana  Edward Mapunda, tunakushukuru sana kwa kutuendeshea Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi. Tunafarijika sana kwa kushiriki nasi,  na kutubariki tunapoanza Mkutano huu muhimu. Kwa moyo wa unyenyekevu tunakushukuru Sana kwa kukubali kuwa mwenyeji wa Mkutano wetu Mkuu, USENGWILE BABA. Baba Mwiru umekuwa daraja la mawasiliano na Baba Askofu toka wakati wa Jubilei ya miaka 50, WAJEFYA BABA. Baba Mossi, pamoja na kamati yote ya maandalizi CHIKUTIA ASANDE!

Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti WAWATA Taifa anayemaliza muda wake
Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti WAWATA Taifa anayemaliza muda wake   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Wapendwa Baba zetu walezi, Idara ya Kichungaji na Idara ya Walei,  Wakurugenzi wa Majimbo tunaomba mpokee Shukrani zetu kwa kuendelea kutulea, kutushauri, kutuelekeza lakini zaidi kuendelea kututuma kumtumikia Mungu. Ahsanteni Sana kwa kutenga muda wenu kujumuika nasi katika Mkutano huu muhimu Sana. Ninawashukuru viongozi wa Kamati Tendaji ya WAWATA Taifa kwa maandalizi yote ya Mkutano. Tunakutana Jimboni Singida kumshukuru Mungu kwa kutembea nasi awamu hii inayomaliza uongozi na kupongezana kwa yote tuliyoweza kufanikisha pamoja, tumshangilie Mungu. Mkutano huu unafanyika siku kumi baada ya siku kuu ya Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, ambayo inaadhimishwa, Jumatatu baada ya Sherehe ya Pentekoste na kwa mwaka huu ilifanyika tarehe 25 Mei 2026. Siku hii kwa mwaka huu wa 2026 ilibeba uzito wa pekee kwani Waraka wa kwanza wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” kwa kifupi “MH” ulizinduliwa rasmi. Lakini pia Mkutano huu unafunguliwa siku moja tu baada ya Kumbukumbu ya mashahidi wa Uganda, Ndungu zetu. Hebu kila mmoja ajihoji, Niko tayari kuifia Imani?

Waraka wa Papa Leo XIV Magnifica humanitas: Utu wa binadamu
Waraka wa Papa Leo XIV Magnifica humanitas: Utu wa binadamu   (@Vatican Media)

Mwaka huu Kanisa na dunia kwa ujumla inatafakari kwa namna ya pekee kuhusu ujenzi wa amani katika kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya teknolojia ya Akili Unde (Artificial Intelligence, AI). Tunashuhudia teknolojia ikibadilisha maisha ya watu, elimu, afya, biashara, mawasiliano na hata namna tunavyohusiana kama familia na jamii katika ujumla wake. Tumerejea kutoka kwenye Hija tarehe 23/05/2026 na siku mbili baadae teknolojia ya Akili Unde ikatumika kutengeneza picha yenye mahujaji feki waliopewa vyeo na majina feki. Swali kubwa tunalohitaji kulijibu sisi kama wanawake Wakatoliki ni hili: Je, maendeleo haya yanajenga amani au yanazalisha  kinzani na migawanyiko? Je, yanakuza utu, heshima na haki msingi za binadamu wa au yanaupunguza? Je, yanasaidia familia kuwa karibu zaidi au yanatuondoa katika mahusiano ya kweli ya upendo na mshikamano? Tumejiandaa vipi kukabiliana na haya yote ikiwa hata kabla ya Mabadiliko haya mkubwa Malezi ya Familia yalishatikiswa, ndoa zinavunjika kila uchwao, maadili na utu wema kuporomoka, ubinafsi uliokithiri, unyanyasaji wa kijinsia, ukosefu wa ajira, uadilifu wa viongozi n.k? Katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” anatukumbusha kuwa maendeleo ya teknolojia yanapaswa kwenda sanjari na maendeleo ya utu na maadili. Akili Unde inaweza kufanya mengi kwa haraka, lakini haiwezi kupenda, kusamehe, kulea mtoto, kujali mgonjwa, wala kuleta amani ya kweli katika moyo wa mwanadamu. Hii ni zawadi ambazo Mungu amempa mwanadamu. Ndiyo maana ajenda ya Amani na Akili Unde si mjadala wa wataalamu wa teknolojia pekee, bali ni wajibu wa kila Mkristo. Tunaitwa kuhakikisha kwamba teknolojia inakuwa daraja la kuunganisha watu badala ya ukuta wa kuwatenganisha; inakuwa chombo cha kulinda maisha badala ya kuyahatarisha; na inakuwa ni njia ya kukuza haki, amani, maridhiano, ukweli na mshikamano badala ya chombo cha udanganyifu, chuki na ukandamizaji.

Teknolojia iwe ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu na wala si vinginevyo
Teknolojia iwe ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu na wala si vinginevyo   (REUTERS)

Sisi wanawake, ambao Mungu ametukabidhi jukumu la kulea familia na jamii, tuna nafasi ya kipekee ya kuhakikisha kwamba kizazi kijacho kinatumia teknolojia kwa hekima, uwajibikaji na hofu ya Mungu. Amani ya dunia inaanzia katika mioyo yetu, familia zetu, na matumizi sahihi ya teknolojia yanaanzia katika malezi tunayowapa watoto wetu. Papa Leo XIV anaona Kanisa si mpinzani wa maendeleo ya kisayansi bali mshiriki katika kuyaelekeza. Kanisa linapaswa kusaidia dunia kutofautisha kati ya maendeleo yanayokuza maisha na yale yanayoweza kuharibu utu, uhuru, na mshikamano na udugu wa kibinadamu. Waraka wa “Magnifica humanitas” ni mwaliko wa kuhakikisha kuwa mapinduzi ya kidijitali yanaongozwa na: Kanuni maadili na utu wema; Busara, hekima, haki, na upendo, ili teknolojia isimtawale mwanadamu bali iwe ni chombo cha huduma. Papa Leo XIV anasisitiza kwamba, mustakabali wa dunia hautaamuliwa na uwezo wa mashine, bali na uwezo wa mwanadamu kubaki mtu: mwenye dhamiri, mwenye huruma, mwenye mahusiano, na mwenye kufunguka kwa Mungu. Kwa lugha rahisi, waraka huu unaweza kufupishwa kwa sentensi moja: “Akili unde” inaweza kuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya dunia, lakini haitawahi kuchukua nafasi ya utu wa mwanadamu; hivyo teknolojia yote lazima ihudumie maisha, haki, na hadhi ya kila mtu.” Mwisho nipende kuomba, tunapojiandaa na uchaguzi tukumbuke kuwa uongozi wa Kikristo unapaswa kujengwa juu ya msingi wa: kusikiliza, uwajibikaji wa pamoja, ukweli, uwazi na umoja na ushirika, huku ukitambua utofauti wa watu na kuongozwa na mahitaji halisi ya nyakati kwa kusoma alama za nyakati. Kiongozi mwaminifu ni yule anayejenga umoja, anakumbatia maoni mbalimbali kwa upendo na unyenyekevu, na daima hutafuta ustawi wa jumuiya na utukufu wa Mungu kuliko maslahi binafsi.

Mkutano wa WAWATA 2026
04 Juni 2026, 15:17